-
Je, Kuna Dalili za Matatizo?Amkeni!—2008 | Agosti
-
-
Je, Kuna Dalili za Matatizo?
“Veu Lesa, mwanakijiji mwenye umri wa miaka 73 huko Tuvalu, hahitaji ripoti za kisayansi ili kutambua kwamba maji ya bahari yanaongezeka,” linasema gazeti The New Zealand Herald. “Fuo alizofurahia akiwa mtoto zinatoweka. Mimea aliyokuwa akitumia kulisha familia yake imeharibiwa na maji ya chumvi. Mnamo Aprili (Mwezi wa 4) [2007], alilazimika kuhama baada ya nyumba yake kupigwa na mawimbi yenye nguvu ambayo yalileta mawe na takataka.”
GAZETI Herald linasema kwamba wakaaji wa Tuvalu hawaoni kuongezeka kwa joto duniani kuwa jambo linalozungumziwa tu na wanasayansi, bali ni “jambo halisi la kila siku,” kwani visiwa hivyo viko mita nne hivi juu ya usawa wa bahari.a Tayari maelfu ya watu wamehama visiwa hivyo na wengine wengi wanajitayarisha kuhama.
Wakati huohuo, Naisula, anayeishi mashariki mwa Kenya, lazima atembee kwa kilomita 10 hivi ili apate maji safi. Kisha anahitaji kusubiri zamu yake ili ajaze mtungi wake kwa maji na kuubeba mtungi huo mzito kurudi nyumbani ili atosheleze mahitaji ya msingi tu ya familia yake. Kwa nini wakati na jitihada nyingi hivyo zinahitajika ili kupata maji? Kwa sababu eneo analoishi limekumbwa na ukame katika miaka ya karibuni. Je, matatizo yanayokumba Kenya na Tuvalu yanathibitisha kwamba kiwango cha joto duniani kinaongezeka?
Matabiri ya Watu Fulani
Wengi wanaamini kwamba shughuli za wanadamu zimechangia kwa sehemu kubwa kuongezeka kwa joto duniani, na huenda hilo likasababisha madhara kwa hali ya hewa na mazingira. Kwa mfano, kuyeyuka kwa kiwango kikubwa cha theluji na kuongezeka kwa kiwango cha joto kunaweza kufanya kiwango cha maji ya bahari kiongezeke sana. Visiwa kama vile Tuvalu ambavyo haviko juu sana ya usawa wa bahari vinaweza kufunikwa, na vilevile sehemu kubwa za Uholanzi na Florida, kutaja tu sehemu mbili nyingine. Mamilioni ya watu wanaweza kulazimika kuhama kutoka maeneo kama vile Shanghai na Calcutta, na pia sehemu fulani za Bangladesh.
Wakati huohuo, kuongezeka kwa viwango vya joto kunaweza kuzidisha uharibifu unaosababishwa na dhoruba, mafuriko, na ukame. Katika milima ya Himalaya, kutoweka kwa miamba ya barafu, iliyo katika maeneo yanayosambazia mito saba maji, kunaweza kutokeza upungufu wa maji safi kwa ajili ya asilimia 40 ya watu duniani. Pia maelfu ya jamii za wanyama zimo hatarini, kutia ndani dububarafu ambao maisha yao yanategemea hasa maeneo ya barafu. Kwa kweli, ripoti zinaonyesha kwamba dubu wengi wanakonda na wengine hata wanakufa njaa.
Pia, kuongezeka kwa kiwango cha joto kunaweza kufanya mbu, kupe, na wadudu wengine wanaoeneza magonjwa kutia ndani kuvu, wafikie maeneo mengi zaidi na hivyo kueneza magonjwa. Kikundi fulani cha wanasayansi (Bulletin of the Atomic Scientists) kinasema kwamba “hatari zinazoweza kutokezwa na mabadiliko katika hali ya hewa ni mabaya kama yale yanayoweza kutokezwa na silaha za nyuklia. Madhara yanaweza kutokea polepole kwa sasa . . . , lakini katika muda wa miaka 30 au 40 ijayo mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kutokeza madhara yasiyoweza kurekebishwa katika maeneo ambayo wanadamu wanategemea ili waendelee kuishi.” Jambo lingine linalotisha zaidi ni kwamba wanasayansi fulani wanaamini mabadiliko yanayotokana na kuongezeka kwa joto duniani yanatokea haraka kuliko walivyotarajia.
Tunaweza kukata kauli gani kutokana na matabiri hayo? Je, maisha duniani yamo hatarini? Watu wenye mashaka kuhusu kuongezeka kwa joto duniani wanasema kwamba matabiri hayo hayana msingi. Wengine hawajui waamini nini. Kwa hiyo, ukweli ni nini? Je, wakati ujao wa dunia, kutia ndani wetu, umo hatarini?
[Maelezo ya Chini]
a Tunapozungumzia kuongezeka kwa joto duniani, hilo linahusisha kuongezeka kwa joto la angahewa na bahari.
-
-
Je, Dunia Inakabili Hatari?Amkeni!—2008 | Agosti
-
-
Je, Dunia Inakabili Hatari?
KUONGEZEKA kwa joto duniani kumefafanuliwa kuwa hatari kubwa zaidi inayowakabili wanadamu. Kulingana na jarida Science, jambo linalowahangaisha watafiti “ni kwamba tumeanzisha mabadiliko ya polepole yasiyoweza kusimamishwa.” Watu wenye mashaka hawakubaliani na hilo. Wengi wanakubali kwamba joto linaongezeka duniani, lakini wana mashaka kuhusu kinachosababisha ongezeko hilo na matokeo yake. Wanasema kwamba huenda wanadamu wanachangia hali hiyo lakini wao si kisababishi kikuu. Kwa nini kuna maoni tofauti?
Kwanza, mifumo inayotegemeza hali ya hewa duniani ni tata na haijaeleweka vizuri. Pia, vikundi vinavyoshughulikia mazingira hutoa maoni yao kuhusu takwimu za kisayansi, kama zile zinazotumiwa kuonyesha kwa nini joto linaongezeka.
Je, Kweli Joto Linaongezeka?
Kulingana na ripoti ya karibuni ya Kamati ya Serikali Mbalimbali Kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC) iliyofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, kuongezeka kwa joto duniani ni jambo hakika; au “lisilotiliwa shaka” na “inawezekana sana” kwamba wanadamu wamechangia kwa sehemu kubwa hali hiyo. Wengine wanaopinga mkataa huo, hasa kuhusiana na shughuli za wanadamu kuchangia, wanasema kwamba huenda majiji yana joto zaidi kwa sababu yanakua. Isitoshe, saruji na chuma huhifadhi joto kwa haraka na kulipoteza joto hilo polepole wakati wa usiku. Watu wenye mashaka wanasema kwamba takwimu kutoka majijini hazionyeshi hali katika maeneo ya vijijini na zinaweza kupotosha takwimu za dunia nzima.
Kwa upande mwingine, Clifford, mzee wa kijiji anayeishi kwenye kisiwa karibu na ufuo wa Alaska anasema kwamba amejionea mabadiliko. Watu katika kijiji chake husafiri juu ya theluji ya bahari hadi kwenye nchi kavu ili kuwinda kuro na kongoni. Hata hivyo, kuongezeka kwa joto kunafanya hilo lisiwezekane. “Mikondo ya maji imebadilika, hali ya barafu imebadilika, na kugandamana kwa Bahari ya Chukchi . . . kumebadilika,” anasema Clifford. Anaeleza kwamba bahari ilikuwa ikigandamana mwishoni mwa Oktoba (Mwezi wa 10), lakini sasa inagandamana mwishoni mwa Desemba (Mwezi wa 12).
Mnamo 2007, joto liliongezeka katika Njia ya Kaskazini-Magharibi, ambayo ingeweza kupitika kwa mara ya kwanza katika historia. “Mwaka huu tumeona kuongezeka kwa kipindi ambacho hakuna theluji,” alisema mwanasayansi mkuu katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Habari za Theluji na Barafu huko Marekani.
Gesi Zinazoongeza Joto Ni Muhimu kwa Uhai
Jambo moja linalosababisha mabadiliko hayo ni kuongezeka sana kwa gesi zinazoongeza joto. Hilo ni tukio la asili ambalo ni muhimu ili kuendeleza uhai duniani. Nishati kutoka kwa jua inapofika duniani, asilimia 70 inafyonzwa na hivyo kuongeza joto la hewa, nchi kavu, na bahari. Kama hakungekuwa na utaratibu huo, kwa wastani kiwango cha joto juu ya dunia kingekuwa Selsiasi 18 chini ya sufuri. Hatimaye, joto hilo linaruhusiwa kutoka na hivyo huzuia dunia isiwe na joto jingi kupita kiasi. Lakini vitu vinavyochafua hewa vinapobadili muundo wa angahewa, hilo huzuia joto lisilohitajiwa lisitoke. Hilo linaweza kufanya joto liongezeke duniani.
Baadhi ya gesi zinazochangia ongezeko la joto ni kaboni dioksidi, nitrasi oksidi, na methini, vilevile mvuke wa maji. Gesi hizo zimeongezeka sana katika miaka 250 iliyopita, tangu mwanzo wa mvuvumko wa kiviwanda na kutumiwa zaidi kwa nishati yenye kaboni, kama vile makaa ya mawe na mafuta. Inaelekea kwamba jambo lingine linaloongeza joto ni kuongezeka kwa wanyama wa kufugwa ambao mfumo wao wa kumeng’enya chakula unatokeza methini na nitrasi oksidi. Watafiti fulani wanataja sababu zingine za kuongezeka kwa joto ambazo wanasema zilitokea kabla wanadamu hawajaathiri mazingira.
Je, Ni Badiliko la Kawaida Tu?
Watu wenye mashaka kuhusu jinsi wanadamu wanavyochangia kuongezeka kwa joto, wanasema kwamba kiwango cha joto kimebadilika sana wakati uliopita. Kama uthibitisho wanataja wakati ambapo dunia ilikuwa na barafu nyingi zaidi kuliko sasa. Na kuhusu kuongezeka kwa joto wanasema kwamba maeneo yenye baridi kama vile Greenland, wakati fulani yalikuwa na mimea inayopatikana hasa katika maeneo yenye joto. Bila shaka, wanasayansi wanakubali kwamba kadiri wanavyochunguza wakati wa zamani zaidi ndivyo uhakika kuhusu hali ya hewa unavyopungua.
Kabla shughuli za wanadamu hazijaathiri mazingira, ni nini kilichofanya kiwango cha joto kibadilike sana? Huenda chanzo kimoja ni utendaji katika jua unaoathiri kiwango cha joto kinachotolewa na jua. Umbali wa dunia kutoka kwa jua hubadilika kwa kuwa njia ambayo dunia hutumia kuzunguka jua hubadilika baada ya maelfu ya miaka. Pia mavumbi ya volkano na mabadiliko katika mikondo ya bahari yanachangia kubadilika kwa kiwango cha joto.
Kuchunguza Mazingira
Hata chanzo kiwe nini, ikiwa kiwango cha joto duniani kinaongezeka, hilo litakuwa na matokeo gani kwetu na kwa mazingira? Ni vigumu kutabiri kwa njia hususa jinsi hali itakavyokuwa. Hata hivyo, siku hizi wanasayansi wana kompyuta za hali ya juu wanazoweza kutumia kutabiri matokeo katika mazingira. Mfumo huo wa kompyuta unatia ndani sheria za fizikia, takwimu za mazingira, na mambo ya asili yanayoathiri hali ya hewa.
Mifumo hiyo ya kompyuta inawawezesha wanasayansi kufanya majaribio kuhusiana na hali ya hewa katika njia ambazo hazingewezekana kihalisi. Kwa mfano, wanaweza “kubadili” kiwango cha joto la jua ili waone jinsi inavyoathiri barafu kwenye ncha za dunia, kiwango cha joto kwenye hewa na bahari, kadiri ambavyo maji yanavukizwa, shinikizo la hewa angani, kufanyizwa kwa mawingu, upepo, na mvua. Wanaweza “kufanyiza” milipuko ya volkano na kuchunguza matokeo ya mavumbi ya volkano katika hali ya hewa. Na wanaweza kuchunguza matokeo ya ongezeko la watu, kuharibiwa kwa misitu, matumizi ya ardhi, mabadiliko katika kutokezwa kwa gesi zinazoongeza joto, na kadhalika. Wanasayansi wanatumaini kwamba hatua kwa hatua mifumo yao ya kompyuta itakuwa sahihi na yenye kutegemeka zaidi.
Mifumo ya sasa ni sahihi kadiri gani? Bila shaka, mengi yanategemea usahihi na wingi wa takwimu zinazoingizwa katika mifumo hiyo. Hivyo kunakuwa na matokeo mbalimbali, mengine yakitabiri mabadiliko madogo na mengine matokeo mabaya. Hata hivyo, kulingana na jarida Science “kunaweza kuwa na mambo yasiyotarajiwa katika mfumo wa [asili] wa hewa.” Tayari kumekuwa na mambo yasiyotarajiwa, kama vile kuyeyuka kwa haraka sana kwa theluji ya Aktiki, ambako kumewashangaza wataalamu wengi wa hali ya anga. Ikiwa wenye mamlaka ya kutunga sheria na viwango wangejua matokeo ya kile ambacho mwanadamu anafanya au hafanyi sasa, wangeweza kufanya maamuzi ambayo yangepunguza matatizo ya wakati ujao.
Wakifikiria uwezekano huo, wanakamati wa IPCC walichunguza majaribio sita ya mifumo ya kompyuta yaliyohusisha hali mbalimbali kila moja ikiathiri hewa na mazingira kwa njia tofauti. Hali hizo zilitia ndani kutokezwa kwa wingi kwa gesi zinazoongeza joto duniani, vizuizi vichache vilivyopo, na pia kuwekwa kwa vizuizi vikali. Kupatana na matarajio hayo, wachanganuzi wanahimiza kuwe na sheria kadhaa. Sheria hizo zinatia ndani vikwazo kwa matumizi ya nishati ya kaboni, adhabu kwa watakaokiuka sheria hizo, kutokezwa kwa nishati nyingi zaidi ya nyuklia, na kuanzishwa kwa teknolojia zisizoathiri mazingira.
Je, Mifumo Hiyo Inategemeka?
Wachambuzi wanasema kuwa mbinu za sasa za kutabiri “zinarahisisha sana mifumo ya hewa ambayo haijaeleweka vizuri” na “zinapuuza mifumo mingine.” Pia wanataja kwamba matokeo ya kompyuta hayapatani nyakati zote. Mwanasayansi mmoja aliyeshiriki mazungumzo katika kamati ya IPCC alisema hivi: “Baadhi yetu tunahisi kwamba kupima na kuelewa mfumo wa hewa ulio tata sana ni kazi kubwa hivi kwamba tuna mashaka kuhusu uwezo wetu wa kujua mfumo huo unafanya nini na kwa nini.”a
Bila shaka, wengine watasema kwamba kukosa kufanya mabadiliko kwa sababu hatuna hakika kuhusu chanzo cha matatizo si uamuzi wa busara. Wanasema hivi: “Tunaweza kuwaelezaje watoto wetu?” Iwe mifumo hiyo ya kompyuta ni sahihi au la, tunaweza kuwa na hakika kwamba dunia imo hatarini. Baadhi ya mambo machache yasiyopingika na yanayoharibu uwezo wa mazingira wa kuendeleza uhai ni uchafuzi, kuharibiwa kwa misitu, kupanuka kwa majiji, na kutoweka kwa jamii za viumbe.
Kulingana na yale tunayojua, je, tunaweza kuwatarajia wanadamu kwa ujumla wabadili mtindo wao wa maisha ili wahifadhi makao yetu yanayopendeza na kutuhifadhi pia? Isitoshe ikiwa shughuli za binadamu zinaongeza kiwango cha joto duniani, huenda tuna miaka tu wala si karne nyingi za kufanya mabadiliko. Kufanya mabadiliko hayo kunamaanisha kushughulikia haraka vyanzo vya matatizo ya dunia, yaani, pupa ya mwanadamu, ubinafsi, kukosa ujuzi, serikali zisizo na uwezo, na kutojali. Je, hilo ni jambo linalowezekana au ni ndoto tu? Ikiwa ni ndoto, je, tuna tumaini lolote? Swali hilo litazungumziwa katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a John R. Christy, msimamizi wa Kituo cha Sayansi cha Mfumo wa Dunia katika Chuo Kikuu cha Alabama, Huntsville, Marekani, kama ilivyoripotiwa katika gazeti The Wall Street Journal la Novemba 1, 2007 (1/11/2007).
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
KIWANGO CHA JOTO CHA DUNIA HUPIMWAJE?
Ili kuonyesha ugumu wa kufanya hivyo, wewe ungepimaje kiwango cha joto katika chumba kikubwa? Kwa mfano, ungeweka wapi kipima-joto? Kwa kuwa joto hupanda, kuna uwezekano kwamba hewa iliyo juu itakuwa yenye joto zaidi ya ile iliyo chini. Vilevile kiwango cha joto kinachoonyeshwa na kipima-joto kitatofautiana ikiwa utakiweka karibu na dirisha, ikiwa kinapigwa na jua, au kikiwa chini ya kivuli. Pia rangi inaweza kufanya kipima-joto kionyeshe vipimo tofauti kwa kuwa maeneo yasiyo na rangi nyangavu hufyonza joto zaidi.
Kwa hiyo, huenda kipimo kimoja hakitatosha. Utahitaji kuchukua kiwango cha joto kutoka sehemu mbalimbali kisha ukadirie wastani. Na huenda vipimo vyenyewe vikabadilika siku tofauti-tofauti na majira tofauti-tofauti. Ili kupata wastani unaotegemeka, utahitaji kuchukua vipimo vingi kwa muda mrefu. Hivyo, hebu wazia jinsi ilivyo vigumu kupima kiwango cha ujumla cha joto cha nchi kavu, angahewa, na bahari! Hata hivyo, takwimu hizo ni muhimu ili kuchunguza kwa usahihi mabadiliko ya hali ya hewa.
[Hisani]
NASA photo
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
JE, NISHATI YA NYUKLIA NDILO SULUHISHO?
Nishati inazidi kutumika ulimwenguni pote kwa wingi zaidi. Kwa kuwa kutumiwa kwa mafuta na makaa ya mawe kunatokeza gesi zinazosababisha ongezeko la joto, serikali fulani zinafikiria kutumia nishati ya nyuklia kwa kuwa haitokezi uchafu mwingi. Lakini hilo linatokeza matatizo pia.
Gazeti International Herald Tribune linasema kwamba huko Ufaransa, ambayo ni mojawapo ya nchi zinazotegemea zaidi nishati ya nyuklia, kila mwaka inahitaji lita bilioni 18,900 za maji ili kupoesha mitambo ya nyuklia. Kulipokuwa na joto kali sana mnamo 2003, maji moto ambayo hutolewa kwa ukawaida katika mitambo hiyo ya nyuklia ilitishia kuongeza kiwango cha joto katika mito hivi kwamba viumbe wote wangehatarishwa. Hivyo, mitambo fulani iliacha kutumiwa. Inatazamiwa kwamba hali hiyo itakuwa mbaya zaidi ikiwa viwango vya joto duniani vitaongezeka.
“Ni lazima tusuluhishe tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ili tutumie nishati ya nyuklia,” mtaalamu wa mambo ya nyuklia David Lochbaum ambaye ni mwanachama wa Muungano wa Wanasayansi Wanaojali.
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 7]
MISIBA ILIYOSABABISHWA NA HALIi YA HEWA MNAMO 2007
Katika mwaka wa 2007, kulikuwa na misiba mingi iliyosababishwa na hali ya hewa. Kufuatia hilo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu, ilitoa wito wa msaada wa dharura mara 14, na hiyo ilikuwa mara 4 zaidi ya rekodi ya awali iliyowekwa mnamo 2005. Misiba iliyoorodheshwa hapa ni baadhi ya ile iliyotukia katika 2007. Kumbuka kuwa kila tukio halionyeshi hali ya muda mrefu ya eneo fulani.
◼ Uingereza: Watu zaidi ya 350,000 waliathiriwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutukia katika zaidi ya miaka 60. Uingereza na Wales zilipata kiwango kikubwa zaidi cha mvua katika miezi ya Mei (Mwezi wa 5) hadi Julai (Mwezi wa 7) tangu rekodi zilipoanza kuwekwa mnamo 1766.
◼ Afrika Magharibi: Mafuriko yaliwaathiri watu 800,000 katika nchi 14.
◼ Lesotho: Kiwango cha juu cha joto na ukame uliharibu mimea. Huenda watu 553,000 hivi wakahitaji msaada wa chakula.
◼ Sudan: Mvua nyingi iliwaacha watu 150,000 bila makao. Angalau watu 500,000 walipokea msaada.
◼ Madagaska: Tufani na mvua kubwa zilipiga kisiwa hicho na kuwaacha watu 33,000 bila makao na kuharibu mimea ya watu 260,000.
◼ Korea Kaskazini: Inakadiriwa kuwa watu 960,000 waliathiriwa sana na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi.
◼ Bangladesh: Mafuriko yaliathiri watu milioni 8.5 na kuua zaidi ya watu 3,000, kutia ndani mifugo milioni 1.25. Nyumba milioni 1.5 hivi ziliharibiwa au kubomolewa kabisa.
◼ India: Mafuriko yaliathiri watu milioni 30.
◼ Pakistan: Mvua inayoambatana na tufani iliwaacha watu 377,000 bila makao huku mamia wakifa.
◼ Bolivia: Watu zaidi ya 350,000 waliathiriwa na mafuriko huku 25,000 wakiachwa bila makao.
◼ Mexico: Mafuriko katika eneo hilo yaliwaacha watu 500,000 bila makao na kuathiri watu zaidi ya milioni moja.
◼ Jamhuri ya Dominika: Mvua iliyonyesha kwa muda mrefu ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, na kufanya watu 65,000 wapoteze makao.
◼ Marekani: Mioto iliyokumba eneo la kusini la California liliwafanya wakaaji 500,000 wahame.
[Hisani]
Based on NASA/Visible Earth imagery
-
-
Je, Dunia Inakabili Hatari?Amkeni!—2008 | Agosti
-
-
Gesi Zinazoongeza Joto Ni Muhimu kwa Uhai
Jambo moja linalosababisha mabadiliko hayo ni kuongezeka sana kwa gesi zinazoongeza joto. Hilo ni tukio la asili ambalo ni muhimu ili kuendeleza uhai duniani. Nishati kutoka kwa jua inapofika duniani, asilimia 70 inafyonzwa na hivyo kuongeza joto la hewa, nchi kavu, na bahari. Kama hakungekuwa na utaratibu huo, kwa wastani kiwango cha joto juu ya dunia kingekuwa Selsiasi 18 chini ya sufuri. Hatimaye, joto hilo linaruhusiwa kutoka na hivyo huzuia dunia isiwe na joto jingi kupita kiasi. Lakini vitu vinavyochafua hewa vinapobadili muundo wa angahewa, hilo huzuia joto lisilohitajiwa lisitoke. Hilo linaweza kufanya joto liongezeke duniani.
Baadhi ya gesi zinazochangia ongezeko la joto ni kaboni dioksidi, nitrasi oksidi, na methini, vilevile mvuke wa maji. Gesi hizo zimeongezeka sana katika miaka 250 iliyopita, tangu mwanzo wa mvuvumko wa kiviwanda na kutumiwa zaidi kwa nishati yenye kaboni, kama vile makaa ya mawe na mafuta. Inaelekea kwamba jambo lingine linaloongeza joto ni kuongezeka kwa wanyama wa kufugwa ambao mfumo wao wa kumeng’enya chakula unatokeza methini na nitrasi oksidi. Watafiti fulani wanataja sababu zingine za kuongezeka kwa joto ambazo wanasema zilitokea kabla wanadamu hawajaathiri mazingira.
Je, Ni Badiliko la Kawaida Tu?
Watu wenye mashaka kuhusu jinsi wanadamu wanavyochangia kuongezeka kwa joto, wanasema kwamba kiwango cha joto kimebadilika sana wakati uliopita. Kama uthibitisho wanataja wakati ambapo dunia ilikuwa na barafu nyingi zaidi kuliko sasa. Na kuhusu kuongezeka kwa joto wanasema kwamba maeneo yenye baridi kama vile Greenland, wakati fulani yalikuwa na mimea inayopatikana hasa katika maeneo yenye joto. Bila shaka, wanasayansi wanakubali kwamba kadiri wanavyochunguza wakati wa zamani zaidi ndivyo uhakika kuhusu hali ya hewa unavyopungua.
Kabla shughuli za wanadamu hazijaathiri mazingira, ni nini kilichofanya kiwango cha joto kibadilike sana? Huenda chanzo kimoja ni utendaji katika jua unaoathiri kiwango cha joto kinachotolewa na jua. Umbali wa dunia kutoka kwa jua hubadilika kwa kuwa njia ambayo dunia hutumia kuzunguka jua hubadilika baada ya maelfu ya miaka. Pia mavumbi ya volkano na mabadiliko katika mikondo ya bahari yanachangia kubadilika kwa kiwango cha joto.
-
-
Wakati Ujao wa Dunia Umo Mikononi mwa Nani?Amkeni!—2008 | Agosti
-
-
Wakati Ujao wa Dunia Umo Mikononi mwa Nani?
“KUONGEZEKA kwa joto duniani kumetokeza mtihani mkubwa zaidi ambao wanadamu wamewahi kukabili,” likasema toleo la Oktoba 2007 la National Geographic. Gazeti hilo lilisema kwamba ili tutatue tatizo hilo kwa mafanikio, tunahitaji “kutenda haraka, kwa njia inayofaa, na kwa ukomavu ambao kwa kawaida sisi wanadamu hatuonyeshi.”
Je, wanadamu watatatua tatizo hilo kwa ukomavu? Kuna vipingamizi vingi: kutojali, pupa, ukosefu wa ujuzi, mapendezi ya vikundi mbalimbali, jitihada za kupata utajiri katika nchi zinazositawi, na mtazamo wa mamilioni wanaotaka kuishi maisha ya kawaida na hivyo kutumia nishati nyingi sana.
Nabii wa kale wa Mungu anachanganua uwezo wetu wa kutatua matatizo ya kimaadili, kijamii, na kiserikali. Aliandika hivi: “Njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake. Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.” (Yeremia 10:23) Historia yenye kusikitisha ya mwanadamu inathibitisha ukweli wa maneno hayo. Ingawa leo kuna maendeleo mengi ya sayansi na tekinolojia, tunakabili hatari ambazo hazikuwaziwa hapo awali. Basi tunawezaje kuwa na hakika kwamba hali zitakuwa nzuri wakati ujao?
Ni kweli kwamba mengi yamesemwa kuhusu kutatua tatizo la kubadilika kwa hali ya hewa na mambo mengine yenye kudhuru, lakini ni machache ambayo yamefanywa. Kwa mfano, mataifa yalitendaje mnamo 2007 Njia ya Kaskazini-Magharibi ilipofunguka na kutumiwa kwa mara ya kwanza? Makala katika gazeti New Scientist inajibu: “Waling’ang’ania bila aibu kujipatia maeneo ambayo wangeweza kuchimba mafuta na gesi zaidi.”
Karibu miaka 2,000 iliyopita Biblia ilitabiri kwa usahihi kwamba wanadamu wangefikia hatua ya ‘kuiharibu dunia.’ (Ufunuo 11:18) Ni wazi kwamba ulimwengu unahitaji kiongozi aliye na hekima na nguvu ili kutimiza mambo ambayo watu wanataka na raia ambao watajitiisha kwake. Je, kuna kiongozi wa kisiasa au mwanasayansi mnyoofu na mwenye uwezo anayeweza kutimiza hilo? Biblia inajibu: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote.”—Zaburi 146:3.
Wakati Ujao wa Dunia Ni Salama!
Kuna Kiongozi mmoja tu anayeweza kutatua kwa mafanikio matatizo yanayoukabili ulimwengu. Biblia ilitabiri hivi kumhusu: “Roho ya Yehova [Mungu] itatua juu yake, roho ya hekima na ya uelewaji, roho ya shauri na ya nguvu, roho ya ujuzi na ya kumwogopa Yehova . . . Atawahukumu kwa uadilifu watu wa hali ya chini, . . . na kumuua mwovu kwa roho ya midomo yake.”—Isaya 11:2-5.
Huyo ni nani? Si mwingine ila ni Yesu Kristo ambaye kwa upendo alitoa uhai wake kwa ajili yetu. (Yohana 3:16) Sasa akiwa kiumbe wa roho mwenye nguvu, Yesu amepewa na Mungu mamlaka na nguvu za kutawala juu ya dunia.—Danieli 7:13, 14; Ufunuo 11:15.
Mojawapo ya mambo yanayomfanya Yesu astahili ni ujuzi wake mwingi kuhusu uumbaji wa Mungu ambao alipata kabla ya kuja duniani. Kwa kweli, miaka mingi sana iliyopita Mungu alipoumba ulimwengu, Yesu alikuwa ‘stadi wake wa kazi.’ (Methali 8:22-31) Hebu wazia hilo: Yesu ambaye alihusika katika uumbaji wa dunia na vitu vyote vilivyo hai, ataongoza katika kurekebisha hali iliyotokezwa na kutojali kwa wanadamu.
Ni nani watakaokuwa raia wa Kristo? Watakuwa watu ambao kwa kweli ni wapole na waadilifu wanaomjua Mungu wa kweli, Yehova, na wanamtii Yesu Kristo akiwa Mtawala. (Zaburi 37:11, 29; 2 Wathesalonike 1:7, 8) Yesu alisema kwamba “watairithi dunia,” ambayo itageuzwa kuwa paradiso.—Mathayo 5:5; Isaya 11:6-9; Luka 23:43.
Unaweza kufanya nini ili ushiriki katika kutimizwa kwa ahadi hizo za Biblia? Yesu mwenyewe anajibu: “Uzima wa milele ndio huu, waendelee kupata ujuzi juu yako wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.”—Yohana 17:3.
Ni kweli kwamba huenda ikaonekana dunia imo hatarini lakini hakuna shaka itaendelea kuwa makao ya wanadamu. Badala yake, wale wanaoendelea kuuvunjia heshima uumbaji wa Mungu na wanaokataa kumtii Yesu Kristo wamo hatarini. Hivyo basi, Mashahidi wa Yehova wanakutia moyo uendelee kupata ujuzi unaoongoza kwenye uzima wa milele.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
SAYANSI HAIWEZI KUTATUA MATATIZO YA DUNIA
Wakijua vema hatari zinazohusika, mamilioni ya watu wanadhuru akili na miili yao kwa kutumia dawa za kulevya, kutumia kileo vibaya, na kuvuta sigara. Kwa maoni yao, uhai si zawadi takatifu kutoka kwa Mungu. (Zaburi 36:9; 2 Wakorintho 7:1) Kwa kusikitisha, mtazamo kama huo kuelekea dunia umesababisha matatizo yake.
Basi suluhisho ni nini? Je, sayansi na elimu zinaweza kutatua matatizo hayo? Haziwezi. Tatizo la kiroho linahitaji suluhisho la kiroho. Biblia inakubaliana na wazo hilo. Hivyo, Biblia inaahidi kwamba wakati utafika ambapo wanadamu “hawatasababisha madhara yoyote wala kusababisha uharibifu wowote” kwa dunia kwa sababu “itajawa na kumjua Yehova kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Chini ya utawala wa Kristo waadilifu watashiriki kazi ya kufanya dunia iwe paradiso
-