Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Utekaji-nyara—Shughuli ya Tufeni Pote
    Amkeni!—1999 | Desemba 22
    • Utekaji-nyara—Shughuli ya Tufeni Pote

      KATIKA mwongo uliopita, kumekuwa na ongezeko kubwa sana katika visa vya utekaji-nyara ulimwenguni pote. Ripoti moja yasema kwamba kati ya 1968 na 1982, takriban mateka elfu moja walichukuliwa katika nchi 73. Lakini katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1990, watu wanaokadiriwa kuwa 20,000 hadi 30,000 walitekwa nyara kila mwaka.

      Utekaji-nyara ni uhalifu ambao unazidi kupendwa na wahalifu tufeni pote, huku watekaji-nyara wakiwa tayari kuteka kiumbe chochote kilicho hai. Katika pindi moja mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja tu alitekwa nyara. Katika Guatemala mwanamke mwenye umri wa miaka 84 akiwa katika kiti cha magurudumu alitekwa nyara na kuzuiliwa kwa miezi miwili. Katika Rio de Janeiro, wahalifu wa mitaani wananyakua watu moja kwa moja barabarani, nyakati nyingine wakidai fidia ya kiasi kidogo kama dola 100 za Marekani.

      Hata wanyama hawako salama. Miaka kadhaa iliyopita wahalifu shupavu huko Thailand waliteka nyara tembo mwenye uzito wa tani sita anayetumiwa kufanya kazi na kudai fidia ya dola 1,500. Magenge ya uhalifu katika Mexico yanasemekana kwamba yanawatia moyo washiriki wake wachanga wajizoeze kuteka nyara wanyama vipenzi na wanyama wa kufugwa kabla ya kuwateka nyara wanadamu.

      Zamani, watekaji-nyara walilenga hasa matajiri, lakini mambo yamebadilika. Ripoti moja kutoka kwa shirika la habari la Reuters yasema: “Utekaji-nyara unatukia kila siku katika Guatemala, ambako watu hukumbuka kwa upendo nyakati nzuri zilizopita ambapo waasi wa mrengo wa kushoto walilenga tu idadi ndogo ya matajiri. Sasa matajiri na maskini, wadogo kwa wakubwa, wanaweza kushambuliwa na magenge ya watekaji-nyara.”

      Visa vinavyojulikana na umma huelekezewa uangalifu mkubwa sana na vyombo vya habari, lakini kwa kiwango kikubwa visa vingi vya utekaji-nyara husuluhishwa bila kutangazwa. Kwa hakika, kwa sababu kadhaa, nchi “hazijishughulishi sana kutangaza tatizo la utekaji-nyara.” Makala ifuatayo itazungumzia sababu kadhaa kati ya hizo.

      [Ramani katika ukurasa wa 3]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      MEXICO

      Kukiwa na watu 2,000 wanaotekwa nyara kwa mwaka mmoja, utekaji-nyara umeitwa “biashara ndogo iliyopangwa.”

      UINGEREZA

      Bima ya utekaji-nyara katika kampuni ya Lloyd ya London imeongezeka kwa asilimia 50 kila mwaka tangu 1990.

      URUSI

      Katika eneo la Caucasus pekee lililo kusini mwa Urusi, idadi ya waliotekwa nyara iliongezeka kutoka 272 mwaka wa 1996 hadi 1,500 mwaka wa 1998.

      FILIPINO

      Kulingana na gazeti “Asiaweek,” “labda Filipino ndicho kituo cha utekaji-nyara cha Asia.” Kuna zaidi ya magenge 40 yaliyopangwa ya utekaji-nyara huko.

      BRAZILI

      Katika mwaka mmoja watekaji-nyara hapo waliripoti kuwa walipata kiasi kikubwa sana cha fedha ya fidia cha dola bilioni 1.2 za Marekani.

      KOLOMBIA

      Katika miaka ya karibuni maelfu ya watu wametekwa nyara kila mwaka. Katika Mei 1999, waasi waliteka nyara wakazi mia moja wa parokia wakati wa Misa.

      [Hisani]

      Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

  • Utekaji-nyara—Tisho la Kujifaidi Kifedha
    Amkeni!—1999 | Desemba 22
    • Utekaji-nyara—Tisho la Kujifaidi Kifedha

      “UTEKAJI-NYARA si kama uhalifu wa mali. Ni kitendo cha hila, ukatili na cha kutojali kikundi cha msingi zaidi cha kibinadamu, familia,” asema Mark Bles, katika kitabu chake The Kidnap Business. Utekaji-nyara husababisha msukosuko wa kihisia-moyo kwa washiriki wa familia. Kila dakika ipitayo na kila saa ipitayo, wanahisi wakiwa na tumaini, na mara wanakata tamaa wanapopambana na hisia za moyoni za hatia, chuki, na kutojiweza. Hali hiyo yenye kuogofya yaweza kuendelea kwa siku, majuma, miezi kadhaa au, nyakati nyingine hata miaka kadhaa.

      Katika utafutaji usiokoma wa fedha, watekaji-nyara hutumia hisia za familia ili kujifaidi. Kikundi cha watekaji-nyara kilimlazimisha mtekwa mmoja aandike mambo yafuatayo katika barua iliyochapishwa kwa ajili ya waandishi wa habari: “Nawaomba Waandishi wa Habari wachapishe habari hii kila mahali ili nisiporudi kosa litakuwa la watekaji-nyara lakini pia litakuwa la familia yangu ambayo inathibitika kuwa inapenda fedha zaidi kuliko mimi.” Watekaji-nyara wa Italia hudai kwa nguvu fedha za fidia kwa kukata sehemu za mwili na kuzipeleka kwa jamaa au kwenye vituo vya televisheni. Mtekaji-nyara wa Mexico hata aliwatesa wahasiriwa wake alipokuwa akijadiliana na familia zao kwa simu.

      Kwa upande mwingine, watekaji-nyara fulani hujaribu kupata upendeleo wa wahasiriwa wao. Kwa mfano, katika Filipino mwanabiashara aliyetekwa nyara aliwekwa kwenye hoteli ya anasa huko Manila, ambako watekaji wake walimpa kileo na kumtumbuiza na makahaba hadi fidia ilipolipwa. Hata hivyo, wahasiriwa wengi hufungiwa huku mahitaji yao ya kimwili au ya usafi wa kiafya yakipuuzwa. Wengi hutendwa kikatili. Kwa vyovyote vile, sikuzote lazima mhasiriwa apatwe na hofu ya kutaka kujua ni nini kitakachompata.

      Kukabiliana na Vurugu Hiyo

      Hata baada ya wahasiriwa kuachiliwa, huenda wakawa na makovu ya kihisia-moyo yatakayoendelea kwa muda. Muuguzi mmoja Msweden aliyetekwa nyara huko Somalia alitoa maoni haya: “Kuna jambo moja lililo la maana zaidi kuliko kitu kingine chochote. Lazima uongee na marafiki na jamaa zako na utafute msaada wa kitaalamu ikiwa unauhitaji.”

      Wanatiba wamebuni njia ya kusaidia wahasiriwa wa namna hiyo. Katika vipindi kadhaa vichache wahasiriwa huchanganua mambo yaliyowapata kwa msaada wa kitaalamu kabla ya kukutana na familia zao na kurudia maisha ya kawaida. “Tiba inayotolewa muda mfupi baada ya tukio hilo hupunguza hatari ya madhara ya kudumu,” asema Rigmor Gillberg, mtaalamu wa tiba ya kupambana na matatizo wa shirika la Msalaba Mwekundu.

      Matokeo Zaidi

      Si wahasiriwa na familia zao peke yao wanaoathiriwa na utekaji-nyara. Hofu ya kutekwa nyara inaweza kukomesha utalii na kupunguza vitega-uchumi; pia husababisha hali ya kutohisi usalama katika jamii. Katika miezi michache tu mwaka wa 1997, makampuni sita ya kimataifa yaliondoka Filipino kwa sababu ya tisho la utekaji-nyara. Mwanamke mmoja Mfilipino anayefanya kazi katika shirika linaloitwa Citizen Against Crime alisema hivi kwa mkazo: “Tunaishi katika hali yenye kutia hofu.”

      Makala moja katika The Arizona Republic yasema: “Miongoni mwa mameneja wa Mexico, hofu ya kutekwa nyara inakaribia kuwa isiyozuilika, kukiwa na sababu zifaazo.” Gazeti la Brazili Veja laripoti kwamba watekaji-nyara na wanyang’anyi wamechukua mahali pa madubwana katika ndoto zenye kuogofya za watoto wa Brazili. Huko Taiwan, somo la kuzuia utekaji-nyara hufundishwa shuleni, na huko Marekani, kamera za usalama zimewekwa katika shule za watoto wadogo ili kuzuia utekaji-nyara.

      Washauri wa Usalama Wapata Faida Kubwa

      Ongezeko la utekaji-nyara na masuala nyeti yanayohusiana nao yamesababisha kuongezeka haraka kwa mapato ya makampuni ya usalama. Katika jiji la Brazili la Rio de Janeiro, kuna makampuni kama hayo zaidi ya 500, yenye mapato ya dola bilioni 1.8 za Marekani.

      Idadi inayoongezeka ya makampuni ya kimataifa ya usalama hufundisha kujizuia na utekaji-nyara, huchapisha ripoti kuhusu maeneo hatari, na hujadili fidia. Yanashauri familia na makampuni, yakiwafundisha mbinu za watekaji-nyara na kuwasaidia wakabiliane kisaikolojia. Makampuni mengine hata hujaribu kuwakamata watekaji-nyara na kupata pesa za fidia baada ya mateka kuachiliwa. Hata hivyo, huduma zao hulipiwa.

      Licha ya jitihada hizo, visa vya utekaji-nyara vinaongezeka katika nchi nyingi. Akitoa maoni kuhusu jinsi hali ilivyo katika Amerika ya Latini, Richard Johnson, makamu msimamizi wa Seitlin & Company, asema: “Tunaweza kutarajia kwamba visa vya utekaji-nyara vitaongezeka.”

      Sababu Zinazochangia Ongezeko Hilo

      Wataalamu wanadokeza sababu kadhaa za ongezeko hilo la hivi karibuni. Moja ni kwamba hali ya kiuchumi imezorota katika maeneo fulani. Mfanyakazi mmoja wa huduma za kuandaa misaada katika mji wa Nal’chik, Urusi, alisema: “Njia bora ya kupata fedha ni kupitia utekaji-nyara ulio mashuhuri.” Katika zile zilizokuwa jamhuri za Sovieti, visa vya utekaji-nyara vinasemekana kuwa vinaandaa fedha kwa ajili ya majeshi ya kibinafsi ya mababe wa kivita wa sehemu hizo.

      Watu wengi wanafunga safari za kibiashara au za utalii kuliko wakati mwingine uliopita, hivyo wakitokeza fursa mpya kwa watekaji-nyara wanaotafuta mawindo. Idadi ya wageni waliotekwa nyara imeongezeka maradufu katika muda wa miaka mitano. Kati ya mwaka wa 1991 na 1997, watalii walitekwa nyara katika nchi 26.

      Watekaji-nyara hao wote hutoka wapi? Mapambano kadhaa ya kijeshi yanakwisha, yakifanya askari-jeshi wa zamani wakose kazi na fedha. Watu hao wana stadi zote za msingi zinazohitajika ili kufanya biashara hii yenye faida.

      Vivyo hivyo, hatua kali za kinidhamu dhidi ya wizi wa benki na ulanguzi wa dawa za kulevya zimesababisha wahalifu wageukie utekaji-nyara ukiwa njia badala ya kujipatia mapato. Mike Ackerman, mtaalamu wa utekaji-nyara, alieleza hivi: “Tunapofanya uhalifu kwa ajili ya mali uwe jambo gumu zaidi katika jamii zote, tunazidisha uhalifu dhidi ya watu.” Kutangaza hadharani malipo ya juu ya fidia kungeweza pia kuchochea watu wawezao kuwa watekaji-nyara.

      Nia Haiwi Ile Ile Sikuzote

      Watekaji-nyara wengi hutaka fedha, fedha peke yake. Madai ya fidia hutofautiana kutoka kiasi kidogo cha dola hadi fidia iliyovunja rekodi ya dola milioni 60 za Marekani zilizolipwa kwa ajili ya mfanya biashara tajiri wa Hong Kong ambaye hakuwahi kuachiliwa licha ya malipo hayo kutolewa.

      Kwa upande mwingine, watekaji-nyara fulani wametumia wahasiriwa wao ili wapate kutangazwa hadharani, wapate chakula, dawa, redio, magari na vilevile shule mpya, barabara, na hospitali. Meneja mmoja aliyetekwa nyara huko Asia aliachiliwa baada ya watekaji-nyara kupewa yunifomu za mpira wa kikapu na mipira. Vikundi fulani pia huteka nyara ili kutisha na kuogofya watega-uchumi wa kigeni na watalii, vikiwa na kusudi la kukomesha kutumiwa vibaya kwa ardhi na mali asili.

      Kwa hiyo kuna nia nyingi, njia nyingi za kutumiwa, na watu wengi wawezao kuwa watekaji-nyara au wahasiriwa. Je, utatuzi unapatikana kwa wingi? Ni nini baadhi ya utatuzi, na je, unaweza kutatua tatizo hilo? Kabla ya kujibu maswali hayo, acheni tuchunguze sababu nyingine kuu na za msingi za ongezeko katika biashara ya utekaji-nyara.

