Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi
    Amkeni!—1996 | Februari 22
    • Mapungukio ya Sayansi ya Kitiba

      Sababu nyinginezo zinazofanya maradhi yenye kuambukiza yarudi na kuongezeka zahusiana na sayansi ya kitiba yenyewe. Bakteria nyingi sasa zashinda viuavijasumu ambavyo viliziua mbeleni. Kwa kushangaza, viuavijasumu vyenyewe vimesaidia kutokeza hali hii. Kwa kielelezo, ikiwa kiuavijasumu huua asilimia 99 ya bakteria zenye kudhuru ndani ya mtu aliyeambukizwa, asilimia moja iliyosalimika ambayo ilikinza kiuavijasumu yaweza sasa kukua na kuzaana kama aina yenye nguvu ya magugu katika shamba lililolimwa hivi majuzi.

      Wagonjwa huchochea hilo tatizo wanapokosa kumaliza kiasi cha viuavijasumu walichoandikiwa na daktari wao. Huenda wagonjwa wakaacha kumeza tembe mara tu wanapoanza kuhisi vyema zaidi. Ingawa huenda vijiumbe-maradhi dhaifu zaidi viliuawa, vyenye nguvu zaidi husalimika na kuzaana kimya-kimya. Mnamo majuma machache, hayo maradhi yanatokea tena, lakini wakati huu ni vigumu zaidi, au haiwezekani, kuyatibu kwa dawa. Aina hizi za vijiumbe-maradhi zenye kukinza dawa zinaposhambulia watu wengine, tatizo zito zaidi la afya ya umma hutokea.

      Wastadi kwenye shirika la WHO walitaarifu hivi majuzi: “Ukinzaji [dhidi ya viuavijasumu na vitu vinginevyo vya kuua vijiumbe-maradhi] umeenea sana katika nchi nyingi na ukinzaji wa dawa nyingi huacha madaktari wakielekea kutoweza kabisa kutibu kwa mafanikio idadi inayoongezeka ya maradhi. Katika hospitali pekee, maambukizo yakadiriwayo kuwa milioni moja hutukia kila siku ulimwenguni pote, na mengi yayo ni yenye kukinza dawa.”

      Utiaji-damu mishipani, ambao unatumiwa kwa kuendelea tangu vita ya ulimwengu ya pili, umesaidia pia kueneza maradhi yenye kuambukiza. Licha ya jitihada za sayansi za kuhakikisha damu haina vijiumbe-maradhi vyenye kufisha, utiaji-damu mishipani umechangia kwa njia kubwa sana kuenezwa kwa mchochota wa ini, cytomegalovirus, bakteria yenye kukinza viuavijasumu, malaria, homa-njano, maradhi ya Chagas, UKIMWI, na maradhi mengine yenye kuogofya.

  • Kisasi cha Vijiumbe-Maradhi
    Amkeni!—1996 | Februari 22
    • Vijiumbe-Maradhi Vinapokinza

      Kijiumbe-maradhi kidogo kinachoitwa bakteria “kina uzani wa gramu chache mno kama 0.00000000001. Nyangumi-Samawi ana uzani wa gramu 100,000,000 hivi. Hata hivyo, bakteria yaweza kumwua nyangumi.”—Bernard Dixon, 1994.

      Miongoni mwa bakteria zinazohofiwa kuliko zote zipatikanazo hospitalini ni aina zenye kukinza dawa za Staphylococcus aureus. Aina hizi hupata wagonjwa na watu waliodhoofika, zikisababisha maambukizo mabaya mno ya damu, mchochota wa pafu, na mshtuko mbaya mno. Kulingana na jumla moja, staphylococcus huua watu 60,000 hivi katika Marekani kila mwaka—wengi kuliko wale ambao hufa katika aksidenti za magari. Kwa kipindi cha miaka kadhaa, aina hizi za bakteria zimekuwa zenye kukinza viuavijasumu hivi kwamba kufikia 1988 kulikuwa na kiuavijasumu kimoja tu kilichokuwa na matokeo dhidi yazo, ile dawa vancomycin. Hata hivyo, mara ripoti za aina zenye kukinza vancomycin zikaanza kuzuka kutoka kotekote ulimwenguni.

      Lakini, hata wakati viuavijasumu vifanyapo kazi vipaswayo kufanya, matatizo mengine yaweza kutokea. Katikati mwa 1993, Joan Ray alienda hospitali katika Marekani kwa ajili ya upasuaji wa kawaida. Alitarajia kurudi nyumbani baada ya siku chache tu. Badala ya hivyo, alilazimika kubaki hospitalini kwa siku 322, sababu hasa ikiwa maambukizo aliyopata baada ya upasuaji. Madaktari walipigana na hayo maambukizo kwa kiasi kingi cha viuavijasumu, kutia ndani vancomycin, lakini vijiumbe-maradhi vilikinza. Joan asema hivi: “Singeweza kutumia mikono yangu. Singeweza kutumia miguu yangu. . . . Singeweza hata kuchukua kitabu kukisoma.”

      Madaktari waling’ang’ana kupata kujua kwa nini Joan bado alikuwa mgonjwa baada ya miezi mingi ya matibabu ya viuavijasumu. Matokeo ya maabara yalionyesha kwamba zaidi ya ambukizo la staphylococcus, Joan alikuwa na aina nyingine ya bakteria katika mfumo wake—enterococcus yenye kukinza vancomycin. Kama jina hilo lidokezavyo, bakteria hii haikudhuriwa na vancomycin; ilielekea pia kuwa na kinga dhidi ya kila kiuavijasumu kinginecho chote.

      Kisha madaktari wakajua jambo ambalo liliwashangaza mno. Hiyo bakteria haikukinza tu dawa ambazo zingeiua lakini, kinyume cha walivyotarajia, hasa ilitumia vancomycin ili kusalimika! Daktari wa Joan, mtaalamu wa maradhi yenye kuambukiza, alisema: “[Hizo bakteria] zahitaji vancomycin hiyo ili kuzaana, zikiikosa hazitaongezeka. Kwa hiyo, katika maana fulani, zinatumia vancomycin kama chakula.”

      Madaktari walipoacha kumpa Joan vancomycin, hizo bakteria zilikufa, na Joan akapata nafuu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki