-
Pambano Langu na Ugonjwa Wenye KudhoofishaAmkeni!—2001 | Machi 8
-
-
Pambano Langu na Ugonjwa Wenye Kudhoofisha
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA TANYA SALAY
Hadi miaka michache tu iliyopita, nilikuwa mama mwenye shughuli nyingi na mtumishi wa wakati wote katika mji huu mdogo wa Luverne, Alabama. Hali ya maisha huku ni tulivu na ya polepole. Maisha yalikuwa mazuri kwangu na kwa mume wangu, Duke, na mwana wangu mdogo, Daniel. Kisha upasuaji wa kawaida ukabadili maisha yetu kabisa.
MATATIZO yetu yalianza mwaka wa 1992, tumbo langu la uzazi lilipoondolewa. Punde baadaye, nilianza kuwa na maumivu makali yenye kuendelea na kukojoa mara nyingi (mara 50 hadi 60 kwa siku). Mwishowe daktari wangu wa magonjwa ya kina mama alipanga nimwone daktari wa mfumo wa mkojo ili kujaribu kujua kiini cha tatizo hilo.
Nilikwenda hospitalini nipimwe. Katika ziara yangu ya kwanza, daktari wa mfumo wa mkojo alitambua ugonjwa wangu—interstitial cystitis (IC), au uvimbe wa kibofu cha mkojo unaoathiri sehemu nyingine zilizoungana na kibofu. Haikuwa rahisi kutambua ugonjwa wangu kwa sababu dalili za ugonjwa huo zafanana na magonjwa mengine ya mfumo wa mkojo. Zaidi ya hayo, hakuna njia maalum ya kupimia ugonjwa huo. Kwa hiyo, lazima madaktari wafutilie mbali uwezekano wa magonjwa mengine kabla ya kukubali kuwapo kwa ugonjwa wa IC.
Daktari wetu alisema wazi kwamba, kwa kuwa hakuna matibabu yanayofanya kazi, hatimaye kibofu cha mkojo lazima kiondolewe! Alisema kwamba matibabu mengine yapo lakini hayana mafanikio. Bila shaka, habari hiyo ilikuwa pigo kwetu. Hadi wakati huo, nilikuwa nimekuwa mwenye afya nzuri. Kama Mashahidi wa Yehova, mimi na Duke tulikuwa tumetumikia katika huduma ya wakati wote kwa muda wa miaka kadhaa, na sasa niliambiwa kwamba kibofu changu cha mkojo lazima kiondolewe. Nashukuru kwamba mume wangu alinisaidia sana.
Tuliamua kumwona daktari mwingine wa mfumo wa mkojo. Tuliwaona madaktari kadhaa. Kwa kusikitisha, wakati huo madaktari wengi hawakuwa na ujuzi mwingi kuhusu ugonjwa huo. Pia, madaktari wengi wa mfumo wa mkojo wana nadharia zao wenyewe kuhusu ugonjwa wa IC, kwa hiyo matibabu yanayopendekezwa hutofautiana. Jarida moja la kitiba lasema: “Mara nyingi ugonjwa huo ni wa kudumu.” Jarida lingine lasema: “Wanasayansi hawajavumbua matibabu ya interstitial cystitis, wala hawajui ni matibabu gani yatakayomfaa mgonjwa fulani. . . . Kwa kuwa madaktari hawajui kile kinachosababisha ugonjwa huo, matibabu ni ya kutuliza maumivu tu.”
Nilikuwa na maumivu makali sana kwa sababu ya mkakamao na kukojoa mara nyingi hivi kwamba nilikuwa tayari kujaribu chochote kile walichopendekeza madaktari. Nimejaribu dawa 40 mbalimbali na vilevile mitishamba, tiba ya vitobo, nusukaputi ya neva fulani za mwili, kudungwa sindano ya utando wa nje wa uti wa mgongo na sindano ya uti wa mgongo. Na pia matibabu ya transcutaneous electrical nerve stimulation, (TENS), ambayo huhusisha mipwito midogo ya umeme ya kuchochea neva inayopitishwa mwilini kupitia ngozi kwa muda wa dakika au saa kadhaa. Nilifanya utafiti kwa kadiri nilivyoweza, nao ukanisaidia angalau kuelewa kwa kiasi fulani ugonjwa huo.
Kwa sasa, natumia methadone, ambayo ni dawa ya kutuliza maumivu, pamoja na dawa nyingine sita. Pia, huwa ninakwenda kwenye kituo cha afya cha kutuliza maumivu ambapo mimi huchomwa sindano ya utando wa nje wa uti wa mgongo na vilevile kupewa steroidi ili kutuliza maumivu. Ili kupunguza kukojoa mara nyingi, ninakwenda hospitalini kila baada ya miezi mitatu au minne kwa matibabu ya kupanua kibofu cha mkojo kwa kutumia umajimaji. Nimetibiwa kwa njia hiyo mara kadhaa. Kwa ukawaida matibabu hayo hunisaidia kwa muda wa miezi kadhaa. Nimelazwa hospitalini zaidi ya mara 30 katika miaka michache iliyopita.
Vipi matibabu ya mwisho, kuondolewa kwa kibofu cha mkojo? Kitabu kimoja chasema: “Madaktari wengi husita kufanya upasuaji huo kwa sababu tokeo la mgonjwa mmoja-mmoja halitabiriki—baadhi ya wagonjwa wanaopasuliwa wanaendelea kuwa na matatizo.” Kwa hiyo, kwa sasa siufikirii upasuaji.
Nyakati nyingine maumivu ni makali na ya kuendelea hivi kwamba ingekuwa rahisi kukata tamaa. Hata nimewahi kufikiria kujiua. Lakini nilifadhaishwa na wazo la jinsi tendo la aina hiyo lingetia suto jina la Yehova. Naweza kuona umuhimu wa sala na funzo la kibinafsi na vilevile wa kuwa na uhusiano wa karibu na Yehova, kwa kuwa hatujui kinachoweza kutukia na kubadili maisha yetu. Uhusiano wa karibu pamoja na Yehova umeokoa maisha yangu nilipokuwa mgonjwa, la sivyo ningekuwa nimejiua.
Ninapofikiria miaka hiyo tisa naona jinsi maisha yawezavyo kubadilika haraka. Naelewa maana ya maneno ya Mhubiri 12:1, lisemalo hivi: “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijaja siku zilizo mbaya, wala haijakaribia miaka utakaposema, mimi sina furaha katika hiyo.” Ninashukuru kwamba nilianza kufanya utumishi wa wakati wote nilipokuwa na umri wa miaka 15 na kuweza kuendelea kwa muda wa miaka 20 hivi. Wakati huo nilisitawisha uhusiano wa karibu na Yehova.
Ninamshukuru Yehova kwa mume wangu na mwana wangu Daniel, ambao wamenisaidia. Pia ninatiwa moyo sana akina ndugu na dada wa kutaniko wanaponipigia simu au kunitembelea. Siwezi kutoka sana wakati wa majira ya baridi kali kwa kuwa baridi huzidisha mkakamao. Kwa hiyo, wakati wa baridi natoa ushuhuda kupitia simu, na jambo hilo lanisaidia kushikilia tumaini la Paradiso na kulidumisha kuwa halisi kwangu. Natazamia wakati magonjwa na mateso yatakapokuwa yamepita na hayatakumbukwa tena.—Isaya 33:24.
-
-
Interstitial Cystitis Ni Ugonjwa wa Aina Gani?Amkeni!—2001 | Machi 8
-
-
Interstitial Cystitis Ni Ugonjwa wa Aina Gani?
UGONJWA wa Interstitial Cystitis ni aina ya uvimbe wa kibofu cha mkojo. Wanawake wengi hushikwa na uvimbe wa kibofu cha mkojo kuliko wanaume. Hata hivyo, kuna uvimbe wa kibofu cha mkojo wa aina nyingi wenye vyanzo mbalimbali.
Baadhi ya dalili za kawaida ni zipi? Kukojoa mara nyingi na kukojoa kwa shida au kwa maumivu makali, kama mwasho mkali sana. Lakini namna gani ugonjwa wa interstitial cystitis wenye kudumu? Huo ni tofauti jinsi gani?a
Dakt. Susan Keay, mtaalamu wa ugonjwa huo, akubali kwamba: “ Ni vigumu kutambulisha ugonjwa huo, na ni vigumu hata zaidi kuutibu.” Kisha akasema kwamba ugonjwa huo “waweza kutaabisha mtu kwa miaka mingi. Ugonjwa wa IC husababisha maumivu makali, ni wa muda mrefu, na wenye kubadili maisha ya mgonjwa, nao waweza kudumu kwa makumi ya miaka.” Kwa kusikitisha, kwa muda mrefu, madaktari hawakukubali kwamba ugonjwa huo ni halisi, nao walidokeza kwamba wagonjwa waliuwazia tu. Hata hivyo, kama vile daktari mmoja asemavyo, “kutambulisha dalili za ugonjwa huo kwaweza kumsaidia mgonjwa kihisia.”
Ripoti moja yaonyesha kwamba watu 700,000 huko Marekani wana ugonjwa wa IC, “na idadi hiyo ni maradufu ya idadi iliyowahi kuripotiwa.” Sasa inajulikana kwamba, wanaume kadhaa wanadhaniwa kuwa na ugonjwa wa tezi kibofu, ilhali wana ugonjwa wa IC. Bila shaka, ugonjwa wa IC huathiri pia watu wengi wasio na ugonjwa huo—hasa washiriki wa familia na wengine wanaoishi na wagonjwa hao ambao daima wana maumivu makali. Kwa wazi, ugonjwa huo humzuia mtu asifanye kazi ifaavyo nyumbani au kazini. Wengi hawana budi kuacha kazi. Mgonjwa aweza kupatwa na maumivu wakati wa ngono.
Kwa kuwa bado hakuna tiba, madaktari wajitahidi kutuliza maumivu. Matibabu ya kutuliza maumivu ni yapi?
Kutuliza Wala Si Kutibu
Matibabu ya kwanza yanayopendekezwa na Dakt. Grannum R. Sant, wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Tuft na Kituo cha Tiba cha New England, ni dawa za mizio, dawa za kupunguza wasiwasi, au pentosan polysulfate, ambazo ni za kumeza.b
Baadhi ya madaktari hupendekeza matibabu ya kupanua kibofu cha mkojo, yaliyoelezwa katika makala iliyotangulia. Kila matibabu yaweza kutuliza maumivu kwa muda wa miezi michache au hata kwa mwaka mmoja. Kisha kuna matibabu ambayo hufanywa ndani ya kibofu cha mkojo kwa kutumia dawa ya dimethyl sulfoxide, (DMSO). Matibabu ya DMSO, ambayo yameidhinishwa na Shirika la Marekani la Usimamizi wa Chakula na Dawa, yaweza kutuliza maumivu kwa muda wa miaka miwili. Hata hivyo, Dakt. Kenneth Peters, ambaye ni daktari wa mfumo wa mkojo, anatilia shaka matibabu hayo, kwa kuwa yaweza kusababisha damu kuganda na matatizo mengine.
Matibabu ambayo yamejaribiwa katika uchunguzi wa majuzi wa Dakt. Peters yahusisha kuingiza bakteria ya Bacillus Calmette-Guerin (BCG) katika kibofu cha mkojo. Aandika kwamba,“BCG ni bakteria dhaifu ya ugonjwa wa kifua kikuu ambayo haina nguvu ya kusababisha ugonjwa huo.” Yaonekana inafanya kazi kwa kuongeza nguvu mfumo wa kinga wa mwili. Jaribio lililofanywa kwenye kituo cha afya lilionyesha kwamba asilimia 60 ya wagonjwa walipata nafuu walipotibiwa kwa BCG. Wagonjwa waliendelea kuchunguzwa kwa muda wa miaka miwili. Matokeo yalikuwa yapi? Dakt. Peters asema kwamba “tatizo la kukojoa mara nyingi na maumivu yalipungua kwa asilimia 90 kwa wale waliopata nafuu walipotibiwa kwa BCG.”
Wagonjwa kadhaa wamepata nafuu kwa kutumia dawa ya Elmiron. Dakt. Raymond Hurm asema kwamba, “dawa hiyo huongeza utando wa kibofu cha mkojo.” Dawa hiyo hufanya kazi polepole, lakini kama vile mgonjwa mmoja alivyosema, ‘dawa ya Elmiron hunisaidia kuvumilia ugonjwa wangu wa kibofu cha mkojo.’
Dawa nyingine itumiwayo katika majaribio ni Cystistat, au hyaluronic acid. “Dawa hiyo huingizwa ndani ya kibofu cha mkojo moja kwa moja, na inadhaniwa kwamba hiyo hubadili utando wenye kasoro wa kibofu cha mkojo na utando mpya. . . . Majaribio yameanzishwa sasa [1988] kwenye vituo vya afya kule Marekani. Matokeo hayajulikani wakati huu.” Dawa hiyo imeidhinishwa kutumiwa Ulaya lakini bado haijaidhinishwa Marekani.
Beth Getz, ambaye ni mwuguzi na pia msimamizi wa kikundi cha wagonjwa wenye ugonjwa wa IC aliandika hivi: “Mara kwa mara wagonjwa husitasita kuwauliza madaktari juu ya matibabu mengine . . . , kwa sababu wanafikiri jambo hilo lingedokeza kwamba hawajaridhika na matibabu wanayopewa. Leo, madaktari wa mfumo wa mkojo wanaotibu wagonjwa wenye ugonjwa huo huamini ubora wa kutumia matibabu mbalimbali, kutia ndani matibabu ya mitishamba na kadhalika, bora matibabu hayo yasihatarishe mgonjwa.”
Njia nyingine ya kukabiliana na maumivu ya kudumu ya nyonga ni kujiandikisha katika kituo cha afya cha kutuliza maumivu. Matibabu yaweza kutia ndani kupitisha mipwito ya umeme ya kuchochea neva, iliyoelezwa katika makala iliyotangulia; nusukaputi ya neva za sehemu fulani za mwili; tiba ya vitobo; matibabu ya kisaikolojia; na ratiba za kusaidia wagonjwa kuishi maisha ya kawaida.
Mwandishi wa Amkeni! alisema na Dakt. Peters, aliyenukuliwa mapema, juu ya matatizo ya wagonjwa wanaokojoa mara 40-50 kwa siku. Apendekeza utumiaji wa chombo cha kuchochea neva za sehemu ya chini ya uti wa mgongo na nyonga, chombo hicho chaweza kupunguza uhitaji wa kukojoa hadi mara sita kwa siku. Wagonjwa wanaochagua matibabu yajulikanayo Marekani kama InterStim Therapy huwekewa kifaa kidogo tumboni. Kifaa hicho hupeleka mipwito ya umeme hadi neva za uti wa mgongo za nyonga, ambazo huongoza utendaji wa kibofu cha mkojo.
Upasuaji, ambao yasemekana ni matibabu ya mwisho, hauna uhakika wa mafanikio. “Matokeo ya upasuaji wa kibofu kwa sababu ya ugonjwa huo hutofautiana,” asema Dakt. Sant. “Wagonjwa wengi ambao wameondolewa kibofu cha mkojo huendelea kuwa na maumivu yenye kudumu nyongani na katika mfupa wa kinena hata baada ya upasuaji.” Kwa hiyo, ushauri wa wataalamu ni kwamba, Usiwe na haraka kupasuliwa ili kuondolewa kibofu cha mkojo, isipokuwa hakuna lingine la kufanya na baada ya kufikiria jambo hilo kwa uzito.
Matumaini ya Wakati Ujao
Shirika la Interstitial Cystitis, la Rockville, Maryland, Marekani, lasema hivi: “Ijapokuwa haielekei kwamba watafiti watapata tiba moja tu itakayosaidia wagonjwa wote wenye ugonjwa huo, yaelekea kwamba wagonjwa wengi watasaidiwa kupitia njia mpya za kutambulisha ugonjwa huo, matibabu mapya, na matibabu mbalimbali yaliyounganishwa. Mara tuelewapo chanzo (huenda kikawa zaidi ya moja) cha ugonjwa huo, kuvumbua tiba (huenda ikawa zaidi ya moja) kutakuwa rahisi zaidi.” Mamilioni ya wagonjwa wenye ugonjwa wa IC wanangoja kwa hamu kusikia jambo hilo!
[Maelezo ya Chini]
a Uvimbe wa kibofu cha mkojo unaosababisha kidonda, unaojulikana kama Hunners, husababisha vidonda kwenye matabaka yote ya ukuta wa kibofu cha mkojo.
b Amkeni! haliungi mkono yoyote kati ya matibabu yanayozungumziwa hapa. Twapendekeza wagonjwa wote waombe madaktari wao ushauri kuhusu matibabu na dawa. Kusudi la Amkeni! ni kuarifu msomaji juu ya matibabu yanayopatikana kulingana na madaktari na wataalamu wengine.
[Sanduku katika ukarasa wa 21]
Kutegemezwa Kihisia
Wataalamu wasema kwamba kuungwa mkono na familia, marafiki na wagonjwa wengine wenye ugonjwa wa IC humsaidia mgonjwa mwenye ugonjwa huo kukabiliana na ugonjwa wake. Na wagonjwa wanaojifunza kuhusu ugonjwa wao na kujishughulisha wenyewe katika matibabu, hupata nafuu haraka zaidi.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Vyakula Vipaswavyo Kuepukwa
Hata ingawa hakuna majaribio yaliyofanywa kwenye kituo cha afya yanayoonyesha kwamba ugonjwa huo huzidishwa na vyakula fulani, madaktari na wagonjwa wengi wameona uhusiano fulani. Dakt. Kenneth Peters, daktari wa mfumo wa mkojo, asema kwamba wagonjwa kadhaa wanaathiriwa na vyakula fulani na kwamba kila mmoja apaswa kuhakikisha ni vyakula vya aina gani vinavyozidisha matatizo. Yeye apendekeza kwamba kafeini na vileo visitumiwe. Nyanya na matunda ya jamii ya chungwa pia yaonekana kuathiri mgonjwa mwenye ugonjwa huo. Hata hivyo, ni muhimu sana mgonjwa ale vyakula mbalimbali vyenye lishe. Baadhi ya wagonjwa wenye ugonjwa wa IC wasema kwamba vyakula vinavyowafaa ni mchele, viazi, makaroni, mboga, nyama, na kuku. Pia, mgonjwa akinywa maji mengi, asidi katika kibofu cha mkojo haitakuwa kali sana na hivyo kupunguza mwasho katika kibofu cha mkojo.
Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya vyakula vya kuepuka.
Anchovy
Apricot
Asidi ya limau
Aspartame
Cantaloupe
Caviar
Chai
Chokoleti
Chumvi
Cranberry
Ini
Jabini chachu
Kiungo cha saladi
Fava
Lima
Makokwa
Makomamanga
Malai yaliyoganda
Mananasi
Maparachichi
Mapichi
Matofaa
Mayonezi
Maziwa yaliyoganda
Rai (rye)
Mkate chachu
Ndizi
Nectarine
Nyama na samaki za mkebe
Nyama ya ng’ombe iliyokaushwa
Plamu
Rubabu
Saccharine
Siki
Soda
Soy sauce
Strawberry (stroberi)
Tofu
Tumbako
Vitunguu
Vyakula visivyo na lishe
Vikolezo
Zabibu
[Hisani]
Urologic Nursing, April 2000, Volume 20, Number 2
-