      [Sanduku katika ukurasa wa 5]

      Endapo Watekwa Nyara

      Wale ambao wamechunguza habari hiyo wanatoa madokezo yafuatayo kwa watu ambao huenda watekwe nyara.

      • Uwe mwenye ushirikiano; epuka tabia ya kuwa mkaidi. Mateka wanaoonyesha uadui mara nyingi hutendwa kikatili, na wanakabili hatari kubwa zaidi ya kuuawa au kutengwa na wengine ili kuadhibiwa.

      • Usihofu. Kumbuka kwamba wahasiriwa wengi huokoka utekaji-nyara.

      • Buni njia fulani ya kuhesabia wakati.

      • Jaribu kuwa na utaratibu fulani wa kila siku.

      • Fanya mazoezi, hata ingawa huenda usiwe na fursa za kutosha za kusonga huku na huko.

      • Uwe mwelekevu; jaribu kukumbuka mambo, sauti, na harufu. Fahamu mambo fulani kuhusu watu wanaokuteka nyara.

      • Piga gumzo ikiwezekana na jaribu kuanzisha mawasiliano. Ikiwa watekaji-nyara wanatambua sifa zako, hawataelekea kukudhuru au kukuua.

      • Wajulishe mahitaji yako kwa njia ya upole.

      • Usijaribu kamwe kujadili fidia yako.

      • Ukijikuta katikati ya jaribio la uokoaji, jilaze chini na kusubiri kwa utulivu tu mambo yanapoendelea.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Bima ya Utekaji-Nyara—Suala Linalobishaniwa

      Bima ni biashara inayokua haraka ambayo inahusiana na kuongezeka kwa visa vya utekaji-nyara. Kampuni ya bima ya Lloyd ya London imekuwa na ongezeko la asilimia 50 kila mwaka katika bima ya utekaji-nyara katika miaka ya 1990. Makampuni mengi yanazidi kutoa bima hiyo. Bima hiyo hushughulikia msaada wa mtu anayejadili utekaji-nyara, malipo ya fidia, na nyakati nyingine jitihada za wataalamu za kupata tena fidia hiyo. Hata hivyo, suala la bima linabishaniwa sana.

      Wapinzani wa bima ya utekaji-nyara hudai kwamba inafanya uhalifu huo uwe shughuli ya kibiashara na kwamba si jambo la kiadili kujifaidi kutokana utekaji-nyara. Pia wanasema kwamba mtu aliyekatiwa bima aweza kupuuza usalama wake mwenyewe na kwamba bima hiyo itafanya iwe rahisi kwa mtekaji-nyara kutwaa pesa kwa nguvu, hivyo kuendeleza uhalifu huo. Wengine hata wanahofu kwamba kuwepo kwa bima kutawatia watu moyo wapange kutekwa nyara ili wapate pesa za bima. Bima ya utekaji-nyara ni haramu katika Italia, Kolombia, na Ujerumani.

      Watetezi wa bima ya utekaji-nyara wanasema kwamba kama ilivyo na makampuni mengine ya bima, jambo hilo hufanya wengi walipie hasara ya watu wachache. Wanasababu kwamba bima hutokeza usalama wa kiasi fulani, kwa kuwa huwezesha familia na makampuni yaliyokatiwa bima yalipie huduma za wataalamu, wanaoweza kufanya hali isiwe mbaya zaidi, kujadili fidia ya kiasi kidogo, na kufanya iwe rahisi zaidi kuwashika watekaji-nyara.

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Tabia Isiyo ya Kawaida ya Stockholm

      Kutekwa nyara kwa Patty Hearst, mnamo mwaka wa 1974, aliyekuwa binti ya bilionea wa kampuni ya magazeti Randolph A. Hearst, kulichukua mwelekeo mpya alipoamua kujiunga na watekaji wake na kushiriki uhalifu wa kutumia silaha pamoja na kikundi hicho. Katika kisa kingine mcheza kandanda Mhispania aliyekuwa ametekwa nyara aliwasamehe watekaji wake na kuwatakia mema.

      Mapema katika miaka ya 1970, tukio hilo liliitwa Tabia Isiyo ya Kawaida ya Stockholm, baada ya tukio lenye kupendeza la utekaji-nyara mwaka wa 1973 kwenye benki moja huko Stockholm, Sweden. Kwenye pindi hiyo baadhi ya mateka hao walianzisha urafiki wa pekee pamoja na watekaji wao. Urafiki wa namna hiyo umekuwa ulinzi kwa mateka, kama ielezwavyo na kitabu Criminal Behavior: “Kadiri mhasiriwa na mtekaji wanavyojuana, ndivyo hupendana zaidi. Tukio hilo laonyesha kwamba baada ya muda fulani huenda mkosaji asimdhuru mateka.”

      Mhasiriwa mmoja Mwingereza huko Chechnya aliyebakwa alisema hivi: “Naamini kwamba mlinzi huyo alipofahamu sisi ni watu wa aina gani alitambua kwamba ilikuwa kosa kunibaka. Aliacha kunibaka na akaomba radhi.”

  • Utekaji-nyara—Sababu Zake za Msingi
    Amkeni!—1999 | Desemba 22
    • Utekaji-nyara—Sababu Zake za Msingi

      UTEKAJI-NYARA umekuwa pigo la kisasa. Lakini ndivyo ilivyo na ubakaji, wizi, kusumbua watoto kingono, na hata maangamizi ya jamii nzima-nzima. Kwa nini maisha yamekuwa hatari sana hivi kwamba mara nyingi watu wanaogopa kujasiria kutoka nje ya nyumba zao usiku?

      Sababu za msingi za kuenea kwa uhalifu, kutia ndani utekaji-nyara, zinahusiana na dosari zilizotia mizizi ndani ya jamii ya kibinadamu. Je, uling’amua kwamba yapata miaka 2,000 iliyopita, Biblia ilikuwa imetabiri nyakati hizi hatari? Tafadhali chunguza yaliyotabiriwa kwenye 2 Timotheo 3:2-5.

      “Watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, wenye kujitanguliza, wenye kiburi, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio waaminifu-washikamanifu, wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, wachongezi, wasio na hali ya kujidhibiti, wakali, wasio na upendo wa wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kututumuka kwa kiburi, wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu, wakiwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakithibitika kuwa si kweli kwa nguvu ya hiyo.”

      Labda unakubali kwamba maneno hayo yaliyorekodiwa muda mrefu uliopita yanafafanua kwa njia nzuri sana hali ya mambo leo. Katika muda wetu wa maisha dosari zimetokea katika jamii ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa kweli kweli. Jambo muhimu ni kwamba ufafanuzi ulio juu wa hali yenye kusikitisha ya mwenendo wa kibinadamu unatangulizwa katika Biblia kwa maneno: “Katika siku za mwisho nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zitakuwa hapa.” (2 Timotheo 3:1) Acheni tufikirie dosari kuu tatu za jamii ambazo zimechangia kuenea kwa utekaji-nyara.

      Matatizo ya Kutekeleza Sheria

      “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.”—Mhubiri 8:11.

      Vikosi vingi vya polisi havina vifaa vya kukabiliana na kuenea kwa uhalifu. Kwa hiyo katika nchi nyingi, utekaji-nyara umekuwa uhalifu ambao huleta pesa. Mnamo mwaka wa 1996, ni asilimia 2 tu ya watekaji-nyara wa Kolombia walioshtakiwa. Katika Mexico, angalau dola milioni 200 za Marekani zililipwa zikiwa fedha ya fidia mnamo mwaka wa 1997. Watekaji-nyara fulani katika Filipino wamekubali malipo ya fidia yafanywe kwa hundi.

      Kwa kuongezea, ufisadi miongoni mwa idara za kutekeleza sheria nyakati nyingine huzuia jitihada za kukabili uhalifu kwa njia yenye matokeo. Viongozi wa vikosi bora vya kukabiliana na utekaji-nyara katika Mexico, Kolombia, na katika zile zilizokuwa jamhuri za Sovieti wamelaumiwa kuwa watekaji-nyara. Katika gazeti Asiaweek, rais wa Bunge la Filipino, Blas Ople, asema kwamba tarakimu rasmi zaonyesha kuwa asilimia 52 ya visa vya utekaji-nyara katika Filipino huhusisha polisi wanaofanya kazi au waliostaafu au wanajeshi. Mtekaji-nyara sugu wa Mexico alisemekana kuwa alizingirwa na “ulinzi rasmi uliowezekana kwa kuwahonga maofisa na waendesha mashtaka wa manispaa, jimbo na serikali.”

      Umaskini na Ukosefu wa Haki wa Kijamii

      “Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo.”—Mhubiri 4:1.

      Watu wengi leo wako katika hali za kiuchumi na za kijamii zilizozorota, na mara nyingi wao ndio huhusika na utekaji-nyara. Kwa hiyo, katika ulimwengu ambamo pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kupanuka na ambamo mara nyingi ni vigumu sana kupata fedha kwa njia ya haki, kishawishi cha utekaji-nyara kitazidi kuwepo. Maadamu kuna uonevu, utekaji-nyara utakuwa njia ya kulipiza kisasi na kuelekeza uangalifu kwa hali inayoonwa kuwa isiyovumilika.

      Pupa na Ukosefu wa Upendo

      “Kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote.” (1 Timotheo 6:10) “Kwa sababu ya kuongezeka kwa uasi-sheria upendo wa idadi iliyo kubwa zaidi utapoa.”—Mathayo 24:12.

      Katika historia yote kupenda fedha kumefanya watu watende mambo ya kuchukiza sana. Na labda hakuna uhalifu mwingine ambao hutokeza faida za kifedha sawa na utekaji-nyara kwa kusababisha wanadamu wapatwe na maumivu makali, kihoro, na kukata tumaini. Kwa wengi ni pupa—kupenda fedha—ndiko huwachochea wamtendee kinyama mtu wasiyemjua na kumtesa na kuiletea familia yake masaibu kwa majuma kadhaa, miezi, na nyakati nyingine miaka kadhaa.

      Kwa wazi, kuna kasoro kubwa sana katika jamii inayokazia fedha na kupuuza maadili ya kibinadamu. Bila shaka, hali hiyo hutokeza hali zinazoendeleza kila aina ya uhalifu, kutia ndani utekaji-nyara.

      Je, hilo lamaanisha kwamba tuko katika zile zinazoitwa na Biblia “siku za mwisho”? Ikiwa ndivyo, jambo hilo litamaanisha nini kwa dunia na kwetu sisi? Je, kuna utatuzi kwa matatizo mabaya sana yanayokabili jamii ya kibinadamu, kutia ndani utekaji-nyara?

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

      Si Jambo Jipya

      Sheria ya Kimusa ilitoa adhabu ya kifo kwa watekaji-nyara huko nyuma katika karne ya 15 K.W.K. (Kumbukumbu la Torati 24:7) Julius Caesar alitekwa nyara ili kupata fidia katika karne ya kwanza K.W.K., ndivyo na Richard wa Kwanza, mfalme wa Uingereza mwenye Moyo Kama wa Simba, katika karne ya 12 W.K. Fidia kubwa zaidi iliyowahi kulipwa ilikuwa tani 24 za dhahabu na fedha ambazo Wainka walimpa mshindi Mhispania Francisco Pizzaro ili aachilie chifu wao mtekwa Atahuallpa katika mwaka wa 1533. Hata hivyo washindi hao walimnyonga hadi akafa.

  • Utekaji-nyara—Je, Kuna Utatuzi?
    Amkeni!—1999 | Desemba 22
    • Utekaji-nyara—Je, Kuna Utatuzi?

      “VISA vya utekaji-nyara vimefikia kiwango kisichoweza kuvumiliwa na taifa zima, na jamii nzima lazima ipambane na uovu huo,” ndivyo alivyosema kwa mkazo waziri mkuu wa Chechnya alipokuwa akiahidi kukomesha pigo hilo katika jamhuri yake iliyoko Urusi iliyokumbwa na visa vya utekaji-nyara.

      Kukomesha utekaji-nyara? Mradi huo ni wenye kusifika, lakini swali ni, Jinsi gani?

      Jitihada Zinazofanywa

      Wenye mamlaka wa Kolombia wameteua maajenti wa siri 2,000, waendesha mashtaka wa umma 24, na hata mratibu wa pekee wa kikundi cha kupambana na utekaji-nyara. Katika Rio de Janeiro, Brazili, maandamano ya hadharani yaliyokuwa yakipinga visa vingi vya utekaji-nyara jijini yalivutia takriban waandamanaji 100,000. Katika Brazili na Kolombia, vikundi vyenye hadhi ya kijeshi vimelipiza kisasi kwa kuteka nyara jamaa za watekaji-nyara. Na Wafilipino fulani wameamua kuchukua sheria mikononi—wamewachoma watekaji-nyara!

      Wenye mamlaka wa Guatemala walianzisha adhabu ya kifo kwa watekaji-nyara, naye rais akatuma jeshi ili kuzuia kuenea kwa utekaji-nyara. Katika Italia serikali ilianzisha hatua madhubuti za kuzuia utekaji-nyara, kwa kuharamisha malipo ya fidia na kutwaa fedha na mali ili kuzuia watu wa jamaa wasilipe. Wenye mamlaka wa Italia wanajisifu kwamba hatua hizo zimechangia kupungua kwa visa vya utekaji-nyara. Hata hivyo, wahakiki wanadokeza kwamba kama tokeo, familia hujaribu kusuluhisha kesi kwa siri na kwamba jambo hilo hupunguza idadi rasmi ya visa vya utekaji-nyara. Washauri wa kibinafsi wa usalama wanakadiria kwamba idadi ya visa vya utekaji-nyara katika Italia kwa kweli vimeongezeka maradufu tangu miaka ya 1980.

      Madokezo Mengi—Utatuzi Usiotosha

      Kwa familia nyingi ambazo watu wao wametekwa nyara, kuna utatuzi mmoja tu unaowezekana—kutoa dhamana kwa ajili ya wapendwa wao haraka iwezekanavyo. Lakini wataalamu wanaonya kwamba ikiwa kiasi cha fidia ni cha juu na kinalipwa haraka sana, huenda watekaji-nyara wakaona familia hiyo kuwa rahisi kushambuliwa na hurudi mara ya pili. Au wanaweza kuomba fidia ya pili kabla ya kumwachilia mhasiriwa.

      Familia fulani zimelipa fidia ya kiasi kikubwa na kugundua kwamba mhasiriwa alikuwa amekufa tayari. Kwa hiyo wataalamu wanasema kwamba mtu hapaswi kamwe kulipa fidia au kuanza majadiliano kabla hajapata uthibitisho kwamba mhasiriwa yuko hai. Uthibitisho huo ungeweza kuwa kwa kuuliza swali ambalo linaweza kujibiwa na mhasiriwa peke yake. Familia fulani huomba picha ya mhasiriwa akiwa amebeba gazeti la hivi karibuni.

      Vipi shughuli za uokoaji? Mara nyingi zinahusisha hatari kubwa. “Asilimia sabini na tisa ya mateka wote huuawa wakati wa majaribio ya uokoaji katika Amerika ya Latini,” asema Brian Jenkins, mtaalamu wa utekaji-nyara. Hata hivyo, nyakati fulani, uokoaji hufaulu.

      Haishangazi kwamba utatuzi mwingi hukazia kuzuia utekaji-nyara. Si wenye mamlaka wa serikali peke yao wanaohusika katika majaribio ya kuzuia utekaji-nyara. Magazeti hufunza watu namna wanavyoweza kuepuka kutekwa nyara, jinsi ya kuruka kutoka kwenye gari lililo mwendoni, na jinsi ya kutumia werevu na kuwashinda watekaji-nyara. Vituo vya kujifunzia judo na karate hutoa mafunzo ya kujilinda dhidi ya kutekwa nyara. Makampuni yanauza transmita ndogo sana za dola 15,000 za Marekani zinazoweza kuingizwa ndani ya meno ya watoto ili kusaidia polisi kuwasaka watoto endapo wanatekwa nyara. Kwa wale walio na fedha za kutosha, watengenezaji-magari hutengeneza magari “yasiyoweza kutekwa nyara” yenye vifaa vinavyotoa gesi ya kutoa machozi, matundu ya kurushia risasi, madirisha yasiyopenya risasi, magurudumu yasiyoweza kutobolewa, na vifaa vinavyotoa utando wa mafuta.

      Baadhi ya watu matajiri huona utatuzi unapatikana kwa kuwa na walinzi wa kibinafsi. Hata hivyo, kuhusu hali ilivyo huko Mexico, mtaalamu wa usalama Francisco Gomez Lerma asema: ‘Walinzi wa kibinafsi hawasaidii kwa sababu huvutia watekaji-nyara.’

      Tatizo la utekaji-nyara ni tata sana na mizizi yake imepenya ndani kabisa hivi kwamba hakuna jambo ambalo mwanadamu anaweza kufanya la kutosha ili kulikomesha. Basi, je, hakuna utatuzi halisi?

      Kuna Utatuzi

      Gazeti hili limetaja tena na tena utatuzi pekee wa matatizo hayo yote yanayokabili wanadamu. Utatuzi huo ni ule ambao Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, alitaja alipowafundisha wanafunzi wake wasali: “Acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.”—Mathayo 6:10.

      Kwa wazi, tunahitaji serikali ya ulimwengu yenye uadilifu ili kusimamia mambo ya watu wa namna mbalimbali duniani—naam, Ufalme wa Mungu ambao Yesu alisema juu yake. Kwa kuwa wanadamu wameshindwa kusimamisha serikali ya namna hiyo, ni hekima kwetu kumtegemea Muumba wetu, Yehova Mungu. Neno lake Biblia lasema kwamba alikusudia kufanya jambo hilihili.—Zaburi 83:18.

      Nabii Danieli alirekodi kusudi la Yehova, alipoandika: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele. . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” (Danieli 2:44) Biblia inaeleza jinsi serikali hii ya Mungu itakavyochukua hatua ili kukomesha uhalifu wote, kutia ndani utekaji-nyara.

      Elimu Inayofaa Ni Muhimu

      Bila shaka utakubali kwamba kukazia kanuni zinazofaa ndani ya watu ni muhimu ili kutatua tatizo la utekaji-nyara. Kwa mfano, fikiria wanadamu wangekuwaje ikiwa wote wangetii onyo hili la upole katika Biblia: “Acheni namna yenu ya maisha iwe bila upendo wa fedha, huku nyinyi mkiridhika na vitu vilivyopo.” (Waebrania 13:5) “Nyinyi watu msiwe mkiwiwa na yeyote hata jambo moja, ila kupendana.”—Waroma 13:8.

      Unaweza kupata mwono wa jinsi ambavyo maisha yangekuwa kwa kuchunguza programu ya elimu inayofanywa na Mashahidi wa Yehova katika nchi zaidi ya 230 duniani kote. Programu hiyo imeathiri watu wengi kwa njia ifaayo ambao zamani walikuwa wenye pupa au wahalifu hatari. Mtekaji-nyara mmoja wa hapo awali alisema hivi: “Baada ya muda niling’amua kwamba ili kumpendeza Mungu nilihitaji kuvua utu wangu wa kale na kuvaa utu mpya—ulio mpole na unaofanana na ule wa Kristo Yesu.”

      Lakini, hata programu nzuri ya elimu haitawabadili wahalifu wote, labda hata si wengi wao. Ni nini kitakachowapata wale wanaokataa kubadilika?

      Kuondolewa kwa Wakosaji

      Wakosaji wa kukusudia hawataruhusiwa wawe raia wa Ufalme wa Mungu. Biblia husema: “Je, hamjui kwamba watu wasio waadilifu hawatarithi ufalme wa Mungu? Msiongozwe vibaya. Wala waasherati, . . . wala watu wenye pupa, . . . wala wanyang’anyi hawataurithi ufalme wa Mungu.” (1 Wakorintho 6:9, 10) “Wanyofu watakaa katika nchi . . . Bali waovu watatengwa na nchi.”—Mithali 2:21, 22.

      Kulingana na Sheria ya Mungu katika nyakati za kale, mtekaji-nyara asiyetubu alipaswa kuuawa. (Kumbukumbu la Torati 24:7) Watu wenye pupa, kama vile watekaji-nyara, hawatakuwa na fungu lolote katika Ufalme wa Mungu. Wahalifu wa leo waweza kukwepa hukumu ya kibinadamu, lakini hawataweza kukwepa hukumu ya Mungu. Wakosaji wowote watalazimika kubadili njia zao ikiwa wataishi chini ya utawala wa uadilifu wa Ufalme wa Yehova.

      Bila shaka, ikiwa hali zinazochangia uhalifu zitabaki, ndivyo itakavyokuwa na uhalifu. Hata hivyo, Ufalme wa Mungu hautaruhusu jambo hilo litukie, kwa kuwa Biblia inaahidi: “Ufalme . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande,” kutia ndani watu wote wanaofanya mabaya. Unabii huo wa Biblia waendelea kusema kwamba Ufalme wa Mungu utasimama milele na milele. (Danieli 2:44) Ebu wazia mabadiliko yatakayotukia!

      Ulimwengu Mpya wa Uadilifu

      Fikiria unabii mwingine wa Biblia. Ni ule unaoeleza juu ya wakati ujao kwa maneno haya yenye kupendeza: “Nao watajenga nyumba na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.”—Isaya 65:21, 22.

      Ufalme wa Mungu utabadili sayari nzima. Wote walio hai watafurahia uhai kwa ukamili, wakisitawisha uwezo wao wa kiasili kwa kushiriki kazi inayoridhisha na tafrija yenye kujenga. Hali ulimwenguni pote zitakuwa kwamba hakuna mtu atakayefikiria kamwe kumteka nyara jirani yake. Kutakuwa na usalama kamili. (Mika 4:4) Hivyo, Ufalme wa Mungu utakuwa umekomesha kabisa utekaji-nyara hivi kwamba hakuna mtu atakayeufikiria tena.—Isaya 65:17.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki