-
Je, Maadili ya Biblia Ndiyo Bora Kabisa?Mnara wa Mlinzi—2000 | Novemba 1
-
-
Unyofu Katika Mambo Yote
Kushikamana kwa uaminifu na mwenzi wa ndoa hutaka nguvu za kiadili na kuazimia kufuata kanuni zifaazo. Sifa hizohizo zahitajika ili kuendelea kuwa mnyofu katika ulimwengu usio mnyofu. Biblia husema mengi kuhusu unyofu. Mtume Paulo aliwaandikia hivi Wakristo wa karne ya kwanza katika Yudea: “Twataka kujiendesha wenyewe kwa kufuata haki katika mambo yote.” (Waebrania 13:18) Hiyo yamaanisha nini?
Mtu mnyofu husema kweli na hadanganyi. Hutendea wengine kwa haki—kwa njia ya waziwazi, kwa heshima, bila kuwadanganya au kuwapotosha. Isitoshe, mtu mnyofu ni mwenye uaminifu-maadili na halaghai wanadamu wenzake. Watu wanyofu huchangia hali ya kutumainiana, ambayo hutokeza mitazamo inayofaa na kuendeleza mahusiano thabiti kati ya watu.
Je, watu wanyofu ni wenye furaha? Naam, wana sababu ya kuwa na furaha. Licha ya kuenea kwa ufisadi na ulaghai—au kwa sababu ya kuwepo kwa mambo hayo—kwa ujumla watu wanyofu huvutia wengine. Kulingana na uchunguzi uliofanyiwa vijana, asilimia 70 ya waliohojiwa walisema kwamba unyofu ni sifa bora sana. Zaidi ya hayo, bila kujali tuna umri gani, unyofu ni sifa muhimu tunayotarajia kutoka kwa rafiki zetu.
Christine alifundishwa kuiba tangu alipokuwa na umri wa miaka 12. Baada ya miaka kadhaa akawa stadi wa kuiba kutoka mifukoni mwa watu. “Kuna siku ambazo nilirudi nyumbani na Maki 5,000 za Ujerumani [Dola 2,200 za Marekani] pesa taslimu,” yeye aeleza. Lakini Christine alikamatwa mara kadhaa, naye aliishi kwa hofu ya kufungwa gerezani. Mashahidi wa Yehova walipomweleza yale ambayo Biblia husema juu ya unyofu, Christine alivutiwa na viwango vya maadili vya Biblia. Akajifunza kutii shauri hili: “Mwibaji na asiibe tena.”—Waefeso 4:28.
Wakati alipobatizwa na kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, Christine alikuwa ameacha kuiba. Alikuwa akijitahidi kuwa mnyofu katika mambo yote, kwa kuwa Mashahidi hukazia sana unyofu na sifa nyingine za Kikristo. Gazeti Lausitzer Rundschau laripoti hivi: “Maadili kama vile unyofu, kiasi, na kupenda jirani yanaonwa kuwa ya maana sana katika imani ya Mashahidi.” Christine anahisije juu ya badiliko hilo katika maisha yake? “Sasa nina furaha zaidi kwa sababu nimeacha kuiba. Ninahisi kuwa mshiriki mwenye kuheshimika katika jamii.”
-
-
Je, Maadili ya Biblia Ndiyo Bora Kabisa?Mnara wa Mlinzi—2000 | Novemba 1
-
-
Jamii Nzima Hunufaika
Watu ambao ni waaminifu kwa wenzi wao wa ndoa na ni wanyofu wana furaha na pia hunufaisha jamii kwa ujumla. Waajiri hupendelea wafanyakazi wasiolaghai. Sote hupenda kuwa na majirani waaminifu, na twapenda kununua vitu kwenye maduka ya wafanyabiashara wanyofu. Je, hatuwaheshimu wanasiasa, polisi, na mahakimu wanaojiepusha na ufisadi? Jumuiya hunufaika sana watu wake wanapokuwa wanyofu kwa sababu ya kupenda kanuni, si wakati tu inapofaa kufanya hivyo.
-