Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kitabu Domesday—Ukaguzi wa Kipekee
    Amkeni!—2011 | Septemba
    • Kitabu Domesday​—Ukaguzi wa Kipekee

      William, dyuki wa Normandy (eneo fulani nchini Ufaransa), alishinda Uingereza mwaka wa 1066. Miaka 19 baadaye, aliamuru milki yake mpya ikaguliwe. Ukaguzi huo uliandikwa katika kitabu kinachoitwa Domesday. Kwa nini kitabu hicho ni mojawapo ya rekodi muhimu zaidi za kihistoria nchini Uingereza?

      WILLIAM alifika karibu na mji wa Hastings, Uingereza mnamo Septemba 1066. Oktoba (Mwezi wa 10) 14, alishinda jeshi la Mfalme Harold wa Uingereza, na akamuua. Siku ya Krismasi mwaka wa 1066, William ambaye baadaye alikuja kuitwa Mshindi, alitawazwa kuwa mfalme huko Westminster Abbey, London. Waingereza wangekuwa na maisha ya aina gani chini ya mtawala huyo mpya?

      Ukaguzi Mkuu

      Mfalme William wa Kwanza aliharibu kabisa eneo kubwa lililoko kaskazini mwa nchi hiyo na kuliacha ukiwa. Trevor Rowley, aliyekuwa mkufunzi wa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Oxford, anaandika hivi: “Hata inapolinganishwa na hali zenye ukatili zilizokuwapo nyakati hizo, ule uharibifu mkubwa aliosababisha katika maeneo ya Kaskazini (1068-1070) ulikuwa wa kinyama.” William alikumbwa na uasi wa mara kwa mara, na wanajeshi wake 10,000 hivi, waliishi katikati ya wakazi wenye chuki wapatao milioni mbili hivi. Watu wa Normandy hatimaye walijenga ngome zaidi ya 500 kote nchini—ngome maarufu zaidi ikiwa ile inayoitwa Mnara wa London.

      Ilipofika Desemba 1085, miaka 19 baada ya shambulizi lake, William alikaa kwa siku tano pamoja na maofisa wa makao yake ya kifalme huko Gloucester, Uingereza, huku akipanga kufanya ukaguzi wa nchi yote isipokuwa mji wa London na ule wa Winchester. Mwanzoni mwa mwaka uliofuata, makamishna wa mfalme walitumwa wakati uleule mmoja kwenda kwenye maeneo yote saba ya majimbo kukusanya habari kutoka kwa wawakilishi wa majimbo hayo ili waweze kukadiria utajiri wa nchi.

      Ilikuwa lazima mfalme atafute pesa za kuwalipa wanajeshi wake. Pia alihitaji kutatua mizozo ya umiliki wa ardhi. Kutimiza miradi hiyo kungehakikisha kwamba watu kutoka Normandy na maeneo mengine ya Ufaransa wangepata makao Uingereza, na hivyo utawala wa Wanormani ungeendelea.

      “Domesday”

      Punde tu baada ya kuwashinda Waingereza, Mfalme William aliwakabidhi Wanormani wenye vyeo mali zote za wakuu wa Uingereza. Ukaguzi alioufanya William ulifunua kwamba kufikia wakati huo, karibu nusu ya mali ya nchi yote ilikuwa mikononi mwa wanaume wasiozidi 200, na ni 2 tu kati yao waliokuwa Waingereza. Iliwabidi Waingereza 6,000 hivi waliokuwa wakipangisha ardhi walipe ili waweze kuishi kwenye ardhi waliyokuwa wamemiliki kihalali kabla ya mwaka wa 1066, ilhali waliokuwa maskini na wasio na makao walihitaji kutumia kila mbinu ili wakabiliane na hali hiyo.

      Ukaguzi huo ulihalalisha unyakuzi wa mali wa Wanormani. Pia ukaguzi huo ulikadiria upya ushuru wa ardhi na wa umiliki wake, pamoja na misitu na maeneo yenye malisho. Pia, kila mnyama—ng’ombe-dume au wa kike, na hata nguruwe—walitiwa ndani ya ukaguzi huo. Waingereza waliokandamizwa walikuwa na wasiwasi sana kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, kwa kuwa walijua kwamba hawangeweza kubadili chochote baada ya hapo. Walifananisha ukaguzi huo mkuu na “Siku ya Hukumu,” au “Siku ya Mabaya.” Ndiyo sababu kilikuja kuitwa Kitabu cha Siku ya Hukumu (Domesday Book).

      Kitabu Domesday kilifanyizwa kwa mabuku mawili yaliyoandikwa katika Kilatini kwenye vipande vya ngozi. Buku moja lililoitwa Great Domesday, lilikuwa na karatasi kubwa 413 za ngozi, na Little Domesday lilikuwa na karatasi ndogo 475 za ngozi.a Kitabu hicho hakikuwa kimekamilishwa wakati William alipokufa mwaka wa 1087.

  • Kitabu Domesday—Ukaguzi wa Kipekee
    Amkeni!—2011 | Septemba
    • [Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 23]

      VITA VYA KIDINI VYA WILLIAM

      William alimwomba papa akweze uvamizi aliokuwa akifanya uwe vita vya kidini, na akamwahidi kwamba angelifanya kanisa la Uingereza lililoasi lirudi chini ya udhibiti wa papa. Papa alikubali haraka. Hiyo ilikuwa “mbinu ya ujanja wa kidiplomasia” ya William, anaandika Profesa David C. Douglas. Mwanahistoria mwingine mashuhuri anayeitwa George M. Trevelyan, katika kitabu chake History of England, alisema kwamba “bendera na baraka kutoka kwa Papa ilikuwa yenye thamani sana kwa William hasa inapozingatiwa kwamba jambo alilokuwa akifanya lilionekana wazi kuwa wizi wa kimabavu badala ya pambano la kidini.”

      [Hisani]

      © The Bridgeman Art Library

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki