-
Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?Amkeni!—2005 | Desemba 8
-
-
Kukosa Makao Mara kwa Mara
Sabrinaa ni mama asiye na mwenzi anayeishi katika eneo lenye umaskini huko Harlem, New York City. Aliacha shule alipokuwa katika kidato cha pili. Sabrina anaishi pamoja na watoto wake watatu katika makao ya manispaa kwa ajili ya watu wasio na makao daima. Anaishi katika nyumba yenye chumba kimoja cha kulala pamoja na wavulana wake watatu wenye umri wa miezi kumi, miaka mitatu, na miaka kumi. Jiji hilo huandaa makao kwa ajili ya watu wasio na mahali pazuri pa kuishi.
Sabrina alihama nyumba ya mama yake miaka kumi iliyopita. Tangu wakati huo, ameishi na rafiki yake wa kiume, marafiki wengine na watu wa ukoo, na hali yake ilipozidi kuwa ngumu, aliamua kuishi katika makao ya manispaa. Sabrina anasema: “Mara kwa mara nimefanya kazi, mara nyingi nimesuka watu nywele, lakini kwa muda mrefu nimekuwa nikitegemea msaada wa serikali.”
Kama ilivyosimuliwa katika gazeti Parents, jambo linalotatanisha ni kwamba matatizo ya Sabrina yalianza alipopata kazi nzuri ya kutunza vyumba katika hoteli fulani. Alipokuwa akifanya kazi huko, mshahara aliopata ulifanya asistahili kupata msaada wa serikali lakini pesa hizo hazikutosha kugharimia mahitaji yake, kutia ndani nyumba, chakula, mavazi, usafiri, na mahitaji ya mtoto. Hivyo, ilikuwa vigumu kwake kulipa kodi ya nyumba na mwenye nyumba alijaribu kumfukuza. Mwishowe, Sabrina aliacha kazi yake na akaamua kwenda kuishi katika makao ya muda ya manispaa hadi alipopata makao ya kudumu ya manispaa anapoishi sasa.
Sabrina anasema: “Maisha yamekuwa magumu kwa watoto wangu. Tayari mwana wangu mkubwa amekuwa katika shule tatu tofauti. Anapaswa kuwa katika darasa la tano lakini amerudia darasa moja . . . Tumelazimika kuhama mara nyingi sana.” Sabrina anasubiri kupewa nyumba ya serikali.
Huenda watu ambao hawana mahali popote pa kwenda wakaona hali ya Sabrina kuwa afadhali. Hata hivyo, si watu wote hufurahia kuishi katika makao ya manispaa. Kulingana na Tume ya Poland ya Kusaidia Jamii, wengine “wanaogopa nidhamu na sheria za makao ya manispaa” nao hukataa msaada unaotolewa. Kwa mfano, wale wanaoishi katika makao hayo wanatazamiwa kufanya kazi na kujiepusha na kileo na dawa za kulevya. Si kila mtu anayetaka kutii sheria hizo.
-
-
Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?Amkeni!—2005 | Desemba 8
-
-
Msaada kwa Wasio na Makao
Makao fulani ya manispaa hutoa huduma zinazokusudiwa kuwasaidia watu wasio na makao waache kuishi hivyo. Watu hao wanaweza kusaidiwa kupata msaada wa serikali, msaada wa kifedha kutoka kwa mashirika mengine, msaada wa kisheria, kusaidiwa wasitawishe tena uhusiano na familia, au kupewa nafasi za kujifunza ufundi fulani. Makao ya vijana huko London hutoa mashauri kuhusu vyakula, upishi, maisha bora, na jinsi ya kupata kazi. Mashauri hayo yamekusudiwa kufanya watu wajiheshimu zaidi na kuwachochea na kuwasaidia waweze kujitegemea zaidi ili wawe na makao yao wenyewe. Bila shaka, vituo hivyo vinastahili sifa kwa ajili ya maandalizi hayo.
Hata hivyo, si nyakati zote makao ya manispaa huwapa wasio na makao msaada wanaohitaji hasa. Jacek, mmoja wa watu wasio na makao huko Warsaw, anaeleza kwamba maisha katika makao hayo hayamtayarishi mtu kukabiliana na ulimwengu. Anahisi kwamba kwa sababu ya kushirikiana na kuzungumza wao kwa wao tu, watu wanaoishi katika makao hayo huanza “kufikiri kwa njia iliyopotoka.” Anasema, “Makao ambayo hututenga na watu wengine hufanya watu wazima waanze kufikiri kama watoto.” Yeye anaona kwamba ‘akili za wakazi wengi hazifanyi kazi vizuri.’
-
-
Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?Amkeni!—2005 | Desemba 8
-
-
[Picha katika ukurasa wa 6]
Kituo kimoja cha gari-moshi huko Pretoria, Afrika Kusini kiligeuzwa kuwa nyumba za watu wasio na makao
[Hisani]
© Dieter Telemans/Panos Pictures
-