-
Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?Amkeni!—2003 | Juni 22
-
-
Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA
RAMIRO ana bonde lililojaa msitu wa mvua.a Bonde hilo liko chini ya Milima ya Andes, huko Amerika ya Kusini na ni mojawapo ya mabonde machache yenye miti ya kale sana katika eneo hilo. Katika eneo hilo lote, milima haina misitu. Wanasayansi kutoka nchi za mbali huja kuchunguza wanyama wa pori katika msitu wa Ramiro, na wamegundua jamii kadhaa ambazo hazijawahi kuonekana. Ramiro anapenda sana kuhifadhi misitu. Anasema: “Sitaruhusu miti ikatwe kwenye msitu wangu.”
Naye Roberto anatunza msitu wa mvua wenye ukubwa wa kilometa 5,600 za mraba kwenye nyanda za chini za bonde la Amazoni. Yeye ni mtunzaji stadi wa misitu naye hukata miti na kuuza mbao za misitu ya mvua katika nchi mbalimbali. Lakini pia Roberto anapenda sana kulinda misitu ya mvua na wanyama wa pori waliomo. “Miti ya misitu ya mvua inaweza kukatwa bila kuangamiza kabisa mimea na wanyama mbalimbali,” anasisitiza.
Ingawa hali zao zatofautiana, Ramiro na Roberto wanahangaishwa sana na uharibifu wa misitu ya mvua. Na bila shaka si wao peke yao wanaohangaishwa na jambo hilo. Katika miaka ya karibuni misitu ya mvua imekuwa ikikatwa ovyoovyo.
Je, hangaiko hilo limepita kiasi? Kwa kweli, watu wameharibu misitu mingi kwenye nchi zenye joto la wastani katika karne zilizopita, hasa kwa ajili ya kilimo. Basi, kwa nini tuhangaike tukiona watu wakifanya vivyo hivyo katika nchi zenye joto? Kuna tofauti kubwa. Kwa mfano, mara nyingi misitu ya mvua hukua kwenye ardhi isiyo na rutuba ambayo haifai kilimo. Pia, kuna viumbe na mimea mingi sana katika misitu ya mvua, na uharibifu wa misitu hiyo huwaathiri wanadamu wote.
Hasara ya Kuharibu Misitu
Zaidi ya nusu ya viumbe wote ulimwenguni hupatikana katika misitu ya mvua. Kuanzia tumbili wadogo na simba-marara hadi kuvumwani zisizo za kawaida na okidi, kuanzia nyoka na vyura hadi vipepeo na kasuku wasiopatikana kwa urahisi. Idadi ya viumbe ni kubwa sana isiweze kuhesabiwa.
Viumbe tofauti-tofauti husitawi katika misitu mbalimbali ya mvua. Kuna misitu ya mvua inayokua polepole milimani, misitu ya mvua yenye giza na majani mengi, misitu ya mvua inayokua katika maeneo yenye majira marefu ya kiangazi, na misitu ya mvua yenye nafasi kubwa. Hata hivyo, watu wengi hawajawahi kufika kwenye msitu wa mvua. Labda wewe pia hujafika kwenye msitu huo. Basi, kwa nini uhangaikie maeneo hayo?
Kuhifadhiwa kwa misitu ya mvua ni muhimu kwako kwa sababu mimea mingi ya chakula na ya biashara ambayo unategemea, kwa njia fulani hutokana na mimea inayokua yenyewe ambayo bado inasitawi kwenye misitu hiyo. Nyakati nyingine mimea hiyo hutumiwa kuzalisha mimea mipya ambayo ina uwezo zaidi wa kukinza magonjwa na wadudu-waharibifu. Kwa hiyo chembe za urithi zinazopatikana katika aina mbalimbali za mimea hiyo ni muhimu.
Pia watafiti wanatengeneza bidhaa muhimu kutokana na misitu ya mvua. Kwa mfano, kiasi kikubwa cha dawa tunazotumia sasa zilitengenezwa kutokana na mimea ya misitu ya mvua. Kwa hiyo, aina mbalimbali za mimea na wanyama katika misitu ya mvua mara nyingi zinaitwa maktaba iliyo hai ambayo ina “vitabu” vingi ambavyo havijafunguliwa bado.
Mimea na Viumbe Wanaoweza Kuangamia kwa Urahisi
Mazingira yenye unyevunyevu ya misitu ya mvua yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na ni tata sana. Idadi kubwa sana ya mimea na viumbe wanategemeana. Kwa mfano, mimea mingi hutegemea ndege, wadudu, au wanyama hususa kwa ajili ya uchavushaji na usambazaji wa mbegu. Misitu hutumia ifaavyo vitu vyote hai vilivyomo kutia ndani mimea, wanyama, wadudu, na vijidudu vidogo kupitia kwa mzunguko tata wa maisha. Jambo la kushangaza ni kwamba mfumo huo wote tata kwa kawaida huwa kwenye udongo usio na rutuba. Ukishaharibiwa, huenda ikawa vigumu au huenda isiwezekane kwa msitu kama huo kusitawi tena.
Watu wengi hujiruzuku kutokana na misitu ya mvua. Mbali na utafiti wa kisayansi na utalii, misitu ya mvua ni muhimu kiuchumi kwa ajili ya bidhaa kama mbao, kokwa, asali, mashina ya mchikichi, mpira, na utomvu. Lakini misitu ya mvua inatoweka haraka sana. Idadi hususa haijulikani lakini jambo moja ni hakika: Misitu hiyo inapungua haraka.
Hasara hiyo ya kimazingira inahuzunisha sana hasa kwa sababu mara nyingi misitu ya mvua inaharibiwa bila sababu nzuri. Misitu mingi imeharibiwa ili kupata sehemu za kulisha ng’ombe. Lakini mara nyingi mimea hushindwa kukua kwenye sehemu hizo na hivyo zinaachwa tu. Imeripotiwa kwamba huko Amazonia, Brazili, ardhi yenye ukubwa wa kilometa 165,000 za mraba imeachwa kwa sababu hiyo.
Je, misitu ya mvua na wanyama-pori waliojaa humo wataokolewa? Ramiro, Roberto, na watu wengine wengi wanajitahidi kulinda misitu ya mvua isiharibiwe na biashara ya ulimwenguni pote, ongezeko kubwa la watu, wauzaji wa wanyama-vipenzi, wakataji-miti na wawindaji haramu. Lakini visababishi vikuu vya uharibifu wa misitu ni vipi? Je, kuna njia yoyote ya kutumia rasilimali nyingi za misitu ya mvua bila kuiharibu?
[Maelezo ya Chini]
a Msitu wa mvua unaopatikana milimani hukua kwenye kimo cha zaidi ya meta 1,000.
[Blabu katika ukurasa wa 3]
Jamii nyingi za wanyama ulimwenguni hupatikana katika misitu ya mvua, pamoja na aina nyingi sana za mimea
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Wakataji-miti na barabara wanazotengeneza zinaweza kuharibu misitu ya mvua
-
-
Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?Amkeni!—2003 | Juni 22
-
-
Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?
WEWE unafikiri kwamba wakataji-miti wana haki ya kuharibu misitu yote ya mvua ulimwenguni? Yaelekea utajibu, la! Hata hivyo, wataalamu fulani wa viumbe na mazingira huenda wakasisitiza kwamba wengi wanaosema la, tayari wamesema ndiyo—kwa mfano, kwa kununua vyombo vya mbao vilivyotengenezwa kwa mbao maridadi na zinazopendwa sana zinazotoka kwenye misitu ya asili ya mvua badala ya misitu inayopandwa na watu.
Mara nyingi kukata miti huonwa kuwa sawa na kuharibu misitu. Na bila shaka, ukataji wa miti huharibu misitu mingi. Hata hivyo, inadaiwa kwamba miti imekatwa kwenye misitu fulani bila kuiharibu. Je, kweli misitu ya mvua na wanyama-pori wataokoka miti ikiendelea kukatwa? Hebu kwanza tuchunguze jinsi ukataji-miti unavyoharibu misitu.
Jinsi Ukataji-Miti Unavyoweza Kuharibu Msitu na Kuwaangamiza Wanyama-Pori
Fikiria kisa hiki: Matingatinga yanaanza kuchimba barabara ndani ya msitu. Punde si punde wakataji-miti wanaanza kufanya kazi kwa misumeno ya minyororo. Kampuni ya kukata miti ina kibali cha muda mfupi cha kupasua mbao, kwa hiyo wafanyakazi wameagizwa wabebe kila mti wenye thamani. Miti hiyo yenye thamani inapoanguka, inaharibu miti mingine iliyo karibu ambayo imeunganishwa na mimea inayotambaa. Kisha, matingatinga makubwa yanapenya vichaka ili kukokota magogo, na yanakanyaga-kanyaga udongo huo mwembamba na kuufanya ukose rutuba.
Kwa kawaida wafanyakazi wa kampuni hiyo wanakula nyama nyingi kuliko wanakijiji. Wanawinda wanyama wengi msituni; mara nyingi hata zaidi ya wanaohitaji. Barabara zinazoachwa na wakataji-miti hufika sehemu ambazo hazingefikika hapo awali. Sasa wawindaji wanaweza kuingia humo kwa magari wakiwa na bunduki ili kumaliza wanyama waliobaki. Wategaji hunasa wanyama wadogo na ndege kwa ajili ya biashara yenye faida kubwa ya wanyama-vipenzi. Wahamaji na maelfu ya watu wasio na makao huja wakitafuta nafasi ya kujiruzuku kwenye maeneo hayo mapya. Njia yao ya kilimo ya kukata na kuchoma misitu humaliza miti inayobaki, na hivyo mvua kubwa huja na kusomba udongo mwembamba wa juu.
Ni kana kwamba msitu umekufa. Uharibifu ulianza miti ilipoanza kukatwa. Lakini je, ni lazima kukata miti kuharibu misitu ya mvua?
Kukata Miti Bila Kuharibu Mazingira
Katika miaka ya karibuni watu wamependezwa kujua mbinu ya kukata miti bila kuharibu mazingira na kutunza misitu kwa njia inayofaa. Lengo ni kukata miti katika njia ambayo itapunguza uharibifu wa misitu na wanyama-pori. Pole kwa pole msitu husitawi tena, na hivyo miti inaweza kukatwa miaka kadhaa baadaye. Kwa sababu ya mkazo kutoka kwa wahifadhi wa misitu, wafanyabiashara fulani sasa hutangaza kwamba mbao zao zinatoka kwenye misitu ambayo imethibitishwa kuwa misitu inayotunzwa ifaavyo. Na tuchunguze utaratibu wa kukata miti bila kuharibu mazingira.
Mtaalamu wa misitu na kikundi cha wasaidizi wanaingia msituni. Kikundi hicho ni baadhi ya vikundi kadhaa ambavyo vitakaa msituni kwa muda wa miezi sita hivi, vikihesabu miti. Kampuni ya kukata miti ina kibali cha muda mrefu, kwa hiyo wafanyakazi wana wakati wa kuchunguza miti ili wahifadhi msitu kwa matumizi ya baadaye.
Mtunzaji wa misitu huandika jina la jamii na nambari ya utambulisho kwenye kila mti. Hapana shaka kwamba ana ujuzi mwingi kwa sababu kuna mamia ya jamii za miti. Hata hivyo, hatua ifuatayo yahitaji tekinolojia ya kisasa.
Akitumia mashine ndogo inayowasiliana na kifaa cha kupokea habari kutoka kwa setilaiti, mtunzaji wa misitu anarekodi ukubwa wa mti, jamii yake, na nambari yake ya utambulisho. Kisha anapohifadhi habari hizo kwenye mashine hiyo, habari zote kuhusu mti huo kutia ndani mahali hususa ulipo, zinawasilishwa kwenye kompyuta iliyo katika jiji kubwa mbali sana.
Baadaye msimamizi wa misitu anatumia kompyuta yake kuchapisha ramani yenye habari kamili kuhusu kila mti wenye thamani msituni. Anachagua miti hususa inayoweza kukatwa kulingana na sheria zilizowekwa. Kuhusu jamii nyingi za miti, inaruhusiwa kukata asilimia 50 tu ya miti yenye kipenyo hususa kilichoonyeshwa kwenye kibali. Miti ya kale na yenye afya zaidi yapaswa kuachwa ili izae mbegu.
Lakini, unawezaje kukata miti bila kuharibu msitu? Mwandishi wa Amkeni! alimwuliza swali hilo Roberto, mtunzaji wa misitu aliyetajwa katika makala iliyotangulia. Alieleza hivi: “Ili kufanya hivyo unahitaji ramani. Tukiwa na ramani ya miti, tunaweza kupanga jinsi ya kukata miti ili tusiharibu sana msitu. Hata tunaweza kupanga upande ambao miti itaanguka tunapoikata ili tusiharibu miti mingine iliyo karibu.
“Pia tunaweza kupanga kuondoa magogo kwa kuyanyanyua kwa kreni, badala ya kutumia matingatinga kwenda kuchukua kila mti mahali ulipo. Kabla ya kukata mti, wakataji hukata mimea inayotambaa kutoka mti huo hadi miti mingine iliyo karibu ili isiharibiwe. Tunakata miti kwa mzunguko, kila mwaka tunachora ramani na kukata miti katika sehemu fulani na hivyo angalau miaka 20 inapita kabla ya kurudi kwenye sehemu hizo. Katika misitu mingine tunarudi baada ya miaka 30.”
Hata hivyo, Roberto ameajiriwa na kampuni ya kukata miti. Kwa hiyo mwandishi wa Amkeni! alimwuliza hivi: “Wakataji-miti wanajitahidi kwa kadiri gani kulinda wanyama-pori?”
Kulinda Wanyama
“Msitu hauwezi kusitawi bila wanyama,” asema Roberto. “Wanyama ni muhimu kwa uchavushaji na usambazaji wa mbegu. Tunajitahidi sana kutosumbua wanyama-pori. Kwa mfano, tunapanga kwa uangalifu barabara za kuingia msituni ili ziwe chache. Iwezekanapo, tunachimba barabara nyembamba ambazo zitaacha majani ya miti yakiwa yameshikana. Hilo huwaruhusu wanyama kama vile dubu wa mitini na tumbili kuvuka barabara bila kushuka miti.”
Roberto aonyesha sehemu fulani zenye rangi kwenye ramani yake. Hizo hazipaswi kuguswa kamwe. Kwa mfano, kuacha safu ya miti kwenye kingo za kila kijito huwaruhusu wanyama watoke sehemu moja hadi nyingine bila kuvuka eneo lisilo na miti.
“Mbali na mazingira muhimu yaliyo kando ya vijito,” anaeleza, “tunalinda pia mapango, miamba mikubwa, miti ya kale yenye mapengo, na miti ya matunda yenye maji mengi, yaani, eneo lolote ambalo ni muhimu kwa viumbe fulani. Ili kuzuia uwindaji haramu, tunawakataza wafanyakazi wetu kuwa na bunduki, na tunawaletea nyama ya ng’ombe na kuku kwenye kambi yao ili wasiwinde wanyama-pori. Kisha, tunapomaliza kukata miti sehemu moja, sisi hufunga au kulinda barabara ili kuzuia wawindaji au wakataji-miti haramu kuingia msituni.
“Mimi binafsi hufurahi kufanya hivyo kwa sababu ninapenda kuhifadhi uumbaji wa Mungu. Lakini karibu hatua zote nilizoeleza ziko kwenye sheria za kimataifa za kupokea cheti cha msitu uliotunzwa ifaavyo. Ili kampuni ipate cheti, lazima iwathibitishie wakaguzi wa mashirika ya kimataifa kwamba inafuata sheria hizo.”
Je, misitu inayotunzwa ifaavyo ina faida? Kwa kawaida wakataji-miti hawakubali kwa utayari kuhifadhi wanyama-pori isipokuwa watunzaji wachache tu wa misitu kama Roberto. Mara nyingi wanaona kwamba sheria hizo zinawazuia kupata faida.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa mashariki mwa Amazonia mwishoni mwa miaka ya 1990 uligundua kwamba gharama ya kuchora ramani za miti, kukata mimea inayotambaa, na kuondoa miti ilikuwa ndogo sana, kwa sababu ya kutumia mbinu bora. Kwa mfano, ni miti michache tu iliyopotea. Mara nyingi bila ramani hizo, watu wanaokata miti kwa msumeno hukata mti lakini wale wanaoikusanya miti hawaupati kwa sababu msitu huo una miti mingi sana.
Pia, mbao ambazo zimeidhinishwa kutoka kwa msitu unaotunzwa ifaavyo zinaweza kuuzwa kwa urahisi. Lakini je, kukata miti bila kuharibu mazingira kwaweza kweli kulinda viumbe? Ni wanyama-pori wangapi ambao hubaki baada ya miti kukatwa kwenye misitu ya mvua?
Je, Wanyama-Pori Wanaweza Kubaki Baada ya Miti Kukatwa?
Ni kweli kwamba, mimea na viumbe walio kwenye misitu ya mvua ni tata na wanahitaji kutunzwa kwa uangalifu. Hata hivyo, kwa kushangaza, wanaweza kuokoka chini ya hali fulani. Kwa mfano, ikiwa miti inakatwa katikati ya msitu, miche ya miti hiyo hukua polepole na kufunika sehemu hizo. Lakini vipi wanyama, ndege, na wadudu?
Jamii chache za wanyama huathiriwa sana, na mara nyingi ukataji wa miti hupunguza idadi ya ndege na wanyama mbalimbali katika sehemu hiyo. Hata hivyo, kwa kawaida kukata miti bila kuharibu mazingira hakuathiri jamii nyingi za viumbe. Ama kweli, kukata miti kadhaa katika msitu kwaweza kuzisaidia jamii fulani ziongezeke. Uchunguzi wa hivi karibuni unadokeza kwamba viumbe mbalimbali wa misitu ya mvua wanaweza kuongezeka kwa sababu ya kuwapo kwa wanadamu—hata kama baadhi yao wanakata miti hususa.
Kwa hiyo ushuhuda mwingi unadokeza kwamba miti inaweza kukatwa katika misitu ya mvua bila kuharibu viumbe mbalimbali. Gazeti Economist la London lilisema: “Asilimia 10 tu ya misitu inayobaki, ambayo inatunzwa ifaavyo, inaweza kutokeza mbao ngumu za kutosha. Sehemu kubwa inayobaki inaweza kulindwa.”
Msitu uliotajwa mwanzoni ni mfano wa msitu unaolindwa kabisa. Ramiro anaulinda kwa sababu wanasayansi wamegundua jamii fulani zilizo katika hatari ya kutoweka. Misitu ya mvua kama hiyo ni haba na ina viumbe wengi sana isivyo kawaida. Ramiro aneleza kwamba “siri ya kuhifadhi misitu ni kuwaelimisha watu. Wanakijiji walipogundua kwamba maji yao yanatokana na msitu huo, walijitahidi kuuhifadhi.”
Ramiro aongezea: “Watalii wa kuhifadhi mazingira ni muhimu pia kwa sababu wanajifunza kwa nini miti na mimea tofauti-tofauti inastahili kulindwa. Wanapoondoka wanakuwa wamethamini zaidi msitu na wanyama-pori.”
Mfano wa Ramiro na Roberto unaonyesha kwamba mwanadamu anaweza kutumia msitu wa mvua bila kuuharibu wala kuangamiza wanyama-pori. Lakini jambo hilo halimaanishi kwamba itakuwa hivyo. Leo watu fulani wanaweza kuhakikisha kwamba mbao wanazonunua zinatoka kwenye msitu uliothibitishwa kuwa unatunzwa ifaavyo. Hata hivyo, wengine hawawezi kuthibitisha jambo hilo. Je, jitihada za kuhifadhi misitu zitaokoa viumbe mbalimbali wenye kupendeza?
[Ramani katika ukurasa wa 7]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BOLIVIA
Ramani iliyo upande wa kulia inatoa habari za kila mti; kama ilivyo juu, ramani hiyo inaonyesha sehemu ndogo tu ya Bolivia
[Hisani]
All maps except top left: Aserradero San Martin S.R.L., Bolivia
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kila mti hutiwa nambari na jina la jamii yake. Kisha, mahali pake hususa hurekodiwa kwa kutumia kifaa (kilicho juu) cha kupokea habari kutoka kwa setilaiti
[Picha katika ukurasa wa 7]
‘Ramani ya kuhesabu miti ni muhimu katika kupanga ukataji wa miti bila kuharibu msitu au wanyama-pori.’—Roberto
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
“Siri ya kuhifadhi misitu imekuwa kuwaelimisha watu.”—Ramiro
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Foto: Zoo de Baños
-
-
Ni Nani Atakayeokoa Misitu ya Mvua?Amkeni!—2003 | Juni 22
-
-
Ni Nani Atakayeokoa Misitu ya Mvua?
MTU yeyote anayetaka kutatua matatizo yanayoipata misitu ya mvua lazima kwanza atatue visababishi vyake. Visababishi gani? Tatizo si kuongezeka tu kwa idadi ya watu. Maeneo yenye rutuba duniani yanaweza kuwalisha watu wote ulimwenguni—na hata wengi zaidi.
Katika nchi kadhaa, serikali zinahangaishwa na kuwapo kwa mazao mengi sana mashambani, ambayo yanafanya bei ya chakula ishuke. Serikali fulani huwatia moyo wakulima watumie mashamba yao kwa shughuli za burudani kama vile, maeneo ya kupiga kambi, viwanja vya gofu, au bustani za wanyama-pori.
Basi kwa nini misitu inapungua ulimwenguni? Ni lazima tuchunguze visababishi vingine vikuu zaidi kuliko vile ambavyo tumetaja.
Visababishi Vikuu vya Uharibifu wa Misitu
Miaka mingi kabla ya watu kuongezeka, serikali nyingi ziliharibu misitu ili kupata mamlaka na utajiri. Kwa mfano, Miliki ya Uingereza ilihitaji mbao za kutengeneza meli na hivyo iliharibu misitu ya mialoni ya Uingereza na misitu ya mivule ya Burma na Thailand. Miliki hiyohiyo iliharibu misitu nchini India ili kupata kuni za tanuru za kuyeyusha chuma. Waliharibu misitu mingine ili wapande mashamba ya mipira, kahawa, na kakao.
Hata hivyo, baada ya vita vya pili vya ulimwengu, misumeno ya minyororo na matingatinga yalitumiwa kuharibu misitu mingi kabisa. Misitu mingi zaidi muhimu iliharibiwa ili kujipatia utajiri.
Makampuni makubwa yalinunua mashamba makubwa yenye rutuba na kutumia mashine kuvuna mazao ya kuuza. Maelfu ya watu walihamia majiji baada ya kupoteza kazi zao. Lakini wengine walihimizwa wahamie misitu ya mvua. Nyakati nyingine maeneo hayo yaliitwa “ardhi isiyo na watu kwa ajili ya watu wasio na mashamba.” Watu walipogundua ugumu wa kulima mahali kama hapo, ilikuwa kuchelewa mno—msitu mkubwa ulikuwa umeharibiwa.
Pia ufisadi wa maofisa wa serikali umeangamiza misitu mingi. Kibali cha kukata miti ni ghali sana. Maofisa fulani wasio wanyofu hutoa kibali cha muda mfupi cha kukata miti baada ya kupokea hongo kutoka kwa makampuni yanayoharibu misitu bila kujali.
Hata hivyo, hatari kubwa zaidi kwa wanyama-pori si ukataji wa miti bali ni kubadili misitu kuwa mashamba. Katika visa fulani, jambo hilo laweza kukubalika ikiwa ardhi hiyo ina rutuba. Lakini mara nyingi, ufisadi au maofisa wasiofaa huwaruhusu watu kukata miti isivyo lazima na kuharibu kabisa misitu.
Wahalifu pia huharibu misitu. Wakataji-miti haramu hukata ovyoovyo miti yenye thamani, hata ile iliyo katika mbuga za kitaifa. Nyakati nyingine wao hupasua mbao humohumo msituni—tabia haramu na yenye kuleta hasara. Wanakijiji hulipwa ili kusafirisha mbao hizo kwa baiskeli au hata mgongoni. Kisha, usiku ukiingia, malori makubwa huzisafirisha kupitia barabara za milimani zisizotumiwa mara nyingi ili kuepuka polisi.
Basi uharibifu wa misitu na kuangamia kwa wanyama-pori hakusababishwi na kuongezeka kwa watu. Mara nyingi husababishwa na usimamizi mbaya, biashara yenye pupa, uhalifu, na serikali zenye ufisadi. Hivyo basi, kuna tumaini gani la kuhifadhi viumbe mbalimbali wanaopatikana katika misitu ya mvua?
Kuna Tumaini Gani kwa Misitu ya Mvua?
“Ni sehemu ndogo tu ya misitu ya mvua ulimwenguni pote inayosimamiwa kwa njia inayofaa,” chasema kitabu The Cutting Edge: Conserving Wildlife in Logged Tropical Forest. Chaongezea hivi: “Kwa sasa, ni misitu michache tu (ikiwa ipo) inayosimamiwa kwa njia inayofaa.” Bila shaka misitu inaweza kusimamiwa kwa njia inayofaa, lakini ukweli ni kwamba misitu inaharibiwa kwa kasi ulimwenguni pote.
Inasemekana kwamba hali ni tofauti sana nchini Bolivia kwa sababu asilimia 25 ya misitu yake ya mvua imethibitishwa kuwa inasimamiwa kwa njia inayofaa. Hata hivyo, misitu inayosimamiwa kwa njia ifaayo ulimwenguni pote haizidi asilimia moja—kiasi kidogo sana chenye kusikitisha. Misitu mingi ya mvua inaharibiwa kabisa. Choyo na pupa ndiyo mambo yanayosababisha uharibifu huo. Je, ni jambo la busara kutumaini kwamba wafanyabiashara na wanasiasa wa ulimwengu watakomesha uharibifu huo na badala yake kuwalinda wanyama na misitu?
Kitabu Forests of Hope chamalizia kwa kuwahimiza wanadamu “wajitahidi kuishi kwa njia inayowafaa watu wote ulimwenguni, bila kuharibu dunia na rasilimali zake.” Mradi huo unavutia lakini je, inawezekana?
Muumba wetu alikuwa na kusudi gani kwa dunia na wanadamu? Aliwaamuru hivi wanadamu wawili wa kwanza: “Mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:28) Kwa hiyo Mungu huwaruhusu wanadamu watumie uumbaji. Lakini ‘kuutiisha’ si kibali cha kuuharibu.
Basi swali ni, Je, wanadamu wanaweza kweli kubadili maisha yao ulimwenguni pote na kuishi “bila kuharibu dunia na rasilimali zake”? Maneno hayo yanaonyesha upendo kwa jirani na staha kwa uumbaji wa Mungu, sifa ambazo ni haba sana katika ulimwengu huu. Kutumaini kwamba viongozi wa kibinadamu wataishi na kuendeleza maisha hayo ni ndoto tu.
Hata hivyo, Neno la Mungu linatabiri wakati ambapo dunia itajaa watu wanaowapenda wanadamu wenzao na Muumba wao. Biblia husema: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:9; Zaburi 37:29; Mathayo 5:5) Ona kwamba watu wa Mungu “hawatadhuru” wala “hawataharibu” kwa sababu wamemjua na kumpenda Yehova, Muumba Mtukufu. Hapana shaka kwamba watu hao wataepuka kuharibu dunia.
Hii si ndoto tu. Hata sasa, Yehova anakusanya watu wanyofu na kuwafundisha. Mamilioni ya watu ulimwenguni pote wamejifunza kutokana na Neno la Mungu kuishi kwa njia inayoonyesha upendo wa kujidhabihu. (Yohana 13:34; 1 Yohana 4:21) Gazeti hili, pamoja na gazeti la Mnara wa Mlinzi, huchapishwa ili kuwasaidia watu wajifunze mengi na kuishi kwa njia hiyo. Twakualika uendelee kujifunza. Ujuzi huo ni wenye kuthawabisha sana.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mwanadamu ataitunza dunia yenye kupendeza badala ya kuiharibu
-