-
Kuchunguza Matibabu ya AsiliAmkeni!—2000 | Oktoba 22
-
-
Matibabu ya Mitishamba
Yaelekea kwamba matibabu haya ndiyo yanayopendwa sana kati ya matibabu yote ya asili. Licha ya kwamba mitishamba imetumiwa kwa matibabu kwa karne nyingi, ni mimea michache sana ambayo imechunguzwa kwa uangalifu na wanasayansi. Ni mimea michache sana na bidhaa zake ambazo zimechunguzwa sana hivi kwamba usalama na uwezo wake wa kuponya umethibitishwa. Habari zilizo nyingi kuhusu mitishamba hutegemea matokeo ya matumizi ya kale.
Lakini katika miaka ya majuzi, kumekuwako na uchunguzi kadhaa wa kisayansi unaoonyesha umuhimu wa mitishamba fulani katika kutibu matatizo kama vile mshuko-moyo wa kiasi, kupoteza kumbukumbu kwa sababu ya uzee, na dalili za uvimbe hafifu wa tezi-kibofu. Mtishamba mmoja uliochunguzwa ni black cohosh, ambao nyakati nyingine huitwa black snakeroot, bugbane, au rattleroot. Wahindi Wekundu walichemsha mizizi yake na kuitumia kuhusiana na matatizo ya hedhi na uzazi. Kwa mujibu wa gazeti la Harvard Women’s Health Watch la Aprili 2000, uchunguzi wa hivi karibuni unadokeza kwamba bidhaa ya black cohosh ya Ujerumani ambayo inauzwa madukani inaweza “kutuliza dalili za koma-hedhi.”
Yaonekana kwamba uhitaji mkubwa wa matibabu hayo ya kiasili hutegemea dhana ya kwamba ni salama kuliko madawa ya kemikali. Ijapokuwa hilo laweza kuwa kweli mara nyingi, mitishamba fulani ina athari mbaya, hasa inapotumiwa pamoja na madawa mengine. Kwa mfano, mtishamba unaojulikana sana ambao unasifiwa kuwa tiba ya kiasili ya mvilio wa damu na ya kupunguza uzito wa mwili unaweza kuzidisha shinikizo la damu na mpigo wa moyo.
Pia kuna mitishamba ambayo humfanya mgonjwa avuje damu nyingi zaidi. Endapo mitishamba hiyo itatumiwa pamoja na madawa ya kitiba ya “kuifanya damu iwe nyepesi,” basi hali hatari yaweza kuzuka. Watu wenye magonjwa ya kudumu, kama vile ugonjwa wa sukari au shinikizo la damu, au wale wanaotumia madawa mengine wapaswa kujihadhari kuhusu kutumia mitishamba.—Ona sanduku lililoonyeshwa.
Hangaiko jingine kuhusu mitishamba ni ukosefu wa uhakikishio wa usafi katika kutengeneza bidhaa hizo. Katika miaka ya karibuni kumekuwako na ripoti za bidhaa zilizochanganywa na metali nzito na vitu vingine vyenye sumu. Kwa kuongezea, bidhaa nyingine za mitishamba zimegunduliwa kuwa na vitu vichache au hata kukosa vitu vyote vilivyotajwa kwenye kibandiko chake. Mifano hiyo yakazia uhitaji wa kununua bidhaa za mitishamba, vilevile bidhaa zozote za afya, kutoka kwa vyanzo vinavyojulikana na vinavyotegemeka.
-
-
Kuchunguza Matibabu ya AsiliAmkeni!—2000 | Oktoba 22
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Kuchanganya Mitishamba na Madawa—KUNA HATARI ZIPI?
Mara kwa mara watu wameonywa dhidi ya kuchanganya madawa au kuyatumia pamoja na vileo. Je, kuna hatari pia kutumia mitishamba fulani pamoja na madawa ya kitiba? Zoea hilo limeenea kadiri gani?
Makala moja katika jarida la The Journal of the American Medical Association iliripoti juu ya “matumizi ya madawa ya kitiba pamoja na mitishamba.” Ilisema hivi: “Kati ya asilimia 44 ya watu wazima waliosema kwamba walitumia kwa kawaida madawa ya kitiba, takriban mtu 1 (asilimia 18.4) kati ya watu 5 alikiri kutumia angalau dawa 1 ya mitishamba, kibonge chenye vitamini nyingi, au vyote viwili.” Ni muhimu kujua hatari ziwezazo kusababishwa na zoea hilo.
Wale wanaotumia madawa fulani ya mitishamba wanapaswa kuwa na tahadhari wapatapo matibabu yanayohitaji unusukaputi. Dakt. John Neeld, msimamizi wa Shirika la Amerika la Wataalamu wa Unusukaputi alieleza hivi: “Watu fulani wameripoti kwamba mitishamba fulani inayopendwa sana, kama vile ginseng na St. John’s wort, yaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya shinikizo la damu. Hilo laweza kuwa hatari sana wakati wa unusukaputi.”
Daktari huyo akaongezea kusema: “Mitishamba mingine kama vile ginkgo biloba, tangawizi na feverfew, yaweza kuvuruga kuganda kwa damu, na kuzusha hatari kubwa sana wakati wa tiba ya unusukaputi wa ngozi ya nje inayofunika ubongo na ya mshipa mkuu wa ufahamu katika uti wa mgongo—iwapo damu inavuja karibu na uti wa mgongo, yaweza kumfanya mgonjwa apooze. Mtishamba wa St. John’s wort waweza pia kuzidisha athari za madawa fulani ya kulevya au madawa ya unusukaputi.”
Kwa wazi, ni muhimu sana kujua hatari iwezayo kukupata unapotumia mchanganyiko wa mitishamba fulani na madawa. Wanawake wajawazito na wale wanyonyeshao wapaswa hasa kujihadhari na madhara yawezayo kuwapata watoto wao wachanga kwa sababu ya mchanganyo wa mitishamba fulani na madawa. Hivyo basi, wagonjwa wanatiwa moyo kuzungumza na madaktari wao kuhusu madawa wanayotumia, yawe ya asili au yasiyo ya asili.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mitishamba fulani imesaidia sana kutibu matatizo ya afya
“Black cohosh”
“Saint-John’s-wort”
[Hisani]
© Bill Johnson/Visuals Unlimited
-