Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mazoea ya Kutupatupa Vitu
    Amkeni!—2002 | Agosti 22
    • Mazoea ya Kutupatupa Vitu

      WATU wanaoishi katika nchi zilizoendelea hutupa takataka nyingi sana. Kwa mfano, wazia kiasi cha takataka ambacho hutupwa huko Marekani kila mwaka. Inasemekana kwamba uzito wa takataka hizo ni ‘sawa na uzito wa maji yanayoweza kujaza madimbwi 68,000 ya kuogelea yenye urefu wa meta 50.’ Yapata miaka kumi iliyopita ilikadiriwa kwamba kila mwaka, wakazi wa New York City walitupa takataka nyingi hivi kwamba zingeweza kufunika bustani ya jiji hilo inayoitwa Central Park kwa tabaka ya meta nne za takataka!a

      Si ajabu kwamba nchi ya Marekani imetajwa kuwa “onyo kwa nchi nyingine duniani” kwa habari ya “kununua na kutupa vitu ovyoovyo.” Lakini hali hiyo inakumba nchi nyingine pia. Imekadiriwa kwamba takataka ambazo hutupwa kila mwaka huko Ujerumani zingeweza kujaza gari-moshi la kubeba mizigo lenye urefu wa kilometa 1,800. Huo ni umbali wa kutoka Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, hadi pwani ya Afrika. Na hapo nyuma ilikadiriwa kwamba kila mwaka familia ya kawaida yenye watu wanne nchini Uingereza hutupa kiasi cha karatasi ambacho kimetengenezwa kutokana na miti sita.

      Hata nchi zinazoendelea zina tatizo la takataka. Gazeti moja maarufu linasema hivi: “Jambo baya hata zaidi ni kwamba hivi karibuni wengi wa wale watu bilioni 6 duniani wameanza kutupa vitu ovyoovyo wakifuata mfano wa Marekani na nchi nyingine zilizoendelea.” Naam, upende usipende, popote tulipo watu hupenda kutupatupa vitu siku hizi.

      Bila shaka watu wamekuwa na vitu vya kutupa tangu zamani. Lakini vyakula vya mikebe na vyakula vilivyofungwa kwa karatasi za aina mbalimbali vyapatikana kwa wingi siku hizi kuliko miaka michache iliyopita. Kwa hiyo, mikebe na karatasi za vyakula hivyo ziko kila mahali. Vilevile, kiasi cha magazeti, karatasi za matangazo ya biashara, na vichapo vingine kimeongezeka kwa haraka.

      Viwanda vingi na vitu vingi vilivyobuniwa na wanasayansi vimesababisha pia aina nyingine za takataka. Gazeti Die Welt la Ujerumani linasema kwamba “magari milioni tisa hivi hutupwa kila mwaka katika nchi za Muungano wa Ulaya.” Kuondosha magari hayo si jambo rahisi. Lakini kuondosha takataka za mitambo ya nyuklia na viwanda vya kemikali ni tatizo kubwa hata zaidi. Yasemekana kwamba katika mwaka wa 1991 huko Marekani kulikuwa na “takataka nyingi sana zenye mnururisho na hapakuwa na mahali pa kuziweka” Iliripotiwa kwamba mapipa milioni moja yenye kemikali zenye sumu ya kufisha yalikuwa yamewekwa katika ghala za muda. Na sikuzote ilihofiwa kwamba mapipa hayo “yangepotea, yangeibwa, au kusababisha uharibifu wa mazingira kwa sababu ya kutoshughulikiwa ifaavyo.” Viwanda 20,000 hivi huko Marekani vilikuwa na zaidi ya tani milioni 40 za takataka zenye sumu katika mwaka wa 1999.

      Jambo jingine linalochangia tatizo hilo ni ongezeko kubwa la idadi ya watu katika karne iliyopita. Watu wanapoongezeka, takataka huongezeka pia. Na watu wengi wana mwelekeo wa kununua vitu ili kuzidisha mali. Hivi majuzi, Taasisi ya Worldwatch ilikata kauli hii: “Tumetumia bidhaa nyingi zaidi na kuhudumiwa kwa njia nyingi zaidi tangu mwaka wa 1950 kuliko wakati mwingine wowote.”

      Bila shaka watu wengi wanaoishi katika nchi zilizoendelea hawataki kukosa ‘bidhaa na huduma’ hizo zote. Kwa mfano, fikiria jinsi ilivyo rahisi kwenda dukani na kununua vyakula ambavyo vimekwisha fungwa kwa njia mbalimbali na kuvipeleka nyumbani katika mifuko ya karatasi au plastiki inayopatikana dukani. Kama watu wangenyimwa huduma hiyo ghafula, labda wangegundua haraka kwamba wameizoea sana. Mbinu mbalimbali za kufunga vyakula huchangia afya nzuri, angalau kwa kadiri ambavyo zinazuia vyakula visichafuliwe.

      Hata hivyo, licha ya faida hizo, je, vitu hutupwa kwa wingi hivi kwamba tunapaswa kuwa na wasiwasi? Bila shaka, kwa kuwa masuluhisho mbalimbali ambayo yamependekezwa ili kupunguza takataka hayajawa na matokeo mazuri. Jambo baya hata zaidi ni kwamba mielekeo ya kutupatupa vitu inaweza kuwa na matokeo mabaya zaidi.

      [Maelezo ya Chini]

      a Bustani hiyo ni yenye eneo la ekari 843.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Kuondosha takataka hatari za viwanda bila kusababisha madhara ni tatizo kubwa sana

  • Je, Kuna Suluhisho?
    Amkeni!—2002 | Agosti 22
    • Je, Kuna Suluhisho?

      UFANYE nini na kitu ambacho huhitaji? Inaonekana kwamba suluhisho rahisi ni kukitupilia mbali. Hata hivyo, kuondosha takataka si jambo rahisi. Zipelekwe wapi? Shirika moja la mazingira huko Italia linakadiria kwamba inachukua miaka 1,000 kwa chupa iliyotupwa baharini kuoza. Kwa upande mwingine, karatasi huoza baada ya miezi mitatu tu. Kichungi cha sigara hubaki baharini kwa miaka 5; mifuko ya plastiki, miaka 10 hadi 20; vitu vilivyotengenezwa kwa nailoni, miaka 30 hadi 40; mikebe, miaka 500; na aina fulani ya plastiki inayoitwa polystyrene, miaka 1,000.

      Takataka za aina hizo zimeongezeka sana. Siku hizi kuna vitu vingi vya kununua, na watangazaji wa bidhaa hizo wanataka tuamini kwamba tunazihitaji zote. Gazeti la Uingereza la The Guardian linasema hivi kifupi: “Watangazaji wa bidhaa hutusaidia kutosheleza mahitaji ambayo hatukujua tulikuwa nayo.” Ndiyo, sisi hushawishiwa kununua vitu vyote vipya vinavyopatikana kwa sababu tunaogopa tutakosa nafasi ya kuvifurahia. Bila shaka, katika matangazo ya biashara “kitu kipya” kinamaanisha “kitu kizuri na kilicho bora,” na “kitu cha zamani” kinamaanisha “kitu duni au kisichofaa tena.”

      Kwa hiyo, tunashawishiwa mara nyingi kununua kitu kipya badala ya kurekebisha kile cha zamani kilichoharibika. Inasemekana kwamba kununua kitu kipya ni rahisi na si bei ghali kama kurekebisha kile kilichoharibika. Jambo hilo ni kweli nyakati nyingine. Hata hivyo, kwa kawaida, kutupa kitu cha zamani na kununua kitu kipya hugharimu pesa nyingi na si jambo la lazima sikuzote.

      Vitu vingi vinavyotengenezwa siku hizi hukusudiwa kutumiwa kwa muda mfupi kisha kutupwa. Huenda visiweze kurekebishwa kwa urahisi, jambo ambalo linapaswa kufikiriwa wakati wa kununua vitu vipya. Gazeti moja la Ujerumani lenye ushauri kwa wanunuzi lilisema hivi: ‘Vitu havidumu kwa muda mrefu kama zamani. Vitu vilivyopendwa muda mfupi uliopita havipendwi leo, navyo hutupwa mara nyingi. Kwa hiyo, vitu vinavyoweza kutumiwa tena hutupwa kila siku kana kwamba ni takataka tu!’

      Je, kununua vitu vingi visivyo vya lazima ni kwa faida ya wanunuzi? Bila shaka wale wanaofaidika hasa ni wanabiashara wanaotaka faida nyingi. Gazeti la Uswisi la Die Weltwoche linatoa hoja hii: “Kwa hakika uchumi ungeharibika iwapo kila mtu angetumia gari lake na fanicha kwa muda wote wa maisha au hata kuvitumia kwa muda mrefu zaidi.” Ni wazi kwamba kuharibu uchumi si suluhisho hata kidogo kwa kuwa jambo hilo lingemaanisha kwamba hata wanunuzi wangepoteza kazi. Basi, tatizo hilo linaweza kusuluhishwa jinsi gani?

      Kutupa, Kutumia Tena, au Kupunguza?

      Ili kutatua tatizo hilo katika nchi zao, baadhi ya nchi zilizoendelea hupeleka takataka zake hadi nchi zinazoendelea. Kwa mfano, ripoti moja inaonyesha kwamba “kwenye jaa moja la takataka linalojulikana sana huko Nigeria, kuna mapipa zaidi ya 8,000 yenye tani 3,500 za kemikali hatari. Mapipa hayo ambayo yameshika kutu yanavuja kemikali hizo ambazo zinaharibu udongo na maji.” Yaelekea hiyo si njia nzuri ya kuondoa takataka wala haionyeshi heshima kwa wengine.

      Namna gani kutengeneza vitu vipya kutokana na vitu visivyohitajika tena, badala ya kuvitupa tu? Ili jambo hili liwezekane ni lazima takataka zitenganishwe. Tayari katika sehemu fulani jambo hilo ni takwa la kisheria. Wenye mamlaka wanaweza kuagiza kwamba karatasi, chuma, kioo, na vyakula vitupwe katika mapipa tofauti-tofauti. Kisha, huenda ikawa lazima kutenganisha vioo kulingana na rangi.

      Ni wazi kwamba kuna faida kutumia vitu visivyohitajiwa ili kutengeneza vitu vipya badala ya kuvitupa. Kitabu 5000 Days to Save the Planet kinasema kwamba kutumia upya alumini “huokoa nishati nyingi sana,” na kunaweza “kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchimbaji wa madini aina ya bauxite.” Kitabu hicho kinaongeza: “Ili kutengeneza karatasi kwa kutumia karatasi zilizotupwa, nusu tu ya nishati na asilimia kumi tu ya maji huhitajika. . . . Takataka za viwanda zinaweza kutumiwa kutengeneza vitu vingine au kutumiwa tena. . . . Hata wakati viwanda fulani visipoweza kutumia takataka zake vyenyewe, huenda viwanda vingine vinaweza kuzitumia . . . Huko Uholanzi, viwanda vimebadilishana takataka kwa mafanikio tangu mwanzoni mwa miaka ya 1970.”

      Baadhi ya watu wenye mamlaka hukazia mbinu za kupunguza takataka badala ya kutafuta njia za kuziondosha. Kitabu kilichotajwa mapema kinaonya kwamba “ni lazima hatua ichukuliwe haraka” ikiwa wanadamu “wataacha uchumi unaoendelezwa na kununua na kutupa vitu ovyoovyo . . . na kujenga jamii inayotumia vitu kwa uangalifu ili kupunguza takataka na matumizi ya mali.”

      Hata hivyo, itawabidi wale wanaotaka “kuacha uchumi unaoendelezwa na kununua na kutupa vitu ovyoovyo” wawe tayari kutumia vitu vyao kwa muda mrefu iwezekanavyo, na kuvitupa tu visipoweza kurekebishwa tena. Ni lazima wawe tayari kuwapa watu wengine vitu visivyoharibika ambavyo hawavihitaji tena. Idara ya Darmstadt ya taasisi fulani ya mazingira huko Ujerumani, inayoitwa Öko-Institut, inakadiria kwamba takataka zingepungua kwa asilimia 75 iwapo watu wangefuata kwa uthabiti kanuni “Tumia badala ya kununua na kutupa.”

      Lakini je, watu wengi watafuata kanuni hizo? La, haielekei hivyo. Tatizo la takataka linalowakumba wanadamu ni dalili tu ya matatizo makubwa zaidi. Siku hizi, mbali na kuwa na tabia ya kununua na kutupa vitu ovyoovyo, watu wengi wamesitawisha mwelekeo wa kutupatupa vitu. Acha tuchunguze mwelekeo huo, na baadhi ya matokeo yake mabaya.

      Hatari Zinazosababishwa na Mwelekeo wa Kutupatupa Vitu

      Mbali na kutupa tu vitu ovyoovyo, mwelekeo huo unaweza kuwafanya watu wakose uthamini na upendo, na kuwafanya watupe chakula kingi bila kujali na kuharibu mali nyinginezo. Watu wenye ubinafsi na wanaofuata mitindo mbalimbali na mapendezi yao yasiyo muhimu, huvutiwa mara nyingi kununua nguo mpya, vyombo vya nyumbani, na vitu vingine vipya, na kutupa vile walivyo navyo.

      Hata hivyo, yaelekea mwelekeo huo wa kutupatupa vitu hauhusishi vitu tu. Hivi majuzi, ripoti iliyohusu mradi mmoja nchini Ujerumani wa kutumia tena vitu vya nyumbani vilivyotupwa, ilisema hivi: ‘Sisi huwatendea wanadamu wenzetu jinsi tunavyozitendea fanicha. Tunazitupa baada ya miaka mitano na kununua mpya kwa sababu hatuzipendi tena. Jamii yetu inaweza kustahimili mwelekeo huo kwa muda gani?’ Ripoti hiyo inaeleza hivi: “Mara tu mtu anaposhindwa kufanya kazi kwa kadiri inavyotakiwa, yeye hufutwa kazi. Kwa vyovyote, kuna watu wengi wa kuajiri.”

      Al Gore, aliyekuwa Makamu wa Rais huko Marekani aliuliza swali hili muhimu katika kitabu chake Earth in the Balance: “Ikiwa tunavitupa ovyoovyo vitu tunavyovitumia, je, tumebadili maoni yetu juu ya wanadamu wenzetu kwa njia iyo hiyo? . . . Je, tumesahau kwamba kila mtu ni wa pekee na muhimu?”

      Kwa watu ambao hawathamini wala hawaheshimu wengine inaweza kuwa jambo rahisi—wala hawalioni kuwa kosa—kuwatupilia mbali marafiki na wenzi wa ndoa. Gazeti Süddeutsche Zeitung la Ujerumani linasema hivi likizungumzia maoni hayo: “Mara mbili kwa mwaka sisi hununua nguo mpya, kila miaka minne sisi hununua gari jipya, na kila miaka kumi sisi hununua fanicha mpya; kila mwaka sisi hutembelea eneo jipya wakati wa likizo; sisi huhama nyumba, na kubadili kazi na biashara kwa ukawaida. Hivyo basi, kwa nini tusibadili mwenzi wa ndoa?”

      Ni kana kwamba baadhi ya watu leo huwa tayari kutupilia mbali chochote kile kinachokuwa mzigo kwao. Kwa mfano, katika nchi moja ya Ulaya, inakadiriwa kwamba paka 100,000 na mbwa 96,000 hivi walitupwa katika mwaka wa 1999. Mtu mmoja anayeshughulikia hali ya wanyama alisema kwamba wananchi wenzake “hawaelewi kwamba mnyama anahitaji kutunzwa kwa muda mrefu. Wao hununua mbwa mwezi wa Septemba na kumwacha [baada ya mwaka mmoja wanapokwenda likizoni] mwezi wa Agosti.” Jambo baya hata zaidi ni kwamba mwelekeo wa kutupatupa unaathiri maoni ya watu kuhusu uhai wa binadamu.

      Kutoheshimu Uhai

      Yaelekea kwamba watu wengi leo hawathamini maisha yao. Kwa nini twasema hivyo? Kwa mfano, hivi majuzi gazeti moja la Ulaya lilisema kwamba idadi ya vijana walio tayari kuhatarisha maisha yao imeongezeka katika miaka ya karibuni. Jambo hilo linaonekana wazi katika utayari wao wa kushiriki katika michezo hatari. Wao wako tayari kuhatarisha maisha ili wajifurahishe kwa muda mfupi tu! Wanabiashara wenye pupa hujipatia faida nyingi kwa sababu ya mwelekeo huo. Mwanasiasa mmoja Mjerumani alisema kwamba wale wanaoendeleza michezo hatari “huona mara nyingi pesa kuwa muhimu kuliko afya na uhai wa binadamu.”

      Vipi kutupilia mbali uhai wa binadamu asiyezaliwa? Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba “ulimwenguni pote mimba milioni 75 hutungwa ambazo hakuna mtu anayezitaka. Wanawake wengi hawana namna nyingine ila kutoa mimba.” Watoto wachanga wamo hatarini hata baada ya kuzaliwa. Kulingana na gazeti la O Estado de S. Paulo la Brazili, “idadi ya watoto wachanga wanaotupwa inaongezeka.” Je, jambo hilo hutukia katika eneo lenu pia?

      Kotekote duniani kuna uthibitisho kwamba uhai wa binadamu huonwa mara nyingi kuwa duni, usio na thamani, kana kwamba ni kitu kinachoweza kutupwa tu. Jambo hilo linaonekana wazi tukifikiria jinsi watu wengi wanavyofurahia kuwaona “watu wanaodhaniwa kuwa mashujaa” wakiwachinja “watu wabaya” wengi katika kipindi kimoja tu cha televisheni au katika sinema mbalimbali. Tunaona jambo hilo pia katika uhalifu wenye ujeuri unaoenea duniani. Wezi huwaua watu kwa sababu ya pesa kidogo sana au hata bila sababu yoyote. Tunaliona vilevile katika habari zenye kusikitisha kuhusu mashambulizi ya magaidi, mauaji ya watu wa makabila mbalimbali, na ya jamii nzimanzima, ambayo yahusisha mauaji ya bila huruma ya wanadamu wengi. Uhai wenye thamani hutupiliwa mbali kana kwamba ni takataka tu.

      Hatuwezi kuepuka kuishi miongoni mwa watu wanaopenda kununua na kutupa vitu ovyoovyo, lakini tunaweza kuepuka kuwa na mwelekeo kama wao. Makala inayofuata inazungumzia jinsi tunavyoweza kukabiliana na tabia ya kununua na kutupa vitu ovyoovyo katika jamii yetu na vilevile mitazamo mibaya inayoambatana na tabia hiyo.

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Katika sehemu nyingi kutengeneza vitu vipya kutokana na vitu vilivyotupwa ni takwa la kisheria

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Je, wewe hushurutishwa kutupa nguo nzuri na kununua mpya kupatana na mtindo?

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Watoto ambao hawajazaliwa wanapaswa kupendwa, bali si kutupwa

      [Hisani]

      Index Stock Photography Inc./BSIP Agency

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Uhai ni wenye thamani sana na haupaswi kuhatarishwa ili kujifurahisha

  • Kuepuka Mwelekeo wa Kutupatupa Vitu
    Amkeni!—2002 | Agosti 22
    • Kuepuka Mwelekeo wa Kutupatupa Vitu

      “HAKUNA kitu kinachopotea bure . . . katika mazingira.” Kulingana na gazeti la Time, hayo ni maoni ya mtaalamu mmoja anayeheshimika wa mbinu za kutumia vitu tena. Alitaja jinsi ambavyo vitu vinavyonyauka na kuoza katika mazingira hunufaisha vitu vingine. Kulingana na gazeti hilo mtaalamu huyo anahisi kwamba “wanadamu wanaweza kuiga mazingira, lakini jambo hilo lingemaanisha kubuni tekinolojia mpya na kubadili mielekeo ya watu kabisa.”

      Si watu wengi wanaoweza kubuni tekinolojia mpya. Lakini tunaweza kudhibiti mwelekeo wetu! Na tukiwa na maoni yanayofaa kuhusu maadili na tabia nzuri tutaweza kukabiliana vizuri zaidi na matatizo yanayosababishwa na kununua na kutupa vitu ovyoovyo.

      Epuka Kutupatupa Vitu

      Mtu mmoja kati ya watano duniani hulala njaa. Kujua jambo hilo kunapaswa kutufanya tuthamini chakula na tuepuke kukitupa. Wenzi wa ndoa waliorudi Ulaya baada ya kufanya kazi ya mishonari barani Afrika kwa miaka 28 walisema kwamba ilikuwa vigumu kuzoea tena maisha katika nchi ya kwao hasa kwa sababu ya kuona jinsi ambavyo “watu hutupa chakula ovyoovyo.”

      Wazazi wenye hekima huwafundisha watoto wao kujipakulia kiasi cha chakula ambacho wanaweza kumaliza. Kufanya hivyo hupunguza takataka na uharibifu wa mali. Ni afadhali kujipakulia chakula kidogo kwanza, kabla ya kuomba kuongezewa. Bila shaka wazazi wanahitaji kuwa mfano mzuri. Yesu alikuwa mfano mzuri kwetu sote kwa kuthamini kwa moyo maandalizi ya kimwili na ya kiroho ya Mungu. Biblia inaonyesha kwamba Yesu hakutupa chakula—hata ingawa kilikuwa kimeandaliwa kwa wingi kwa njia ya mwujiza!—Yohana 6:11-13.

      Vilevile, haifai kutupa vitu ambavyo havijaharibika kama vile nguo, fanicha, na mashine. Sisi huonyesha kwamba tunathamini vitu tulivyo navyo kwa kuvitunza na kuvitumia kwa muda mrefu iwezekanavyo. Tusidanganywe na watangazaji wa biashara ambao hujitahidi kutufanya tusiridhike na vitu tulivyo navyo kwa kutangaza vitu vikubwa, bora, vinavyofanya kazi kwa kasi zaidi, na vyenye nguvu zaidi. Ni wazi kwamba tuna uhuru wa kununua vitu vipya hata ingawa vitu tulivyo navyo havijaharibika. Lakini kabla ya kufanya hivyo, huenda ikafaa tuchunguze mwelekeo wetu na kile kinachotusukuma kufanya hivyo.

      Epuka Pupa

      Waisraeli waliposafiri jangwani wakiwa njiani kuelekea Nchi ya Ahadi, walipewa chakula kilichoitwa mana. Kulingana na Biblia, kulikuwa na mana ya kutosha. Hata hivyo, Waisraeli walionywa wasiwe wenye pupa; walikuwa wachukue kiasi cha kutosha tu kwa kila siku. Wale ambao hawakutii waligundua kwamba pupa haikuwafaidi, kwa kuwa mabuu waliingia katika mana iliyobaki na ikawa na harufu mbaya. (Kutoka 16:16-20) Biblia inashutumu pupa waziwazi mara nyingi.—Waefeso 5:3.

      Si Biblia pekee inayoshutumu pupa. Kwa mfano, mwanafalsafa Mroma, Seneca, aliyekuwa pia mwandishi wa michezo ya kuigiza katika karne ya kwanza, alitambua kwamba mtu mwenye pupa haridhiki kamwe. Alisema hivi: “Vitu vyote duniani haviwezi kutosheleza pupa.” Erich Fromm, mwanafalsafa aliyeishi katika karne ya 20, alikata kauli hiyohiyo: “Jitihada ya kutosheleza tamaa za pupa ni kama kujaribu kujaza shimo lisilo na mwisho. Jitihada hiyo isiyo na mwisho ya kutosheleza tamaa humchosha mtu bila kumtosheleza kamwe.” Mbali na kuepuka pupa na kuharibu mali bure, kuna mambo mengine ambayo watu wengi wameamua kufanya.

      Jifunze Kutoa

      Badala ya kutupa tu vitu ambavyo havijaharibika, mpe mtu ambaye angeweza kufurahia kuvitumia. Kwa mfano, nguo za watoto zisipowatosha tena, je, watoto wengine wangeweza kuzitumia? Je, ungeweza kumpa mtu mwingine vitu vingine pia ambavyo havijaharibika lakini huvitumii tena? Mpe mtu mwingine kitu ambacho wewe umefurahia ili yeye pia akifurahie. Mwandishi na mchekeshaji Mmarekani, Mark Twain, aliandika hivi: “Ili furaha yako iwe kamili ni lazima mtu mwingine aishiriki.” Huenda ikawa umeona kwamba furaha yako huongezeka unapomruhusu mtu mwingine kufurahi pamoja nawe. Zaidi ya hayo, kwa kutoa kwa njia hiyo, wewe hupunguza matokeo mabaya yanayosababishwa na mwelekeo wa kutupatupa vitu.

      Kutoa husifiwa sana katika Biblia. (Luka 3:11; Waroma 12:13; 2 Wakorintho 8:14, 15; 1 Timotheo 6:18) Naam, hali ingekuwa bora sana duniani iwapo watu wote wangekuwa tayari kutoa!

      Ridhika na Vitu vya Lazima

      Mtu anayeridhika ni mtu mwenye furaha. Maneno hayo ni ya kweli kila mahali na kila wakati. Methali moja ya Kigiriki inasema hivi: “Mtu ambaye haridhiki na kidogo haridhiki kamwe.” Na Wajapani husema hivi: “Mtu ambaye haridhiki ndiye maskini.” Biblia pia inasifu sana uradhi. Biblia inasema hivi: “Kwa hakika, huo ni njia ya kupata faida kubwa, ujitoaji-kimungu huu pamoja na ujitoshelevu. Kwa maana hatukuleta kitu katika ulimwengu, wala hatuwezi kupeleka kitu chochote nje. Kwa hiyo, tukiwa na riziki na cha kujifunika, tutakuwa wenye kuridhika na vitu hivi.”—1 Timotheo 6:6-8; Wafilipi 4:11.

      Huenda tukahitaji ‘kubadili mwelekeo kabisa’ ili turidhike na vitu tulivyo navyo. Hivi majuzi, mwanamke kijana anayeitwa Susanne alitambua kwamba alihitaji kufanya badiliko hilo. Alisema hivi: “Niliazimia kwamba kwa kuwa sikuweza kupata kila kitu nilichopenda, ilinibidi kuanza kupenda vitu nilivyokuwa navyo. Sasa mimi ni mwenye furaha na nimeridhika.”

      Kuridhika huleta furaha kwelikweli. Mtaalamu wa uzee huko Bulgaria, profesa Argir Hadjihristev, anasema hivi: ‘Ubaya wenyewe hasa ni kutoridhika na vile vitu vichache alivyo navyo mtu.’ Anapoongea juu ya jinsi kuridhika kunavyochangia afya nzuri, anaongeza hivi: “Mtu asiyeng’ang’ania kuwa na mali nyingi kuliko majirani wake wala kuongeza mali sikuzote, hashindani na wengine na kwa hiyo yeye huepuka mfadhaiko. Na jambo hilo hupunguza wasiwasi.”

      Naam, kununua na kutupa vitu ovyoovyo hakuwezi kuleta furaha ya kweli, wala kuwa na mwelekeo wa kufanya hivyo. Inaonekana kwamba watu wengi zaidi wanaelewa jambo hilo. Vipi wewe?

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Watoto wanahitaji kujifunza jinsi ya kuepuka kuharibu chakula

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Yesu alionyesha mfano bora kwa kutotupa chakula

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Mbona usiwapatie wengine vitu ambavyo huvitumii badala ya kuvitupa?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki