Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Chuki Imeenea Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2001 | Agosti 8
    • Chuki Imeenea Ulimwenguni Pote

      KUNA hali ya kutisha inayoenea. Hali hiyo ni chuki. Nayo inaongezeka ulimwenguni pote.

      Katika jimbo moja katika nchi za Balkani, watu bado wanateseka baada ya mauaji ya jamii nzimanzima yaliyotukia hivi karibuni. Uadui ambao umekuwepo kwa karne nyingi umesababisha mauaji mengi, ubakaji, kuhamishwa kutoka nyumbani, uchomaji na uporaji wa nyumba na vijiji, uharibifu wa mazao na mifugo, na njaa. Mabomu ya ardhini bado yapo.

      Katika Timor Mashariki, Kusini-mashariki mwa Asia, watu 700,000 wenye hofu walilazimika kutoroka mauaji, kupigwa, kupigwa risasi ovyoovyo, na kuhamishwa kinguvu kutoka makwao. Maeneo waliyoacha yaliharibiwa na majeshi ya mgambo. Mwathiriwa mmoja aliomboleza hivi: “Ninahisi kama mnyama anayewindwa.”

      Huko Moscow, nyumba moja ya orofa ililipuliwa kwa bomu la magaidi. Miili ya watu 94 wasio na hatia—wakiwemo watoto—ilirushwa kila mahali kwa mlipuko huo. Zaidi ya watu 150 walijeruhiwa. Tendo kama hilo lenye kuogofya litukiapo, watu hujiuliza hivi, ‘Ni nani wengine watakaopatwa na maovu hayo?’

      Huko Los Angeles, California, mbaguzi mmoja wa rangi aliwapiga risasi watoto Wayahudi wa shule ya watoto wadogo na baadaye akamfyatua tarishi mmoja Mfilipino.

      Yafaa kusema kwamba chuki imeenea ulimwenguni pote. Karibu kila siku, ripoti za habari huonyesha matendo ya kijeuri yanayosababishwa na uadui wa kijamii, wa kikabila, na wa kidini. Sisi huona mataifa, jamii, na familia zikivunjika. Sisi huona nchi mbalimbali zikishiriki katika mauaji ya kikatili ya watu wengi. Sisi huona matendo ya kinyama yakifanywa eti kwa sababu watu fulani wako “tofauti.”

      Ili chuki imalizwe, twapaswa kuelewa vyanzo vya ujeuri wa aina hiyo. Je, chuki imeingizwa ndani ya chembe za urithi za wanadamu? Je, ni tabia ambayo watu hujifunza? Je, chuki yaweza kukomeshwa?

      [Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

      Kemal Jufri/Sipa Press

  • Vyanzo vya Chuki
    Amkeni!—2001 | Agosti 8
    • Vyanzo vya Chuki

      CHUKI ilianza mapema katika historia ya mwanadamu. Simulizi la Biblia kwenye Mwanzo 4:8 lasema hivi: “Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.” “Na ni kwa ajili ya nini yeye alimchinja?” aliuliza Yohana mwandikaji wa Biblia. “Kwa sababu kazi zake mwenyewe zilikuwa mbovu, lakini zile za ndugu yake zilikuwa za uadilifu.” (1 Yohana 3:12) Habili aliuawa kwa sababu ya chanzo kimoja cha chuki, yaani, wivu. “Wivu ni ghadhabu ya mtu,” yasema Mithali 6:34. Leo, watu huchukiana kwa sababu ya kuoneana wivu kwa sababu ya cheo, utajiri, kazi, na mafanikio mengine.

      Kutojua Mambo Fulani na Woga

      Lakini kuna vyanzo vingine vingi vya chuki licha ya wivu. Mara nyingi, chuki husababishwa na kutojua mambo fulani na woga. “Kabla sijajifunza kamwe kuchukia, nilijifunza kuogopa,” asema kijana mmoja aliye mshiriki wa kikundi kijeuri cha ubaguzi wa rangi. Woga huo husababishwa na kutojua mambo fulani. Kwa mujibu wa kichapo The World Book Encyclopedia, watu wenye ubaguzi huwa na mwelekeo wa kushikilia maoni ‘yasiyotegemea uthibitisho uliopo. . . . Watu wenye ubaguzi hugeuza, hupotosha, huelewa kimakosa, au hata hupuuza mambo ya hakika yasiyopatana na maoni yao.’

      Maoni hayo hutoka wapi? Ripoti moja ya habari ya Internet yasema hivi: “Historia huchangia maoni mengi ya kitamaduni yasiyobadilika, lakini pia historia yetu binafsi huchangia mambo mengi tunayobagua.”

      Kwa mfano, nchini Marekani biashara ya watumwa ilizusha migogoro inayoendelea hadi leo kati ya Wazungu wengi na watu wa asili ya Kiafrika. Mara nyingi, wazazi huwapitishia watoto wao maoni mabaya kuhusu jamii fulani. Mzungu mmoja aliyejitambulisha waziwazi kuwa mbaguzi alikubali kwamba alisitawisha maoni mabaya ya ubaguzi “bila kushirikiana hata kidogo na watu weusi.”

      Pia kuna watu wanaowadharau tu watu walio tofauti. Huenda wakawa na maoni kama hayo baada ya kuchukizwa mara moja tu na mtu wa jamii au utamaduni tofauti. Kutokana na hayo, wao hukata kauli mara moja kwamba kila mtu wa jamii au utamaduni huo ana tabia zisizopendeza.

      Mtu mwenye ubaguzi huudhi, lakini ubaguzi unapoenea katika taifa au jamii nzima, waweza kusababisha maafa. Mtu anapoamini kwamba taifa lake, rangi yake ya ngozi, utamaduni wake, au lugha yake humfanya awe bora kuliko wengine hilo laweza kumfanya ashikilie sana maoni ya ubaguzi au kudharau mtu yeyote au kitu chochote kigeni. Katika karne ya 20, mara nyingi ubaguzi wa aina hiyo ulisababisha jeuri.

      Si lazima chuki au ubaguzi uwe wa rangi ya ngozi au wa kitaifa tu. Mchunguzi Clark McCauley wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania aliandika kwamba ‘kuwagawanya watu tu katika vikundi viwili, kwaweza kuwafanya wapendelee vikundi vyao.’ Katika majaribio maarufu kuhusu jambo hilo, mwalimu mmoja wa darasa la tatu alionyesha hilo alipowagawanya wanafunzi wake katika vikundi viwili—kikundi cha watoto wenye macho ya bluu na kikundi cha watoto wenye macho ya kahawia. Baada ya muda mfupi, uadui ulisitawi kati ya vikundi hivyo viwili. Hata vikundi vinavyofanyizwa kwa sababu ya mambo madogo kama kupendelea timu fulani ya michezo vyaweza kusababisha mapambano ya kijeuri.

      Kwa Nini Kuna Ujeuri Mwingi Sana?

      Lakini ni kwa nini uadui huo huonyeshwa kwa njia za kijeuri? Wachunguzi wamechunguza masuala hayo kwa undani lakini bado wanatoa makisio tu. Clark McCauley alitayarisha orodha ndefu ya utafiti kuhusu ujeuri na ugomvi wa wanadamu. Yeye anukuu uchunguzi mmoja uliochapishwa unaosema kwamba “uhalifu wa kijeuri hutokea wakati wa vita na baada ya ushindi.” Wachunguzi hao waligundua kwamba “mataifa yaliyoshiriki katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu na Vita ya Pili ya Ulimwengu, hasa mataifa yaliyoshinda, yamekuwa na visa vingi vya mauaji baada ya vita hivyo.” Kulingana na Biblia, twaishi katika kipindi cha vita. (Mathayo 24:6) Je, yawezekana kwamba vita hivyo vimechangia kwa njia fulani ongezeko la ujeuri wa aina nyingine?

      Wachunguzi wengine wanatafuta sababu ya kibiolojia inayosababisha ugomvi wa wanadamu. Uchunguzi mmoja uliofanywa ulidokeza kwamba ugomvi mwingine husababishwa na “viwango vidogo vya kemikali ya serotonin katika ubongo.” Dokezo jingine linalojulikana sana ni kwamba ugomvi u katika chembe zetu za urithi. Mtaalamu mmoja wa siasa alisema kwamba “huenda sehemu kubwa ya [chuki] ni ile tuliyorithi.”

      Biblia yenyewe yasema kwamba wanadamu wasiokamilika wamezaliwa wakiwa na tabia mbaya na kasoro. (Mwanzo 6:5; Kumbukumbu la Torati 32:5) Kwa wazi, maneno hayo yanawahusu wanadamu wote. Lakini si wanadamu wote wanaochukia wengine isivyofaa. Watu hujifunza kuchukiana. Hivyo, mwanasaikolojia maarufu, Gordon W. Allport, alitambua kwamba vitoto vichanga ‘havina mwelekeo mkubwa wa kuharibu vitu. . . . Mtoto huwa na maoni mazuri, naye hukaribia kila kitu kinachompendeza na kila mtu.’ Mambo kama hayo yaonyesha kwamba ugomvi, ubaguzi, na chuki ni tabia ambazo watu hujifunza! Uwezo huo wa kujifunza chuki hutumiwa kwa urahisi na watu wanaoeneza chuki.

      Kufisidi Akili

      Wanaofanya hivyo hasa ni viongozi wa magenge mbalimbali yanayoeneza chuki, kama vile genge linalofuata sera za Nazi linalonyoa kipara na genge la Ku Klux Klan. Magenge hayo huwachochea hasa vijana wanaovutiwa na mambo kwa urahisi ambao wanatoka kwenye familia zenye matatizo ili wajiunge nao. Huenda vijana wasiojiamini na wanaohisi kuwa hawafai wakaona kwamba magenge ya kueneza chuki yanawafanya wapendwe.

      Njia moja ambayo imetumiwa na watu fulani kueneza chuki sana kwa matokeo ni Internet. Kwa mujibu wa hesabu iliyochukuliwa hivi karibuni, kuna vituo 1,000 kwenye Internet vya kueneza chuki. Gazeti la The Economist lilimnukuu mmiliki mmoja wa kituo cha Internet cha kueneza chuki akijigamba hivi: “Internet imetupa fursa ya kuwasilisha maoni yetu kwa mamia ya maelfu ya watu.” Kituo chake cha Internet kina “Sehemu ya Watoto.”

      Matineja wanapotafuta muziki kwenye Internet, wanaweza kupata vituo vinavyosambaza muziki unaoeneza chuki. Muziki wa aina hiyo huchezwa kwa sauti kubwa na ni wa kijeuri, ukiwa na maneno yanayopitisha ujumbe mkali wa kubagua jamii fulani. Vituo hivyo vya Internet huunganisha watu na vikundi vinavyozungumzia habari, sehemu za kupigia gumzo, au vituo vingine vinavyoeneza chuki.

      Vituo fulani vya Internet vya kueneza chuki huwa na sehemu maalum kwa ajili ya michezo na mambo mengine ya vijana. Kituo kimoja cha Internet cha genge linalofuata sera za Nazi hujaribu kutumia Biblia ili kutetea ubaguzi wa kijamii na wa Wayahudi. Vilevile, genge hilo limefungua kituo cha Internet chenye mafumbo ya kujaza maneno yaliyo na maelezo ya ubaguzi wa kijamii. Lengo ni nini? “Ili kuwasaidia vijana Wazungu wafahamu mambo tunayopigania.”

      Lakini, watu wengine wanaoeneza chuki si washiriki wa magenge yanayoshikilia maoni ya ubaguzi. Mwanasosiolojia mmoja aliyeandika kuhusu mapambano yaliyotokea hivi karibuni katika nchi za Balkani alisema hivi kuhusu waandishi fulani wanaoheshimiwa na pia watu fulani wenye uvutano katika jamii: “Nilishangaa ku[wa]ona wakiandika kwa njia inayowapendeza wananchi wenzao wenye maadili yaliyopotoka, njia inayochochea chuki yao kali, inayovuruga kufikiri kwao kwa kuwahimiza wasione kuwa kitu chochote kimekatazwa . . . , na kupotosha ukweli.”

      Kwa habari hii, hatupaswi kusahau fungu la makasisi. Katika kitabu chake Holy Hatred: Religious Conflicts of the ‘90’s, mwandishi James A. Haught asema jambo hili linaloshtua: “Jambo la kushangaza katika miaka ya 1990 ni kwamba dini—inayopaswa kuwa yenye fadhili na kuwahangaikia wanadamu—imekuwa chanzo kikuu cha chuki, vita, na ugaidi.”

      Basi, vyanzo vya chuki ni vingi na vyahusisha mambo mengi. Je, hiyo yamaanisha kwamba wanadamu hawana njia ya kuacha upumbavu wa kuchukiana ambao umekuwepo sana katika historia yao? Je, kuna jambo lolote linaloweza kufanywa na watu mmoja-mmoja na vilevile watu wote ulimwenguni ili kujitahidi kukomesha kutoelewana, kutojua, na woga unaosababisha chuki?

      [Blabu katika ukurasa wa 6]

      Ubaguzi na chuki ni tabia ambazo watu hujifunza!

      [Picha katika ukurasa wa 4, 5]

      Hatukuzaliwa na . . .

      . . . hisia za chuki na ubaguzi

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Vikundi vinavyoeneza chuki vinatumia Internet ili kuwavutia vijana wajiunge nao

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Mara nyingi, dini imechochea mapambano

      [Hisani]

      AP Photo

  • Kukomesha Chuki
    Amkeni!—2001 | Agosti 8
    • Kukomesha Chuki

      ‘Pendeni maadui wenu.’—MATHAYO 5:44.

      KWA siku kadhaa viongozi wawili wa mataifa yanayozozana walifanya mashauri ya amani. Rais wa nchi yenye uwezo iliyositawi kiviwanda alikuwepo kwenye mashauri hayo akijaribu kuwapatanisha viongozi hao wawili kwa kutumia mamlaka yake na ustadi wake wa kushughulika na watu. Lakini jitihada hizo zilisababisha matatizo mengi zaidi. Baada ya majuma kadhaa mataifa hayo mawili yalihusika katika ule ambao gazeti la Newsweek lilitaja kuwa “ujeuri mbaya zaidi kati yao katika kipindi cha miongo miwili.”

      Kotekote ulimwenguni, chuki na uhasama kati ya vikundi mbalimbali vya kikabila na kitaifa haikomi, licha ya jitihada nyingi za viongozi wa mataifa. Chuki huongezeka sana kwa kuchochewa na kutojua, ubaguzi, na habari za uwongo. Lakini, huku viongozi wanapojaribu kutafuta masuluhisho mapya pasipo kufua dafu, wao hukosa kung’amua kwamba suluhisho bora kabisa ni la kale—la kale kama Mahubiri ya Mlimani. Katika mahubiri hayo, Yesu Kristo aliwatia moyo wasikilizaji wake wafuate njia za Mungu. Katika mahubiri hayo alitoa taarifa iliyonukuliwa juu, yaani, ‘Pendeni maadui wenu.’ Shauri hilo ndilo suluhisho bora la chuki na ubaguzi na ndilo suluhisho pekee lenye matokeo!

      Watu wenye kutia shaka huona kumpenda adui kuwa wazo bure lisiloweza kutumika. Hata hivyo, ikiwa watu hujifunza kuchukiana, si ni jambo la akili kusema kwamba wanaweza kujifunza kutochukiana? Basi, maneno ya Yesu yanawapa wanadamu tumaini hakika. Yanaonyesha kwamba inawezekana kuacha hata uhasama wa muda mrefu.

      Fikiria hali ilivyokuwa katika siku za Yesu kati ya wasikilizaji wake Wayahudi. Hawakuhitaji kwenda mbali ili kuwa na maadui. Majeshi ya Roma yalitawala eneo lao, yakiwatoza Wayahudi kodi nyingi, kuwadhibiti kisiasa, kuwadhulumu, na kuwatumia ovyoovyo. (Mathayo 5:39-42) Hata hivyo, yamkini hata wengine wangewaona Wayahudi wenzao kuwa maadui kwa sababu ya kuruhusu tofauti ndogondogo zikue badala ya kuzisuluhisha. (Mathayo 5:21-24) Je, kweli Yesu angewatazamia wasikilizaji wake wawapende watu ambao waliwaumiza?

      Maana ya “Upendo”

      Kwanza, tambua kwamba Yesu aliposema juu ya “upendo” hakumaanisha shauku kati ya marafiki wa karibu. Neno la Kigiriki lililotumiwa kwenye Mathayo 5:44 kwa ajili ya upendo latokana na neno a·gaʹpe. Neno hilo lamaanisha upendo unaoongozwa au kuelekezwa na kanuni. Si lazima uhusishe shauku changamfu. Kwa kuwa unaongozwa na kanuni ya uadilifu, upendo huo humchochea mtu kufanya mambo yanayowapendeza wengine haidhuru wana tabia gani. Basi upendo wa a·gaʹpe waweza kushinda uadui. Yesu mwenyewe alionyesha upendo wa aina hiyo kwani hakuwatukana maaskari Waroma waliomtundika. Badala yake, alisali hivi: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui wanalofanya.”—Luka 23:34.

      Je, twaweza kutarajia kwamba watu wote ulimwenguni watakubali na kufuata mafundisho ya Yesu na kwamba wataanza kupendana? La, kwa kuwa Biblia huonyesha kwamba ulimwengu huu utaendelea kutumbukia kwenye msiba. Andiko la 2 Timotheo 3:13 latabiri kwamba “watu waovu na walaghai wataendelea kutoka ubaya hadi ubaya zaidi.” Hata hivyo, watu mmoja-mmoja wanaweza kuacha chuki kwa kujifunza kabisa kanuni za uadilifu kupitia funzo la Biblia. Mambo ya hakika yanaonyesha wazi kwamba watu wengi wamejifunza kuacha chuki inayowazunguka. Fikiria mifano kadhaa ya kweli.

      Kujifunza Kupenda

      Alipokuwa na umri wa miaka 13, José alihusika katika vita vya kuvizia akiwa mshiriki wa kikundi cha ugaidi.a Alifunzwa kuwachukia watu walioshukiwa kuwa walisababisha dhuluma alizoona. Lengo lake lilikuwa kuwaua ikiwezekana. Kwa kuwaona waandamani wake wengi wakifa, José alihisi uchungu sana na akataka sana kulipiza kisasi. Alipokuwa akitengeneza makombora, alijiuliza hivi, ‘Kwa nini kuna kuteseka kwingi? Ikiwa kuna Mungu, kwani hata haoni?’ Alilia mara nyingi, akavurugika na kushuka moyo.

      Hatimaye, José alifika kwenye kutaniko moja la karibu la Mashahidi wa Yehova. Kwenye mkutano wake wa kwanza, alitambua mara moja upendo uliokuwepo. Kila mtu alimsalimu kwa uchangamfu na kwa urafiki. Baadaye, mazungumzo juu ya kichwa “Sababu Gani Mungu Huruhusu Uovu?” yalijibu maswali yaleyale aliyokuwa ameuliza.b

      Muda si muda, ujuzi zaidi wa Biblia ulimsukuma José kubadili maisha yake na kufikiri kwake. Alijifunza kwamba ‘yeye ambaye hapendi hukaa katika kifo. Kila mtu ambaye huchukia . . . ni muua-binadamu-kikatili na . . . hakuna muua-binadamu-kikatili aliye na uhai udumuo milele ukikaa katika yeye.’—1 Yohana 3:14, 15.

      Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake kuwaacha washiriki wenzake magaidi. Kila mara alipoenda kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova, alifuatwa. Baadhi ya washiriki wake wa zamani hata walihudhuria mikutano michache ili kuelewa kilichomfanya José abadilike. Baada ya kutosheka kwamba hakuwa msaliti au hangewaletea matatizo, walimwacha. José alibatizwa alipokuwa na umri wa miaka 17, akawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Punde si punde, akawa mhubiri wa wakati wote. Sasa, badala ya kupanga njama za kuwaua watu, yeye huwapelekea ujumbe wa upendo na tumaini!

      Kuacha Ukabila

      Je, watu wa makabila mbalimbali wanaweza kukomesha chuki inayowatenganisha? Fikiria mfano wa kikundi cha Mashahidi wa Yehova huko London, Uingereza, wanaozungumza Kiamhara. Kikundi hicho kina watu 35—Waethiopia 20 na Waeritrea 15. Wao huabudu pamoja kwa amani na umoja licha ya kwamba katika Afrika, Waeritrea na Waethiopia walipigana vita kali hivi majuzi.

      Shahidi mmoja Mwethiopia aliambiwa hivi na washiriki wengine wa familia yake: ‘Usiwaamini kamwe Waeritrea!’ Lakini sasa, zaidi ya kuwaamini Wakristo wenzake Waeritrea, yeye huwaita ndugu na dada! Ijapokuwa kwa kawaida Waeritrea hao huzungumza lugha ya Kitigrinya, waliamua kujifunza Kiamhara—lugha ya ndugu zao Waethiopia—ili wajifunze Biblia pamoja nao. Ni ushuhuda mzuri kama nini unaoonyesha nguvu ya upendo wa kimungu ukiwa “kifungo kikamilifu cha muungano”!—Wakolosai 3:14.

      Kusahau Yaliyopita

      Lakini vipi ikiwa mtu alitendewa ukatili? Si ni jambo la kawaida kuwachukia watu waliotenda ukatili huo? Fikiria mfano wa Manfred, Shahidi mmoja kutoka Ujerumani. Alifungwa kwa miaka sita katika gereza la Kikomunisti eti kwa sababu tu alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Je, aliwahi kuwachukia waonezi wake au kutaka kulipiza kisasi? “La,” yeye alijibu. Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la Saarbrücker Zeitung, Manfred alisema hivi: “Kudhulumu au kulipiza kisasi kwa sababu ya dhuluma . . . hutokeza dhuluma nyingine.” Manfred alitumia kabisa maneno haya ya Biblia: “Msirudishe ovu kwa ovu kwa yeyote. . . . Ikiwezekana, kwa kadiri itegemeavyo nyinyi, iweni wenye kufanya amani na watu wote.”—Waroma 12:17, 18.

      Ulimwengu Usio na Chuki!

      Mashahidi wa Yehova hawadai kuwa wakamilifu kwa habari hii. Mara nyingi wao huona kwamba kuacha uadui na chuki si jambo rahisi. Jitihada zenye kuendelea zinahitajiwa ili kutumia kanuni za Biblia maishani. Lakini kwa ujumla, Mashahidi wa Yehova ni mfano unaoonyesha jinsi Biblia ilivyo na nguvu za kukomesha chuki. Kupitia programu ya kujifunza Biblia nyumbani, kila mwaka Mashahidi wanawasaidia maelfu ya watu kuacha kabisa ubaguzi wa rangi.c (Ona sanduku “Shauri la Biblia Husaidia Kumaliza Chuki.”) Mafanikio hayo yanaonyesha tu kimbele matokeo ya programu ya elimu ya ulimwenguni pote ambayo hivi karibuni itasaidia kumaliza kabisa chuki na vyanzo vyake. Programu hiyo ya elimu ya wakati ujao itaelekezwa na Ufalme wa Mungu, au serikali yake ya ulimwenguni pote. Yesu alitufundisha kusali kwa ajili ya Ufalme huo katika ile Sala ya Bwana, aliposema hivi: “Acha ufalme wako uje.”—Mathayo 6:9, 10.

      Biblia yaahidi kwamba chini ya mwelekezo wa serikali hiyo ya kimbingu, “dunia itajawa na kumjua BWANA.” (Isaya 11:9; 54:13) Kisha, maneno haya ya nabii Isaya yanayonukuliwa mara nyingi yatatimizwa ulimwenguni pote: “[Mungu] atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” (Isaya 2:4) Hivyo, Mungu mwenyewe atakomesha chuki kabisa.

      [Maelezo ya Chini]

      a Si jina lake.

      b Ona sura ya 8, “Sababu Gani Mungu Huruhusu Kuteseka?” katika kitabu Ujuzi Uongozao Kwenye Uhai Udumuo Milele, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

      c Mpango waweza kufanywa kwa ajili ya funzo la Biblia la nyumbani bila malipo kwa kuwasiliana na Mashahidi wa Yehova walio karibu nawe au kwa kuwaandikia wachapishaji wa gazeti hili.

      [Sanduku katika ukurasa wa 11]

      Shauri la Biblia Husaidia Kumaliza Chuki

      ● “Vita vyatokana na chanzo gani na mapigano miongoni mwenu yatokana na chanzo gani? Je, si kutoka katika chanzo hiki, yaani, kutokana na tamaa zenu za kufurahisha hisi za mwili ambazo huendeleza pambano katika viungo vyenu?” (Yakobo 4:1) Mikwaruzano yaweza kumalizwa tukijifunza kudhibiti tamaa za ubinafsi.

      ● “[Fulizeni] kuangalia, si masilahi ya kibinafsi ya mambo yenu wenyewe tu, bali pia masilahi ya kibinafsi yale ya wengine.” (Wafilipi 2:4) Kutanguliza masilahi ya wengine kabla ya masilahi yetu wenyewe ni njia nyingine ya kumaliza mikwaruzano isiyo ya lazima.

      ● “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.” (Zaburi 37:8) Twaweza na twapaswa kudhibiti hasira.

      ● “Mungu . . . alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” (Matendo 17:24, 26) Si jambo la akili kujiona kuwa bora zaidi ya watu wa rangi tofauti, kwani sisi sote ni washiriki wa familia moja ya wanadamu.

      ● ‘Msifanye jambo lolote kwa ugomvi au kwa majisifu ya bure, bali kwa hali ya akili ya kujishusha chini mkifikiria kwamba wengine ni wakubwa kuliko nyinyi.’ (Wafilipi 2:3) Ni upumbavu kuwadharau wengine—kwa kuwa watu wengine wana sifa nzuri na vipawa ambavyo sisi wenyewe hatuna. Hakuna jamii wala utamaduni unaofanya mambo yote vizuri.

      ● “Basi, kwa kweli maadamu tuna wakati wenye kufaa kwa ajili ya hilo, acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote.” (Wagalatia 6:10) Kuwa mwenye urafiki na kuwasaidia wengine bila kujali jamii au utamaduni wao, kwaweza kuziba pengo la mawasiliano na kumaliza kutoelewana.

      [Picha katika ukurasa wa 9]

      Mashahidi Waethiopia na Waeritrea huabudu pamoja kwa amani

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Manfred, aliyeokoka gereza la Kikomunisti, alikataa kuchukia watu kabisa

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Biblia yaweza kusaidia kuondoa vikwazo vinavyowatenganisha watu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki