Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Kazi ya Muda Mrefu Yamalizika”
    Amkeni!—1998 | Novemba 22
    • “Kazi ya Muda Mrefu Yamalizika”

      MIAKA 50 iliyopita, mwanamke aliyekuwa katika umri wa miaka 60 alizungumza, ulimwengu ukasikiliza. Ilitukia Paris mnamo Desemba 10, 1948. Kusanyiko Kuu la Umoja wa Mataifa lilikuwa limekusanyika katika jengo la Palais Chaillot lililokuwa limejengwa karibuni wakati msimamizi wa Tume ya UM ya Haki za Kibinadamu alipoamka ili kutoa hotuba. Kwa sauti yenye nguvu, Eleanor Roosevelt, mjane mrefu wa aliyekuwa Rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt, aliwaambia hivi wale waliokusanyika: “Leo tumefikia tukio kuu la Umoja wa Mataifa na maisha ya wanadamu, yaani idhini ya Kusanyiko Kuu la Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu.”

      Baada ya kusoma mafungu yaliyo wazi sana ya dibaji ya Azimio hilo na mafungu yake 30, Kusanyiko Kuu liliidhinisha hati hiyo.a Kisha, ili kutoa heshima kwa uongozi usio na kifani wa Bi. Roosevelt, washiriki wa UM walimpa heshima huyo “Bibi wa Kwanza wa Dunia,” kama alivyokuwa akiitwa, kwa kumshangilia. Mwishoni mwa siku hiyo, aliandika: “Kazi ya muda mrefu yamalizika.”

      Kutoka Maoni Mengi Hadi Azimio Moja

      Miaka miwili awali, mnamo Januari 1947, punde tu baada ya kazi ya tume ya UM kuanza, ilikuwa dhahiri kwamba kutunga hati ya haki za kibinadamu ambayo ingekubaliwa na washiriki wote wa UM kungekuwa kazi ngumu sana. Kutoka mwanzo, kutokubaliana kwingi kuliingiza tume hiyo yenye washiriki 18 kwenye mabishano mengi. Mjumbe wa Wachina alihisi kwamba hati hiyo ilipaswa kutia ndani falsafa za Confucius, mshiriki Mkatoliki wa tume hiyo aliendeleza mafundisho ya Thomas Aquinas, Marekani iliunga mkono Mswada wa Haki wa Marekani, na Wasovieti walitaka mawazo ya Karl Marx yatiwe ndani—na haya yalikuwa baadhi ya maoni machache tu yenye kushikiliwa sana yaliyotajwa!

      Bi. Roosevelt alivumilia mabishano yenye kuendelea baina ya washiriki wa tume hiyo. Mnamo 1948, wakati alipokuwa akitoa hotuba katika Paris, Sorbonne, alitaja kwamba alifikiri kwamba kulea familia yake kubwa kulimfanya avumilie mpaka mwisho. Hata hivyo, inaripotiwa kuwa aliwafurahisha wasikilizaji kwa kusema kwamba, “kusimamia Tume ya Haki za Kibinadamu kulihitaji saburi hata zaidi.”

      Ijapokuwa hivyo, ni wazi kwamba uzoefu aliokuwa nao akiwa mama ulisaidia. Wakati huo, ripota mmoja aliandika kwamba namna Bi. Roosevelt alivyoshughulika na washiriki wa tume ilimkumbusha mama “anayesimamia familia kubwa yenye wavulana wenye kelele, ambao nyakati nyingine ni watukutu lakini wenye moyo mzuri, ambao pindi kwa pindi huhitaji nidhamu imara.” (Eleanor Roosevelt—A Personal and Public Life) Ingawa hivyo, kwa kuongezea uthabiti kwenye uzuri wake, aliweza kuwasadikisha wengine bila kufanya wapinzani wake kuwa maadui.

      Tokeo likawa kwamba baada ya miaka miwili ya mikutano, mamia ya marekebisho, maelfu ya taarifa, na duru 1,400 za kupigia kura karibu kila neno na kila kifungu, tume hiyo iliweza kutokeza hati iliyoorodhesha haki za kibinadamu ambazo iliamini kwamba wanaume na wanawake wote ulimwenguni, wanapaswa kuwa nazo. Hati hiyo iliitwa Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu. Hivyo kazi ambayo nyakati fulani ilionekana kuwa haiwezekani, ikakamilishwa.

      Mataraja Makuu

      Bila shaka, haikutazamiwa kwamba uonezi ungemalizika kwa kuanzishwa kwa hili azimio la haki za kibinadamu. Na bado, kuidhinishwa kwa hilo Azimio kwa Wote kulitokeza mataraja makuu. Msimamizi wa Kusanyiko Kuu la UM wakati huo, Dakt. Herbert V. Evatt wa Australia, alitabiri kwamba “mamilioni ya wanaume, wanawake, na watoto ulimwenguni pote, wanaoishi mbali sana na Paris na New York, wataendea hati hii kwa msaada, mwongozo, na kichocheo.”

      Miaka 50 imepita tangu Dakt. Evatt aseme maneno hayo. Katika kipindi hicho, kwa kweli wengi wameliona Azimio hilo kuwa mwongozo na wamelitumia kupima kiwango cha kuheshimu haki za kibinadamu ulimwenguni pote. Walipofanya hivyo, walipata nini? Je, mataifa wanachama wa UM wanafikia kipimo hiki? Hali ya haki za kibinadamu ikoje ulimwenguni leo?

      [Maelezo ya Chini]

      a Nchi 48 ziliunga mkono uamuzi huo, hakuna iliyopinga. Hata hivyo, leo, mataifa yote 185 ambayo ni wanachama wa UM, kutia ndani yale yaliyojiondoa katika mwaka wa 1948, yameidhinisha Azimio hilo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 4]

      Haki za Kibinadamu Ni Nini?

      Umoja wa Mataifa wafasili haki za kibinadamu kuwa “zile haki ambazo tumerithi kiasili na ambazo bila hizo hatuwezi kuishi kama binadamu.” Pia haki za kibinadamu zimefafanuliwa kuwa “lugha ya kawaida ya binadamu”—na kwa kufaa. Kama vile uwezo wa kusema lugha ulivyo sifa ya kurithi ambayo hututofautisha sisi wanadamu, kuna mahitaji na sifa nyingine za kuzaliwa ambazo hututofautisha na viumbe vinginevyo duniani. Mathalani, wanadamu wana uhitaji wa ujuzi, kujieleza vizuri, na hali ya kiroho. Binadamu ambaye ananyimwa kutimiza mahitaji haya ya msingi hulazimika kuishi maisha yasiyostahili binadamu. Ili kuwalinda wanadamu wasinyimwe uhitaji huo, aeleza wakili mmoja wa haki za kibinadamu, “sisi hutumia neno ‘haki za kibinadamu’ badala ya ‘mahitaji ya binadamu’ kwa sababu kwa kusema kisheria neno ‘uhitaji’ si nzito kama neno ‘haki.’ Kwa kutumia neno ‘haki’ tunakuza utoshelezaji wa haki za kibinadamu kuwa kitu ambacho kila binadamu anapaswa kuwa nacho kiadili na kisheria.”

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

      Azimio la Haki za Kibinadamu kwa Wote

      Mwandishi aliye pia mshindi wa Tuzo la Nobel Aleksandr Solzhenitsyn alitaja Azimio kwa Wote kuwa “hati bora kabisa” iliyopata kuandikwa na UM. Kutazama kifupi yaliyomo huonyesha kwa nini wengi hukubaliana naye.

      Falsafa ya msingi ya Azimio hilo inapatikana katika Kifungu cha 1: “Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika adhama na haki. Wamejaliwa kuwa na uwezo wa kusababu na dhamiri na wanapaswa kutendeana kwa roho ya udugu.”

      Kwenye msingi huu, wenye kubuni Azimio hilo walipata vikundi viwili vya haki za kibinadamu. Kikundi cha kwanza kinaonyeshwa katika Kifungu cha 3: “Kila mtu ana haki ya kuishi, kuwa na uhuru na usalama.” Kifungu hiki chaweka msingi wa haki za mtu za kiraia na kisiasa zinazoorodheshwa katika Kifungu cha 4 hadi cha 21. Kikundi cha pili chategemea Kifungu cha 22, ambacho kwa sehemu chasema kwamba kila mtu ana haki za kutambua haki “za lazima za kukuza adhama yake na kuendeleza uhuru wa utu wake.” Kinaunga mkono Kifungu cha 23 hadi 27, kinachoonyesha waziwazi haki za mwanadamu za kiuchumi, kijamii, na kitamaduni. Azimio kwa Wote lilikuwa hati ya kwanza ya kimataifa kutambua kikundi hiki cha pili cha haki kuwa kimetiwa ndani ya haki za msingi za kibinadamu. Pia lilikuwa hati ya kwanza kabisa ya kimataifa kutumia usemi “haki za kibinadamu.”

      Mwanasoshiolojia Mbrazili Ruth Rocha aeleza waziwazi kile ambacho Azimio kwa Wote lituambiavyo: “Haidhuru wewe ni wa jamii gani. Haidhuru kama wewe ni mwanamume au mwanamke. Haidhuru unasema lugha gani, dini yako ni gani, maoni yako ya kisiasa ni gani, wewe ni wa nchi gani au familia yako ni gani. Haidhuru kama u tajiri au maskini. Haidhuru unatoka sehemu gani ya ulimwengu; kama nchi yako ni ufalme au ni jamhuri. Haki hizi na uhuru huu wapaswa kufurahiwa na kila mmoja.”

      Tangu lianze kutumiwa, Azimio kwa Wote limetafsiriwa katika lugha 200 na limekuwa sehemu ya katiba za nchi nyingi. Hata hivyo, leo, viongozi fulani wanahisi kwamba Azimio hilo lapaswa kuandikwa upya. Lakini Katibu Mkuu wa UM Kofi Annan anapinga jambo hilo. Ofisa mmoja wa UM anamnukuu akisema: “Kama vile hakuna uhitaji wa kuandika upya Biblia au Korani, hakuna uhitaji wa kurekebisha Azimio hilo. Kinachohitaji kurekebishwa, si maandishi ya Azimio kwa Wote, bali mwenendo wa wafuasi wake.”

      Katibu Mkuu wa UM Koffi Annan

  • Mataraja Kutoka Orofa ya 29
    Amkeni!—1998 | Novemba 22
    • Mataraja Kutoka Orofa ya 29

      UNAPOTOKA katika lifti kwenye orofa ya 29 ya jengo la Umoja wa Mataifa katika New York City, ishara ndogo ya samawati huonyesha njia inayoelekeza kwenye Ofisi ya Mjumbe Mkuu wa Haki za Kibinadamu (OHCHR). Ofisi hii ya upatanisho huwakilisha makao makuu ya OHCHR katika Geneva, Uswisi—kitovu cha utendaji wa UM wa haki za kibinadamu. Huku Mary Robinson, Mjumbe Mkuu wa Haki za Kibinadamu, akisimamia ofisi za OHCHR katika Geneva, Elsa Stamatopoulou mzaliwa wa Ugiriki ndiye msimamizi wa ofisi ya New York. Mapema mwaka huu, Bi. Stamatopoulou alimpokea vizuri mwandishi wa Amkeni! wakachunguza utendaji wa haki za kibinadamu katika miongo mitano iliyopita. Yafuatayo ni madondoo ya mahojiano hayo.

      Swali. Unahisi ni maendeleo gani yamefanywa kuendeleza haki za kibinadamu?

      Jibu. Nitakupa mifano mitatu ya maendeleo: Kwanza, miaka 50 iliyopita hakukuwa na wazo la haki za kibinadamu katika ajenda ya kimataifa; leo linapatikana kila mahali na linatenda. Serikali ambazo hazikupata kusikia juu ya haki za kibinadamu miongo kadhaa iliyopita sasa zinazungumza juu yake. Pili, sasa tuna mfumo wa sheria wa kimataifa, au kitabu cha sheria, chenye mikataba mingi ya kimataifa inayoambia serikali kwa maandishi daraka lake kuelekea raia zake. [Ona sanduku “Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu,” katika ukurasa wa 7.] Ilichukua muda wa miaka mingi kubuni mfumo huu wa sheria. Tunauonea fahari sana. Kielelezo cha tatu ni kwamba leo watu wako tayari kuliko wakati mwingine wowote kujiunga na harakati za haki za kibinadamu na wanaweza kujieleza wenyewe waziwazi kuhusu masuala ya haki za kibinadamu.

      Swali. Kuna vizuizi vipi?

      Jibu. Bila shaka, baada ya kufanya kazi na mashirika ya UM ya haki za kibinadamu kwa miaka 17, natambua kwamba tunakabili matatizo yenye kuvunja moyo. Tatizo kubwa zaidi ni kwamba mara nyingi serikali huona haki za kibinadamu kuwa suala la kisiasa badala ya suala la kibinadamu. Huenda zisiwe tayari kutekeleza mikataba ya haki za kibinadamu kwa sababu zinahisi kuwa zinatishwa kisiasa. Katika visa hivyo, mikataba ya haki za kibinadamu haitumiki. Kizuizi kingine kimekuwa kushindwa kwa UM kuzuia ukiukaji mzito wa haki za kibinadamu katika sehemu kama vile ile iliyokuwa Yugoslavia, Rwanda na hivi karibuni zaidi, Algeria. Kushindwa kwa UM kuzuia mauaji ya kinyama yaliyotokea katika nchi hizi ni kosa kubwa sana. Kuna njia za kutekeleza haki za kibinadamu, lakini mtu fulani apaswa kuzitekeleza. Ni nani atakayezitekeleza? Ikiwa faida za nchi ambazo zingeandaa ulinzi hazihatarishwi, mara nyingi nchi hizo hukosa nia ya kisiasa ya kujitokeza kukomesha ukiukaji.

      Swali. Ni nini unachotazamia?

      Jibu. Ninaona tisho na ahadi kwenye barabara inayoelekeza kwenye haki za kibinadamu kwa wote. Kinachonitia wasiwasi ni tisho linalotokezwa na uchumi wa tufeni pote unaochochea mashirika makubwa yaanze kutenda katika nchi ambako ni rahisi kupata wafanyakazi wa malipo ya chini. Leo, ikihitajika, tunaweza kuzilaumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kuziwekea msongo mkubwa. Lakini ni nani tunayeweza kumlaumu kwa ukiukaji huu wakati ambapo mikataba ya kibiashara inayohusisha pande nyingi inapozidi kupunguza nguvu za serikali na kuimarisha mashirika ya kiuchumi? Kwa kuwa hatudhibiti mashirika haya ya kiuchumi, inadhoofisha msimamo wa mashirika baina ya serikali mbalimbali kama vile UM. Kuhusu haki za kibinadamu, mwelekeo huu ni wenye kudhuru. Sasa ni jambo muhimu kuhusisha mashirika ya kibiashara katika haki za kibinadamu.

      Swali. Vipi juu ya ahadi uliyotaja?

      Jibu. Ukuzi wa utamaduni wa haki za kibinadamu wa tufeni pote. Namaanisha kwamba kupitia elimu twapaswa kufahamisha watu juu ya haki za kibinadamu. Bila shaka, hilo ni tatizo gumu kwa sababu linatia ndani badiliko la akili. Ndiyo sababu, miaka kumi iliyopita, UM ulianzisha kampeni ya habari ya peupe ya ulimwenguni pote ili kuelimisha watu kuhusu haki zao na kuelimisha nchi juu ya madaraka yao. Kwa kuongezea, UM umechagua miaka ya 1995 hadi 2004 kuwa “Mwongo wa Elimu ya Haki za Kibinadamu.” Inatumainiwa kwamba huenda elimu ikabadili akili na mioyo ya watu. Huenda jambo hili likasikika kuwa Gospeli, lakini inapohusu elimu ya haki za kibinadamu, mimi ni mwamini wa kweli. Ninatumaini ulimwengu utatumia utamaduni wa haki za kibinadamu kuwa itikadi yake katika karne inayofuata.

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu

      Mbali na Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu, pia kuna Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu. Zinahusianaje?

      Naam, ukilinganisha Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu na kitabu chenye sura tano, basi Azimio kwa Wote laweza kulinganishwa na sura ya 1. Sura ya 2 na ya 3 ni Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni. Na kila moja ya sura ya 4 na ya 5 ina Itifaki ya Hiari.

      Ingawa Azimio kwa Wote linaonwa kuwa lina mafaa ya maadili, likiyaambia mataifa mambo yapaswayo kufanya, hati hizi nne za ziada ni makubaliano ya kisheria, zikiambia mataifa mambo ambayo ni lazima yafanye. Ingawa kazi kuhusu hati hizi ilianza katika mwaka wa 1949, ilichukua miongo kadhaa kabla hazijaanza kutenda. Leo, hati hizi nne pamoja na Azimio kwa Wote hufanyiza Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu.

      Mbali na huu Mswada wa Kimataifa, UM umeidhinisha zaidi ya mikataba mingine 80 ya haki za kibinadamu. “Kwa hiyo ni kosa kufikiri kwamba mikataba ya haki za kibinadamu katika Mswada wa Kimataifa ndiyo ya maana zaidi,” asema mtaalamu mmoja wa haki za kibinadamu. “Kwa kielelezo, Mkataba wa 1990 juu ya Haki za Mtoto ndiyo hati ambayo imekubaliwa zaidi na ya ulimwenguni pote ya UM, na bado hiyo si sehemu ya Mswada wa Kimataifa. Usemi ‘Mswada wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu’ ulitungwa kwa makusudi ya kujulikana badala ya kuwa dhana rasmi. Na utakubali kwamba ni usemi wenye kuvutia.”a

      [Maelezo ya Chini]

      a Kufikia wakati wa kuandika, mataifa 191 (mataifa wanachama 183 wa UM pamoja na mataifa 8 yasiyokuwa wanachama) yameidhinisha Mkataba wa Haki za Mtoto. Ni nchi mbili tu ambazo hazijauidhinisha: Somalia na Marekani.

  • Haki za Kibinadamu na Makosa Leo
    Amkeni!—1998 | Novemba 22
    • Haki za Kibinadamu na Makosa Leo

      HIVI karibuni watetezi wa haki za kibinadamu walitimiza jambo kubwa. Kwanza, waliunganisha mashirika zaidi ya 1,000 katika nchi 60 katika harakati iliyoitwa Kampeni ya Kimataifa ya Kupiga Marufuku Makombora ya Ardhini (ICBL). Kisha, wakahimiza mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku silaha hizi. Baada ya hilo, harakati ya ICBL na mkurugenzi wake asiyechoka, mtetezi Mmarekani Jody Williams, akashinda Tuzo la Amani la Nobel la 1997.

      Ingawa hivyo, mafanikio kama haya, hufuatana na matangazo yenye kuamsha fikira. Kama lisemavyo Human Rights Watch World Report 1998, haki za kibinadamu za kotekote zingali “zinashambuliwa.” Na si kwamba udikteta wa hali ya chini na usiofaa ndio unaolaumiwa tu. “Mataifa yenye nguvu,” yasema ripoti hiyo, “yalionyesha mwelekeo dhahiri wa kupuuza haki za kibinadamu zilipohitilafiana na mapendezi yao ya kiuchumi—taabu iliyo kawaida katika Ulaya na Marekani.”

      Kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote, ni vigumu kupuuza ukiukaji wa haki za kibinadamu. Hali yao mbaya ya kila siku ingali ina ubaguzi, umaskini, njaa, mnyanyaso, kubakwa, kutenda watoto vibaya, utumwa, na kifo chenye jeuri. Kwa wahasiriwa hawa hali zenye kutumainiwa zilizoahidiwa katika mikataba mingi ya haki za kibinadamu haziwezi kufikiwa wala hazina maana yoyote kwao. Kwa kweli, kwa wanadamu wengi, hata haki za msingi zinazoorodheshwa katika vifungu 30 vya Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu zimekosa kutimizwa. Kwa kielelezo, fikiria kifupi jinsi haki nyingine bora zilizotajwa katika Azimio zinavyotumika katika maisha ya kila siku.

      Usawa kwa Wote?

      Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika adhama na haki.—Kifungu cha 1.

      Mswada wa kwanza wa Kifungu cha 1 cha Azimio kwa Wote ulisema: “Wanaume wote . . . ni sawa.” Hata hivyo, ili kuhakikisha kwamba taarifa hii haitaeleweka kumaanisha kwamba wanawake hawatiwi ndani, washiriki wa kike kwenye tume iliyotayarisha mswada huu walisisitiza kwamba lugha hiyo ibadilishwe. Walishinda, na “wanaume wote . . . ni sawa” ikawa “wanadamu wote . . . ni sawa.” (Italiki ni zetu.) Lakini je, kubadilishwa kwa lugha ya kifungu hiki kulibadili fungu la wanawake?

      Mnamo Desemba 10, 1997, Siku ya Haki za Kibinadamu, Mke wa Rais wa Marekani, Hillary Clinton, aliuambia UM kwamba ulimwengu unaendelea “kuwatenda wanawake kama raia duni.” Alitoa vielelezo kadhaa: Kati ya watu maskini ulimwenguni, asilimia 70 ni wanawake. Thuluthi mbili ya watoto milioni 130 ulimwenguni wasio na uwezo wa kwenda shuleni ni wasichana. Thuluthi mbili za watu milioni 96 wasiojua kusoma na kuandika ni wanawake. Pia wanawake huteseka sana kutokana na jeuri ya kinyumbani na ya kingono, ambayo ingali, aongezea Bi. Clinton, “mmojawapo wa ukiukaji wa haki za kibinadamu usioripotiwa zaidi na ulioenea sana ulimwenguni.”

      Wanawake fulani hufanyiwa jeuri hata kabla hawajazaliwa. Hasa katika nchi fulani za Asia, mama fulani hutoa mimba za watoto wa kike kwa sababu wanapendelea wana badala ya mabinti. Katika sehemu fulani kupendelea wana kumefanya mbinu ya kutambua jinsia ya mtoto iwe biashara inayovuma. Kliniki moja ya kugundua jinsia ilitangaza huduma zake kwa kudokeza kwamba ilikuwa bora kutumia dola 38 sasa ili kuharibu kijusu cha kike kuliko kutumia dola 3,800 baadaye kumlipia mahari. Matangazo ya biashara kama hayo hufanya kazi. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika hospitali moja kubwa ya Asia ulipata kwamba asilimia 95.5 ya vijusu vilivyotambuliwa kuwa vya kike vilitolewa. Kupendelea wana ni zoea lililoko katika sehemu nyingine za ulimwengu vilevile. Mtu mmoja aliyekuwa bingwa wa zamani wa ndondi Marekani alipoulizwa alikuwa baba wa watoto wangapi, alijibu: “Mvulana mmoja na makosa saba.” Kichapo cha UM Women and Violence chasema kwamba “kubadili mtazamo na nia ya watu kuelekea wanawake kutachukua muda mrefu—wengi wanaamini angalau kizazi kimoja, na labda muda mrefu zaidi.”

      Watoto Wasioweza Kufurahia Utoto wa Kawaida

      Hakuna mtu atakayewekwa utumwani au kutumikishwa; utumwa na biashara ya utumwa itazuiwa katika namna zake zote.—Kifungu cha 4.

      Kinadharia, utumwa umekwisha. Serikali zimetia sahihi mikataba mingi sana inayofanya utumwa uwe haramu. Hata hivyo, kulingana na Shirika la Uingereza la Kupinga Utumwa, linalojulikana kuwa shirika la haki za kibinadamu la zamani zaidi, “kuna watumwa wengi leo kuliko wakati mwingine wowote.” Utumwa wa siku hizi unatia ndani ukiukaji wa namna mbalimbali wa haki za kibinadamu. Kulazimisha watoto wafanye kazi kunasemekana kuwa namna moja ya utumwa wa siku hizi.

      Kielelezo kimoja chenye kuhuzunisha ni cha mvulana mmoja wa Amerika Kusini anayeitwa Derivan. ‘Mikono yake midogo imechunika ngozi kwa kushughulika na majani magumu ya mkonge, ambao hutokeza katani za kutengenezea magodoro. Kazi yake ni kubeba majani mpaka kwenye ghala na kuyabeba hadi kwenye mashine ya utengenezaji kwa umbali wa meta 90. Ufikapo mwisho wa kila siku ya kazi ya saa 12, anakuwa amebeba tani moja ya majani. Derivan alianza kufanya kazi alipokuwa na umri wa miaka mitano. Leo ana umri wa miaka 11.’—World Press Review.

      Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Wafanyakazi inakadiria kwamba watoto robo bilioni walio na umri wa kati ya miaka 5 na 14 hufanyizwa kazi leo—wafanyakazi wadogo wengi wanaokaribia kutoshana na jumla ya idadi ya watu wa Brazili na Mexico! Wengi wa watoto hawa wasiofurahia utoto humenyeka kwenye migodi, wakikokota karai zilizojaa makaa ya mawe; hutembea kwa taabu katikati ya matope ili kuvuna mazao; au huinama kwenye vitanda vya kufuma ili kutengeneza mazulia manene madogo. Hata watoto wanaoanza kutembea—wenye umri wa miaka mitatu, minne, na mitano—hufungwa pamoja katika vikundi ili kulima kwa plau, kupanda mbegu, na kuokota masazo ya mashamba kuanzia mapambazuko hadi machweo. “Watoto,” asema mwenye shamba mmoja katika nchi fulani ya Asia, “wanagharimu kiasi kidogo kuliko trekta na wana akili kuliko fahali.”

      Kuchagua na Kubadili Dini

      Kila mtu ana haki ya uhuru wa kuwaza, dhamiri na dini; haki hii yatia ndani uhuru wa kubadili dini.—Kifungu cha 18.

      Mnamo Oktoba 16, 1997, Kusanyiko Kuu la UM lilipokea “ripoti ya muda juu ya kuondolewa kwa kila namna ya kutovumilia dini.” Ripoti hiyo iliyotayarishwa na Mwandishi Maalumu wa Tume ya Haki za Kibinadamu, Abdelfattah Amor, yaorodhesha ukiukaji unaoendelea wa Kifungu cha 18. Ikizungumza kuhusu nchi nyingi, ripoti hiyo yanukuu visa vingi sana vya ‘kusumbuliwa, kutishwa, kutendwa vibaya, kukamatwa, vizuizi, kutoweka, na mauaji.’

      Vivyo hivyo, 1997 Human Rights Reports, iliyokusanywa na shirika la Marekani la Demokrasia, Haki za Kibinadamu, na Wafanyakazi, yataja kwamba hata nchi ambazo zimezoea demokrasia kwa muda mrefu “zimejaribu kuzuia uhuru wa mchanganyiko wa vikundi vidogo-vidogo vya kidini, wakivijumlisha pamoja kuwa ‘madhehebu.’” Mielekeo kama hiyo inatokeza hangaiko. Willy Fautré, msimamizi wa shirika la Haki za Kibinadamu Lisilo na Mipaka lenye makao makuu Brussels, asema: “Uhuru wa kidini ni mmojawapo wa vionyeshi bora vya hali ya ujumla ya uhuru wa kibinadamu katika jamii yoyote.”

      Kazi Nyingi Mshahara Kidogo

      Kila mtu anayefanya kazi ana haki ya kulipwa ifaavyo ili apate kujiruzuku pamoja na familia yake katika njia inayofaa adhama ya binadamu.—Kifungu cha 23.

      Wakataji wa miwa katika Karibea waweza kuchuma dola tatu kwa siku, lakini gharama ya kukodi nyumba na vifaa huwafanya wawe na deni la wenye mashamba hayo. Kwa kuongezea, hawalipwi pesa taslimu bali kwa vocha. Na kwa kuwa duka la kampuni ya wenye mashamba ndilo duka la pekee ambalo wakataji wa miwa wanaweza kuliendea, wanalazimika kununua mafuta yao ya kupikia, mchele, na maharagwe huko. Hata hivyo, kama gharama za huduma za kukubali vocha za wafanyakazi, duka hilo hupunguza thamani ya vocha hiyo kwa kiwango cha asilimia 10 hadi 20. Bill O’Neill, naibu wa mkurugenzi wa Kamati ya Mawakili ya Haki za Kibinadamu, alisema hivi kwenye tangazo la redio ya UM: “Mwishoni mwa msimu, hawana pesa zozote zilizosalia kwa majuma na miezi ya kazi ngumu sana yenye jasho. Hawana akiba yoyote, na wameweza tu kujiruzuku kwenye huo.”

      Matibabu ya Kitiba kwa Wote?

      Kila mtu ana haki ya kuwa na kiwango cha maisha kinachofaa kwa ajili ya afya na hali njema yake na familia yake, kutia ndani chakula, makao, na matibabu.—Kifungu cha 25.

      ‘Ricardo na Justina ni wakulima maskini wa Amerika ya Latini wanaoishi kilometa zipatazo 80 kutoka jiji lililo karibu. Wakati binti yao mchanga Gemma alipougua, walimpeleka kwenye kliniki ya kibinafsi iliyokuwa karibu, lakini wafanyakazi wa huko walikataa kumtibu mtoto huyo kwa sababu ilikuwa wazi kwamba Ricardo hangeweza kulipia gharama hiyo. Siku iliyofuata, Justina alikopa pesa kutoka kwa majirani ili asafiri kwa magari ya umma kwenda kwenye jiji. Hatimaye Justina na mtoto huyo walipofika kwenye hospitali ya serikali ya jiji hilo, Justina aliambiwa kwamba hakuna vitanda na kwamba arudi keshoye asubuhi. Kwa kuwa hakuwa na jamaa zake walioishi katika jiji hilo na hakuwa na pesa za kukodisha chumba, usiku alijilaza juu ya meza katika soko la umma. Justina alimshikilia mtoto huyo kwa ukaribu ili amfariji na kumtunza, lakini haikusaidia. Usiku huo Gemma mchanga alikufa.’—Human Rights and Social Work.

      Ulimwenguni pote, mtu 1 kati ya 4 hujikimu kwa dola moja (ya Marekani) kwa siku. Wanakabili utatanishi uleule kama Ricardo na Justina: Matibabu ya kibinafsi yanapatikana lakini hayawezi kugharimiwa, huku matibabu ya umma yanaweza kugharimiwa lakini hayapatikani. Kwa kuhuzunisha, ingawa zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni walio maskini wamepokea ‘haki ya kupata matibabu,’ bado hawawezi kupata manufaa za kitiba.

      Orodha ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu haina mwisho. Hali kama hizo zilizotajwa juu zaweza kuzidishwa mara mamia ya mamilioni. Licha ya jitihada kubwa sana za mashirika ya haki za kibinadamu na licha ya kujitoa kwa maelfu ya watetezi ambao kwa kweli huhatarisha uhai wao ili kuboresha hali ya wanaume, wanawake, na watoto ulimwenguni pote, haki za kibinadamu kwa wote zingali ndoto tu. Je, zitapata kuwa halisi? Bila shaka zitakuwa hivyo, lakini lazima mabadiliko fulani yatukie kwanza. Makala ifuatayo itachunguza mabadiliko mawili.

  • Haki za Kibinadamu kwa Wote—Uhalisi wa Ulimwenguni Pote!
    Amkeni!—1998 | Novemba 22
    • Haki za Kibinadamu kwa Wote—Uhalisi wa Ulimwenguni Pote!

      “NI NINI kisababishi kikuu cha ukiukaji wa haki za kibinadamu?” wakili mmoja mwenye uzoefu wa haki za kibinadamu aliulizwa swali hili. Wakili huyo alijibu, “pupa.” “Pupa ya kutaka mamlaka ya kisiasa na kiuchumi.” Na kwa kuwa pupa husitawi katika akili za binadamu, ukiukaji wa haki za kibinadamu hatimaye huonyesha hali ya akilini. Kisababishi kingine ni utukuzo wa taifa. Falsafa ya nchi yangu kwanza huchochea ukiukaji wa haki za kibinadamu. Kwa hiyo haki za kibinadamu zitapatikana tu ‘ikiwa kutakuja serikali ya ulimwengu itakayokuwa na uwezo wa kuchukua hatua imara,’ asema profesa wa sheria na uchumi wa Uholanzi Jan Berkouwer.

      Yaani, ili haki za kibinadamu ziweze kupatikana tufeni pote, angalau mambo mawili yapasa kutokea kwanza: badiliko la akili na badiliko la serikali. Je, ni kufikiri kuzuri kutarajia mambo haya yatukie?

      Sababu Yenye Mambo Mawili kwa Badiliko

      Huku Mwongo wa Elimu ya Haki za Kibinadamu wa UM ukikaribia kuingia mwaka wake wa tano, kwa miongo mingi programu ya kimataifa ya elimu isiyokuwa ya serikali tayari imekuwa ikifaulu kubadili akili za mamilioni ya watu. Tokeo ni kwamba watu hawa sasa wanawatendea wanadamu wenzao kwa adhama. Programu hii inayotekelezwa na Mashahidi wa Yehova, inatenda katika zaidi ya nchi 230. Kwa nini inafanya kazi?

      Jambo moja ni kwamba, programu hii ya elimu ya Biblia hupanua uelewevu wa watu kuhusu chanzo cha haki za kibinadamu. Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu lasema kwamba mwanadamu ana haki kwa sababu ana uwezo wa kufikiri na kufuatia adili.

      Lazima mwanadamu awe alipokea uwezo wake wa kufikiri kutoka chanzo cha juu zaidi. (Ona sanduku “Chanzo cha Haki za Kibinadamu,” kwenye ukurasa wa 13.) Kutambua chanzo hiki cha juu cha kimungu hutokeza sababu yenye nguvu ya kumheshimu mwanadamu mwenzako. Kisha unawatendea wengine kwa adhama si kwa sababu tu dhamiri yako inakusukuma ufanye hivyo bali, la maana zaidi, kwa sababu ya heshima na upendo wako kwa Muumba hukusukuma utendee uumbaji wake kwa adhama. Mfikio huu wenye sababu mbili wategemea maneno ya Yesu Kristo: “Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote” na, “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” (Mathayo 22:37-39) Mtu anayemheshimu sana Muumba hangekiuka kamwe haki za mwenzake kwa sababu ni urithi kutoka kwa Mungu. Mkiukaji wa haki za kibinadamu ni mpokonyaji wa urithi huo.

      Elimu Inayotokeza Mabadiliko

      Programu hii ya elimu ya Biblia ya Mashahidi wa Yehova ina matokeo kadiri gani katika kupunguza ukiukaji wa haki za kibinadamu? Njia bora ya kujibu swali hilo ni kutazama matokeo ya programu hiyo, kwa kuwa Yesu alisema, “hekima huthibitishwa kuwa yenye uadilifu kwa kazi zayo.”—Mathayo 11:19.

      Mwandiko unaojulikana vizuri kwenye ukuta wa Jengo la Umoja wa Mataifa katika New York City wasema hivi: “Watafua panga zao ziwe majembe. Na mikuki yao kuwa miundu: Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa lingine. Wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Kwa nukuu hili kutoka kitabu cha Biblia cha Isaya sura ya 2, mstari wa 4, tafsiri ya King James Version, UM wataja njia kubwa ya kupunguza ukiukaji mkubwa sana wa haki za kibinadamu—kukomesha vita. Kwani, vita ni ‘kinyume cha haki za kibinadamu,’ kama kielezavyo kichapo kimoja cha UM.

      Programu ya elimu ya Mashahidi wa Yehova yaenda hatua zaidi ya wazo la kuandika maneno ya Isaya kwenye ukuta wa mawe. ‘Inaandika’ maneno ya Isaya katika mioyo ya wanadamu. (Linganisha Waebrania 8:10.) Jinsi gani? Programu hiyo huondoa vizuizi vya kijamii na kikabila na kuondoa utukuzo wa kitaifa kwa kufundisha maoni ya Biblia kuhusu jamii: Kuna jamii moja tu—jamii ya kibinadamu. (Matendo 17:26) Wale walioandikishwa katika programu hiyo wanasitawisha tamaa ya ‘kuwa waigaji wa Mungu,’ ambaye Biblia husema hivi kumhusu: “[Yeye] si mwenye ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye humhofu na kutenda uadilifu akubalika kwake.”—Waefeso 5:1; Matendo 10:34, 35.

      Likiwa tokeo la elimu hii inayotegemea Biblia, mamilioni ya watu leo ‘hawajifunzi vita tena kamwe.’ Badiliko la akili na moyo limetukia. Na badiliko hilo hudumu. (Ona sanduku “Elimu kwa Ajili ya Amani,” kwenye ukurasa wa 14.) Kwa sasa, zaidi ya watu 1,000 kila siku kwa wastani hukamilisha mitaala ya msingi ya kujifunza inayofanywa na Mashahidi wa Yehova na kujiunga na kundi hili la amani la ulimwenguni pote.

      Badiliko hili la akili ni thabiti kadiri gani na uamuzi unaofuatia wa kuheshimu haki za kibinadamu kwa kutoshiriki katika vita? Ni lenye nguvu sana. Kwa kielelezo: Kina cha Mashahidi cha kustahi haki za kibinadamu kilijaribiwa vikali wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, hasa katika Ujerumani ya Nazi. Mwanahistoria Brian Dunn alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova hawakupatana na itikadi ya Wanazi. Kipingamizi kikubwa zaidi kwa Wanazi kilikuwa msimamo wao wa kutokuwamo katika mambo ya kisiasa. Hili lilimaanisha kwamba hakuna mwamini ambaye angebeba silaha.” (The Churches’ Response to the Holocaust) Katika A History of Christianity, Paul Johnson alisema: “Wengi walihukumiwa kifo kwa kukataa kujiunga na utumishi wa kijeshi . . . , au waliishia Dachau au makao ya wenye kurukwa akili.” Ijapokuwa hivyo, walisimama imara. Mwanasoshiolojia Anna Pawełczyńska aliwafafanua Mashahidi hao kuwa “kikundi kidogo sana chenye nguvu za [adili] za daima katika taifa lililotishwa.”

      Ebu wazia tu kungekuwa na upungufu mkubwa kama nini wa ukiukaji wa haki za kibinadamu ulimwenguni pote ikiwa watu wote wangechukua msimamo huo leo na ‘kutojifunza vita tena kamwe’!

      Serikali ya Ulimwengu—‘Je, Ni Ndoto Tu’?

      ‘Ni vigumu kubadili akili, lakini kuunda serikali ya ulimwengu ni ndoto tu,’ ndivyo alivyosema mfanyakazi mmoja wa UM. Na kwa kweli, uhakika wa kwamba mataifa hayajawa tayari kusalimisha enzi zao kwa UM, au kwa shirika lolote, wakazia mkataa huu. Hata hivyo, wale wanaopuuza wazo la serikali ya ulimwengu, asema Profesa Berkouwer, “wana wajibu wa kuonyesha njia nyinginezo za kutatua matatizo ya ulimwengu. Hata hivyo, utatuzi-badala haupatikani.” Hakuna utatuzi wa kibinadamu. Lakini kuna utatuzi unaozidi nguvu za kibinadamu. Ni gani huo?

      Kama vile Biblia ionyeshavyo kwamba Muumba ndiye chanzo cha mambo yaliyo msingi wa haki za kibinadamu, pia inatujulisha kwamba ndiye chanzo cha serikali ya ulimwengu ambayo inazitokeza. Serikali hii ya kimbingu haionekani lakini ni halisi. Kwa kweli, mamilioni ya watu, labda pasipo kujua, wanasali kwa serikali hii ya ulimwengu wanaposema ile inayoitwa kwa kawaida Sala ya Bwana: “Acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.” (Mathayo 6:10) Kiongozi aliyechaguliwa na Mungu wa serikali hiyo ya Ufalme ni Mkuu wa Amani, Yesu Kristo.—Isaya 9:6.

      Serikali hii ya ulimwengu itafaulu katika kutokeza utamaduni wa kweli wa tufeni pote wenye haki za kibinadamu zitakazodumu kwa kuondoa vita milele. Biblia inatabiri: “[Muumba] avikomesha vita hata mwisho wa dunia; avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.”—Zaburi 46:9.

      Jambo hili litatukia haraka kadiri gani tufeni pote? Programu ya kujifunza Biblia inayoandaliwa na Mashahidi wa Yehova inatia ndani jibu lenye kuridhisha kwa swali hili. Twakutia moyo ufahamu programu hii.a Ikiwa unahangaikia haki za kibinadamu, hutatamaushwa.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ukipenda kupokea habari zaidi kuhusu programu hii ya elimu ya Biblia, wasiliana na wachapishaji wa gazeti hili au Mashahidi wa Yehova katika jumuiya yenu. Programu hii inatolewa bila malipo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 13]

      Chanzo cha Haki za Kibinadamu

      Kifungu cha 1 cha Azimio kwa Wote la Haki za Kibinadamu chasema kwamba “wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na sawa katika hadhi na haki.” Hivyo, haki za kibinadamu zinafafanuliwa kuwa haki ya uzaliwa ambayo hupitishwa kutoka kwa wazazi hadi kwa watoto, kama vile tu mto hupeleka maji kwa watu wanaoishi kandokando ya kingo zake. Ni wapi ulipoanzia mto huu wa haki za kibinadamu?

      Kulingana na Azimio kwa Wote, wanadamu wana haki kwa sababu “wamepewa uwezo wa kusababu na dhamiri.” Kichapo kimoja cha UM chaeleza hivi: “Kwa sababu mwanadamu ni kiumbe kiwezacho kusababu na kufuatia maadili, yeye ni tofauti na viumbe vingine vilivyoko duniani na kwa hiyo anapaswa kuwa na haki na uhuru fulani ambao viumbe vingine haviwezi kufurahia.” (Italiki ni zetu.) Hivyo, kuwa na uwezo wa kusababu na kuwa na dhamiri kunasemekana kuwa msingi wa kupata haki za kibinadamu. Mambo yakiwa namna hiyo, chanzo cha uwezo wa kusababu na dhamiri ya mwanadamu ndicho chanzo pia cha haki zake za kibinadamu.

      Kwa wapiganiaji wa haki za kibinadamu wanaoamini nadharia ya mageuzi, taarifa ya kwamba haki za kibinadamu zinahusiana na uwezo wa kusababu na dhamiri hutokeza ugumu. Kitabu chenye kuunga mkono mageuzi Life Ascending chakiri: “Tunapojiuliza kwa nini utaratibu wa [mageuzi] . . . ungeweza kutokeza sifa kama vile kupenda uzuri na kweli, huruma, uhuru, na zaidi ya yote, kina cha mtazamo wa kibinadamu, tunatatanika.” Na kwa kufaa. Kwa vyovyote, kusisitiza kwamba uwezo wa mwanadamu wa kusababu na wa dhamiri unatokana na wazazi wa kale walio duni wasioweza kusababu na wasio na dhamiri ni sawa na kusema kwamba mto huchipuka kutoka kwenye kisima kisichokuwa na maji.

      Kwa kuwa uwezo wa mwanadamu wa kusababu na wa dhamiri hauwezi kutoka kwa chanzo kilicho duni kuliko wanadamu, lazima uwezo huu utokane na chanzo kinachozidi uwezo wa kibinadamu. Ni wanadamu tu walio na sifa zinazohusiana na haki za kibinadamu—kusababu na dhamiri—kwa sababu tofauti na wanyama, wanadamu waliumbwa kwa “mfano” wa Mungu, yaeleza Biblia. (Mwanzo 1:27) Kwa hiyo, kama kisemavyo kitabu Human Rights—Essays on Justification and Applications, jibu halali kwa swali kwa nini watu wana haki za kiadili ni kwamba “wana thamani ya kiasili au adhama au wao ni . . . watoto wa Mungu.”

      [Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]

      Elimu kwa Ajili ya Amani

      Miaka kadhaa iliyopita, vita ilipokuwa ikigawanya Wabalkani, Branko alikuwa anatumika akiwa mlinzi mwenye silaha katika kliniki moja iliyokuwa sehemu ya Kroatia katika Bosnia.b Daktari fulani huko alikuwa akijifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, na usiku mmoja alimweleza Branko alichokuwa amejifunza kutokana na funzo hili. Kile alichosikia Branko kilimfanya aache silaha zake. Wakati fulani baadaye, baada ya kuhamia nchi fulani ya Ulaya, Branko alihudhuria mkutano wa Mashahidi wa Yehova, na hapo akakutana na Slobodan.

      Slobodan alitoka Bosnia pia. Alikuwa ameshiriki katika vita hiyohiyo kama vile Branko—lakini katika upande wa adui. Slobodan alikuwa amepigania Waserbia dhidi ya Wakroatia. Wakati watu hawa wawili walipokutana, tayari Slobodan alikuwa Shahidi wa Yehova, na alijitolea kujifunza Biblia pamoja na Branko, adui wake wa zamani. Funzo lilipoendelea, upendo wa Branko kwa Muumba, Yehova, ulikua. Baada ya muda mfupi akaamua kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.c

      Slobodan mwenyewe alikuwa Shahidi pia kwa msaada wa adui wake wa zamani. Jinsi gani? Naam, baada ya kuondoka kwenye eneo la vita katika Bosnia, Slobodan alitembelewa na Mujo, ambaye pia alitoka Bosnia lakini aliyelelewa katika dini iliyokuwa tofauti sana na ya Slobodan. Ikawa kwamba Mujo alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Ingawa walikuwa maadui, Slobodan alikubali pendekezo la Mujo la kujifunza Biblia pamoja naye, na baadaye akachukua hatua ya kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.

      Ni nini kilichosababisha wanaume hawa washinde chuki kali ya kikabila na kubadilika kutoka kuwa maadui hadi kuwa marafiki? Kupitia funzo lao la Biblia, walikuza upendo kwa Yehova. Baada ya hilo, walikuwa tayari ‘kufundishwa na Mungu kupendana.’ (1 Wathesalonike 4:9) Kama vile Profesa Wojciech Modzelewski alivyosema kuhusu Mashahidi wa Yehova kwa ujumla, “sababu ya msingi kwa msimamo wao wenye amani ni wazo la kufuata kwa sasa kanuni zilizofunuliwa katika Biblia.”

      [Maelezo ya Chini]

      b Majina yote yaliyotajwa katika sanduku hili yamebadilishwa.

      c Baadaye, Branko alipendezwa kujua kwamba daktari aliyezungumza naye mara ya kwanza alikuja kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova vilevile.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki