Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Chakula Kinaweza Kukudhuru?
    Amkeni!—2001 | Desemba 22
    • Je, Chakula Kinaweza Kukudhuru?

      JE, UNAKULA mara tatu kwa siku? Ikiwa ndivyo, utakapofikia umri wa miaka 70 utakuwa umekula zaidi ya mara 75,000. Hiyo inamaanisha kwamba Mzungu wa kawaida, atakuwa amekula mayai 10,000, mikate 5,000, magunia 100 ya viazi, ng’ombe 3, na kondoo 2, mbali na vyakula vingine. Je, inachosha kula vyakula hivyo vyote? La hasha! Tunafurahia kuambiwa maneno kama “karibu chakula.” Mkuu mmoja wa shule ya upishi alisema hivi: “Chakula ndicho jambo muhimu maishani.”

      Kwa kawaida tunaamini kwamba chakula tunachokula ni chenye kujenga afya. Lakini ikiwa mlo mmoja tu kati ya ile milo 75,000 ungekuwa na kitu kinachodhuru, tungeweza kuwa wagonjwa mahututi. Je, tunaweza kuwa na uhakika kwamba chakula tunachokula hakitatudhuru? Siku hizi watu wengi hawana uhakika juu ya jambo hilo. Katika nchi kadhaa watu wameanza kuwa na wasiwasi mwingi kuhusu chakula. Kwa nini?

      Kwa Nini Wana Wasiwasi?

      Kila mwaka, asilimia 15 hivi ya wakazi wa Ulaya wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula. Kwa mfano, mapema katika miaka ya 1980, mafuta ya kupikia yenye sumu yaliua watu 1,000 huko Hispania na kufanya watu 20,000 wawe wagonjwa mahututi. Katika mwaka wa 1999, Wabelgiji walishtuka walipojua kwamba chakula kama vile mayai, kuku, jibini, na siagi huenda kikawa na sumu inayoitwa dioxin. Hivi majuzi, Waingereza walishtuka sana—na biashara ya nyama ya ng’ombe ikaharibika—ng’ombe walipoambukizwa ugonjwa wa kichaa cha ng’ombe. Kisha ugonjwa wa midomo na miguu ulienea, na mamilioni ya ng’ombe, kondoo, nguruwe, na mbuzi wakachinjwa na kutupwa.

      Hata ingawa mambo hayo yanaogopesha, kuna matisho mengine pia kuhusiana na vyakula. Mbinu mpya za kukuza na kutengeneza vyakula huwatia watu wasiwasi. Tume ya Ulaya ilitaarifu hivi mwaka wa 1998: “Tekinolojia mpya ya kunururisha vyakula na kurekebisha maumbile ya mbegu kwa kuingiza chembe tofauti za urithi imesababisha mabishano mengi.” Je, mbinu hizo za kisayansi huboresha chakula chetu au hukiharibu? Na tunaweza kufanya nini ili kuhakikisha kwamba chakula tunachokula hakitatudhuru?

  • Je, Tunaharibu Chakula Chetu?
    Amkeni!—2001 | Desemba 22
    • Je, Tunaharibu Chakula Chetu?

      KUJARIBU kuboresha vyakula kwa njia mbalimbali si jambo jipya. Kwa vizazi vingi wanadamu wamejaribu kuboresha vyakula kwa ukuzaji na uzalishaji mzuri ambao umetokeza namna mbalimbali za mazao, ng’ombe, na kondoo. Mwakilishi mmoja wa Usimamizi wa Chakula na Dawa wa Marekani alisema kwamba “karibu vyakula vyote unavyonunua vimeboreshwa kwa ukuzaji na uzalishaji.”

      Lakini wanadamu wamejaribu kuboresha vyakula kwa njia nyingine pia. Mbinu nyingi za kutengeneza vyakula zimebuniwa ili kuboresha ladha au rangi yake, kuvihifadhi au kuvifanya viwe na umbo na ladha inayotakiwa. Watu wamezoea kula vyakula vilivyoboreshwa kwa njia hizo.

      Lakini watu wengi wana wasiwasi kwamba mbinu mpya za kujaribu kuboresha vyakula huviharibu. Kwa nini? Baadhi ya watu wanahofu kwamba mbinu za siku hizi hufanya vyakula viwe hatari kwa afya. Je, hivyo ndivyo ilivyo? Tuchunguze mbinu tatu zinazotiliwa shaka.a

      Homoni na Viuavijasumu

      Katika miaka ya 1950, kiasi kidogo cha viuavijasumu kilianza kuongezwa kwenye chakula cha kuku, nguruwe, na ng’ombe katika nchi kadhaa. Dawa hiyo inaongezwa ili kupunguza magonjwa, hasa mahali ambapo wanyama wanasongamana sana. Katika nchi fulani, vyakula vya wanyama huongezewa pia homoni, ili wanyama wakue haraka. Inadhaniwa kwamba homoni na viuavijasumu hulinda wanyama wasiambukizwe magonjwa na kufanya ufugaji ulete faida nyingi za kifedha. Wateja hunufaika kwa kuwa vyakula hivyo ni vya bei nafuu.

      Sababu hizo zinaonekana zinafaa. Lakini, je, nyama ya wanyama waliolishwa dawa hizo inaweza kumdhuru mlaji? Ripoti ya Kamati ya Jumuiya ya Ulaya ya Uchumi na Jamii ilionya kwamba mlaji anaweza kuambukizwa bakteria zisizouawa na viuavijasumu. Ripoti hiyo ilisema kwamba “baadhi ya bakteria hizo, kama vile Salmonella na Campylobacter, huenda zikasababisha magonjwa mabaya.” Isitoshe, vipi ikiwa vyakula vina mabaki ya viuavijasumu pia? Inahofiwa kwamba magonjwa yasiyotibika kwa viuavijasumu yangeweza kutokea hatua kwa hatua.

      Namna gani nyama ya wanyama waliolishwa homoni? Profesa mmoja wa Munich huko Ujerumani, Dakt. Heinrich Karg anasema: “Wataalamu wote wanakubaliana kwamba nyama ya wanyama waliolishwa homoni haitadhuru afya, iwapo wanyama hao watalishwa homoni hiyo kwa kiwango kinachotakikana.” Hata hivyo, gazeti la Die Woche linaripoti kwamba ‘watafiti wamebishana kwa miaka 15 na hawajaweza kukubaliana’ kwamba nyama hiyo haidhuru afya. Na nchini Ufaransa kuwalisha wanyama homoni kumekatazwa katakata. Ni wazi kwamba mgogoro bado unaendelea.

      Vyakula Vilivyonururishwa

      Tangu majaribio yalipoanzishwa Sweden mwaka wa 1916, angalau nchi 39 zimekubali kuua viini kwenye chakula kama viazi, mahindi, matunda, na nyama kwa kiwango kidogo cha mnururisho. Kwa nini? Inasemekana kwamba mnururisho huua karibu bakteria, vimelea, na wadudu wote, hivyo mlaji anaepuka kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na vyakula. Mnururisho pia hufanya vyakula visiharibike.

      Wataalamu wanasema kwamba, vyakula bora ni vyakula safi visivyotengenezwa viwandani. Lakini ni watu wachache sana katika nchi zilizoendelea wanaotumia wakati mwingi kupika. Gazeti la Test linasema kwamba kwa kawaida watu katika nchi hizo wanatumia “muda wa dakika kumi kupika kiamsha kinywa, na dakika kumi na tano kupika chakula cha mchana na muda huohuo kupika mlo wa jioni.” Kwa hiyo, si ajabu kwamba watu wengi hupendelea vyakula vya mikebe na vinavyodumu kwa muda mrefu. Lakini, je, vyakula vilivyonururishwa vinadhuru afya?

      Katika mwaka wa 1999, Shirika la Afya Ulimwenguni lilichapisha matokeo ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa mataifa mbalimbali. Walifikia mkataa kwamba vyakula vilivyonururishwa “havidhuru afya navyo vina virutubishi vya kutosha.” Wale wanaounga mkono mbinu hiyo wanasema ni kama kunururisha vitambaa vya kufunga vidonda hospitalini ili kuua vijidudu, au kuchunguza mizigo kwenye uwanja wa ndege kwa kutumia mnururisho. Hata hivyo, wachambuzi wanasisitiza kwamba mnururisho huharibu vyakula na huenda pia kukawa na madhara yasiyojulikana bado.

      Kubadilisha Maumbile ya Mbegu

      Kwa muda fulani wanasayansi wameweza kubadilisha maumbile ya mbegu kwa kuingiza chembe ya urithi ya kiumbe kimoja ndani ya kiumbe kingine cha aina hiyohiyo. Hata hivyo, wanasayansi wanaweza kufanya mengi zaidi leo. Kwa mfano, wanasayansi wamebadilisha maumbile ya aina fulani za nyanya na vilevile tunda la stroberi (strawberry) kwa kuingiza chembe ya urithi ya samaki ili matunda hayo yaweze kusitawi katika hali ya baridi.

      Mbinu ya kubadilisha maumbile ya vyakula kwa kuingiza chembe tofauti za urithi imetetewa sana na vilevile kushutumiwa vikali.b Watetezi wa mbinu hiyo wanasema kwamba inaweza kutegemeka zaidi kuliko ukuzaji wa kawaida, na kwamba itaongeza mazao na kupunguza njaa. Lakini je, vyakula hivyo vinaweza kudhuru afya?

      Wanasayansi wa vyuo vya elimu ya juu katika nchi ya Uingereza na Marekani, na vilevile Brazili, China, India, Mexico, na nchi nyingine zinazoendelea, waliandika ripoti kuhusu habari hiyo. Ripoti hiyo iliyochapishwa mwezi wa Julai, 2000 ilisema: “Kufikia leo, mbegu zilizorekebishwa maumbile zimepandwa kwenye mashamba ya hektari zaidi ya milioni 30 [ekari milioni 70], na mazao hayo hayajasababisha madhara yoyote ya afya.” Katika maeneo fulani vyakula hivyo huonwa kuwa vyenye kujenga afya kama tu vyakula vya kawaida.

      Hata hivyo, watu katika maeneo mengine wana wasiwasi mwingi. Baadhi ya watu nchini Austria, Ufaransa, na Uingereza, wanatilia shaka ubora wa vyakula hivyo. Mwanasiasa mmoja wa Uholanzi alisema hivi juu ya vyakula vilivyobadilishwa maumbile: “Hatuvipendi vyakula vya aina hiyo.” Watu wanaopinga vyakula vya aina hiyo wanasema kwamba mbinu hiyo si ya asili, na huenda ikadhuru mazingira.

      Baadhi ya wanasayansi huonelea kwamba uchunguzi zaidi unahitajika ili kuona ikiwa vyakula vilivyoongezwa chembe tofauti hudhuru walaji au la. Kwa mfano, Shirika la Tiba la Uingereza linaonelea kwamba vyakula hivyo vitanufaisha watu. Hata hivyo, shirika hilo linasema kwamba kwa kuwa kuna wasiwasi fulani kuhusu mambo kadhaa—kama vile mizio (allergy) ya vyakula hivyo—“ni lazima uchunguzi zaidi ufanywe.”

      Kufanya Maamuzi Yanayofaa

      Katika nchi fulani asilimia 80 ya vyakula vinatengenezwa viwandani. Mara nyingi vyakula hivyo huongezewa kemikali mbalimbali ili viwe na ladha na rangi inayotakiwa, na visiharibike. Kitabu kimoja chasema kwamba “ni lazima kemikali ziongezwe kwenye vyakula vingi vya kisasa, kama vile vyakula visivyo na kalori nyingi, vitafunio, na vyakula vya mikebeni.” Mara nyingi vyakula hivyo vina viungo vilivyobadilishwa maumbile.

      Kwa miaka mingi ukulima ulimwenguni pote umeendeshwa kwa njia ambazo watu wengi wanaona ni zenye madhara. Kwa mfano, dawa za kuua wadudu zimetumiwa. Isitoshe, vyakula vinavyotengenezwa viwandani vimetiwa kemikali ambazo zimeathiri baadhi ya walaji. Je, mbinu mpya za ukuzaji ni hatari zaidi kuliko hizo za hapo awali? Hata maoni ya wataalamu hutofautiana. Uthibitisho mbalimbali wa kisayansi huunga mkono pande zote mbili.

      Kwa kuwa watu wengi leo wanaona ni vigumu sana kuepuka vyakula vilivyotengenezwa na kukuzwa kwa mbinu za kisasa, na kwa sababu wana matatizo mengine makubwa zaidi, wameazimia kutohangaikia jambo hilo. Hata hivyo, wengine wana wasiwasi mwingi. Wewe na familia yako mnaweza kufanya nini endapo mna wasiwasi juu ya vyakula vilivyotengenezwa na kukuzwa kwa mbinu za kisasa? Huenda mwongozo unaotolewa katika sehemu inayofuata unaweza kuwasaidia. Hata hivyo, ni jambo la busara kwanza kuhakikisha kwamba tuna maoni yanayofaa kuhusu habari hiyo.

      Chakula ni kama afya. Kwa sasa hatuna njia ya kupata wala chakula wala afya kamili. Kulingana na gazeti natur & kosmos la Ujerumani, hata watu wanaochagua vyakula na kuvitayarisha kwa uangalifu sana hawawezi kuhakikisha kwamba vyakula vyote wanavyokula vinajenga afya kabisa. Chakula kinachofaa mtu mmoja kinaweza kumdhuru mwingine. Kwa hiyo, tunahitaji kutumia busara tunapofanya uamuzi juu jambo hilo.

      Biblia haituelezi uamuzi unaofaa kuhusu vyakula vilivyopo leo. Hata hivyo, inatufundisha sifa moja ambayo itatusaidia. Andiko la Wafilipi 4:5 linasema: “Hali yenu ya kukubali sababu na ijulikane kwa watu wote.” Tukiwa na busara tunaweza kufanya maamuzi mazuri bila kupita kiasi. Busara inaweza kutuzuia tusiwashurutishe wengine kukubali maoni yetu. Na inaweza kutuepusha tusibishane na wale walio na maoni tofauti.

      Hata hivyo, hatari nyingi zinazohusu vyakula hazibishaniwi. Baadhi ya hatari hizo ni zipi, na unaweza kufanya nini uziepuke?

      [Maelezo ya Chini]

      a Kwa kawaida, kila mtu hula vyakula anavyopendelea. Gazeti la Amkeni! halipendekezi vyakula mbalimbali vinavyozungumziwa, wala halipendekezi kutokula vyakula fulani, iwe vimetengenezwa kwa njia gani. Mfululizo huu umeandikwa ili kuwajulisha wasomaji juu ya mambo yanayojulikana sasa kuhusiana na habari hiyo.

      b Tafadhali soma toleo la Amkeni! la Aprili 22, 2000.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Je, mla-nyama anaathiriwa na homoni na viuavijasumu ambavyo ng’ombe hulishwa?

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Ni jambo la busara kusoma maandishi kwenye vyakula vilivyotengenezwa viwandani

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Kuna faida kununua vyakula vilivyotolewa shambani karibuni

  • Jinsi ya Kuchagua Chakula Kisichodhuru Afya
    Amkeni!—2001 | Desemba 22
    • Jinsi ya Kuchagua Chakula Kisichodhuru Afya

      JE, NI hatari kula chakula? Huenda takwimu zifuatazo zinaweza kufanya mtu afikiri hivyo. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kila mwaka watu milioni 130 hivi katika Eneo la WHO huko Ulaya wanaambukizwa magonjwa yanayosababishwa na chakula. Katika mwaka wa 1998, zaidi ya watu 100,000 nchini Uingereza walikuwa wagonjwa kwa sababu ya kula chakula kibaya, na 200 kati yao walikufa. Inakadiriwa kwamba kila mwaka watu milioni 76 hivi wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula huko Marekani, na 325,000 kati yao hulazwa hospitalini, na 5,000 hufa.

      Si rahisi kujua hesabu kamili ya ulimwenguni pote. Hata hivyo, shirika la WHO linaripoti kwamba watu milioni 2.2 hivi walikufa kutokana na magonjwa ya kuharisha katika mwaka wa 1998, na milioni 1.8 kati yao walikuwa watoto. Ripoti hiyo inasema: “Wengi kati ya wagonjwa hao waliambukizwa magonjwa yanayosababishwa na chakula au maji machafu.”

      Huenda ukashtuka kusikia takwimu hizo kubwa. Lakini je, takwimu hizo zikufanye uwe na wasiwasi mwingi juu ya chakula? Bila shaka la. Ebu fikiria mfano mwingine. Kila mwaka watu milioni 4.2 hivi nchini Australia wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula, yaani watu 11,500 hivi kila siku! Huenda hiyo ikaonekana kuwa idadi kubwa sana. Lakini kwa upande mwingine: Waaustralia hula milo bilioni 20 kila mwaka, kwa hiyo ni milo michache sana inayosababisha magonjwa.

      Hata hivyo, hatari ipo. Ni kwa nini chakula kinafanya watu wawe wagonjwa, na tunaweza kufanya nini kupunguza hatari hiyo?

      Jinsi Vyakula Vinavyosababisha Magonjwa

      Jarida la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200 yanaweza kusababishwa na chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha magonjwa hayo yote si vingi sana. Dakt. Iain Swadling, afisa wa shirika la Huduma ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Chakula, anasema kwamba asilimia 90 hivi ya magonjwa yote yanayosababishwa na chakula, huenda yanasababishwa na jamii za vijidudu “zisizozidi 24.” Visababishi vya magonjwa kama vile virusi, bakteria, vimelea, sumu, na kadhalika, huingiaje katika chakula?

      Dakt. Swadling anataja mambo matano ambayo kwa kawaida husababisha magonjwa: “Kula chakula kibichi chenye vijidudu; kula chakula kilichotayarishwa na watu wagonjwa au walioambukizwa viini; kutohifadhi vyakula vizuri na kutayarisha chakula saa kadhaa kabla ya kukila; kuchafua chakula safi kwa kukiweka pamoja na chakula chenye vijidudu wakati wa kukitayarisha; kutopika chakula vizuri au kutopasha moto vya kutosha chakula kilichopikwa kimbele.” Ingawa orodha hiyo inaweza kushtua, inaonyesha jambo zuri pia. Jambo hilo ni kwamba karibu magonjwa yote yanayosababishwa na chakula yanaweza kuzuiwa. Soma sanduku kwenye ukurasa wa 8 na 9 ili ujue kile unachoweza kufanya usiambukizwe ugonjwa unaosababishwa na chakula.

      Kufanya Maamuzi Yanayofaa

      Leo, watu fulani wanaoelewa kwamba vyakula vinaweza kusababisha magonjwa wameamua kununua, kutayarisha, na kula vyakula vilivyotolewa shambani karibuni. Endapo wewe unapendezwa na jambo hilo, nenda kwenye maduka na masoko yenye vyakula vilivyotolewa shambani karibuni na visivyotiwa dawa yoyote. Kitabu kimoja cha mwongozo kinaeleza: ‘Watu wengi wanawaendea wakulima moja kwa moja—ama sokoni au kwenye mashamba yao—ili wapate vyakula vilivyotolewa shambani karibuni, wajue jinsi vilivyokuzwa na mahali vinapokuzwa.’ Inafaa kufanya hivyo hasa unapotaka kununua nyama.

      Hali kadhalika, afadhali ununue vyakula katika majira yake, kwa kuwa mara nyingi vyakula hivyo ndivyo vizuri zaidi. Hata hivyo, kumbuka kwamba ukifanya hivyo, utakosa matunda na mboga fulani wakati ambapo hazipatikani.

      Je, unapaswa kula tu vyakula vilivyokuzwa bila kutumia dawa yoyote wala mbolea ya kikemikali? Wewe mwenyewe utaamua. Bila shaka wengi wanapenda vyakula vilivyokuzwa hivyo kwa sababu wanatilia shaka mbinu mpya za kukuza na kutengeneza vyakula. Lakini si wote wanaokubali kwamba vyakula vilivyokuzwa bila dawa za kuua wadudu na mbolea ya kemikali ni bora.

      Hata iwe unapendelea vyakula gani, chunguza kwa uangalifu vyakula unavyonunua. Mtaalamu mmoja aliyenukuliwa katika gazeti la Die Zeit, alisema kwamba “watu huangalia bei tu wanaponunua vyakula.” Kufikiria bei ni jambo la maana, lakini chunguza pia maandishi yanayoonyesha vilivyomo. Inakadiriwa kwamba karibu nusu ya watu wa nchi za Magharibi hawachunguzi maandishi yanayoeleza ni virutubishi vipi vilivyomo katika vyakula wanavyonunua. Ni kweli kwamba katika nchi nyingine maandishi hayo hayaonyeshi habari nyingi. Lakini ukitaka vyakula vinavyojenga afya chunguza sana vyakula unavyonunua.

      Hata uamuzi wako kuhusu vyakula uwe nini, bila shaka itakubidi kubadilika mara kwa mara kupatana na hali ya nchi unamoishi. Watu wengi leo hawana fedha za kutosha, wala wakati, wala uwezo wa kuhakikisha kwamba vyakula vyote wanavyokula ni vyenye kujenga afya kabisa.

      Je, tunatia chumvi tunaposema hivyo? La, hivyo ndivyo ilivyo. Lakini, mambo yatabadilika karibuni.

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

      Kile Unachoweza Kufanya

      ◼ Safisha. Nawa mikono kwa maji ya moto na sabuni kabla ya kuanza kutayarisha kila aina ya chakula. Nawa mikono baada ya kwenda chooni, na baada ya kushughulikia mtoto (iwe ni kumbadilisha nepi au kumpangusa makamasi), au kushika mnyama yeyote, hata mnyama-kipenzi. Osha vyombo, mbao za kukatia, na meza kwa maji ya moto na sabuni baada ya kutengeneza kila aina ya chakula—hasa baada ya kukata nyama, kuku, au samaki na vyakula vingine vinavyotoka baharini. Gazeti la Test linapendekeza “kuosha matunda na mboga katika maji ya uvuguvugu” ili kuondoa wadudu na mabaki ya dawa ya kuua wadudu. Mara nyingi kutoa maganda na kuchemsha vyakula ni njia bora za kuvisafisha. Toa na utupe majani ya nje-nje ya kabichi na letusi (lettuce). Katika sehemu zenye maji machafu huenda ikawa muhimu kutia dawa ya kuua vijidudu, kama vile dawa ya kung’arisha, permanganate, au mvinyo wa siki, katika maji ya kuosha matunda au mboga zitakazoliwa zikiwa mbichi.

      ◼ Pika Vizuri. Karibu bakteria zote, virusi vyote, na vimelea vyote vitakufa ikiwa chakula kitapikwa kufikia nyuzi Selsiasi 70 (moto kabisa), na si lazima kupika kwa muda mrefu. Kuku anahitaji kupikwa hadi aive kabisa kufikia nyuzi Selsiasi 80. Chakula kinachopashwa moto chapasa kufikia nyuzi Selsiasi 75 au kuwa moto na kutoa mvuke. Usile kuku ambaye bado ni mwekundu au mayai yasiyopikwa vizuri. Samaki anapasa kupikwa hadi awe laini na kubadilika rangi.

      ◼ Usiweke Vyakula Pamoja. Usiweke kamwe nyama, kuku, au samaki mbichi pamoja na vyakula vingine unapofanya ununuzi, unapohifadhi vyakula hivyo, au unapovitayarisha. Usiache maji ya vyakula hivyo yatone wala kutiririka kwenye vyakula vingine. Usiweke kamwe chakula kilichopikwa kwenye chombo kilichokuwa na nyama, samaki, au kuku mbichi ila chombo hicho kiwe kimeoshwa vizuri kwa maji ya moto na sabuni.

      ◼ Hifadhi Vyakula Ifaavyo. Friji inaweza kuzuia bakteria zisiongezeke, lakini halijoto yake inapasa kuwa nyuzi Selsiasi 4 tu. Mashine ya barafu inapasa kuwa na nyuzi Selsiasi 17 chini ya kiwango cha kuganda. Weka vyakula vinavyoweza kuharibika kwenye friji kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Ukiweka vyakula mezani mapema, vifunike ili kuzuia inzi.

      ◼ Ujihadhari Unapokula Kwenye Mikahawa. Inakadiriwa kwamba katika nchi fulani zilizoendelea, asilimia 60 hadi 80 ya watu waliopata magonjwa yanayosababishwa na chakula walikula vyakula vilivyopikwa mikahawani. Hakikisha kwamba mkahawa unamokula unafuata sheria za usafi zilizowekwa na serikali. Agiza nyama iliyopikwa vizuri. Unaponunua chakula mkahawani na kukileta nyumbani, kile kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Endapo muda zaidi ungepita kabla hujala chakula hicho, kipashe moto vizuri kufikia nyuzi Selsiasi 75.

      ◼ Tupa Chakula Unachoshuku Kimeharibika. Afadhali utupe chakula ambacho unashuku kimeharibika. Si vizuri kutupa chakula kizuri, lakini matibabu ya ugonjwa uliosababishwa na chakula kilichoharibika yatakugharimu fedha nyingi hata zaidi.

      [Hisani]

      —Mengi kati ya madokezo hayo yanapatikana katika kichapo Food Safety Tips, kilichochapishwa na Baraza la Tekinolojia ya Chakula Kisichodhuru la Marekani.

  • Chakula Chenye Kujenga Afya kwa Wote
    Amkeni!—2001 | Desemba 22
    • Chakula Chenye Kujenga Afya kwa Wote

      KULA vyakula vyenye afya hupendeza sana. Lakini kama vile tulivyoona, si rahisi kupata vyakula hivyo. Jambo linalosikitisha hata zaidi ni kwamba inawabidi mamilioni ya watu kula vyakula vyovyote wanavyoweza kupata bila kujali ikiwa vitawadhuru. Wanapambana kupata chakula cha kutosha. Je, hayo ni mapenzi ya Mungu?

      Ebu fikiria. Mungu alipomwumba mwanamume na mwanamke duniani, je, walikuwa na sababu yoyote ya kuwa na wasiwasi juu ya chakula? Hata kidogo! Simulizi katika kitabu cha Biblia cha Mwanzo linasema: “BWANA Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa.” (Mwanzo 2:9) Kwa hiyo, Adamu na Hawa walikuwa na vyakula vingi mbalimbali. Mungu aliyewaumba alijua virutubishi walivyohitaji; na alijua pia kile ambacho kingewafurahisha. Bila shaka, hatumo katika shamba la Edeni leo. Lakini je, kusudi la Mungu kuhusiana na mwanadamu na dunia limebadilika?

      Tuna sababu nzuri kutarajia kwamba hivi karibuni kila mtu duniani atakuwa na chakula kingi chenye kujenga afya! Tumaini hilo linaweza kutusaidia sana kuwa na maoni yanayofaa juu ya chakula leo. Tukiwa na tumaini hilo, hatutahangaika kupita kiasi.

      Kwa nini tunaweza kuamini kwamba maisha yatabadilika hivi karibuni? Watu wanaojifunza Neno la Mungu kwa makini wanajua kwamba tunaishi katika “siku za mwisho” za ulimwengu huu. Ulimwengu huu unaongozwa kwa hekima ya wanadamu, ambayo mara nyingi haiaminiki wala haijathibitishwa kuwa yenye manufaa. Kufikia sasa haijathibitishwa kikamili kama vyakula vinavyotayarishwa viwandani vinadhuru afya ama la. Kutokuwa na uhakika na jambo hilo husababisha wasiwasi na mabishano.—2 Timotheo 3:1-5.

      Muumba wa wanadamu ameahidi kwamba ataondoa ulimwengu huu na kuleta ulimwengu mpya. Kusudi lake la awali kwa dunia litatimia—dunia yote itakuwa paradiso kama bustani ya Edeni, nayo itakaliwa na watu wenye furaha na afya njema. Hekima ya Mungu inayounganisha wanadamu itaenea kotekote. (Isaya 11:9) Hekima isiyoaminika ya wanadamu haitaongoza mambo tena. Katika ulimwengu huo mpya, utakaofanyizwa na Mungu, wanadamu hawatakuwa na wasiwasi tena kuhusu chakula. Kwa hakika, Mungu aliyetuumba anajua vyakula tunavyohitaji.

      Muumba Ataandaa Chakula Kisichodhuru

      Katika Biblia kuna unabii mbalimbali kuhusu maisha katika ulimwengu unaokuja. Nabii Isaya aliandika hivi: “[Mungu] atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.”

      Unabii wa Isaya pia unasema: “Katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.” Biblia Habari Njema inatafsiri sehemu ya mwisho hivi, “karamu ya vinono na divai nzuri, nyama tamu na mafuta, pamoja na divai safi.”—Isaya 25:6; 30:23, 24.

      Je, hali hiyo inakuvutia? Unabii wa Isaya unatuhakikishia kwamba kila mtu atakayeishi katika ulimwengu mpya wa Mungu atakuwa na chakula cha kutosha. Je, chakula hicho kitakuwa chenye kujenga afya? Bila shaka. Unabii mwingine hutuhakikishia kwamba watu wa Mungu “wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu.” (Mika 4:4) Usalama huo utaletwa na Ufalme wa Mungu wa Kimesiya ambao utaanza kuitawala dunia yote hivi karibuni.—Isaya 9:6, 7.

      Watu hawatakuwa na wasiwasi tena kamwe juu ya chakula. Badala yake, tutafurahia tunapoambiwa: “Karibu chakula.”

      [Blabu katika ukurasa wa 12]

      Hivi karibuni kila mtu duniani atakuwa na chakula kingi chenye kujenga afya

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Mungu amewaahidi watu wote chakula kisichodhuru na chenye afya

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki