Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?
    Amkeni!—2005 | Desemba 8
    • Kukosa Makao Mara kwa Mara

      Sabrinaa ni mama asiye na mwenzi anayeishi katika eneo lenye umaskini huko Harlem, New York City. Aliacha shule alipokuwa katika kidato cha pili. Sabrina anaishi pamoja na watoto wake watatu katika makao ya manispaa kwa ajili ya watu wasio na makao daima. Anaishi katika nyumba yenye chumba kimoja cha kulala pamoja na wavulana wake watatu wenye umri wa miezi kumi, miaka mitatu, na miaka kumi. Jiji hilo huandaa makao kwa ajili ya watu wasio na mahali pazuri pa kuishi.

      Sabrina alihama nyumba ya mama yake miaka kumi iliyopita. Tangu wakati huo, ameishi na rafiki yake wa kiume, marafiki wengine na watu wa ukoo, na hali yake ilipozidi kuwa ngumu, aliamua kuishi katika makao ya manispaa. Sabrina anasema: “Mara kwa mara nimefanya kazi, mara nyingi nimesuka watu nywele, lakini kwa muda mrefu nimekuwa nikitegemea msaada wa serikali.”

      Kama ilivyosimuliwa katika gazeti Parents, jambo linalotatanisha ni kwamba matatizo ya Sabrina yalianza alipopata kazi nzuri ya kutunza vyumba katika hoteli fulani. Alipokuwa akifanya kazi huko, mshahara aliopata ulifanya asistahili kupata msaada wa serikali lakini pesa hizo hazikutosha kugharimia mahitaji yake, kutia ndani nyumba, chakula, mavazi, usafiri, na mahitaji ya mtoto. Hivyo, ilikuwa vigumu kwake kulipa kodi ya nyumba na mwenye nyumba alijaribu kumfukuza. Mwishowe, Sabrina aliacha kazi yake na akaamua kwenda kuishi katika makao ya muda ya manispaa hadi alipopata makao ya kudumu ya manispaa anapoishi sasa.

      Sabrina anasema: “Maisha yamekuwa magumu kwa watoto wangu. Tayari mwana wangu mkubwa amekuwa katika shule tatu tofauti. Anapaswa kuwa katika darasa la tano lakini amerudia darasa moja . . . Tumelazimika kuhama mara nyingi sana.” Sabrina anasubiri kupewa nyumba ya serikali.

      Huenda watu ambao hawana mahali popote pa kwenda wakaona hali ya Sabrina kuwa afadhali. Hata hivyo, si watu wote hufurahia kuishi katika makao ya manispaa. Kulingana na Tume ya Poland ya Kusaidia Jamii, wengine “wanaogopa nidhamu na sheria za makao ya manispaa” nao hukataa msaada unaotolewa. Kwa mfano, wale wanaoishi katika makao hayo wanatazamiwa kufanya kazi na kujiepusha na kileo na dawa za kulevya. Si kila mtu anayetaka kutii sheria hizo. Kwa hiyo, ikitegemea majira, watu wasio na makao wanaweza kupatikana wakiwa wamelala katika vituo vya gari-moshi, chini ya ngazi, kwenye ghala zilizo chini ya ardhi, na pia kwenye benchi za bustani, chini ya madaraja, na kwenye maeneo ya viwandani. Hali kama hizo ziko ulimwenguni pote.

      Kitabu kimoja kinachozungumzia suala la ukosefu wa makao kinataja mambo mengi yanayochangia tatizo hilo nchini Poland. Yanatia ndani kupoteza kazi, kuwa na madeni, na matatizo ya familia. Kuna ukosefu wa makao kwa wazee, walemavu, na watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI. Watu wengi wasio na makao wana matatizo ya akili na ya kimwili au uraibu, hasa wa kileo. Wanawake wengi wamekuwa bila makao baada ya kuwaacha au kuwatoroka waume zao, kufukuzwa nyumbani kwao, au kwa sababu ya ukahaba. Inaonekana kwamba kila mtu asiye na makao amekuwa na maisha yenye kusikitisha.

      Watu Walioathiriwa na Hali

      Stanisława Golinowska, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya kiuchumi na kijamii, anasema: “Hapa [Poland] hakuna mtu ambaye amekosa makao kwa kupenda. . . . Badala yake, hali hiyo imesababishwa na kukosa mafanikio maishani, ambako kumewafanya watu wavurugike akili na kukata tamaa ya kuishi.” Inaonekana kwamba watu ambao kwa sababu fulani hawawezi kutatua matatizo yao hujikuta bila makao. Kwa mfano, wengine wameachiliwa kutoka gerezani na kupata nyumba zao zimeporwa. Wengine wamefukuzwa. Wengi wamepoteza makao kwa sababu ya misiba ya asili.b

      Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba karibu nusu ya watu wasio na makao nchini Poland wakati mmoja walikuwa na familia na waliishi na wenzi wao, ingawa mara nyingi familia hizo zilikuwa na matatizo. Wengi wao walifukuzwa kutoka nyumbani au walilazimika kuhama kwa sababu ya hali ngumu sana. Ni asilimia 14 pekee walioamua kuondoka.

      Baada ya kuishi katika makao ya manispaa kwa muda fulani, wengine huweza kujiruzuku tena na kujipatia makao. Kwa wengine, inakuwa vigumu sana kutatua tatizo hilo. Labda watu hao huwa bila makao daima kwa sababu ya ugonjwa wa akili au wa kimwili, kutumia vibaya kileo au dawa za kulevya, kutokuwa na kichocheo cha kufanya kazi, mazoea mabaya ya kazi, kukosa elimu ya kutosha, au mchanganyiko wa mambo hayo. Nchini Marekani, asilimia 30 hivi ya watu wasio na makao wameshindwa kujiepusha na kile ambacho shirika moja lisilojipatia faida huita “mfumo wa kutokuwa na makao,” yaani, wakati fulani wanakuwa katika makao ya manispaa, wakati mwingine wako hospitalini, na kwa kusikitisha, nyakati nyingine wanakuwa gerezani. Inasemekana kwamba wale ambao hawawezi kujitoa katika hali hiyo hutumia karibu asilimia 90 ya mapato ya kitaifa yaliyotengwa ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa makao.

  • Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?
    Amkeni!—2005 | Desemba 8
    • [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

      Matokeo ya Ufukara

      Mamia ya maelfu ya watu wanaishi kwenye barabara za majiji ya India. Makadirio ya awali yanaonyesha kwamba watu 250,000 hivi huishi kando ya barabara katika jiji la Mumbai pekee. Makao yao yamejengwa kwa chandarua iliyofungwa kwenye miti na majengo yaliyo karibu. Kwa nini wanaishi hapa badala ya kuishi katika nyumba za bei ya chini karibu na vitongoji vya jiji? Kwa sababu wao ni wafanyabiashara wa rejareja, wachuuzi, waendesha-mikokoteni, au watu wanaookota mikebe na chupa karibu na jiji. Kichapo Strategies to Combat Homelessness kinasema: “Hawana la kufanya. Kwa sababu ya umaskini hawana pesa za kulipa kodi ya nyumba, wana pesa za chakula tu.”

      Wanaume, wanawake, na watoto wapatao 2,300 huishi katika Kituo cha Gari-Moshi cha Park, huko Johannesburg, Afrika Kusini. Wao hulala kwenye sehemu iliyoinuka kando ya njia ya reli, wakilalia matambara ya blanketi au katoni. Wengi wao hawana kazi na hawana matumaini ya kupata kazi. Maelfu ya watu wanaishi katika hali kama hizo kotekote jijini. Hawana maji, vyoo, na umeme. Magonjwa huenea sana katika hali kama hizo.

      Vikundi hivyo viwili vya watu na wengine kama wao hawana makao kwa sababu ya ufukara.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki