Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Walishinda Licha ya Mateso
    Mnara wa Mlinzi—2003 | Machi 1
    • Walishinda Licha ya Mateso

      FRIEDA JESS alizaliwa mwaka wa 1911 nchini Denmark, na baadaye yeye na wazazi wake wakahamia Husum kaskazini mwa Ujerumani. Miaka mingi baadaye alipata kazi Magdeburg, na mwaka wa 1930 akabatizwa akawa Mwanafunzi wa Biblia, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo. Baada ya Hitler kuanza kutawala mwaka wa 1933, Frieda aliteseka kwa muda wa miaka 23 chini ya tawala mbili za kimabavu.

      Mnamo Machi 1933, serikali ya Ujerumani ilipanga kuwe na uchaguzi. Mwanahistoria Dakt. Detlef Garbe, msimamizi wa Jumba la Makumbusho la Kambi ya Mateso ya Neuengamme, karibu na Hamburg, anasema hivi: “Wanazi walitaka kuwalazimisha watu wote wampigie Adolf Hitler kura, aliyekuwa mtawala na kiongozi wao.” Mashahidi wa Yehova walitii himizo la Yesu la kutounga mkono upande wowote wa mambo ya siasa na kutokuwa “sehemu ya ulimwengu,” kwa hiyo, hawakupiga kura. Matokeo yalikuwa nini? Mashahidi walipigwa marufuku.—Yohana 17:16.

      Frieda aliendelea na shughuli zake za Kikristo kisirisiri, hata alisaidia kuchapa magazeti ya Mnara wa Mlinzi. Alisema hivi: “Baadhi ya magazeti yaliingizwa kwenye kambi za mateso kisiri kwa ajili ya waamini wenzetu.” Alikamatwa mwaka wa 1940 na kuhojiwa na Gestapo, kisha akafungwa kifungo cha upweke kwa miezi kadhaa. Alivumiliaje? Anasema: “Sala ilinisaidia sana. Nilianza kusali asubuhi na mapema na nilisali mara nyingi kwa siku. Niliimarishwa niliposali na nikasaidiwa nisiwe na wasiwasi kupita kiasi.”—Wafilipi 4:6, 7.

      Frieda aliachiliwa, lakini akakamatwa tena na Gestapo mwaka wa 1944. Wakati huu alihukumiwa kifungo cha miaka saba katika gereza la Waldheim. Frieda anaongeza: “Walinzi wa gereza walinipa kazi ya kusafisha bafu na vyoo nikiwa pamoja na wanawake wengine. Mara nyingi nilifanya kazi pamoja na mfungwa mwenzangu kutoka Chekoslovakia. Kwa hiyo, niliongea naye sana kumhusu Yehova na kuhusu imani yangu. Mazungumzo hayo yaliniimarisha.”

      Kuachiliwa, Lakini kwa Muda Tu

      Wanajeshi wa Sovieti waliwaachilia wafungwa katika gereza la Waldheim mnamo Mei 1945. Frieda akawa huru kurudi Magdeburg kuendelea na utumishi wake, lakini kwa muda mfupi tu. Mashahidi walionewa tena, lakini wakati huu walionewa na watu wenye mamlaka ya eneo lililotekwa na Sovieti. Gerald Hacke wa Taasisi ya Hannah-Arendt ya Utafiti Kuhusu Utawala wa Kimabavu anaandika hivi: “Mashahidi wa Yehova ni mojawapo ya mashirika machache yaliyoendelea kuteswa na tawala zote mbili za kimabavu nchini Ujerumani.”

      Kwa nini walionewa tena? Kwa mara nyingine, walionewa kwa sababu ya msimamo wao wa Kikristo wa kutounga mkono upande wowote wa mambo ya siasa. Serikali ya Ujerumani Mashariki iliagiza watu wapige kura mwaka wa 1948. Hacke anaeleza hivi: “Sababu kuu iliyofanya [Mashahidi wa Yehova wateswe] ilikuwa kwamba hawakupiga kura.” Mashahidi wa Yehova walipigwa marufuku huko Ujerumani Mashariki mnamo Agosti 1950. Wengi walikamatwa, kutia ndani Frieda.

      Frieda alijikuta tena mahakamani na akahukumiwa kifungo cha miaka sita. “Wakati huu nilikuwa pamoja na waamini wenzangu, na kushirikiana nao kulinisaidia sana.” Baada ya kuachiliwa huru mwaka wa 1956, alihamia Ujerumani Magharibi. Sasa, Frieda aliye na miaka 90 anaishi Husum, na bado anamtumikia Yehova, Mungu wa kweli.

      Frieda aliteswa kwa miaka 23 chini ya tawala mbili za kimabavu. “Wanazi walijaribu kuniangamiza; Wakomunisti nao wakajaribu kuniponda roho. Nilipataje nguvu ya kuvumilia? Nilijifunza Biblia kwa bidii nilipokuwa huru, nilisali nilipokuwa peke yangu, nilishirikiana na waamini wenzangu ilipowezekana, na niliongea na wengine kuhusu imani yangu nafasi ilipopatikana.”

  • Walishinda Licha ya Mateso
    Mnara wa Mlinzi—2003 | Machi 1
    • [Picha katika ukurasa wa 5]

      Frieda Jess (sasa Thiele) alipokamatwa na wakati huu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki