-
Kujitibu—Manufaa na HatariAmkeni!—1998 | Julai 8
-
-
Kujitibu—Manufaa na Hatari
Na Mleta-habari Wa Amkeni! Katika Brazili
“ULIMWENGUNI pote soko la dawa za kujitibu linapanuka,” adai msimamizi wa kampuni kubwa ya madawa. “Watu wanataka kudhibiti afya yao wenyewe.” Ingawa yaweza kuwa hivyo, je, kuna hatari zozote unazopaswa kujua?
Bila shaka, dawa zaweza kutibu zikitumiwa vizuri. Kwa kielelezo, insulini na dawa za viuavijasumu na vilevile hata mchanganyiko usio ghali na ulio sahili wa chumvi, sukari na maji safi huokoa uhai wa wengi. Ugumu wa kujitibu huwa ni kujua wakati ambapo manufaa ni bora kuliko hasara.
Ni kweli kwamba katika nchi fulani matabibu wanostahili waweza kuwa mbali sana au ghali sana. Kwa sababu hiyo, watu wengi hutegemea maoni ya marafiki na jamaa au vitabu vya mwongozo ili kupata habari kuhusu tiba. Pia, “matangazo ya biashara hutoa wazo la kwamba kwa kununua tembe fulani tu ya dawa, unaweza kuwa na afya nzuri na hali njema,” asema Fernando Lefèvre, profesa katika Chuo Kikuu cha São Paulo, Brazili.a Matokeo yanakuwa kwamba wengi huanza kutumia dawa ili kuondoa athari za kufanya kazi kupita kiasi, lishe isiyofaa, na hata matatizo ya kawaida ya kihisiamoyo. Lefèvre aongezea hivi: “Badala ya kuboresha maisha yao, watu hujaribu kutatua matatizo yao kwa dawa za kujinunulia.” Na ni nani ajuaye ikiwa wagonjwa hata hutambua ugonjwa wao?
Mbali na kutumia dawa kutibu magonjwa kama vile kuumwa kichwa, msongo wa damu, na kuchafuka tumbo, wengi hutumia dawa ili kukabiliana na hangaiko, hofu, na upweke. “Watu hutafuta msaada wa daktari kwa sababu wao hufikiri kwamba tembe itawatibu,” asema Dakt. André Feingold. “Hata wataalamu wa kitiba huelekea kutoa maagizo ya dawa za kutumia na kupendekeza kupimwa mara nyingi. Hakuna jitihada inayofanywa ya kufahamu malezi ya mgonjwa, ambaye mara nyingi huwa na mtindo-maisha uliovurugika, uliojaa mkazo, na usiofaa.” Akiri hivi Romildo Bueno, wa Baraza la Ulimwengu la Kuzuia Matumizi Mabaya ya Madawa Yanayoathiri Akili: “Daktari huwa na muda mfupi wa kumwona mgonjwa mmoja mmoja, na daktari humwacha upesi mtu aende nyumbani, akitibu dalili peke yake.” Kutumia dawa “ndiyo njia ya [kutatua] matatizo ya jamii.” Hata hivyo, daktari mwingine atahadharisha kwamba wagonjwa wengi wahitaji maagizo yenye uangalifu ya kutumia dawa zinazoathiri akili.
Baada ya kuzungumzia “mtindo wa kutumia dawa ya Prozac,” gazeti la kila siku la Brazili O Estado de S. Paulo lasema hivi: “Tiba ambayo huwa mtindo wa muda tu, kama vile mtindo mpya wa nywele, kwa kweli, ni ya ajabu.” Gazeti hilo lamnukuu tabibu wa magonjwa ya akili Arthur Kaufman akisema: “Ukosefu wa maoni sawa ya akilini na kusudi maishani hutokeza jambo ambalo hufanya tiba yenye matokeo kuwa suluhisho la magonjwa yote.” Kaufman aongezea hivi: “Binadamu anajishughulisha zaidi na zaidi na tiba za mara moja, na kwa hiyo, kwa kuwa hapendezwi na kutafuta visababishi vya matatizo yake, yeye hupendelea kutumia tembe ili kuyatatua.” Lakini je, ni salama kujitibu?
Kujitibu—Je, ni Hatari?
“Jambo moja lenye kutokeza sana katika karne ya 20 katika uwanja wa tiba limekuwa kutokezwa kwa dawa mpya,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Lakini pia yasema: “Labda kutiwa sumu kwingi husababishwa na matumizi mabaya ya dawa kuliko chanzo kingine chochote.” Kwa kweli, kama vile dawa iwezavyo kutibu, ndivyo iwezavyo kudhuru pia. Tembe za kupunguza hamu ya chakula “huathiri mfumo wa neva na kwa hiyo zaweza kuchochea dalili zisizofaa kama ukosefu wa usingizi, mabadiliko katika tabia, na katika visa fulani hata kuona vitu ambavyo havipo,” aeleza mwandishi Cilene de Castro. Aongezea hivi: “Lakini mtu yeyote ambaye hufikiri kwamba tembe hizo hupunguza tu hamu ya chakula anajidanganya. Tembe moja yaweza kuwa mwanzo wa tiba nyingi zisizokoma, kila tiba ikiondoa athari ya nyingine.”
Dawa nyingi zinazotumiwa kwa ukawaida zaweza kusababisha mwasho wa tumbo na hata kichefuchefu, kutapika, na kutokwa damu. Dawa fulani zaweza kuanzisha mazoea au kusababisha madhara kwa mafigo na ini.
Hata dawa za kiafya zipendwazo zaweza kudhuru. “Mtindo huu wa kutumia vitamini za ziada ni hatari sana,” aonya Dakt. Efraim Olszewer, msimamizi wa shirika la kitiba la Brazili. “Watu hawajitibu tu bali madaktari fulani wasio na ujuzi kamili wanatoa maagizo yenye kutiliwa shaka, bila kujali hatari zinazohusika.” Hata hivyo, daktari mwingine ataarifu kwamba vitamini za ziada katika viwango vinavyofaa zaweza kuwa za lazima au zenye kunufaisha katika kutibu magonjwa na upungufu fulani.
Tiba ya Kibinafsi Iliyo Salama—Jinsi Gani?
Kwa kuwa hatuwezi kumwona daktari wakati wote tunaposumbuka, elimu ya kitiba na njia zifaazo za kujitibu zaweza kunufaisha familia zetu. Hata hivyo, kabla ya kutumia utibabu wowote, ni muhimu kutambulisha ugonjwa kwa usahihi na kwa njia yenye matokeo. Ikiwa hakuna daktari karibu au huwezi kugharimia kumwona, kuchunguza kitabu kinachofaa cha kitiba kwaweza kukusaidia kutambulisha dalili za kweli. Kwa kielelezo, Shirika la Kitiba la Marekani huchapisha mwongozo wa kitiba kwa familia unaotia ndani sehemu yenye kurasa 183 juu ya chati za dalili. Hizi humsaidia mgonjwa apitie maswali ambayo yaweza kujibiwa ama ndiyo ama la. Kwa kutumia njia hii, mara nyingi tatizo laweza kutambulishwa.
Lakini namna gani daraka la madaktari? Ni wakati gani tuhitajipo kutafuta msaada wa daktari? Twaweza kuepukaje kuwa wenye wasiwasi mwingi kupita kiasi juu ya afya yetu au wenye kuipuuza? Kwa kweli, katika ulimwengu ambao maradhi na magonjwa ya kiakili yameenea, twaweza kufurahiaje afya njema ya kadiri fulani?
[Maelezo ya Chini]
a Katika nchi nyingi, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matangazo ya “kupatikana kwa urahisi” kwa dawa zilizokuwa zikipatikana tu kwa agizo la daktari licha ya madaktari wengi na mashirika mengi ya kitiba kuchambua hali hiyo.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Hakuna jitihada inayofanywa ya kufahamu malezi ya mgonjwa, ambaye mara nyingi huwa na mtindo-maisha uliovurugika, uliojaa mkazo, na usiofaa.”—Dakt. André Feingold
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Tiba za Mitishamba za Nyumbani
Kwa maelfu ya miaka, watu katika tamaduni mbalimbali wametibu magonjwa yao kwa mitishamba, wakitumia mimea inayopatikana shambani na misituni. Hata dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mimea, kama vile digitali, ambayo hutumiwa kutibu matatizo ya moyo. Hivyo, Penelope Ody, mshiriki wa Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Mitishamba katika Uingereza, ataarifu katika kitabu chake kwamba “kuna tiba salama zaidi ya 250 za kusaidia kutibu matatizo ya kawaida—kutoka kikohozi cha kawaida, mafua, na kuumwa kichwa kufikia matibabu maalumu ya ngozi, matatizo ya umeng’enyaji tumboni, na magonjwa ya watoto.”
Aandika hivi: “Sikuzote tiba ya mitishamba imeonwa kuwa ‘dawa ya watu wa kawaida’—tiba sahili zinazoweza kutumiwa nyumbani kwa magonjwa madogo-madogo au kuongezea tiba zaidi zenye nguvu zinazoagizwa na madaktari kwa ajili ya hali mbaya na zenye kudumu.” Aendelea kusema: “Ingawa kwa asili mitishamba mingi ni salama sana, inapaswa kutumiwa kwa uangalifu. Usipitishe vipimo vilivyowekwa au kuendelea na tiba za nyumbani ikiwa ugonjwa unadumu, unakuwa mbaya zaidi, au ikiwa ugonjwa wako haujajulikana vizuri.”—The Complete Medicinal Herbal.
-
-
Unaweza Kufurahiaje Afya Njema?Amkeni!—1998 | Julai 8
-
-
Unaweza Kufurahiaje Afya Njema?
TIBA za aina mbalimbali ni mazungumzo yanayopendwa sana. Yaonekana kwamba karibu kila rafiki au jirani ana suluhisho alipendalo zaidi kwa kila hali ya kitiba. Kwa kueleweka, msukumo wa kujitibu waweza kuwa wenye nguvu sana. Hata hivyo, kuna watu ambao “hutafuta daktari wakati tu hali inapokuwa mbaya,” asema daktari Mbrazili. “Waweza kuwa na vidonda kwenye ngozi ambavyo haviponi licha ya kujitibu kwa miezi kadhaa. Wamwonapo daktari, inapatikana kwamba wana aina ya kansa ambayo ingeweza kutibiwa mwanzoni.”
Kwa kuwa mara nyingi kutambuliwa kwa magonjwa mapema huokoa uhai, kuchelewa kwaweza kusababisha madhara sana. “Hedhi ya mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 30 ilikawia naye alikuwa na maumivu ya kiasi katika fumbatio ya chini. Alijitibu kwa kutumia dawa nyingi za kuondoa maumivu na za kuzuia uvimbe, na maumivu yakapungua,” aeleza daktari-mpasuaji. “Lakini siku tatu baadaye, alipatwa na mshtuko uliosababishwa na kupoteza damu nyingi akapelekwa hospitalini upesi. Nilimfanyia upasuaji mara moja, nikapata kwamba alikuwa na mimba katika mrija wa Falopio. Nusura afe!”
Mwanamke mmoja kijana katika São Paulo alifikiri kwamba alikuwa na tatizo la kupungukiwa na damu, kumbe figo lake lilikuwa na tatizo la daima la kukosa nguvu ya kutenda. Kwa sababu alikawiza matibabu, ikawa kwamba njia ya pekee ni kupachikwa figo lingine. Daktari huyo amalizia hivi: “Mara nyingi mgonjwa husita kutafuta matibabu, hujitibu mwenyewe au hutafuta njia nyingine zilizopendekezwa na watu ambao si madaktari, na huishia kuwa na matatizo makubwa ya kiafya.”
Bila shaka, hatutaki kupuuza dalili ambazo mwili wetu hutoa. Lakini twaweza kuepukaje kushughulika kupita kiasi na tiba au kujitibu? Afya hufafanuliwa kuwa “hali ya kuwa timamu kimwili, kiakili, au kiroho” au “kukosa maradhi ya kimwili au maumivu.” Kwa kupendeza, inakubalika kwamba kwa kiwango kikubwa au kidogo, leo maradhi mengi yaweza kuzuilika. Kulingana na Dakt. Lewis Thomas: “badala ya kuumbwa kwa njia isiyo stadi tukiwa kitu kizima, kwa kushangaza sisi ni wenye nguvu, viumbe wenye kudumu, na wenye afya tele.” Kwa sababu hiyo, badala ya ‘kuwa na shaka juu ya afya kufikia kiwango cha kuwa wagonjwa na kuharakisha kifo chetu,’ twapaswa kushirikiana na mwili na uwezo wake usio wa kawaida wa kujiponya wenyewe. Daktari hodari au mtaalamu wa afya aweza kutusaidia pia.
Wakati wa Kutafuta Matibabu
Daktari mmoja Mbrazili apendekeza msaada wa daktari “ikiwa dalili kama vile homa, kuumwa kichwa, kutapika, au maumivu katika fumbatio, kidari, au fupanyonga zisipotulizwa na dawa za kawaida na zinarudi mara kwa mara bila sababu yoyote au maumivu yakiwa makali sana.” Daktari mwingine apendekeza matibabu wakati wowote tunapokosa uhakika kuhusu jinsi ya kushughulika na dalili zetu au tuhisipo kasoro isiyo ya kawaida. Aongezea hivi: “Mtoto awapo mgonjwa, badala ya kumtibu mtoto, kwa kawaida wazazi hupendelea kupata msaada wa daktari.”
Lakini je, dawa huwa za lazima sikuzote? Je, matumizi ya dawa yatazuia kupona? Je, kuna athari zozote, kama vile kuvurugika kwa tumbo au madhara kwa ini au mafigo? Namna gani kuchanganyikana na dawa nyingine? “Wagonjwa wachache hufikiri juu ya matatizo yao bila wasiwasi au hata kwa ufahamu,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Lakini, daktari mwenye kudhamiria aweza kutusaidia kuona kwamba dawa zote zaweza kudhuru na kwamba ni dawa chache zinazotumiwa leo ambazo hazina athari. Soma tu onyo juu ya athari zinazoweza kutokea kwenye kibandiko cha maagizo ya dawa unazonunua! Hata dawa zinazouzwa kihalali bila maagizo zaweza kusababisha madhara au kifo zitumiwapo vibaya au zitumiwapo kwa kupita kiasi.
Uhitaji wa kuwa wenye hadhari wasisitizwa na ripoti ya Richard A. Knox katika The Boston Globe: “Mamilioni ya watu wanaougua ugonjwa wa baridi yabisi ambao hutumia dawa za kuondoa maumivu kila siku wanakabiliwa na hatari ya ghafula ya kutokwa damu kunakoweza kusababisha kifo, waripoti watafiti katika Chuo Kikuu cha Stanford.” Aongezea hivi: “Isitoshe, watafiti waonya kwamba kuchanganya dawa za kuondoa maumivu pamoja na dawa za kutuliza kiungulia au tembe zipendwazo za kuzuia kiungulia hakuzuii matatizo mabaya ya tumbo na hata kwaweza kuongeza hatari.”
Namna gani ukawaida wa kujitibu mwenyewe? Asema daktari katika Ribeirão Prêto, Brazili: “Nafikiri ingenufaisha sana ikiwa wote wangekuwa na kabati ndogo ya dawa . . . Hata hivyo, dawa hizi zapaswa kutumiwa kwa busara na maarifa.” (Ona sanduku, ukurasa wa 7.) Pia, elimu ya msingi ya kiafya huchangia kuboresha maisha. Kwa kuwa hali hutofautiana kwa kila mtu, Amkeni! haipendekezi dawa hususa, tiba, au tiba za kiasili.
Afya Njema—Waweza Kufanya Nini?
“Madaktari walio bora zaidi ulimwenguni ni Daktari Mlo, Daktari Mtulivu na Daktari Furaha,” akaandika Jonathan Swift, mwandishi wa karne ya 18. Kwa kweli, mlo kamili, pumziko linalofaa, na uradhi ni mambo ya maana katika afya njema. Kwa kutofautisha, ijapokuwa madai ya utangazaji wenye werevu, hatuwezi kununua afya njema kwa kutumia dawa tu. “Matumizi ya dawa zisizo za lazima na zilizo hatari” yaweza kudhoofisha mfumo wa kinga.—Dicionário Terapêutico Guanabara.
Hata hivyo, kwa kuwa watu wenye kuwajibika kuhusu mtindo-maisha wetu na kuepuka matumizi ya dawa za kulevya, kuvuta sigareti, unywaji wa kupindukia, na mkazo mwingi mno, twaweza kufanya mengi kuboresha hali njema yetu. Asema Marian, akiwa katika umri wa miaka ya 60 na mishonari wa muda mrefu katika Brazili: “Nimefurahia afya njema kwa kadiri fulani kwa kuishi kwa kiasi na kula namna mbalimbali za vyakula vyenye afya.” Pia aeleza hivi: “Kwa kawaida mimi hupenda kuamka mapema, kwa hiyo ni muhimu kulala mapema.” Kutumia akili na mazoea mazuri hayapasi kupuuzwa, wala umuhimu wa kupimwa na daktari mara kwa mara na mawasiliano mazuri pamoja na daktari stadi wa familia.
Ingawa ataka kubaki akiwa mwenye afya, Marian ni mwangalifu asipuuze afya yake wala asiihangaikie kupita kiasi. Asema hivi: “Mimi husali pia ili kupata msaada wa Yehova katika maamuzi yoyote yahusuyo afya ambayo nahitajika kufanya, ili nifanye maamuzi ambayo yatanifaa wakati ujao na nisitumie wakati na mali kupita kiasi katika jitihada za kuboresha afya yangu.” Aongezea hivi: “Kwa kuwa ni muhimu kuwa mtendaji, mimi husali Mungu anisaidie niwe mwenye kiasi kuhusu namna nitumiavyo wakati na nguvu zangu, ili kwamba nisijizuie isivyo lazima, na wakati huohuo, nisiruke mipaka yangu.”
Ili kuwa wenye furaha kwelikweli, hatuwezi kupuuza wakati ujao. Hata ikiwa tumejaliwa kuwa na afya njema kiasi kwa sasa, maradhi, maumivu, kuteseka, na hatimaye kifo yangaliko. Je, kuna tumaini lolote kwamba tutapata kufurahia afya kamili?
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Manufaa za Kujitunza kwa Kiasi
Sanasana afya yako hutegemea kile ulacho na kunywa. Ukijaribu kuendesha gari kwa kutumia petroli iliyotiwa maji au kuongeza sukari kwenye petroli, punde si punde utaharibu injini. Hali kadhalika, ukijaribu kuishi kwa kutegemea vyakula na vinywaji visivyofaa, hatimaye utasumbuka kutokana na afya mbaya. Katika ulimwengu wa kompyuta, jambo hili huitwa GIGO, linalomaanisha ukijaza kompyuta data zisizo sahihi, itakuandalia habari zisizo sahihi.”
Dakt. Melanie Mintzer, profesa wa utunzaji wa afya, aeleza hivi: “Kuna aina tatu za wagonjwa: wale wanaoona daktari kwa mambo ambayo wao wenyewe waweza kushughulikia kwa urahisi nyumbani, wale watumiao kwa njia inayofaa mambo ya utibabu, na wale wasioona daktari hata wakati wanapopaswa kufanya hivyo. Wale walio katika kikundi cha kwanza mara nyingi hupoteza wakati wa tabibu na wakati wao na pesa zao. Walio katika kikundi cha tatu waweza kuhatarisha maisha zao kwa kuchelewa kupata utibabu wa daktari. Madaktari hutamani kama watu wengi wangekuwa katika kikundi cha katikati.” “Mambo saba yanayotokeza afya njema ni: kula na kunywa kinachofaa, kufanya mazoezi kwa ukawaida, usivute sigareti, pumzika vizuri, dhibiti mkazo wako wa kazi, dumisha uhusiano wa karibu na marafiki, na kuwa mwangalifu ili kupunguza hatari za kupatwa na magonjwa na aksidenti.”—Before You Call the Doctor—Safe, Effective Self-Care for Over 300 Medical Problems, cha Anne Simons, M.D, Bobbie Hasselbring, na Michael Castleman.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Sanduku la Dawa la Nyumbani
“Imekadiriwa kwamba karibu asilimia 90 ya dalili—kuumwa, maumivu, kuchubuliwa na dalili nyingine zenye kusumbua au maradhi—zinazohisiwa na watu wazima wenye afya hupuuzwa tu na haziripotiwi kwa mtu yeyote. . . . Mara nyingi tiba ya mara moja hutumiwa, kama vile tembe 2 za aspirini kwa ajili ya kuumwa kichwa.”
“Mara nyingi linalowezesha hilo ni sanduku la dawa la nyumbani. Hupunguza safari zisizohitajika na zenye gharama za kumwona daktari au kwenda kwenye kliniki.”—Complete Home Medical Guide, The Columbia University College of Physicians and Surgeons.
Kitabu hichohicho hupendekeza sanduku la dawa la nyumbani ambalo hutia ndani Kanda, ukanda mwembamba, shashi safi kabisa, pads, pamba, bandeji, dawa mbalimbali za kupaka, spiriti ya kuua vijidudu, makasi, kipimajoto cha mdomo, na vyombo vingine vyenye kutumika.
Kwa ajili ya matibabu, kitabu hicho chapendekeza tembe ili kupunguza homa na maumivu, dawa za kutuliza kiungulia, dawa ya kunywa ya kukohoa, dawa za mizio na mafua, dawa isiyo kali ya kuharisha.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Onyo Fupi
“Hata ingawa hazihitaji maagizo, dawa zinunuliwazo bila maagizo ya daktari ni dawa halisi. Kama ilivyo na dawa zenye kuagizwa na daktari, hazipaswi kuchanganywa na dawa nyinginezo au na vyakula fulani au alkoholi fulani. Kama dawa nyingine, hizo zaweza kuficha matatizo mengine makubwa zaidi au kusababisha uraibu. Na nyakati fulani dawa zisizo na maagizo hazipaswi tu kuchukua mahali pa daktari.
“Hata hivyo, nyingi ni salama na ni zenye matokeo . . . Huwa na matokeo mazuri.”—Using Medicines Wisely.
-