-
Herode Mkuu—Mjenzi StadiAmkeni!—2009 | Septemba
-
-
Mradi mwingine wenye kustaajabisha ulikuwa ujenzi wa jumba la kifalme lenye ngome linaloitwa Herodium, lililojengwa kwenye mlima ulioinuka ambao ulikuwa karibu kilomita 5 kusini mashariki ya Bethlehemu. Jumba hilo lilikuwa na sehemu mbili kuu: Herodium ya Juu na Herodium ya Chini. Sehemu ya juu ya ilikuwa na jumba la kifalme lililojengwa kama ngome lililokuwa na mnara wenye orofa tano upande wa mashariki ambalo wakati mmoja lilikuwa jengo refu zaidi katika eneo hilo lakini sasa ni magofu. Miaka miwili iliyopita vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa viliripoti kwamba magofu ya kaburi la Herode yaligunduliwa katika miteremko ya Herodium, na vilisema kwamba hilo lilithibitisha ripoti ya Yosefo wa karne wa kwanza kwamba kulikuwa na msafara wa mazishi ya Herode hapo.
Wakati mmoja, kulikuwa na ofisi na majengo mengine madogo kando ya jumba la kifalme la Herodium ya Chini. Katikati kulikuwa na bustani ya Kiroma iliyopambwa kwa nguzo na iliyozunguka bwawa kubwa lililokuwa na kisiwa bandia katikati. Bwawa hilo lilikuwa na ukubwa karibu maradufu wa bwawa la kisasa la Olimpiki. Bwawa hilo lilitumiwa hasa kama hifadhi ya maji, lakini pia lilikuwa bwawa la kuogelea na hata kuendesha mashua. Maji yaliingia kwenye bwawa hilo kupitia mfereji uliotoka kwenye chemchemi iliyokuwa umbali wa kilomita 5.
Miaka kadhaa iliyopita, mtu fulani aliyetembelea eneo hilo alisema hivi kuhusu mandhari yake: “Upande wa mashariki, ungeweza kuona eneo lote hadi Bahari ya Chumvi. Mbele yetu kulikuwa na nyika ya Yudea ambapo huenda ndipo Daudi alijificha kutoka kwa Sauli, aliyekuwa akimsaka. Tulipotazama eneo hilo lililojaa mawe, tulielewa jinsi Daudi angeweza kujificha hapo hasa tukizingatia kwamba alilijua eneo hilo vizuri tangu ujana wake. Pia tuliwazia kwamba alipokuwa akilisha kondoo wake, huenda mara kwa mara Daudi alipanda mlima huo ili atazame mandhari nzuri tuliyokuwa tukiitazama.”
-
-
Herode Mkuu—Mjenzi StadiAmkeni!—2009 | Septemba
-
-
[Picha katika ukurasa wa 26]
“HERODIUM”
Mchoro wa msanii
-