Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • ‘Mabadiliko Makubwa Zaidi’
    Amkeni!—1999 | Desemba 8
    • ‘Mabadiliko Makubwa Zaidi’

      “Karne ya 20 imepatwa na mabadiliko makubwa na yenye kuenea zaidi kuliko karne yoyote katika historia ya binadamu.” —The Times Atlas of the 20th Century.

      TUNAPOTAFAKARI juu ya karne ya 20, bila shaka wengi watakubaliana na Walter Isaacson, mhariri msimamizi wa gazeti Time, ambaye alisema: “Kwa kulinganishwa na karne nyinginezo, karne hii imekuwa mojawapo ya karne zenye kushangaza zaidi: yenye kutokeza, nyakati nyingine yenye kutisha, yenye kuvutia sana sikuzote.”

      Hali kadhalika, Gro Harlem Brundtland, aliyekuwa waziri mkuu wa Norway, asema kwamba karne hii imeitwa “karne yenye hali zinazopita kiasi, . . . ambapo kumekuwa na uovu wa kibinadamu usio na kifani.” Asema kwamba imekuwa “karne ya maendeleo makubwa [na katika sehemu fulani ya] ukuzi wa kiuchumi usio na kifani.” Hata hivyo, wakati huohuo, maeneo ya mjini yenye umaskini yanakabili wakati ujao usio na tumaini wenye “idadi kubwa ya watu na visa vya maradhi yanayoletwa na umaskini na mazingira yasiyofaa.”

      Mabadiliko Makubwa ya Kisiasa

      Karne ya 20 ilipoanza, nasaba ya wafalme ya Manchu katika China, Milki ya Waturuki, na milki kadhaa za Ulaya zilidhibiti sehemu kubwa ya ulimwengu. Milki ya Uingereza pekee ilidhibiti robo moja ya tufe na kutawala mtu 1 kati ya watu 4 duniani. Muda mrefu kabla ya karne hiyo kwisha, milki hizo zote hazikuwapo tena. “Mnamo 1945,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century, “enzi ya ubeberu ilikuwa imekwisha.”

      Kuporomoka kwa ukoloni kulitokeza ongezeko la utukuzo wa taifa lililoenea Ulaya kote kati ya karne ya 17 na ya 19 na kufikia sehemu nyingine za ulimwengu. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema: “Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili shauku nyingi ya uzalendo ilipungua katika mataifa mengi ya Ulaya . . . Hata hivyo, katika Afrika na Asia, utukuzo wa taifa ulikua haraka, hasa ikiwa ni itikio dhidi ya ukoloni.” Hatimaye, kulingana na The Collins Atlas of World History, “Nchi Zinazositawi zilikuwa zimejitokeza kwenye mandhari ya kihistoria, na enzi iliyoanza karne tano mapema kukiwa na mwanzo wa upanuzi wa Ulaya, sasa ilikuwa imefikia kikomo.”

      Milki zilipoporomoka, mataifa huru yaliibuka—mengi yakiwa serikali za kidemokrasia. Mara nyingi, utawala wa kidemokrasia ulipingwa vikali na serikali kama zile za kiimla zenye nguvu katika Ulaya na Asia katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Tawala hizo zilizuia uhuru wa kibinafsi na kudhibiti kwa nguvu uchumi, vyombo vya habari, na majeshi. Hatimaye jitihada zao za kuutawala ulimwengu zilikomeshwa, lakini ni baada tu ya kutumia pesa nyingi na kuangamiza wanadamu wengi.

      Karne ya Vita

      Kwa kweli, jambo hususa linalofanya karne ya 20 iwe tofauti na karne nyingine za awali ni vita. Mwanahistoria Mjerumani Guido Knopp aandika hivi kuhusu Vita ya Ulimwengu ya Kwanza: “Agosti 1, 1914: Hakuna mtu aliyewazia kwamba karne ya 19 iliyokuwa imewapa Wazungu kipindi kirefu cha amani iliisha siku hiyo; na hakuna mtu aliyetambua kwamba kwa kweli karne ya 20 ilikuwa imeanza tu wakati huo—kikiwa kipindi cha vita kilichodumu kwa miongo mitatu na kuonyesha uhaini ambao mwanadamu anaweza kuwafanyia wanadamu wenzake.”

      Hugh Brogan, profesa wa historia, alitukumbusha kwamba “vita hiyo iliathiri sana Marekani, ilifadhaisha, na bado inahisiwa leo [katika mwaka wa 1998].” Profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Harvard, Akira Iriye, aliandika: “Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ilikuwa tukio kubwa lililobadili historia ya Asia Mashariki na Marekani kwa njia nyingi.”

      Basi yaeleweka ni kwa nini kichapo The New Encyclopædia Britannica chataja vita ya ulimwengu ya kwanza na ya pili kuwa “mabadiliko makubwa ya karne ya 20 ya historia ya siasa ya nchi.” Kinasema kwamba “Vita ya Ulimwengu ya Kwanza iliongoza kwenye kuporomoka kwa nasaba nne kubwa za kifalme . . . , ikatokeza Mapinduzi ya Bolsheviki katika Urusi, na . . . kuweka msingi wa Vita ya Ulimwengu ya Pili.” Pia kinatuambia kwamba karibu vita vya ulimwengu viwe “bila kifani katika uuaji, umwagaji-damu, na uharibifu.” Hali kadhalika Guido Knopp asema hivi: “Ukatili na unyama wa kibinadamu ulizidi mataraja mabaya zaidi. Kwenye mitaro . . . mbegu zilipandwa kwa ajili ya muhula ambao wanadamu walionwa kuwa vitu, wala si watu.”

      Ili kuzuia vita zaidi vya namna hiyo vyenye kuleta msiba, Ushirika wa Mataifa ulianzishwa mnamo mwaka wa 1919. Uliposhindwa kutimiza mradi wake wa kudumisha amani duniani, mahali pake palichukuliwa na Umoja wa Mataifa. Ijapokuwa UM umefaulu kuzuia vita ya ulimwengu ya tatu, ulishindwa kuzuia Vita Baridi, ambayo kwa miongo kadhaa ilielekea kuongezeka na kuwa maangamizi ya nyuklia. Wala haujazuia mapambano madogo zaidi ulimwenguni kote, kama vile katika Balkani.

      Kadiri idadi ya mataifa inavyoongezeka ulimwenguni, ndivyo na ugumu wa kudumisha amani miongoni mwao. Ulinganifu wa ramani ya kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Kwanza na ramani ya kisasa wafunua kwamba mwanzoni mwa karne, angalau mataifa 51 ya Afrika na 44 ya Asia yaliyoko sasa hayakuwepo wakati huo. Kuhusu washiriki wa sasa 185 wa Umoja wa Mataifa, 116 hawakuwako wakiwa nchi huru UM ulipoanzishwa mwaka wa 1945!

      “Mojawapo ya Mambo Yenye Kutazamisha Zaidi”

      Karne ya 19 ilipokuwa ikikaribia kumalizika, Milki ya Urusi ndiyo iliyokuwa mamlaka iliyotawala sehemu kubwa zaidi ulimwenguni. Lakini ilikuwa ikipoteza utegemezo wake haraka sana. Kulingana na mtungaji Geoffrey Ponton, watu wengi walifikiri kwamba “mapinduzi badala ya marekebisho yalikuwa ya lazima.” Aongezea hivi: “Lakini ni kufuatia vita kubwa, Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, na mchafuko uliofuata baadaye, ndipo mapinduzi halisi yalipoanza kwa ghafula.”

      Wabolsheviki walipopata mamlaka huko Urusi wakati huo msingi wa milki mpya uliwekwa—Ukomunisti wa ulimwengu uliofadhiliwa na Muungano wa Sovieti. Ijapokuwa ulianzishwa katikati ya vita ya ulimwengu, Milki ya Sovieti haikuishia vitani. Kitabu cha Michael Dobbs Down With Big Brother, chadai kwamba mwisho-mwisho wa miaka ya 1970, Muungano wa Sovieti ulikuwa “milki kubwa sana yenye mataifa mengi ambayo tayari ilikuwa ikididimia katika hali isiyoweza kurekebika.”

      Hata hivyo, anguko lake lilikuja kwa ghafula. Kitabu Europe—A History, cha Norman Davies, chaeleza: “Mwendo wa anguko lake umeshinda maanguko mengi makubwa katika historia ya Ulaya,” na “lilitokezwa na visababishi vya asili.” Kwa kweli, “kuibuka, kukua na kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti,” asema Ponton, kulikuwa “mojawapo ya mambo yenye kutokeza zaidi ya karne ya ishirini.”

      Kwa kweli, kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti kulikuwa mojawapo ya mabadiliko makubwa ya karne ya 20 ambayo yamekuwa na matokeo yenye kuenea kote. Bila shaka, mabadiliko ya kisiasa si mambo mapya. Yamekuwa yakitukia kwa maelfu ya miaka.

      Hata hivyo, badiliko moja la maana sana hasa katika karne ya 20 linahusu serikali. Badiliko hilo na jinsi linavyokuathiri kibinafsi litazungumziwa baadaye.

      Ingawa hivyo, ebu tuzungumzie kwanza, baadhi ya mafanikio ya sayansi katika karne ya 20. Kuhusu mafanikio hayo, Profesa Michael Howard amalizia hivi: “Watu wa Magharibi mwa Ulaya na Amerika Kaskazini walikuwa na sababu ya kukaribisha karne ya ishirini ikiwa mwanzo wa enzi mpya na yenye furaha zaidi katika historia ya mwanadamu.” Je, maendeleo hayo yangeongoza kwa yale yanaoitwa eti maisha ya hali ya juu?

      [Chati/Picha katika ukurasa wa 2-7]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      1901

      Malkia Victoria afa baada ya kutawala kwa miaka 64

      Idadi ya watu ulimwenguni yafikia bilioni 1.6

      1914

      Dyuki -mkuu Ferdinand auawa. Vita ya ulimwengu ya kwanza yaanza

      Zari wa mwisho, Nicholas wa Pili, pamoja na familia yake

      1917

      Lenin aongoza Urusi kwenye mapinduzi

      1919

      Ushirika wa Mataifa waanzishwa

      1929

      Kuporomoka kwa soko la hisa la Marekani kwa sababisha Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi

      Gandhi aendelea kupigania uhuru wa India

      1939

      Adolf Hitler avamia Poland, na kuanzisha Vita ya Ulimwengu ya Pili

      Winston Churchill awa waziri mkuu wa Uingereza mwaka wa 1940

      1941

      Japani yapiga bomu Pearl Harbor

      1945

      Marekani yaangusha mabomu ya atomu huko Hiroshima na Nagasaki. Vita ya Ulimwengu ya Pili yaisha

      1946

      Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lafanya mkutano wa kwanza

      1949

      Mao Tse-tung atangaza Jamhuri ya Watu wa China

      1960

      Mataifa mapya 17 ya Afrika yaanzishwa

      1975

      Vita ya Vietman yaisha

      1989

      Ukuta wa Berlin wabomolewa huku ukomunisti ukipoteza uwezo wake

      1991

      Muungano wa Sovieti wavunjika

  • Kutafuta Maisha ya Hali ya Juu
    Amkeni!—1999 | Desemba 8
    • Kutafuta Maisha ya Hali ya Juu

      “Karne ya ishirini ilipoendelea, maisha ya kila siku ya watu wengi . . . yalibadilishwa na maendeleo ya kisayansi na ya kitekinolojia.”—The Oxford History of the Twentieth Century.

      MOJAWAPO ya mabadiliko makubwa katika enzi hii yahusu idadi ya watu. Hakuna karne nyingine ambayo imekuwa na ongezeko kubwa la watu kadiri hiyo. Lilifikia takriban bilioni moja mapema katika miaka ya 1800 na takriban bilioni 1.6 kufikia miaka ya 1900. Mwaka wa 1999, idadi ya watu ulimwenguni ilifikia bilioni sita! Na wengi wa watu hao wanaoongezeka wametaka vile vinavyoitwa eti vitu bora maishani.

      Maendeleo katika tiba na kupatikana kwa utunzaji wa afya kumechangia ongezeko hilo la watu. Matarajio ya muda wa kuishi kwa wastani yaliongezeka katika sehemu kama vile Australia, Japani, Marekani na Ujerumani—kutoka miaka inayopungua 50 mwanzoni mwa karne hii hadi kufikia zaidi ya 70 sasa. Hata hivyo, mwelekeo huo unaofaa si mkubwa sana kwingineko. Watu wanaoishi katika angalau nchi 25 bado wana matarajio ya muda wa kuishi wa miaka 50 au inayopungua hiyo.

      ‘Mlifanikiwaje Hapo Awali . . . ?’

      Nyakati fulani vijana hawaelewi jinsi babu zao wa zamani walivyofanikiwa bila ndege, kompyuta, televisheni—vitu ambavyo sasa vinaonwa kuwa vya kawaida na hata vya lazima na watu fulani katika nchi tajiri zaidi. Kwa mfano, fikiria jinsi ambavyo gari limebadili maisha yetu. Lilivumbuliwa mwishoni mwa karne ya 19, lakini hivi karibuni gazeti Time lilisema: “Gari ni mojawapo ya uvumbuzi uliotofautisha karne ya 20 kuanzia mwanzo hadi mwisho.”

      Mnamo mwaka wa 1975 ilikadiriwa kwamba mtu mmoja kati ya kumi miongoni mwa wafanyakazi Wazungu angekosa kazi iwapo magari yangetoweka ghafula. Licha ya matokeo yaliyo wazi katika viwanda vya magari, mikahawa ambako watu huingia na magari yao, na biashara nyingine zinazotegemea wateja wenye magari zingefungwa. Wakulima wakikosa namna ya kupeleka bidhaa zao sokoni, mifumo ya ugawanyaji chakula ingekoma. Wafanyakazi wa jijini wanaoishi kwenye vitongoji wangekosa kufika kazini. Barabara kuu zinazovuka nchi hazingetumiwa tena.

      Ili kuongeza utengenezaji wa magari na kupunguza gharama, mashine za kufanya kazi hatua kwa hatua katika kuunda vitu ambavyo sasa ni vya kawaida katika viwanda vingi, zilianzishwa mapema katika karne hii. (Mashine za kufanya kazi hatua kwa hatua katika kuunda vitu ziliwezesha kutokezwa kwa wingi kwa bidhaa nyingine, kama vile vyombo vya jikoni.) Mwanzoni mwa karne, gari lilionwa kuwa chombo cha anasa cha matajiri katika nchi chache tu, lakini sasa ndiyo namna ya usafiri kwa watu wa kawaida katika sehemu nyingi za ulimwengu. Kama mtungaji mmoja alivyosema, “ni kama sasa haiwezekani kuwazia maisha bila magari katika karne ya 20.”

      Ufuatiaji Raha

      Kusafiri kulimaanisha kwenda mahali ulipolazimika kwenda. Lakini katika karne ya 20, mambo yalibadilika—hasa katika nchi zilizositawi. Kazi zenye mshahara mkubwa zilipozidi kupatikana na saa za kufanya kazi zilipopungua kufikia saa 40 au zinazopungua hizo, watu walikuwa na pesa na wakati wa kusafiri. Sasa kusafiri kulimaanisha kwenda mahali ulipotaka kwenda. Magari, mabasi, na ndege ziliwezesha watu kwenda tafrija mahali pa mbali. Utalii wa watu wengi ukawa biashara kubwa.

      Kulingana na The Times Atlas of the 20th Century, utalii “uliathiri sana nchi zilizopokea watalii na nchi walikotoka.” Kumekuwa na athari fulani isiyofaa. Mara nyingi sana watalii wamechangia pia kuharibu vitu vyenye kuvutia walivyokuja kuviona.

      Sasa watu walikuwa na wakati zaidi wa kufuatilia michezo. Wengi wakaanza kuishiriki; wengine wakaridhika kuwa mashabiki sugu na wakati mwingine wakitokeza ghasia kwa ajili ya timu na wanariadha wanaowapenda zaidi. Televisheni ilipotokea, matukio ya michezo yakawa yanafikia karibu kila mtu. Michezo ya nchini na ya kimataifa ilivutia mamia ya mamilioni ya watazamaji wa televisheni wenye shauku.

      “Michezo na filamu iliweka msingi wa biashara kubwa ya vitumbuizo, ambayo sasa ni mojawapo ya sekta za biashara ambazo zimeajiri watu wengi sana na hupata faida kubwa sana,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century. Kila mwaka watu hutumia mabilioni ya dola kwa vitumbuizo, kutia ndani kucheza kamari, aina ya tafrija inayopendwa na wengi. Kwa mfano, uchunguzi mmoja wa mwaka wa 1991 uliorodhesha kucheza kamari kuwa biashara namba 12 kwa ukubwa katika Jumuiya ya Ulaya, yenye faida ya kila mwaka ya angalau dola za Marekani bilioni 57.

      Tafrija hiyo ilipokuwa jambo la kawaida, watu walianza kutafuta mambo mapya ya kuwasisimua. Kwa mfano, majaribio yao ya dawa za kulevya, yalienea sana hivi kwamba kufikia katikati ya miaka ya 1990, biashara ya dawa za kulevya haramu ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 500 kwa mwaka na kuifanya kuwa, kama kichapo kimoja kisemavyo, “sekta pekee ya biashara yenye faida kubwa zaidi ulimwenguni.”

      “Kujiburudisha Kupita Kiasi”

      Tekinolojia ilisaidia kugeuza ulimwengu kuwa kijiji kimoja cha dunia nzima. Sasa watu huathiriwa karibu mara moja na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni. “Kwa wazi, kumekuwa na nyakati fulani maishani ambapo mabadiliko makubwa yalifanyiza historia,” akasema Profesa Alvin Tofller, mtungaji wa Future Shock, mnamo mwaka wa 1970. Aliongezea: “Lakini mambo hayo yenye kushtua na mabadiliko makubwa yaliathiri tu kikundi kimoja au vikundi vya jamii zinazoishi karibu-karibu. Ilichukua vizazi kadhaa, hata karne kadhaa, ili kuathiri sehemu zilizo ng’ambo ya mipaka hiyo. . . . Leo mifumo ya ushirikiano wa kijamii imefungamanishwa sana hivi kwamba matokeo ya matukio ya wakati uleule huenea mara moja ulimwenguni pote.” Televisheni za setilaiti na Internet pia zimechangia fungu fulani katika kuathiri watu ulimwenguni pote.

      Wengine wanasema kwamba televisheni imekuwa chombo chenye uvutano zaidi cha karne ya 20. Mwandikaji mmoja alisema: “Ingawa watu fulani huchambua mambo yaliyomo katika televisheni, hakuna yeyote anayebisha juu ya uwezo wake.” Lakini televisheni si bora kuliko wanadamu ambao hutokeza vipindi hivyo. Hivyo pamoja na uwezo wake wa kuathiri watu kwa njia inayofaa, ina uwezo wa kuathiri watu kwa njia isiyofaa. Ingawa programu zenye mambo yasiyofaa, zilizojaa jeuri na ukosefu wa adili, zina mambo ambayo watu fulani wanataka kuona, programu hizo zilishindwa kuboresha uhusiano wa kibinadamu na mara nyingi kuuzorotesha zaidi.

      Neil Postman, katika kitabu chake Amusing Ourselves to Death, ataja hatari nyingine, akisema: “Tatizo si kwamba televisheni hututolea mambo ya kutumbuiza bali kwamba mambo yote huonyeshwa kuwa yenye kutumbuiza . . . Bila kujali ni nini kinachoonyeshwa au ni kwa kutegemea maoni gani, sababu kuu ni kwamba kiko hapo ili kututumbuiza na kutufurahisha.”

      Watu walipozidi kutanguliza raha, kanuni za kiroho na za kiadili zilizorota haraka sana. “Dini nyingi za ulimwengu zilizopangwa kitengenezo zimepoteza uvutano katika karne ya 20,” chasema kichapo The Times Atlas of the 20th Century. Huku hali ya kiroho ikididimia, utafutaji anasa ulitangulizwa kupita kiasi kuliko ulivyostahili.

      “King’aacho . . .”

      Mabadiliko mengi yanayofaa yanabainisha karne ya 20, lakini, kama msemo usemavyo, “King’aacho usidhani ni dhahabu.” Ingawa watu wamenufaika na kurefushwa kwa muda wa maisha, kuongezeka kwa idadi ya watu ulimwenguni kumetokeza matatizo mapya makubwa. Hivi majuzi gazeti National Geographic lilisema: “Huenda ikawa ukuzi wa idadi ya watu ndilo suala la hima zaidi tunalokabili tuingiapo milenia mpya.”

      Magari ni yenye mafaa na yanafurahisha lakini pia ni ya kufisha, kama ithibitishwavyo na takriban vifo robo milioni kila mwaka vinavyosababishwa na aksidenti za magari ulimwenguni pote. Na magari ndiyo kisababishi kikuu cha uchafuzi. Watungaji wa kitabu 5000 Days to Save the Planet wasema kwamba uchafuzi “sasa unatukia tufeni pote, ukiharibu au kudhoofisha uwezo wa mifumikolojia kutoka kizio kimoja hadi kingine.” Wanaeleza: “Tumevuka mipaka ya kuharibu mifumikolojia na sasa tunavuruga mambo yanayohitajiwa hasa ili kudumisha Dunia ikiwa mahali panapofaa wanyama wa hali ya juu.”

      Katika karne ya 20, uchafuzi umekuwa tatizo ambalo halikujulikana katika karne zilizotangulia. “Hadi hivi majuzi hakuna mtu aliyejua kwamba utendaji wa kibinadamu ungeweza kuathiri ulimwengu kwa kiwango cha tufeni pote,” lasema National Geographic. “Sasa wanasayansi fulani wanaamini kwamba kwa mara ya kwanza katika historia iliyorekodiwa mabadiliko hayo yanatokea.” Kisha laonya: “Athari ya kibinadamu kwa ujumla ni kubwa kiasi cha kwamba kutoweshwa kwa kiwango kikubwa kungeweza kutukia katika kizazi kimoja cha kibinadamu.”

      Kwa kweli karne ya 20 imekuwa ya pekee. Watu waliobarikiwa na fursa zisizo na kifani za kufurahia maisha ya hali ya juu sasa wanaona uhai wenyewe ukiwa hatarini!

      [Chati/Picha katika ukurasa wa 8, 9]]

      (Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

      1901

      Marconi apeleka ishara ya kwanza ya redio inayovuka Atlantiki

      1905

      Einstein achapisha nadharia yake ya pekee ya uwiano wa vipimo vya mwendo, nafasi na wakati

      1913

      Ford afungua kiwanda cha kutengeneza gari aina ya Ford T

      1941

      Kituo cha televisheni cha kibiashara chaanzishwa

      1969

      Mwanadamu atembea kwenye mwezi

      Utalii wa watu wengi wawa biashara kuu

      Internet yazidi kupendwa

      1999

      Idadi ya watu ulimwenguni yafikia bilioni sita

  • Badiliko Muhimu Litakalokuwa Bora
    Amkeni!—1999 | Desemba 8
    • Badiliko Muhimu Litakalokuwa Bora

      “Katika miaka ya 1900 ulimwengu ulikaribia kuingia mojawapo ya vipindi muhimu vya badiliko katika historia ya kibinadamu. Utaratibu mpya ulikuwa ukichukua mahali pa ule wa kale.”—The Times Atlas of the 20th Century.

      MAPEMA katika karne ya 20, “ulimwengu uliingia katika muhula wenye maasi na jeuri isiyo na kifani,” chasema kitabu cha ramani kilichonukuliwa juu. Karne hii ingeshuhudia vita zaidi kuliko karne nyingine yoyote, kukiwa na watu zaidi ya milioni 100 waliokufa.

      Katika muhula huu, vita vimeua raia wengi kuliko wakati mwingine wowote. Katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, asilimia 15 ya watu waliokufa walikuwa raia. Lakini katika Vita ya Ulimwengu ya Pili, katika nchi fulani raia waliokufa walikuwa wengi kuliko wanajeshi. Kati ya mamilioni waliouawa vitani tangu wakati huo, wengi walikuwa raia. Jeuri hiyo yote imetimiza unabii wa Biblia kuhusu mpandaji aliye juu ya “farasi mwenye rangi-moto,” ambaye ‘alipewa ruhusa kuondolea mbali amani katika dunia.’—Ufunuo 6:3, 4; Mathayo 24:3-7.

      Badiliko la Maadili

      Karne ya 20 imetimiza unabii katika 2 Timotheo 3:1-5, unaosema: “Katika siku za mwisho nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zitakuwa hapa. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, wenye kujitanguliza, wenye kiburi, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio waaminifu-washikamanifu, wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, wachongezi, wasio na hali ya kujidhibiti, wakali, wasio na upendo wa wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kututumuka kwa kiburi, wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu, wakiwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakithibitika kuwa si kweli kwa nguvu ya hiyo.”

      Kwa kiwango fulani, wanadamu ambao si wakamilifu wamedhihirisha sifa za namna hiyo sikuzote. Katika karne ya 20, tabia hizo zimeongezeka na kuenea. Watu wanaojiendesha katika njia zilizofafanuliwa juu wakati mmoja walionwa kuwa wanaojitenga na watu—ikiwa si waovu waziwazi. Sasa hata watu ‘walio na namna ya ujitoaji-kimungu’ wanazidi kuona tabia hiyo kuwa ya kawaida.

      Wakati mmoja watu wa dini waliliona kuwa jambo lisilofikirika kwa wenzi kuishi pamoja bila kufunga ndoa. Hali ya kuwa mama bila kufunga ndoa ilionwa kuwa yenye kuaibisha, ndivyo na uhusiano wa wagoni-jinsia-moja. Watu wengi waliona utoaji-mimba kuwa jambo lisilokubalika kabisa na ndivyo na talaka. Ukosefu wa ufuatiaji haki katika biashara ulilaumiwa. Lakini leo, kama asemavyo mtu fulani, “jambo lolote linaruhusiwa.” Kwa nini? Sababu moja ni kwamba, “inaridhisha mapenzi ya watu wasiotaka kuambiwa na wengine mambo wasiyopaswa kufanya.”

      Kupuuzwa kwa viwango vya juu vya adili katika karne hii kumefanya mambo ya kutangulizwa yabadilike. Kitabu The Times Atlas of the 20th Century chaeleza: “Katika miaka ya 1900 watu na mataifa bado walikuwa wakikadiria thamani yao pasipo kutegemea pesa. . . . Kufikia mwisho wa karne mataifa yalipima mafanikio yao kwa kutegemea pesa karibu katika visa vyote. . . . Mabadiliko kama hayo yalitukia katika njia ambayo watu waliiona mali.” Leo, zoea la kucheza kamari ambalo limeenea pote huchochea upendo wa pesa, huku redio, televisheni, sinema, na vidio zikichochea tamaa ya vitu vya kimwili. Hata maonyesho ya michezo na mashindano ya biashara hutoa wazo la kwamba ikiwa pesa si mambo yote, angalau ndicho kitu kinachokaribia kuwa cha maana zaidi.

      Twaishi Pamoja Lakini Tukiwa Tumetengana

      Mwanzoni mwa karne ya 20, watu wengi waliishi mashambani. Inasemekana kwamba mapema-mapema mwa karne ya 21, nusu ya idadi ya watu wataishi mijini. Kitabu 5000 Days to Save the Planet chasema: “Kazi ya kuandaa kiwango cha maisha kinachofaa kwa wakazi wa mijini leo, acha vizazi vinavyokuja, yatokeza matatizo yasiyo na kifani.” Gazeti World Health la UM lilisema: “Kiwango cha watu ulimwenguni wanaoishi katika miji kinaongezeka. . . . Mamia ya mamilioni . . . sasa wanaishi katika hali ambazo ni zenye kudhuru afya yao na hata kuhatarisha uhai wao.”

      Ni jambo lisilo la kawaida kwamba watu wanapoishi karibu-karibu katika miji, pia wanazidi kutengana! Televisheni, simu, na Internet, pamoja na mfumo wa ununuzi ingawa ni zenye manufaa, zinafanya uhusiano wa ana kwa ana upuuzwe. Kwa hiyo gazeti la Kijerumani Berliner Zeitung lamalizia: “Karne ya 20 si karne ya kuzidi kwa idadi ya watu pekee. Pia ni karne ya upweke.”

      Jambo hilo huongoza kwenye misiba kama ule uliotukia Hamburg, Ujerumani, ambapo mwili wa mwanamume mmoja ulipatikana ndani ya chumba chake miaka mitano baada ya kufa! Hakuna aliyemkosa, wala watu wa jamaa wala majirani wala wenye mamlaka,” likasema gazeti Der Spiegel, likiongezea: “Kwa raia wengi kisa hicho chaonyesha kiwango chenye kufadhaisha cha kila siku cha kutojulikana na kukosa kujishughulisha na jamii katika miji mikubwa.”

      Makosa kwa hali hizo za kulaumika hayasababishwi tu na sayansi na tekinolojia. Yanasababishwa hasa na watu. Karne hii imetokeza watu wengi kuliko wakati mwingine wowote ambao ni “wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, . . . wasio na shukrani, . . . wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, . . . wasio na upendo wa wema, . . . wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu.”—2 Timotheo 3:1-5.

      1914, Mwaka wa Pekee

      Kulingana na Winston Churchill, “mwanzo wa karne ya ishirini ulionekana kuwa shwari na wenye matumaini.” Wengi walifikiri kwamba ungeleta muhula wa amani na ufanisi usio na kifani. Lakini, mnamo mwaka wa 1905, Mnara wa Mlinzi, Septemba 1 lilionya: “Baada ya muda mfupi kutakuwa na vita vingi zaidi,” pia ukataja kwamba “msiba mkuu” ungeanza mwaka wa 1914.

      Kwa hakika, mapema mwaka wa 1879, kichapo hicho kilitaja mwaka wa 1914 kuwa tarehe muhimu. Katika miaka ya baadaye kilitaja kwamba unabii wa Biblia katika kitabu cha Danieli ulikazia tarehe hiyo kuwa wakati ambapo Ufalme wa Mungu ulisimamishwa huko mbinguni. (Mathayo 6:10) Ingawa mwaka wa 1914 haukuwa wakati wa Ufalme huo kusimamia kabisa mambo duniani, ulikuwa wakati wa kuanza utawala wake.

      Unabii wa Biblia ulitabiri: “Katika siku za wafalme hao [walioko katika siku zetu] Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme [huko mbinguni] ambao hautaangamizwa milele.” (Danieli 2:44) Ufalme huo, Kristo akiwa Mfalme wake, ulianza kukusanya watu wenye kumhofu Mungu hapa duniani wanaotamani kuwa raia wake.—Isaya 2:2-4; Mathayo 24:14; Ufunuo 7:9-15.

      Kwa kusadifiana na kile kilichotukia mbinguni, mwaka wa 1914 ulikuwa mwanzo wa “siku za mwisho,” mwanzo wa kipindi cha wakati ambacho kingeishia kwenye uharibifu wa umalizio wa mfumo wa mambo uliopo sasa. Yesu alitabiri kwamba mwanzo wa kipindi hiki ungeashiriwa na vita vya ulimwengu, upungufu wa chakula, magonjwa ya mlipuko, matetemeko ya dunia yenye kuleta uharibifu na kuongezeka kwa uasi-sheria na vilevile kupoa kwa upendo wa watu kuelekea Mungu na wanadamu. Mambo hayo yote, alisema, yangeashiria “mwanzo wa maumivu makali ya ghafula.”—Mathayo 24:3-12.

      Kutakuwa na Ulimwengu Mpya Kabisa Hivi Karibuni

      Sasa tumeishi katika “siku za mwisho” kwa miaka 85, na tunakaribia haraka sana mwisho wa mfumo huu wa mambo usioridhisha. Karibuni Ufalme wa Mungu, chini ya utawala wa Kristo, “utavunja falme hizi zote [zilizoko sasa] vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:44; 2 Petro 3:10-13.

      Naam, Mungu ataondoa kabisa uovu duniani na kuingiza watu wenye moyo wa uadilifu kwenye ulimwengu mpya kabisa. “Wanyofu watakaa katika nchi, na wakamilifu watadumu ndani yake. Bali waovu watatengwa na nchi.”—Mithali 2:21, 22.

      Ni ujumbe wenye shangwe kama nini—kwa hakika unastahili kutangazwa kila mahali! Hivi karibuni Ufalme wa Mungu utatatua matatizo ambayo yamezidishwa tu na karne ya 20: vita, umaskini, magonjwa, ukosefu wa haki, chuki, kutovumiliana, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, uhalifu, hali ya kutokuwa na furaha, kifo.—Ona Zaburi 37:10, 11; 46:8, 9; 72:12-14, 16; Isaya 2:4; 11:3-5; 25:6, 8; 33:24; 65:21-23; Yohana 5:28, 29; Ufunuo 21:3, 4.

      Je, unavutiwa na taraja la kuishi milele katika ulimwengu wenye uadilifu ulio na furaha isiyoelezeka? Waombe Mashahidi wa Yehova wakupe habari zaidi. Kupitia nakala yako mwenyewe ya Biblia watakuonyesha kwamba miaka muhimu ya badiliko iliyoashiria karne ya 20 itaisha hivi karibuni na kwamba baada ya hapo unaweza kufurahia baraka zisizo na kikomo!

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki