Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?
    Amkeni!—1999 | Januari 8
    • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?

      Mwanzo wa wazo la uhuru wa kidini uliambatana na uchungu wa uzazi katika Jumuiya ya Wakristo. Ulikuwa ni pambano dhidi ya kulazimisha kauli, ubaguzi, na kutovumiliana. Ulisababisha kupotezwa kwa maisha ya maelfu yasiyohesabika katika mapambano ya kidini yenye umwagikaji mwingi wa damu. Historia hii yenye kuhuzunisha hutufundisha nini?

      “MNYANYASO umekuwa jambo linaloendelea la historia ya Kikristo,” aandika Robin Lane Fox katika kitabu Pagans and Christians. Wakristo wa mapema waliitwa farakano na walilaumiwa kuwa walitisha utengamano. (Matendo 16:20, 21; 24:5, 14; 28:22) Tokeo lilikuwa kwamba, wengine walivumilia mateso na kuuawa na hayawani-mwitu katika nyanja za michezo za Roma. Kwa kuona mnyanyaso huo mkali, wengine, kama vile mwanatheolojia Tertullian (ona picha katika ukurasa wa 8), waliomba kuwepo uhuru wa kidini. Mwaka wa 212 W.K., aliandika hivi: “Ni haki ya kibinadamu ya msingi, pendeleo la asili, kwamba kila mtu apaswa kuabudu kulingana na masadikisho yake.”

      Mnamo 313 W.K., mnyanyaso dhidi ya Wakristo uliofanywa na mamlaka ya Roma ulifikia kikomo chini ya utawala wa Konstantino, kwa kutolewa kwa Amri ya Milan, ambayo ilitoa uhuru wa kidini kwa Wakristo na wapagani vilevile. Kuhalalishwa kwa “Ukristo” katika Milki ya Roma kulikomesha wimbi la mnyanyaso dhidi ya Wakristo. Hata hivyo, karibu mwaka wa 340 W.K., mwandishi aliyedai kuwa Mkristo alitoa mwito wapagani wanyanyaswe. Hatimaye, mwaka wa 392 W.K., kupitia kwa Amri ya Constantinople, Maliki Theodosius wa Kwanza alipiga marufuku upagani katika milki hiyo, na uhuru wa kidini ukakoma kabla haujasitawi. “Ukristo” wa Kiroma ukiwa dini ya Serikali, Kanisa na Serikali zilianzisha kampeni ya mnyanyaso ambayo iliendelea kwa karne kadhaa, ikifikia upeo wake katika Krusedi zenye umwagikaji wa damu za karne ya 11 hadi ya 13 na katika ukatili wa Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi, yaliyoanza katika karne ya 12. Wale waliothubutu kutilia shaka imani iliyothibitishwa, kuwapo pekee kwa fundisho hilo, waliitwa wazushi na kusakwa katika mazingira ya uonevu ya wakati huo. Ni nini kilichochochea hatua hizi?

      Hali ya kutovumiliana kwa kidini ilikubaliwa kwa msingi wa kwamba muungano wa kidini ulitokeza msingi ulio thabiti zaidi kwa Serikali na kwamba mahitilafiano ya kidini yalitisha utengamano. Nchini Uingereza, katika mwaka wa 1602, mmojawapo wa mawaziri wa Malkia Elizabeth alitoa hoja: “Serikali haiwezi kuwa salama kamwe inaporuhusu dini mbili.” Kwa kweli, ilikuwa rahisi zaidi kupiga marufuku wapinzani wa kidini kuliko kutafuta kama kwa kweli wanasababisha tisho kwa Serikali au kwa dini iliyothibitishwa. Kichapo The Catholic Encyclopedia chasema: “Wala mamlaka za kilimwengu wala za kidini hazikupambanua tofauti ndogo sana kati ya wazushi walio hatari na wasiodhuru.” Hata hivyo, badiliko lingetokea karibuni.

      Mwanzo Wenye Maumivu wa Uvumiliano

      Badiliko katika Ulaya lilichochewa na mageuzi yaliyosababishwa na Uprotestanti, harakati ya kifarakano ambayo haikukoma. Kwa mwendo wenye kushangaza, Marekebisho ya Uprotestanti yaligawanya Ulaya kwa misingi ya kidini, hilo likatokeza wazo la uhuru wa dhamiri. Kwa kielelezo, Mleta Mabadiliko mashuhuri Martin Luther, alitetea maoni yake katika mwaka wa 1521, akasema: “Dhamiri yangu imetiishwa kwa Neno la Mungu.” Migawanyiko pia ilichochea Vita vya Miaka Thelathini (1618-1648), mfululizo wa vita vyenye ukatili vya kidini ambavyo viliharibu kabisa Ulaya.

      Ingawa hivyo, katikati ya vita, wengi walikuja kutambua kwamba mapambano hayakuwa namna ya maendeleo. Hivyo, mfululizo wa amri kama vile Amri ya Nantes katika Ufaransa (1598), ilijaribu bila ya mafanikio kurejesha amani katika Ulaya iliyokumbwa na vita. Ni kupitia kwa amri hizi kwamba wazo la kisiku hizi la uvumiliano likatokea hatua kwa hatua. Hapo kwanza, “uvumiliano” ulidokeza mawazo yasiyofaa. “Ikiwa chini ya hali fulani tungevumilia mafarakano . . . , bila shaka lingekuwa jambo ovu—kwa kweli, uovu mbaya sana—lakini si mbaya kama vita,” akaandika mwanafunzi mashuhuri wa elimu ya binadamu Erasmus katika mwaka wa 1530. Kwa sababu ya maoni haya yasiyofaa, watu fulani kama vile Mfaransa Paul de Foix katika mwaka wa 1561, walipendelea kuongea juu ya “uhuru wa kidini” badala ya “uvumiliano.”

      Ingawa hivyo, baada ya muda, uvumiliano haukuonwa tena kuwa uovu hata kidogo, wala uovu wa kiwango cha chini, bali kuwa mlinzi wa uhuru. Haukuonwa tena kuwa kuruhusu udhaifu bali kuwa uhakikisho kamili. Itikadi mbalimbali na haki za kufikiri tofauti zilipoanza kukubaliwa kuwa msingi wa jamii ya kisasa, ushabiki ulianza kupungua.

      Kufikia mwisho wa karne ya 18, uvumiliano ukahusianishwa na uhuru na usawa. Hilo lilionyeshwa kupitia sheria na maazimio kadhaa, kama vile Azimio mashuhuri la Haki za Kibinadamu na Raia (1789), katika Ufaransa, au Mswada wa Haki (1791), katika Marekani. Kwa kuwa hati hizi ziliathiri kufikiri kwa uhuru kuanzia karne ya 19 na kuendelea, uvumiliano na hivyo uhuru haukuonwa tena kuwa laana bali baraka.

  • Uhuru wa Kidini—Je, Ni Baraka au Laana?
    Amkeni!—1999 | Januari 8
    • Watetezi wa Uhuru wa Kidini

      Maombi yaliyo dhahiri ya kutaka uhuru wa kidini yalitokana na mauaji ya kikatili ya mapambano ya kidini katika Ulaya mnamo karne ya 16. Maombi haya yangali yanahusu mazungumzo ya uhuru wa kidini.

      Sébastien Chateillon (1515-1563): “Mzushi ni nani? Sina jingine isipokuwa kwamba tunawaona wazushi kuwa watu wote ambao hawakubaliani na maoni yetu. . . . Ikiwa katika jiji hili unaonwa kuwa mwamini wa kweli, katika jiji jingine utaonwa kuwa mzushi.” Mtafsiri wa Biblia Mfaransa aliye mashuhuri na mtetezi shupavu wa uvumiliano, Chateillon alitaja jambo moja kuu katika mjadala wa uhuru wa kidini: Ni nani anayefasiri mzushi ni mtu gani?

      Dirck Volckertszoon Coornhert (1522-1590): “Twasoma kwamba katika nyakati za kale . . . hata Kristo mwenyewe katika Yerusalemu na kisha wafia-imani wengi katika Ulaya . . . walivuruga [jamii] kwa maneno yao ya kweli. . . . Maana ya neno ‘vuruga’ yahitaji kufafanuliwa kwa usahihi na waziwazi.” Coornhert alitoa hoja kwamba tofauti ya kidini haipasi kulinganishwa na kuvuruga utengamano. Aliuliza: Je, watu ambao ni waadilifu sana katika kutii na kustahi sheria kwa kweli ni tisho kwa utengamano?

      Pierre de Belloy (1540-1611): Ni “kukosa ujuzi kuamini kwamba dini zikiwa nyingi huleta na kuendeleza msukosuko Nchini.” Mwanasheria Mfaransa Belloy, akiandika wakati wa Vita vya Dini (1562-1598), alitoa hoja kwamba upatano wa Nchi hautegemei usare wa kidini isipokuwa, bila shaka, serikali iwe inajinyenyekeza chini ya misongo ya kidini.

      Thomas Helwys (karibu 1550–karibu 1616): “Ikiwa watu wake [wa Mfalme] ni raia watiifu na waaminifu kwa sheria zote za binadamu, hawezi kuwadai mengi zaidi.” Helwys, mmojawapo wa waanzilishi wa Baptisti ya Uingereza, aliandika kwa kuunga mkono mtengano wa Kanisa na Serikali, akimhimiza mfalme atoe uhuru wa kidini kwa makanisa na mafarakano yote na aridhike na mamlaka ya kiraia na mali. Maandishi yake yalikazia swali la hivi karibuni: Serikali yapasa kudhibiti hali ya kiroho ya watu kadiri gani?

      Mwandishi Asiyejulikana (1564): “Ili kuanzisha uhuru wa dhamiri, haitoshi kumruhusu mtu aepuke kufuatia dini ambayo haipendelei ikiwa, kwa sababu hiyohiyo, hakuna uhuru wa kufuatia dini anayoipenda.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki