-
Jitihada za Muda Mrefu za Kuboresha AfyaAmkeni!—2004 | Mei 22
-
-
Jitihada za Muda Mrefu za Kuboresha Afya
JOANNE alikuwa akiishi New York, naye alikuwa na ugonjwa wa kifua-kikuu (TB). Lakini TB yake haikuwa ya kawaida. Alikuwa na aina sugu ya ugonjwa huo ambayo haiwezi kutibiwa na karibu dawa zote na ambayo huua nusu ya watu wanaoipata. Hata hivyo, Joanne hakutibiwa kwa ukawaida na tayari alikuwa amewaambukiza watu wengine. Daktari wake aliyekuwa amekata tamaa alisema kwamba ‘anapaswa kufungiwa.’
TB ni ugonjwa wa zamani ambao huua. Mamilioni ya watu wameugua na kufa kutokana na ugonjwa huo. Uthibitisho wa kuwapo kwa ugonjwa huo umepatikana katika maiti za Misri ya kale na Peru. Leo, aina mbalimbali za ugonjwa huo zinazozuka upya huua watu wapatao milioni mbili kila mwaka.
Akiwa amelala kitandani katika kibanda kidogo huko Afrika, Carlitos alikuwa akitokwa na jasho kwenye paji la uso. Malaria ilikuwa imemdhoofisha sana hata hangeweza kulia. Wazazi wake hawakujua la kufanya kwa kuwa hawakuwa na pesa za dawa, wala hakukuwa na kliniki karibu ambapo mtoto wao angeweza kutibiwa. Ugonjwa wake ulizidi, na katika muda wa saa 48 alikuwa amekufa.
Malaria huua watoto wapatao milioni moja kila mwaka, kama ilivyomuua Carlitos. Katika vijiji vya Afrika Mashariki, watoto wengi huumwa na mbu wenye viini vya malaria mara 50 hadi 80 kwa mwezi. Mbu hao wanaenea katika maeneo mapya na dawa za malaria hazina nguvu tena. Inakadiriwa kwamba watu milioni 300 huugua malaria kali kila mwaka.
Kenneth, mwenye umri wa miaka 30, aliyekuwa akiishi huko San Francisco, California, alimwona daktari wake kwa mara ya kwanza mwaka wa 1980. Alikuwa akiendesha na kuhisi uchovu. Mwaka mmoja baadaye alikuwa amekufa. Ingawa alitibiwa na madaktari stadi, alizidi kukonda na hatimaye akafa kutokana na nimonia.
Miaka miwili baadaye, mwanamke mmoja huko kaskazini mwa Tanzania, umbali wa kilometa 16,000 kutoka San Francisco, alikuwa na dalili kama hizo. Baada ya majuma machache akashindwa kutembea, kisha akafa muda mfupi baadaye. Wanakijiji waliuita ugonjwa huo wa ajabu ugonjwa wa Juliana kwa sababu mwanamume aliyekuwa akiuza vitambaa vyenye jina Juliana, alimwambukiza mwanamke huyo na wanawake wengine ugonjwa huo.
Kenneth na mwanamke huyo wa Tanzania walikuwa na ugonjwa uleule: UKIMWI. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, wakati ambapo ilionekana kana kwamba wataalamu wa tiba walikuwa wamekomesha viini vilivyo hatari zaidi, ugonjwa huo hatari ulizuka na kuanza kuwasumbua wanadamu. Kwa miaka 20 tu, idadi ya watu waliokufa kutokana na UKIMWI ikafikia idadi ya watu waliokufa kutokana na tauni iliyokumba bara la Ulaya na Asia katika karne ya 14, tauni ambayo haikusahaulika kamwe barani Ulaya.
Tauni
Yaonekana kwamba tauni hiyo ilianza mwaka wa 1347, wakati meli kutoka Crimea ilipotia nanga huko Messina, kwenye kisiwa cha Sicily. Mbali na shehena yake ya kawaida, meli hiyo ilileta tauni pia.a Punde si punde, tauni hiyo ikaenea kotekote nchini Italia.
Mwaka uliofuata Agnolo di Tura, wa Siena, Italia, alisimulia hali yenye kuogofya iliyokumba mji wao: ‘Watu walianza kufa Siena mnamo mwezi wa Mei. Lilikuwa pigo kali lenye kuogofya. Wagonjwa walikufa punde baada ya kuambukizwa. Mamia ya watu walikufa usiku na mchana.’ Aliongezea hivi: ‘Niliwazika watoto wangu watano, na ndivyo walivyofanya wengine wengi pia. Hakuna aliyeomboleza, hata awe alifiwa na nani, kwa kuwa kila mtu alikuwa akitazamia kifo. Watu wengi sana walikufa hivi kwamba wote walidhani mwisho wa dunia umefika.’
Wanahistoria fulani wanasema kwamba tauni hiyo ilienea kotekote barani Ulaya kwa kipindi cha miaka minne na kwamba thuluthi moja hivi ya watu walikufa, watu kati ya milioni 20 na milioni 30. Hata katika nchi ya mbali ya Iceland watu wengi sana walikufa. Inasemekana kwamba katika Mashariki ya Mbali, idadi ya wakaaji wa China ilishuka kutoka milioni 123 mwanzoni mwa karne ya 13 hadi milioni 65 katika karne ya 14, huenda kutokana na tauni hiyo pamoja na njaa kali iliyozuka wakati huohuo.
Hakuna ugonjwa mwingine wowote, vita, au njaa kali iliyokuwa imesababisha kuteseka kulikoenea hivyo. “Ulikuwa msiba usio na kifani katika historia ya wanadamu,” chasema kitabu Man and Microbes. “Ugonjwa huo uliangamiza kati ya asilimia 25 na asilimia 50 ya watu barani Ulaya, Afrika Kaskazini, na sehemu mbalimbali za Asia.”
Mabara ya Amerika hayakupatwa na tauni hiyo kwa sababu yalikuwa mbali na sehemu nyingine za ulimwengu. Hata hivyo, meli zilipoanza kufika huko, magonjwa hayo yakaanza kuenea huko pia. Katika karne ya 16, magonjwa hatari hata kupita tauni yalikumba mabara hayo.
Ndui Yashambulia Mabara ya Amerika
Columbus alipowasili West Indies mwaka wa 1492, alisema kwamba wenyeji walikuwa na ‘sura nzuri, maumbo mazuri, kimo cha wastani, na maungo.’ Hata hivyo, licha ya kuwa na afya nzuri, bado walikumbwa kwa urahisi na magonjwa yaliyoenea kutoka Ulaya.
Mnamo mwaka wa 1518, ugonjwa wa ndui ulizuka katika kisiwa cha Hispaniola. Waamerika wenyeji hawakuwa wameugua ugonjwa huo hapo awali, na matokeo yakawa mabaya sana. Mhispania mmoja aliyejionea hali hiyo, alikadiria kwamba watu elfu moja tu ndio waliookoka katika kisiwa hicho. Punde baadaye ugonjwa huo ulifika Mexico na Peru ukiwa na matokeo hayohayo.
Wakoloni Waingereza walipowasili Massachusetts huko Amerika Kaskazini katika karne iliyofuata, waligundua kwamba wakaaji wengi walikuwa wamekufa kutokana na ndui. Kiongozi wao, John Winthrop, aliandika hivi: “Karibu wenyeji wote wamefagiliwa mbali na ugonjwa wa ndui.”
Zaidi ya ndui, magonjwa mengine pia yalizuka. Kulingana na kitabu kimoja, miaka mia moja hivi baada ya Columbus kuwasili huko, magonjwa kutoka nchi nyingine yalikuwa yameua asilimia 90 ya wakaaji wa mabara ya Amerika. Idadi ya watu wa Mexico ilikuwa imepungua kutoka milioni 30 hadi milioni 3, na ya Peru kutoka milioni 8 hadi milioni moja. Bila shaka si wenyeji wa Amerika tu walioathiriwa na ndui. Kitabu Scourge—The Once and Future Threat of Smallpox kinasema hivi: “Katika historia yote ya binadamu, ndui iliua mamia ya mamilioni ya watu, wengi kuliko waliouawa na tauni . . . na vita vyote vya karne ya ishirini.”
Magonjwa Hayajakomeshwa Kabisa
Magonjwa hatari ya tauni na ndui huenda yasionekane kuwa tisho leo. Katika karne ya 20, wanadamu walikomesha magonjwa mengi ya kuambukiza, hasa katika nchi zilizoendelea. Madaktari waligundua vyanzo vya magonjwa mengi na kuvumbua njia za kuyatibu. (Ona sanduku.) Ilionekana kwamba chanjo mpya na viuavijasumu vipya vitamaliza magonjwa yote, hata magonjwa sugu.
Hata hivyo, Dakt. Richard Krause, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Mizio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani, anasema kwamba “tauni ni kama kifo na kodi, haziepukiki.” Magonjwa ya TB na malaria hayajakomeshwa. Na kwa kusikitisha, kuzuka kwa UKIMWI hivi majuzi kunathibitisha kwamba magonjwa ya kuambukiza yangali duniani. Kitabu Man and Microbes kinasema hivi: “Magonjwa ya kuambukiza yangali kisababishi kikuu cha vifo ulimwenguni, na hivyo ndivyo mambo yatakavyoendelea kwa muda mrefu.”
Madaktari fulani wanahofia kwamba licha ya mafanikio katika kutibu magonjwa, mafanikio ambayo yamepatikana katika miongo michache iliyopita si ya kudumu. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Robert Shope, anaonya hivi: “Hatari ya magonjwa ya kuambukiza haijatoweka, inazidi kuongezeka.” Makala inayofuata itaeleza sababu.
[Maelezo ya Chini]
a Tauni hiyo ilijitokeza kwa njia mbalimbali, kama vile tauni ya majipu na tauni ya nimonia. Viroboto vya panya hasa vilieneza tauni ya majipu, nayo tauni ya nimonia ilienezwa hasa na watu wenye ugonjwa huo, walipokohoa au kupiga chafya.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Kwa miaka 20 tu, idadi ya watu waliokufa kutokana na UKIMWI ikafikia idadi ya watu waliokufa kutokana na tauni iliyokumba bara la Ulaya na Asia katika karne ya 14
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Mambo ya Hakika na Ushirikina
Katika karne ya 14, wakati ambapo tauni ilikumba nyumba ya papa huko Avignon, daktari wake alimjulisha kwamba mpangilio wa sayari tatu, yaani Zohali, Sumbula, na Mars, uliofanyiza umbo la Aquarius ndio uliosababisha tauni hiyo.
Karne nne hivi baadaye, George Washington alianza kuwashwa na koo. Madaktari watatu maarufu waliutibu ugonjwa huo kwa kumtoa lita mbili za damu. Mgonjwa huyo akafa baada ya saa chache. Matibabu ya kutoa damu yalitumiwa sana kwa miaka 2,500 tangu wakati wa Hippocrates hadi katikati ya karne ya 19.
Ingawa ushirikina na mapokeo yalichelewesha maendeleo ya kitiba, madaktari walijitoa mhanga kugundua vyanzo na dawa za magonjwa ya kuambukiza. Yafuatayo ni baadhi ya mafanikio yao.
◼ Ndui. Mnamo 1798, Edward Jenner alivumbua chanjo ya ndui. Katika karne ya 20, chanjo zimezuia magonjwa mengine kama polio, homa ya manjano, na ukambi, na surua.
◼ Kifua-kikuu. Mnamo 1882, Robert Koch aligundua bakteria inayosababisha kifua-kikuu na kuvumbua njia ya kuupima ugonjwa huo. Miaka 60 hivi baadaye, kiuakijasumu kinachoitwa streptomycin kinachotibu ugonjwa wa kifua-kikuu kikavumbuliwa. Dawa hiyo ilitumiwa pia kutibu tauni ya majipu.
◼ Malaria. Tangu karne ya 17, kwinini inayotokana na gamba la mti wa cinchona iliokoa uhai wa mamilioni ya watu waliougua malaria. Mnamo 1897, Ronald Ross aligundua kwamba mbu anayeitwa Anopheles ndiye hueneza viini vya ugonjwa huo, na jitihada zilifanywa kuwaangamiza mbu ili kupunguza idadi ya vifo katika nchi za tropiki.
[Picha]
Chati ya nyota za unajimu (juu) na kutoa damu
[Hisani]
Both: Biblioteca Histórica “Marqués de Valdecilla”
[Picha katika ukurasa wa 3]
Leo, aina mbalimbali za kifua-kikuu zinazozuka upya huua watu wapatao milioni mbili kila mwaka
[Hisani]
X ray: New Jersey Medical School–National Tuberculosis Center; man: Photo: WHO/Thierry Falise
[Picha katika ukurasa wa 4]
Mchongo wa Kijerumani wa mwaka wa 1500 hivi, unaoonyesha daktari ambaye amejifunika kitambaa ili kujikinga na tauni. Sehemu iliyofunika mdomo ina marashi
[Hisani]
Godo-Foto
[Picha katika ukurasa wa 4]
Bakteria iliyosababisha tauni ya majipu
[Hisani]
© Gary Gaugler/Visuals Unlimited
-
-
Matokeo ya Jitihada za Kupambana na MagonjwaAmkeni!—2004 | Mei 22
-
-
Matokeo ya Jitihada za Kupambana na Magonjwa
MNAMO Agosti 5, 1942, Dakt. Alexander Fleming aligundua kwamba mmoja wa wagonjwa wake, rafiki yake, alikuwa anakaribia kufa. Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 52 alikuwa na homa ya uti wa mgongo na licha ya jitihada zote za Fleming, sasa rafiki yake alikuwa amepoteza fahamu.
Miaka 15 mapema, Fleming alikuwa amegundua kitu fulani chenye kustaajabisha kilichofanyizwa na kuvu ya rangi ya bluu-kijani. Alikiita penisilini. Aligundua kwamba inaweza kuua bakteria; lakini hakuweza kutenganisha sehemu aliyohitaji kutoka katika zile sehemu nyingine za kuvu, basi akaitumia kuzuia ukuzi wa bakteria tu. Hata hivyo, katika mwaka wa 1938, Howard Florey pamoja na kikundi chake cha watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford walijitahidi kutengeneza kiasi cha kutosha cha penisilini ili ijaribiwe kwa binadamu. Fleming akampigia simu Florey, aliyekubali kumtumia penisilini yote aliyokuwa nayo. Hiyo ndiyo iliyokuwa nafasi ya mwisho ya Fleming kumwokoa rafiki yake.
Kumdunga sindano ya penisilini kwenye misuli hakukutosha, kwa hiyo Fleming akamdunga rafiki yake dawa hiyo moja kwa moja kwenye uti wa mgongo. Penisilini hiyo iliangamiza viini vya ugonjwa huo; na baada ya juma moja tu, mgonjwa wa Fleming akaondoka hospitalini akiwa amepona kabisa. Tangu wakati huo, viuavijasumu vikaanza kutumiwa. Mwanadamu akawa amepiga hatua kubwa katika jitihada zake za kupambana na magonjwa.
Enzi ya Viuavijasumu
Viuavijasumu vilipoanza kutumiwa kwa mara ya kwanza, vilionwa kuwa dawa ya magonjwa yote. Magonjwa yaliyosababishwa na bakteria, kuvu, au viini vingine, ambayo hayakuwa na tiba awali, sasa yangeweza kutibiwa kabisa. Kwa sababu ya dawa hizo mpya, idadi ya watu waliokuwa wakifa kutokana na homa ya uti wa mgongo, nimonia, na homa ya vipele vyekundu ikapungua sana. Magonjwa ambayo watu waliambukizwa wakiwa hospitalini ambayo hapo awali yalisababisha kifo, sasa yalitibiwa kwa siku chache.
Tangu wakati wa Fleming, watafiti wamevumbua viuavijasumu vingi nao wanaendelea kutafuta vingine. Katika miaka 60 iliyopita, viuavijasumu vimekuwa muhimu katika jitihada za kupambana na magonjwa. Kama George Washington angekuwa hai leo, bila shaka madaktari wangeutibu mwasho wake wa koo kwa kiuakijasumu na huenda angepona kwa muda wa juma moja hivi. Viuavijasumu vimesaidia wengi wetu kupona magonjwa kadhaa. Hata hivyo, ni wazi kwamba viuavijasumu vimepungukiwa kwa njia fulani.
Viuavijasumu havitibu magonjwa yanayosababishwa na virusi kama vile UKIMWI au homa kali. Isitoshe, watu fulani huathiriwa na viuavijasumu fulani. Na viuavijasumu ambavyo huua viini vya aina nyingi vinaweza kuua vijiumbe muhimu katika miili yetu. Lakini huenda tatizo kubwa hata zaidi likawa kutumia kupita kiasi dawa hizo au kupunguza kiasi kilichopendekezwa.
Wagonjwa wengine wanapopata nafuu hawamalizi dawa walizopendekezewa na daktari, labda kwa sababu wanahisi vizuri au kwa sababu itawabidi watumie dawa hizo kwa muda mrefu. Kwa hiyo, huenda dawa hizo zisiue bakteria zote zinazoshambulia na hivyo bakteria sugu hubaki na kuongezeka. Watu wengi wanaotibiwa kifua-kikuu wamepatwa na hali hiyo.
Madaktari na wakulima hutumia dawa hizo mpya kupita kiasi. Kitabu Man and Microbes kinasema: “Madaktari huko Marekani wamependekeza viuavijasumu hata wakati ambapo havihitajiwi, na katika nchi nyinginezo vinatumiwa ovyoovyo sana. Mifugo imepewa viuavijasumu vingi, si kwa kusudi la kuponya magonjwa, bali kuharakisha ukuzi; na hilo hufanya bakteria ziwe sugu.” Kitabu hicho kinasema kwamba “huenda viuavijasumu vipya visipatikane.”
Lakini, licha ya mahangaiko hayo kuhusu kutofanikiwa kwa viuavijasumu, kulikuwa na mafanikio mengi ya kitiba katika nusu ya pili ya karne ya 20. Ilionekana kwamba watafiti wa kitiba wangeweza kupata dawa za kutibu karibu kila ugonjwa. Pia, ilitazamiwa kwamba chanjo zingeweza kuzuia magonjwa.
Mafanikio ya Sayansi ya Tiba
Jarida la The World Health Report 1999 lilisema hivi: “Kumekuwa na mafanikio mengi sana katika kukinga magonjwa.” Mamilioni ya watu wameokolewa kwa sababu ya miradi ya kuchanja watu ulimwenguni. Mradi wa ulimwenguni pote wa kuchanja watu umekomesha ugonjwa wa ndui, ule ugonjwa hatari ulioua watu wengi kuliko vita vyote vya karne ya 20. Mradi mwingine kama huo unakaribia kukomesha ugonjwa wa polio. (Ona Sanduku “Kushinda Ndui na Polio.”) Leo, watoto wengi huchanjwa ili kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari ambayo yameenea sana.
Magonjwa mengine yamepunguzwa kwa kutumia njia nyingine. Magonjwa yanayoenezwa kupitia maji, kama vile kipindupindu, hayaelekei kutokea mahali penye mazingira safi na maji safi. Katika nchi nyingi ambapo ni rahisi kwa watu kwenda hospitalini, magonjwa mengi yanaweza kutambuliwa na kutibiwa kabla hayajawa hatari. Chakula kizuri na makao mazuri, pamoja na kufuata sheria za kushughulikia na kuhifadhi chakula vizuri, ni mambo ambayo yamechangia afya bora ya umma.
Wanasayansi walipogundua vyanzo vya magonjwa ya kuambukiza, maofisa wa afya wangeweza kuchukua hatua za kuzuia magonjwa. Hebu fikiria mfano mmoja. Tauni ya majipu ilipozuka huko San Francisco mwaka wa 1907, ni watu wachache tu waliokufa kwa sababu jiji hilo lilianzisha mara moja mradi wa kuangamiza panya wote, kwa kuwa viroboto vya panya ndivyo vilivyokuwa vikieneza ugonjwa huo. Kwa upande mwingine, kwa miaka 12, kuanzia mwaka wa 1896, ugonjwa huohuo uliua watu milioni kumi nchini India kwa sababu chanzo chake hakikuwa kimegunduliwa.
Kulemewa na Magonjwa
Ni wazi kwamba, kumekuwa na mafanikio mengi makubwa. Hata hivyo, baadhi ya mafanikio hayo yamepatikana katika nchi tajiri tu. Magonjwa yanayoweza kutibiwa bado yanaua mamilioni ya watu kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kutosha. Katika nchi zinazoendelea bado watu wengi hawana mazingira safi, hawapati matibabu, wala hawana maji safi. Tatizo hilo linazuka hasa kwa sababu watu wengi katika nchi hizo wanahama kutoka mashambani kwenda katika majiji makubwa. Kwa hiyo, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, watu wanaoishi katika nchi maskini ulimwenguni “hulemewa na magonjwa mengi kuliko wale wanaoishi katika nchi tajiri.”
Tatizo hilo hutokana hasa na ubinafsi unaowazuia watu kupangia mambo ya wakati ujao. Kulingana na kitabu Man and Microbes: “Baadhi ya magonjwa hatari ya kuambukiza hayapatikani katika nchi zilizoendelea. . . . Baadhi yake yanapatikana hasa katika maeneo maskini ya tropiki au yaliyo karibu na tropiki.” Kwa kuwa huenda zisifaidike moja kwa moja, nchi tajiri na kampuni za dawa hutoa pesa za kutibu magonjwa hayo shingo upande.
Kutojali kwa watu pia kumechangia kuenea kwa magonjwa. Hilo laonekana wazi hasa katika kisa cha UKIMWI, ambao huenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine kupitia umajimaji wa mwili. Kwa miaka michache tu, ugonjwa huo umeenea ulimwenguni pote. (Ona sanduku “UKIMWI—Tauni ya Siku Zetu.”) Mtaalamu mmoja wa magonjwa ya kuambukiza, Joe McCormick anasema: “Wanadamu wamejiletea wenyewe tatizo hilo. Hatujaribu kuchambua maadili ya watu, huo ndio ukweli wa mambo.”
Wanadamu walienezaje UKIMWI bila kujua? Kitabu The Coming Plague kinataja mambo yafuatayo: Mabadiliko ya maisha ya watu—hasa yale mazoea ya kufanya ngono na watu wengi—yalisababisha kuenea kwa magonjwa ya zinaa, jambo ambalo hufanya virusi viongezeke sana na iwe rahisi mtu mmoja kuwaambukiza watu wengine wengi. Kutibu watu katika nchi zinazoendelea kwa kutumia sindano ambazo tayari zimetumiwa au kujidunga dawa za kulevya kwa sindano ambazo tayari zimetumiwa kulichangia pia kuenea kwa ugonjwa huo. Biashara ya damu inayoleta mabilioni ya dola pia iliwezesha virusi vya UKIMWI kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa watu wengi.
Kama ilivyotangulia kutajwa, kutumia viuavijasumu kupita kiasi au kupunguza kiasi kilichopendekezwa kumechangia kuwapo tena kwa viini sugu. Hilo ni tatizo kubwa na linaendelea kuzidi. Bakteria inayoitwa staphylococcus, ambayo mara nyingi huambukiza vidonda, ilikuwa ikikomeshwa kwa urahisi kwa kutumia dawa zenye penisilini. Lakini sasa, viuavijasumu hivyo vya zamani mara nyingi havifaulu. Kwa hiyo, ni lazima madaktari waanze kutumia viuavijasumu vipya ambavyo ni ghali na huenda nchi zinazoendelea zisiweze kuvigharimia. Hata viuavijasumu vipya kabisa huenda visiangamize viini fulani, hivyo kufanya magonjwa ambayo watu huambukizwa hospitalini yaenee na kuwa hatari zaidi. Dakt. Richard Krause, aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Mizio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani, alifafanua waziwazi hali ya sasa kuwa “mlipuko wa viini sugu.”
“Je, Mambo Ni Afadhali Leo?”
Ni wazi kwamba tisho la magonjwa bado liko hata sasa, mwanzoni mwa karne hii ya 21. Kuenea kwa UKIMWI, kuzuka kwa viini sugu, na kutokea upya kwa magonjwa hatari ya zamani kama vile kifua-kikuu na malaria kwaonyesha kwamba vita dhidi ya magonjwa vinaendelea.
Joshua Lederberg aliyeshinda Tuzo ya Nobeli, aliuliza hivi: “Je, mambo ni afadhali leo kuliko yalivyokuwa karne moja iliyopita? Katika nyanja nyingi, mambo ni mabaya zaidi. Tumepuuza viini, nasi tunavuna matokeo ya uzembe wetu.” Je, jitihada za sayansi ya tiba na mataifa yote ya ulimwengu zitasuluhisha matatizo hayo? Je, hatimaye magonjwa ya kuambukiza yatakomeshwa kama vile ugonjwa wa ndui ulivyokomeshwa? Makala yetu inayofuata itajibu maswali hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Kushinda Ndui na Polio
Mwishoni mwa Oktoba 1977, Shirika la Afya Ulimwenguni lilimpata mtu wa mwisho aliyekuwa akiugua ugonjwa wa ndui. Ali Maow Maalin, mpishi wa hospitali aliyekuwa akiishi Somalia, hakulemewa sana na ugonjwa huo, naye alipona baada ya majuma machache. Watu wote waliokuwa wameshirikiana naye walichanjwa.
Madaktari walisubiri kwa miaka miwili. Mtu yeyote ambaye angeripoti kisa kingine cha kweli cha mtu anayeugua ndui angepata zawadi ya dola 1,000. Hakuna yeyote aliyeripoti kisa cha kweli, na mnamo Mei 8, 1980, Shirika la Afya Ulimwenguni likatangaza rasmi kwamba “Ulimwengu na wakazi wake wote wameushinda ugonjwa wa ndui.” Miaka kumi tu iliyotangulia, ugonjwa wa ndui ulikuwa ukiua watu milioni mbili kila mwaka. Kwa mara ya kwanza katika historia, ugonjwa hatari wa kuambukiza ukawa umekomeshwa.a
Ugonjwa wa polio, ambao hulemaza watu utotoni, ulionekana pia ungeweza kukomeshwa. Mwaka wa 1955, Jonas Salk, alivumbua chanjo ya polio, na miradi ya kuchanja watu dhidi ya polio ikaanza Marekani na katika nchi nyingine. Baadaye, chanjo iliyopitishwa mdomoni ikavumbuliwa. Mwaka wa 1988, Shirika la Afya Ulimwenguni lilianzisha mradi wa ulimwenguni pote wa kuondoa polio.
Dakt. Gro Harlem Brundtland, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, anaeleza hivi: “Tulipoanza jitihada za kuondolea mbali polio ulimwenguni katika mwaka wa 1988, ugonjwa huo ulikuwa ukilemaza watoto 1000 kila siku. Katika mwaka wa 2001, kulikuwa na visa vinavyopungua 1000 kwa mwaka mzima.” Sasa polio inapatikana katika chini ya nchi kumi, ingawa pesa zaidi zitahitajiwa kusaidia nchi hizo kuukomesha kabisa ugonjwa huo.
[Maelezo ya Chini]
a Ugonjwa wa ndui ulifaulu kukomeshwa ulimwenguni pote kupitia chanjo kwa sababu, tofauti na magonjwa mengine ambayo huenezwa vinginevyo kama vile kupitia panya na wadudu, virusi vya ndui huishi mwilini mwa binadamu tu.
[Picha]
Mvulana Mwethiopia apokea chanjo ya polio
[Hisani]
© WHO/P. Virot
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
UKIMWI—Tauni ya Siku Zetu
UKIMWI umekuwa tisho ulimwenguni pote. Miaka 20 hivi tangu ulipogunduliwa, watu zaidi ya milioni 60 wameambukizwa. Maofisa wa afya wanaonya kwamba UKIMWI ungali katika “hatua za kwanza-kwanza.” Idadi ya watu wanaoambukizwa “inazidi kuongezeka kuliko ilivyodhaniwa awali,” nayo matokeo katika sehemu zenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaougua ugonjwa huo yanasikitisha.
Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inaeleza hivi: “Walio wengi kati ya watu wanaougua UKIMWI ulimwenguni wako katika umri ambao wanaweza kufanya kazi vizuri zaidi.” Kwa hiyo, inasemekana kwamba nchi nyingi zilizo kusini mwa Afrika zitapoteza asilimia 10 hadi 20 ya wafanyakazi wake kufikia mwaka wa 2005. Ripoti hiyo pia inasema: “Katika nchi zilizo kusini mwa Sahara, watu hutarajiwa kuishi miaka 47. Bila UKIMWI watu wangeweza kuishi wastani wa miaka 62.”
Kufikia sasa chanjo ya UKIMWI haijapatikana, na ni asilimia 4 tu ya watu milioni 6 wanaougua UKIMWI katika nchi zinazoendelea ambao wanapata matibabu ya aina fulani. Kwa sasa hakuna dawa ya UKIMWI, na madaktari wanahofia kwamba watu wengi ambao wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo hatimaye wataugua UKIMWI.
[Picha]
Chembe za “T lymphocyte” zilizoambukizwa virusi vya UKIMWI
[Hisani]
Godo-Foto
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mfanyakazi katika maabara achunguza aina sugu ya virusi
[Hisani]
CDC/Anthony Sanchez
-
-
Ulimwengu Usio na MagonjwaAmkeni!—2004 | Mei 22
-
-
Ulimwengu Usio na Magonjwa
“Nchi zote zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha kwamba watu wote wanapata matibabu ya msingi, kwani, watu wa nchi moja wakiwa na afya nzuri watu katika nchi nyingine watafaidika.” —AZIMIO LA ALMA-ATA, SEPTEMBA 12, 1978.
MIAKA 25 iliyopita watu fulani walionelea kwamba haingewezekana kwa kila mtu duniani kupata matibabu ya msingi. Wajumbe katika Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Matibabu ya Msingi, uliofanywa huko Alma-Ata, panapoitwa Kazakhstan leo, waliazimia kwamba wanadamu wote wachanjwe dhidi ya magonjwa hatari ya kuambukiza kufikia mwaka wa 2000. Pia, walitumainia kwamba kufikia mwaka huo, watu wote duniani wangekuwa na mazingira safi na maji safi. Mataifa yote yaliyo wanachama wa Shirika la Afya Ulimwenguni yalitia sahihi azimio hilo.
Bila shaka mradi wenyewe ulistahili pongezi, lakini kutekelezwa kwa azimio hilo kumekuwa jambo lenye kuvunja moyo sana. Matibabu ya msingi hayapatikani kwa watu wote ulimwenguni, nayo magonjwa ya kuambukiza yanazidi kuhatarisha afya ya mabilioni ya watu duniani. Mara nyingi magonjwa hayo hatari huwashambulia watoto na watu wazima walio katika upeo wa maisha yao.
Hata tisho la yale magonjwa matatu, UKIMWI, kifua-kikuu, na malaria, halijachochea ‘nchi zishirikiane.’ Hazina ya Kupambana na UKIMWI, Kifua-kikuu na Malaria iliyoanzishwa majuzi, iliomba serikali zichange dola bilioni 13 ili kusaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa hayo. Hata hivyo, kufikia katikati ya mwaka wa 2002, dola zipatazo bilioni 2 tu ndizo zilizokuwa zimetolewa. Mwaka huohuo dola bilioni 700 hivi zilitumiwa katika shughuli za kijeshi! Ni jambo lenye kusikitisha kwamba katika ulimwengu wa leo uliogawanyika, ni mambo machache sana yanayoweza kuunganisha mataifa yote kwa faida ya watu wote.
Ingawa maofisa wa afya wana nia njema, hawana uwezo wa kupambana na magonjwa ya kuambukiza. Huenda serikali zisitoe pesa zinazohitajiwa. Dawa nyingi hazina nguvu ya kuangamiza bakteria sugu, na watu wengi wanaishi maisha yanayohatarisha afya yao. Isitoshe, matatizo makubwa kama vile umaskini, vita, na njaa hufanya iwe rahisi kwa mamilioni ya watu kushambuliwa na viini mbalimbali.
-