Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wauzaji wa Kale wa Vitabu na Bidhaa
    Amkeni!—2001 | Desemba 8
    • ‘Wafanya-Magendo wa Imani’

      Mtambo wa kuchapa ulipovumbuliwa, watu walianza kusoma vitabu, vijarida, na vijitabu vya dini kwa hamu. Biblia ilichapwa kwanza katika Kilatini na baadaye katika lugha za kawaida. Mamilioni ya Biblia zilichapwa Ujerumani, na wauzaji wa vitabu walizisambaza haraka kwa watu walioishi mashambani. Hata hivyo, ugawaji huo haukupendwa na wote.

      Yapata mwaka wa 1525, Bunge la Ufaransa lilipiga marufuku utafsiri wa Biblia katika Kifaransa, na mwaka uliofuata, watu walikatazwa wasimiliki Biblia ya Kifaransa. Licha ya marufuku hayo, maelfu ya Biblia zilichapwa, na wauzaji jasiri wa vitabu walisambaza Biblia nyingi kotekote Ufaransa kisiri. Mmojawapo wa wauzaji hao alikuwa kijana aliyeitwa Pierre Chapot. Alikamatwa mwaka wa 1546 na kuuawa.

      Hatimaye, katika mwaka wa 1551, Serikali ya Kikatoliki ya Ufaransa ilipiga marufuku kazi ya wauzaji hao ya kuuza vitabu, kwa kuwa waliuza “kisiri” vitabu “vilivyotoka Geneva,” yaani, kutoka kwa Waprotestanti. Hata hivyo, mambo hayakubadilika. Biblia nyingi ziliingizwa Ufaransa kwa njia zozote zile. Biblia nyingi zilikuwa ndogo, nazo zilifichwa kisiri chini ya pipa za divai, katika pipa za kokwa aina ya chestnut, au mahali pa mizigo katika merikebu. Mwanamume hodari aliyeitwa Denis Le Vair alikamatwa alipokuwa akisafirisha pipa lililojaa Biblia. Yeye pia aliuawa. Mkatoliki mmoja aliyechukia wauzaji hao wa vitabu alisema kwamba “kwa muda mfupi, walisambaza Agano Jipya la Kifaransa kotekote nchini Ufaransa.”

      ‘Wafanya-magendo [hao] wa imani,’ kama mwandishi mmoja anavyowaita, walikuwa hatarini daima katika karne ya 16. Wauzaji wengi wa vitabu walikamatwa, walifungwa gerezani, walipelekwa kuvuta makasia katika merikebu, walifukuzwa nchini, au kuuawa. Baadhi yao walichomwa kwa moto pamoja na vitabu vyao. Ni wauzaji wachache tu wa vitabu wanaojulikana kwa majina. Hata hivyo, kwa sababu ya jitihada za wauzaji wengi sana jasiri, familia nyingi za Waprotestanti walipata Biblia.

  • Wauzaji wa Kale wa Vitabu na Bidhaa
    Amkeni!—2001 | Desemba 8
    • Viwanda vikubwa vilipoanzishwa katika karne ya 19 hali ilibadilika sana na kazi ya kutembeza vitabu iliyokuwa imeendelea kwa vizazi vingi ilikoma kabisa. Hata hivyo, tangu mashirika mbalimbali ya Biblia yaanzishwe, Biblia imesambazwa kwa kiasi kisicho na kifani. Lakini, Kanisa Katoliki bado lilipinga ugawanyaji wa Biblia. Watu waliosambaza Biblia waliendelea kunyanyaswa na kushtakiwa mahakamani mpaka mwishoni mwa miaka ya 1800. Hata hivyo, kuanzia mwaka wa 1804 hadi 1909, waligawanya nakala milioni sita za Biblia nzima au za sehemu ya Biblia nchini Ufaransa pekee.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki