Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Walishinda Licha ya Mateso
    Mnara wa Mlinzi—2003 | Machi 1
    • Ufashisti Nchini Hungaria

      Mashahidi wa Yehova walionewa kwa miaka mingi nchini Hungaria pia. Baadhi yao waliteswa na tawala tatu za kimabavu. Ádám Szinger alikuwa mmoja wao. Ádám alizaliwa huko Paks, Hungaria, mwaka wa 1922 na alilelewa na wazazi Waprotestanti. Wanafunzi wa Biblia walimtembelea Ádám nyumbani kwake mwaka wa 1937, na mara moja akapendezwa na ujumbe wao. Kile ambacho alijifunza katika Biblia kilimsadikisha kwamba mafundisho ya kanisa lake hayakupatana na Biblia. Kwa hiyo aliacha Kanisa la Protestanti, kisha akajiunga na Wanafunzi wa Biblia katika huduma yao.

      Ufashisti ulikuwa ukipata nguvu nchini Hungaria. Mara kadhaa polisi walimwona Ádám akihubiri nyumba kwa nyumba, na kumkamata ili wamhoji. Mashahidi walizidi kukandamizwa, na kazi yao ikapigwa marufuku mwaka wa 1939. Ádám alikamatwa mwaka wa 1942, akapelekwa gerezani, na kupigwa vibaya sana. Ni nini kilichomsaidia kijana mwenye umri wa miaka 19 kuvumilia mateso na kufungwa kwa miezi mingi gerezani? “Nilipokuwa ningali nyumbani, nilijifunza Biblia kindani na kuelewa vizuri makusudi ya Yehova.” Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani ndipo Ádám alipobatizwa akawa Shahidi wa Yehova. Alibatizwa usiku mmoja mnamo Agosti 1942, katika mto ulio karibu na nyumba yao.

      Katika Gereza Nchini Hungaria na Katika Kambi za Kazi Ngumu Nchini Serbia

      Wakati vita ya pili ya ulimwengu ilipokuwa ikiendelea, Hungaria ilijiunga na Ujerumani kupinga Muungano wa Sovieti, na mwishoni mwa mwaka wa 1942 Ádám aliitwa kujiandikisha jeshini. Anasema hivi: “Niliwaambia kwamba singekubali kuwa mwanajeshi kwa sababu ya yale ambayo nilikuwa nimejifunza katika Biblia. Nikaeleza msimamo wangu wa kutounga mkono upande wowote.” Alihukumiwa kifungo cha miaka 11. Lakini Ádám hakukaa huko Hungaria kwa muda mrefu.

      Mwaka wa 1943, Mashahidi wa Yehova 160 hivi walikusanywa na wakaingizwa katika meli ya mizigo iliyosafiri kwenye Mto Danube na wakapelekwa hadi Serbia. Ádám alikuwa mmoja wao. Wakiwa huko Serbia, wafungwa hao walikuwa chini ya utawala wa Nazi. Walifungwa katika kambi ya kazi ngumu huko Bor na kulazimishwa kufanya kazi katika migodi ya shaba. Mwaka mmoja hivi baadaye, wakarudishwa Hungaria, ambapo Ádám aliachiliwa na wanajeshi wa Sovieti mapema mwaka wa 1945.

      Hungaria Yatawaliwa na Wakomunisti

      Lakini uhuru haukudumu kwa muda mrefu. Mwishoni mwa mwaka wa 1940, Wakomunisti wenye mamlaka walizuia kazi ya Mashahidi wa Yehova, kama vile tu Wafashisti walivyofanya kabla ya vita. Kufikia mwaka wa 1952, Ádám alikuwa na umri wa miaka 29, na alikuwa ameoa na akapata watoto wawili. Mwaka huo alikamatwa na kushtakiwa alipokataa tena kujiandikisha jeshini. Ádám alijitetea hivi mahakamani: “Hii si mara yangu ya kwanza kukataa kujiandikisha jeshini. Wakati wa vita nilifungwa gerezani kwa sababu hiyohiyo, kisha nikahamishwa Serbia. Sikubali kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yangu. Mimi ni Shahidi wa Yehova, na siwezi kuunga mkono upande wowote wa siasa.” Ádám alihukumiwa kifungo cha miaka minane gerezani, baadaye kikapunguzwa kuwa miaka minne.

      Ádám alizidi kuonewa hadi katikati ya miaka ya 1970, hiyo ikiwa zaidi ya miaka 35 baada ya Wanafunzi wa Biblia kuwatembelea wazazi wake kwa mara ya kwanza. Katika kipindi hicho chote, mahakama sita zilimhukumu vifungo mbalimbali vya jumla ya miaka 23 katika angalau magereza na kambi kumi. Alivumilia mateso ambayo yaliendelezwa na tawala tatu, yaani, Wafashisti wa kabla ya vita ya pili ya ulimwengu nchini Hungaria, Wanazi nchini Serbia, na Wakomunisti wakati wa vita baridi nchini Hungaria.

      Ádám angali anaishi mjini kwao, Paks, akimtumikia Mungu kwa uaminifu. Je, ana vipawa visivyo vya kawaida ambavyo vilimwezesha kuvumilia magumu kwa ushindi? La. Anaeleza:

      “Funzo la Biblia, sala, na kushirikiana na waamini wenzangu, yalikuwa mambo muhimu. Lakini ningependa kukazia mambo mengine mawili. Kwanza, Yehova ndiye Chanzo cha nguvu. Uhusiano wa karibu naye ulikuwa msaada mkubwa kwangu. Na pili, nilikumbuka sura ya 12 ya Waroma, inayosema hivi: ‘Msijilipizie kisasi.’ Kwa hiyo, sikuweka kinyongo kamwe. Mara nyingi nilikuwa na nafasi ya kulipiza kisasi, lakini sikufanya hivyo kamwe. Hatupaswi kutumia nguvu ambayo Yehova anatupatia kulipa ovu kwa ovu.”

  • Walishinda Licha ya Mateso
    Mnara wa Mlinzi—2003 | Machi 1
    • [Picha katika ukurasa wa 7]

      Ádám Szinger alipofungwa na wakati huu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki