-
Historia Je, Tuitumaini?Amkeni!—2001 | Machi 8
-
-
Historia Je, Tuitumaini?
“Kujua mambo yaliyopita hutufanya . . . tujione tukiwa sehemu ya jamii ambayo imekuwapo kwa miaka mingi kabla hatujazaliwa na itakayokuwapo baada ya kifo chetu.”—Kitabu A COMPANION TO THE STUDY OF HISTORY, CHA MICHAEL STANFORD.
KUTOJUA historia ni kutokuwa na kumbukumbu lolote maishani. Pasipo historia ni kana kwamba wewe, familia yako, kabila lako, au hata taifa lako halina asili, wala mwanzo. Matukio ya sasa hayangekuwa na msingi wala maana yoyote pasipo historia.
Historia yaweza kuwa na masomo muhimu sana maishani. Inaweza kutusaidia kuepuka kufanya makosa yaleyale kila mara. Mwanafalsafa mmoja alisema kwamba watu wanaosahau mambo yaliyopita hawana budi kuyarudia. Kufahamu historia kwaweza kutuelimisha kuhusu ustaarabu wa kale, ugunduzi wenye kustaajabisha, watu mashuhuri, na kutusaidia kuona mambo kwa njia mbalimbali.
Lakini kwa kuwa historia ni elimu inayohusiana na watu na matukio ya kale, tutajuaje iwapo inaweza kutumainiwa? Ikiwa tutajifunza masomo muhimu kutokana na historia, basi bila shaka ni sharti masomo hayo yategemee ukweli. Na tunapofahamu ukweli, tunapaswa kuukubali, japo huenda usipendeze nyakati zote. Mambo yaliyopita yanaweza kulinganishwa na bustani ya maua ya waridi—ni maridadi na pia ina miiba; inaweza kupendeza sana, na inaweza pia kudunga.
Katika makala zifuatazo, tutachunguza nyanja mbalimbali za historia ambazo zinaweza kutusaidia kuchanganua usahihi wa yale tunayosoma. Tutachunguza pia jinsi rekodi zenye kutegemeka za historia zinavyoweza kumnufaisha msomaji mwenye utambuzi.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Malkia Nefertiti
[Picha katika ukurasa wa 3]
Twaweza kujifunza masomo gani kutokana na historia?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Nefertiti: Ägyptisches Museum der Staatlichen Museen Preußischer Kulturbesitz, Berlin
Pambizoni: Photograph taken by courtesy of the British Museum
-
-
Twajifunza Nini Kutokana na Mambo Yaliyopita?Amkeni!—2001 | Machi 8
-
-
Twajifunza Nini Kutokana na Mambo Yaliyopita?
“Wanahistoria wanathamini sana ubainishaji wa kisababishi na matokeo.”—GERALD SCHLABACH, PROFESA-MSAIDIZI WA HISTORIA.
WANAHISTORIA huuliza hivi mara nyingi, Ni jinsi gani na kwa nini mambo fulani yalitukia? Kwa mfano, twajua kutokana na historia kwamba Milki ya Roma iliporomoka. Lakini kwa nini iliporomoka? Je, ni kwa sababu ya ufisadi au anasa? Je, ilikuwa vigumu mno kuongoza milki hiyo na gharama za kudumisha majeshi yake zikawa juu sana? Je, maadui wa Roma walikuwa wengi mno na wenye nguvu mno?
Hivi majuzi, Ukomunisti wa Ulaya Mashariki, ambao pindi moja ulikuwa tisho kwa nchi za Magharibi, uliporomoka kana kwamba kwa usiku mmoja nchi baada ya nchi. Lakini kwa nini? Na twaweza kujifunza masomo yapi? Hayo ni baadhi ya maswali ambayo wanahistoria hujaribu kujibu. Lakini wanapojibu maswali hayo, maamuzi yao huathiriwa na upendeleo kadiri gani?
Je, Historia Yaweza Kutumainiwa?
Wanahistoria ni kama wapelelezi wala si kama wanasayansi. Wao huchunguza, hufanya udadisi, na kuchanganua rekodi za mambo yaliyopita. Lengo lao ni kubaini ukweli, lakini mara nyingi mradi wao si dhahiri. Kwa sehemu ni kwa sababu kazi yao huhusu hasa watu, na wanahistoria hawawezi kusoma akili za watu—hasa akili za wafu. Wanahistoria wanaweza pia kuwa na dhana na upendezi fulani wa kibinafsi. Kwa hiyo, nyakati nyingine historia inayoonwa kuwa bora kwa kweli huwa ni fasiri inayotegemea maoni ya mwandishi.
Bila shaka, hatuwezi kusema kwamba kazi ya mwanahistoria si sahihi kwa sababu ya maoni yake. Masimulizi ya Biblia ya Samweli, Wafalme na Mambo ya Nyakati yatia ndani masimulizi sambamba ambayo yaliandikwa na watu watano mbalimbali, na bado yaweza kuthibitishwa kwamba hayapingani wala hayana makosa. Ndivyo ilivyo kuhusu zile Gospeli nne. Waandikaji wengi wa Biblia hata walirekodi dosari na makosa yao ya kipumbavu—jambo ambalo ni nadra sana katika vitabu vya kilimwengu.—Hesabu 20:9-12; Kumbukumbu la Torati 32:48-52.
Mbali na uwezekano wa kuwapo kwa upendezi wa kibinafsi, jambo jingine muhimu la kuzingatia unaposoma historia ni madhumuni ya mwandikaji. “Historia yoyote inayosimuliwa na wenye mamlaka, au na wale wenye tamaa ya uongozi au na rafiki zao, ni sharti ichunguzwe kwa uangalifu sana,” asema Michael Stanford katika kitabu A Companion to the Study of History. Madhumuni yenye kutiliwa shaka hudhihirika pia vitabu vya historia vinapotetea utaifa na uzalendo kwa hila au hata waziwazi. Kwa kusikitisha, nyakati nyingine dhana hizo huandikwa katika vitabu vya mafunzo shuleni. Sheria ya serikali ya nchi moja ilitaarifu waziwazi kwamba kusudi la kufunza historia ni “kuimarisha hisia za utaifa na uzalendo katika mioyo ya watu . . . kwa sababu kujua historia ya taifa ni mojawapo ya mambo muhimu sana katika kusitawisha uzalendo.”
Historia Iliyopotoshwa
Mbali na kupendelea, nyakati nyingine historia huwa imepotoshwa. Kwa mfano, ule uliokuwa Muungano wa Sovieti “ulifuta jina Trotsky kutoka kwenye rekodi, hivi kwamba uthibitisho wa kuwapo kwa kiongozi huyo wa kisiasa ulitokomea,” chasema kitabu, Truth in History. Trotsky alikuwa nani? Alikuwa kiongozi wa Mapinduzi ya Bolsheviki ya Urusi naye alikuwa na cheo cha pili baada ya Lenin. Baada ya kifo cha Lenin, Trotsky alikosana na Stalin, akafukuzwa kutoka Chama cha Kikomunisti, kisha akauawa baadaye. Jina lake hata lilifutwa kutoka katika ensaiklopedia za Sovieti. Kupotoshwa kama huko kwa historia, hata kufikia hatua ya kuteketeza vitabu visivyokubaliana na malengo fulani, ni zoea la kawaida la serikali nyingi za kimabavu.
Hata hivyo, kupotosha historia ni zoea la kale sana, lililoanza mapema angalau katika Misri na Ashuru. Mafarao, wafalme, na maliki wenye kiburi na majivuno walihakikisha kwamba waliacha historia ya matendo yenye kusifika. Kwa hiyo mafanikio yalitiliwa chumvi mara nyingi, ilhali mambo yoyote yenye kufedhehesha au ya aibu, kama vile kushindwa vitani, yalifichwa, yalisahauliwa kabisa, au hata kutoripotiwa nyakati nyingine. Kinyume kabisa cha hilo, historia ya Waisraeli iliyorekodiwa kwenye Biblia inatia ndani makosa na sifa nzuri za wafalme na raia pia.
Wanahistoria huchunguzaje usahihi wa maandishi ya kale? Wao huyalinganisha na rekodi za kale za kodi, mifumo ya sheria, matangazo ya minada ya watumwa, barua za kibiashara na za kibinafsi, maandishi yaliyoandikwa kwenye vipande vya vyungu, maandishi ya safari za meli, na vifaa vilivyopatikana makaburini. Vitu hivyo hutoa habari zaidi au habari mpya kuhusu maandishi rasmi yaliyopo. Kunapokuwa na mapengo au tashwishi, wanahistoria waaminifu kwa kawaida hukiri jambo hilo, japo wanaweza kubuni nadharia zao wenyewe ili kujaza mapengo hayo. Kwa vyovyote vile, wasomaji wenye hekima huchunguza vichapo mbalimbali endapo wanataka maelezo yenye usawaziko kuhusu matukio.
Licha ya magumu yote yanayowakabili wanahistoria, kazi yao huandaa habari muhimu sana. Kitabu kimoja cha historia chaeleza hivi: “Ijapokuwa si rahisi kuandika historia ya ulimwengu, . . . historia hiyo ni ya maana, hata ni muhimu sana kwetu.” Mbali na kutuelewesha kuhusu mambo yaliyopita, historia inaweza kutufahamisha mengi zaidi kuhusu hali ya sasa ya mwanadamu. Mathalani, sisi hugundua mara moja kwamba hata watu wa kale walidhihirisha sifa zilezile za kibinadamu zinazodhihirishwa na watu leo. Sifa hizo za kawaida zimeathiri sana historia, na labda zimetokeza msemo wa kwamba hakuna jambo jipya duniani. Lakini je, mkataa huo unategemea uhakika na kufikiri kuzuri?
Je, Hakuna Jambo Jipya Duniani?
Je, kweli tunaweza kutabiri kwa uhakika mambo ya wakati ujao tukitegemea mambo yaliyopita? Matukio fulani-fulani hutukia tena. Kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger alisema hivi: “Kila ustaarabu uliowahi kuwapo uliporomoka hatimaye.” Akaongezea hivi: “Historia ni simulizi la jitihada zilizoambulia patupu, na miradi isiyotimizwa. . . . Kwa hiyo, mtu akiwa mwanahistoria, hana budi kukubali kwamba misiba haiepukiki.”
Hakuna milki zozote mbili zilizoporomoka kwa njia ileile. Babiloni ilishindwa usiku mmoja na Wamedi na Waajemi mwaka wa 539 K.W.K. Ugiriki ilisambaratika na kuwa falme kadhaa baada ya kifo cha Aleksanda Mkuu, hatimaye ilishindwa na Milki ya Roma. Hata hivyo, kuporomoka kwa Roma kumezusha ubishi. Mwanahistoria Gerald Schlabach auliza hivi: “Roma iliporomoka lini? Je, kweli iliporomoka? Jambo fulani lilibadilika huko Ulaya Magharibi kati ya mwaka wa 400 W.K. na 600 W.K. Lakini mengi zaidi yalibaki vilevile.”a Ni wazi kwamba mambo fulani ya historia hutukia tena, ilhali mengine hayatukii tena.
Somo moja la historia linalotokea tena na tena ni kushindwa kwa utawala wa mwanadamu. Miaka nenda miaka rudi jitihada za kutafuta serikali nzuri zimeharibiwa na ubinafsi, kutozingatia wakati ujao, pupa, ufisadi, ubaguzi, na hasa tamaa ya kupata na kushikilia mamlaka. Hivyo basi, enzi zilizopita zilikuwa na harakati za kurundika silaha, mikataba isiyofua dafu, vita, michafuko ya kijamii na jeuri, ubaguzi katika ugawanyaji wa mali, na kuzorota kwa uchumi wa nchi mbalimbali.
Kwa mfano, ona mambo yanayosemwa na kichapo The Columbia History of the World kuhusu jinsi ustaarabu wa Magharibi ulivyoathiri ulimwengu wote: “Baada ya Colombus na Cortes kuwahamasisha wenyeji wa Ulaya Magharibi kuhusu fursa zilizopo, tamaa yao ya kupata wafuasi, faida, na umashuhuri ilichochewa sana na ustaarabu wa Magharibi ukaenezwa kwa lazima karibu ulimwenguni pote. Wakiwa na tamaa kubwa ya kusambaa na kwa kutumia silaha kali, washindi hao waliutiisha ulimwengu kwa nguvu chini ya mamlaka ya serikali kubwa za Ulaya . . . Kwa ufupi, wenyeji wa mabara hayo [Afrika, Asia, na Amerika] walitumiwa vibaya sana na kikatili.” Maneno yapatikanayo kwenye Biblia katika Mhubiri 8:9 (Chapa ya 1989): ‘Mtu amekuwa na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake’ ni ya kweli kama nini!
Huenda rekodi hiyo yenye kusikitisha ndiyo iliyomchochea mwanafalsafa mmoja Mjerumani aseme kwamba somo pekee tunalojifunza kutokana na historia ni kwamba wanadamu hawajifunzi jambo lolote kutokana na historia. Andiko la Yeremia 10:23 lasema: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” Twapaswa kuhangaikia kushindwa kwetu kuelekeza hatua zetu hasa leo. Kwa nini? Kwa sababu tunakumbwa na matatizo mabaya sana yasiyo na kifani. Basi tutakabilianaje nayo?
Matatizo Yasiyo na Kifani
Katika historia yote ya wanadamu, dunia nzima haijawahi kamwe kutishwa na matatizo chungu nzima kama ya kuharibiwa kwa misitu, mmomonyoko wa udongo, kuenea kwa jangwa, kuangamia kwa jamii nzimanzima za mimea na wanyama, kuharibiwa kwa ozoni ya angahewa, uchafuzi, kuongezeka kwa joto duniani, kuchafuliwa sana kwa bahari, na kuongezeka kasi kwa idadi ya watu.
“Tatizo jingine linalokabili jamii za kisasa ni jinsi mabadiliko hufanyika haraka,” chasema kitabu A Green History of the World. Ed Ayres, mhariri wa gazeti la World Watch, aandika hivi: “Tunakabili jambo fulani tusiloweza kuelewa kamwe kiasi cha kutolitambua, kujapokuwa na ushuhuda wa kutosha. Kwetu sisi, ‘jambo’ hilo ni kutokea ghafula kwa mabadiliko makubwa sana ya kibiolojia katika ulimwengu ambao umekuwa ukitutegemeza.”
Kwa sababu ya matatizo hayo na mengine mengi, mwanahistoria Pardon E. Tillinghast asema hivi: “Mwelekeo wa jamii umezidi kuwa tata zaidi, na utata huo unaogofya wengi wetu. Wanahistoria wenye ujuzi wanaweza kuandaa mwelekezo gani kwa watu waliotatanika leo? Yaonekana si mwelekezo madhubuti.”
Huenda wanahistoria wenye ujuzi wasijue jambo la kufanya wala shauri la kutoa, lakini bila shaka Muumba wetu hawezi kushindwa. Isitoshe, alitabiri kwenye Biblia kwamba katika siku za mwisho, kungekuwa na “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo,” ulimwenguni. (2 Timotheo 3:1-5) Lakini Mungu amefanya jambo ambalo hata wanahistoria hawawezi kufanya—ameandaa suluhisho, kama tutakavyoona kwenye makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Maoni ya Schlabach yanapatana na utabiri wa nabii Danieli kwamba mahali pa Milki ya Roma pangechukuliwa na ufalme mwingine ulioibuka kutoka kwa Roma. Ona sura ya 4 na 9 ya kitabu Sikiliza Unabii wa Danieli!, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
“Historia yoyote inayosimuliwa na wenye mamlaka . . . ni sharti ichunguzwe kwa uangalifu sana.”—MICHAEL STANFORD, MWANAHISTORIA
[Picha katika ukurasa wa 4]
Maliki Nero
[Hisani]
Roma, Musei Capitolini
[Picha katika ukurasa wa 7]
Katika miaka yote ‘mtu amekuwa na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake’
[Hisani]
“The Conquerors,” na Pierre Fritel. Kutia ndani (kushoto hadi kulia): Ramses wa Pili, Attila, Hannibal, Tamerlane, Yulio Kaisari (katikati), Napoléon wa Kwanza, Aleksanda Mkuu, Nebukadneza, na Charlemagne. Kutoka kwa kitabu The Library of Historic Characters and Famous Events, buku la Tatu, 1895; ndege: USAF photo
-
-
Biblia Je, Ina Historia Inayotegemeka?Amkeni!—2001 | Machi 8
-
-
Biblia Je, Ina Historia Inayotegemeka?
WALIWASHUTUMU watawala. Waliwakemea vikali makuhani. Waliwakaripia watu wa kawaida kwa ajili ya uovu wao. Hata walieleza hadharani dhambi zao na makosa yao wenyewe. Walifukuzwa na kunyanyaswa, na hata wengine waliuawa kwa kusema na kuandika ukweli. Ni nani hao? Manabii wa Biblia, wengi wao waliandika pia Maandiko Matakatifu.—Mathayo 23:35-37.
Katika kitabu chake cha The Historian and History, Page Smith aandika: “[Waebrania] waliandika waziwazi kuhusu mashujaa wao na wahalifu pia, juu yao wenyewe na juu ya maadui wao, kwa sababu waliandika chini ya mwelekezo wa Mungu na kuficha ukweli hakungewafaidi.” Smith aliandika pia kwamba “masimulizi kuhusu taabu na ushindi wa watu walioteuliwa na Mungu yanasisimua sana . . . yalinganishwapo na maandishi yenye kuchosha ya wafalme wapiganaji wa Ashuru au Misri. Waandikaji Waebrania walifahamu mojawapo ya mambo muhimu sana katika uandishi wa historia—ya kwamba inahusu watu halisi, wakiwa na dosari zao na makosa yao yote.”
Waandishi wa Biblia waliandika pia kwa usahihi mkubwa. Baada ya kuichanganua Biblia kwa kuzingatia historia na akiolojia, mwandishi Werner Keller alisema hivi katika utangulizi wa kitabu chake The Bible as History: “Kwa kuzingatia uthibitisho mkubwa uliopo wenye kutegemeka, . . . wazo hili moja lilinijia akilini mara nyingi: ‘Biblia haina kosa lolote kama ilivyodhaniwa!’”
Historia Yenye Kuchochea na Yenye Masomo Muhimu
Waandikaji wengi wa Biblia walikuwa watu wa kawaida—wakulima, wachungaji, wavuvi. Lakini, mambo waliyoandika kwa muda wa miaka 1,600 yameathiri watu wengi zaidi kuliko maandishi mengine yoyote, yawe ya kale au ya kisasa. Isitoshe, maandishi yao yamechambuliwa katika njia mbalimbali, lakini yamestahimili. (Isaya 40:8; 1 Petro 1:25) Leo Biblia inaweza kupatikana ikiwa nzima au kwa sehemu katika lugha zipatazo 2,200—zaidi ya kitabu kingine chochote! Kwa nini Biblia ni ya pekee hivyo? Maandiko yafuatayo yanajibu swali hilo.
“Andiko lote limepuliziwa na Mungu na ni lenye manufaa kwa kufundisha, kwa kukaripia, kwa kunyoosha mambo, kwa kutia nidhamu katika uadilifu, ili mtu wa Mungu apate kuwa hodari, aliyeandaliwa vifaa kikamili kwa ajili ya kila kazi njema.”—2 Timotheo 3:16, 17.
“Kwa maana mambo yote yaliyoandikwa wakati wa mbele yaliandikwa kwa kufunzwa kwetu, ili kupitia uvumilivu wetu na kupitia faraja kutokana na Maandiko tupate kuwa na tumaini.”—Waroma 15:4.
“Mambo hayo yaliendelea kuwapata [Waisraeli] kuwa vielelezo, nayo yaliandikwa kuwa onyo kwetu sisi [Wakristo] ambao juu yetu miisho ya mifumo ya mambo imewasili.”—1 Wakorintho 10:11.
Naam, Biblia ni kitabu bora kuliko vitabu vyote kwa kuwa ni rekodi ya watu halisi iliyopuliziwa na kuhifadhiwa na Mungu. Baadhi ya watu hao walimpendeza Mungu na wengine hawakumpendeza. Bila shaka si orodha yenye sheria kali za mambo ya kufanya na ya kutofanya au mkusanyo wa hadithi fupifupi zenye kupendeza zinazonuiwa kufurahisha watoto. Ni kweli kwamba Mungu alitumia wanadamu kuiandika, lakini jambo hilo liliboresha tu Biblia, na kuifanya iwe na ujumbe mchangamfu wenye kuvutia ambao umegusa mioyo ya wasomaji kizazi hadi kizazi. Mwakiolojia William Albright alisema hivi: “Ujuzi wenye kina wa kiadili na kiroho wa Biblia, ambao Mungu amewafunulia wanadamu kwa njia ya pekee na kuuwasilisha kupitia kwa wanadamu, ni wa kweli leo kama ulivyokuwa miaka elfu mbili au tatu iliyopita.”
Ili kutoa kielezi cha kudumu kwa shauri la Biblia, acheni tufikirie mwanzo wa historia ya wanadamu—ni Biblia tu inayoweza kutufahamisha juu yake—na tufikirie masomo fulani muhimu kutoka kwa kitabu cha Mwanzo.
Masomo Muhimu Sasa Kutokana na Simulizi la Kale
Miongoni mwa mambo mengine, kitabu cha Mwanzo chaeleza mwanzo wa jamii ya wanadamu—majina na mambo mengine yoyote. Hakuna kichapo kingine chochote cha historia kinachozungumzia barabara habari hiyo. ‘Lakini tunanufaikaje leo kwa kufahamu mwanzo wetu?’ huenda ukauliza. Kuna manufaa makubwa sana, kwa kuwa kitabu cha Mwanzo kinapoeleza kwamba wanadamu wote—haidhuru rangi, kabila, au taifa—wanatoka kwa wazazi walewale, kinaondolea mbali sababu yoyote ya kuwa na ubaguzi.—Matendo 17:26.
Kitabu cha Mwanzo huandaa pia mwongozo kuhusu adili. Kina simulizi la Sodoma, Gomora, na miji jirani, iliyoharibiwa na Mungu kwa sababu ya upotovu mkubwa wa adili wa wenyeji wake. (Mwanzo 18:20–19:29) Mstari wa 7 wa kitabu cha Biblia cha Yuda wasema hivi: “Sodoma na Gomora na majiji yaliyo kando-kando yayo, baada ya hayo kuwa yamefanya uasherati kwa kuzidi mno na kutoka kwenda kufuatia mwili kwa ajili ya utumizi usio wa asili, . . . yamewekwa mbele yetu kuwa kielelezo cha kuonya.” Watu wa Sodoma na Gomora hawakupewa na Mungu sheria zozote za adili; hata hivyo, kama wanadamu wengine wote, walikuwa na dhamiri waliyopewa na Mungu. Hivyo basi, Mungu alikuwa na haki ya kuwaona kuwa na wajibu kuelekea matendo yao. (Waroma 1:26, 27; 2:14, 15) Vivyo hivyo leo, wanadamu wote watawajibika mbele za Mungu kwa ajili ya matendo yao, iwe watakubali Neno lake, Biblia Takatifu, au la.—2 Wathesalonike 1:8, 9.
Somo la Historia Kuhusu Wokovu
Mchoro mmoja kwenye Tao la Tito huko Roma laonyesha askari Waroma wakibeba vyombo vitakatifu kutoka kwenye hekalu la Yerusalemu baada ya kuharibiwa kwa jiji hilo mnamo mwaka wa 70 W.K. Wayahudi zaidi ya milioni moja waliuawa. Lakini, Wakristo watiifu waliokoka kwa sababu ya kufuata onyo la mapema la Yesu: “Mwonapo Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwalo kumekaribia. Ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbia hadi kwenye milima, na waacheni wale walio katikati yalo waondoke, na waacheni wale walio katika sehemu za mashambani wasiingie ndani yalo; kwa sababu hizi ni siku za kupatiliza haki.”—Luka 21:20-22.
Mbali na kuwa tukio la kale tu, dhiki iliyopata Yerusalemu ilionyesha kimbele mambo yatakayotukia wakati wa dhiki kubwa zaidi ambayo karibuni itaupata ulimwengu wote. Lakini kwa mara nyingine tena, kutakuwa na waokokaji. Wanaelezwa kuwa “umati mkubwa . . . kutoka katika mataifa yote na makabila na vikundi vya watu na lugha.” “Wanatoka katika dhiki kubwa” kwa sababu ya imani yao katika damu ya Yesu iliyomwagwa—imani ambayo inategemea kabisa historia na unabii wa Biblia.—Ufunuo 7:9, 14.
Matukio ya Kihistoria Ambayo Hayatarudiwa Kamwe
Leo tunaishi wakati wa utawala wa Serikali ya Ulimwengu ya Uingereza na Marekani, tukio la mwisho la kiunabii lililotabiriwa na Biblia. Kwa kuchunguza yale yaliyotukia awali tunaweza kufikia mkataa wa kwamba Serikali hiyo itafikia kikomo kama serikali nyingine zilizotangulia. Lakini jinsi gani? Kulingana na Biblia, mwisho wa serikali hiyo utakuwa wa pekee sana. Likitabiri kuhusu mwaka wa 1914 W.K., andiko la Danieli 2:44 lilisema hivi kuhusu serikali za kisiasa zinazotawala, au “falme”: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”
Naam, Ufalme wa Mungu—serikali yake ya kimbingu inayoongozwa na Kristo Yesu—utaharibu kabisa kila sehemu ya utawala wa wanadamu wenye uonevu kwenye Har–Magedoni, upeo wa “dhiki kubwa” iliyotajwa awali. Baada ya hapo, “watu wengine hawataachiwa enzi” ya Ufalme huo, kumaanisha kwamba hautapinduliwa kamwe wala kuondolewa mamlakani kupitia upigaji wa kura. Enzi yake itaenea “hata miisho ya dunia.”—Zaburi 72:8.
Hatimaye, mamlaka mbalimbali katili za dini bandia, siasa zenye uonevu, na biashara zenye pupa zitakoma. Zaburi 72:7 yaahidi: “Mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.” Sifa kuu ya Mungu ya upendo ndiyo itakayoenea ulimwenguni pote badala ya ubinafsi na kiburi. (1 Yohana 4:8) Yesu alisema: ‘Pendaneni.’ Kuhusu hilo, mwanahistoria Will Durant alisema hivi: “Jambo muhimu ambalo nimejifunza kutokana na historia yote ya wanadamu lafanana na la Yesu. . . . Upendo ndio jambo muhimu zaidi ulimwenguni.”
Upendo wa Mungu kwa wanadamu ulimchochea kupulizia uandikaji wa Biblia. Ndiyo pekee inayoeleza waziwazi mambo ya wakati uliopita, ya sasa, na ya wakati ujao. Tafadhali thamini ujumbe wake wenye kutoa uhai kwa kutumia wakati fulani kujifunza Biblia. Ili kufikia lengo hilo na kwa kutii amri ya Yesu, Mashahidi wa Yehova huwajulisha majirani zao “habari njema za ufalme.” Hivi karibuni habari hizo njema hazitakuwa unabii tu. Zitakuwa matukio halisi yaliyopita.—Mathayo 24:14.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
“Biblia haina kosa lolote kama ilivyodhaniwa!”—WERNER KELLER
[Blabu katika ukurasa wa 11]
“Ujuzi wenye kina wa kiadili na kiroho wa Biblia . . . ni wa leo kama ulivyokuwa miaka elfu mbili au tatu iliyopita.”—WILLIAM ALBRIGHT, MWAKIOLOJIA
[Picha katika ukurasa wa 9]
Jiwe la Moabu: Lina maelezo ya Mfalme Mesha kuhusu pambano kati ya Moabu na Israeli (2 Wafalme 3:4-27), lina majina ya sehemu mbalimbali za Kibiblia, na jina la Mungu katika herufi za kale za Kiebrania.
[Hisani]
Musée du Louvre, Paris.
Sarafu ya dinari ya fedha: Sarafu hiyo ina picha na mwandiko wa Kaisari Tiberio (Marko 12:15-17).
Maandishi ya Tarehe ya Matukio ya Nabonido: Bamba la kikabari linalothibitisha kushindwa ghafula kwa Babiloni na Sairasi. (Danieli, sura ya 5)
[Hisani]
Photograph taken by courtesy of the British Museum.
Bamba la jiwe: Lina jina la Pontio Pilato katika Kilatini. Photograph
[Hisani]
© Israel Museum, Jerusalem; courtesy of Israel Antiquities Authority.
Picha Iliyo Nyuma ya Hati-kunjo ya Bahari ya Chumvi: Uchunguzi wa maandishi ya Isaya ulithibitisha kwamba kitabu hicho hakijabadilika baada ya kunakiliwa kwa mkono kwa muda wa zaidi ya miaka 1,000.
[Hisani]
Shrine of the Book, Israel Museum, Jerusalem.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mchoro kwenye Tao la Tito wathibitisha kuharibiwa kwa Yerusalemu mwaka wa 70 W.K.
[Hisani]
Soprintendenza Archeologica di Roma
-