Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maadili Yalipoporomoka Ghafula
    Amkeni!—2007 | Aprili
    • Wakati wa hali hizo zenye kutisha sana za Vita vya Pili vya Ulimwengu, badala ya kushikamana na viwango vya maadili vilivyokuwepo kwa muda mrefu, watu walianzisha viwango vyao wenyewe vya maadili. Kitabu (Love, Sex and War—Changing Values, 1939-1945) kinachozungumzia kubadilika kwa kanuni za maadili kilisema hivi: “Ilionekana kwamba viwango vyote vya maadili kuhusu ngono vilikuwa vimeondolewa wakati wa vita, kwani ukosefu wa maadili ambao uliruhusiwa kwa watu waliokuwa vitani uliwaathiri pia raia. . . . Hekaheka na msisimko wa vita ulimomonyoa maadili, na uhai wa raia ulionekana kuwa usio na thamani kubwa kama tu ule wa askari waliokuwa vitani.”

      Hofu ya kwamba mtu anaweza kufa wakati wowote iliwafanya watu watamani sana kuwa na mahusiano ya kimahaba, hata kwa muda mfupi tu. Akitetea utovu huo wa maadili katika ngono wakati wa miaka hiyo ya vita, mwanamke mmoja Mwingereza alisema hivi: “Si eti tulikuwa na maadili mapotovu, ni kwamba tu vita vilikuwa vikiendelea.” Askari mmoja Mmarekani alikiri hivi, “Kwa maoni ya watu wengi, tulikuwa na maadili mapotovu, lakini tulikuwa vijana na tungeweza kufa wakati wowote.”

  • Maadili Yalipoporomoka Ghafula
    Amkeni!—2007 | Aprili
    • Viwango Vipya

      Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, uchunguzi mbalimbali ulichapishwa kuhusu tabia ya watu kuelekea ngono. Uchunguzi mmoja kama huo nchini Marekani katika miaka ya 1940 uliitwa Ripoti ya Kinsey iliyokuwa na zaidi ya kurasa 800. Kwa sababu hiyo, watu wengi walianza kuzungumza waziwazi kuhusu mambo ya ngono ambayo kabla ya hapo hayangeweza kuzungumziwa waziwazi. Ingawa baadaye ilionekana kwamba takwimu zilizotolewa katika ripoti hiyo kuhusu watu wanaofanya ngono na watu wa jinsi yao na matendo mengine mapotovu ya ngono zilikuwa zimetiliwa chumvi, uchunguzi huo ulifunua jinsi maadili yalivyoporomoka baada ya vita hivyo.

      Kwa kipindi fulani, kulikuwa na jitihada ya kudumisha maadili yanayofaa. Kwa mfano, kwenye redio, sinema, na televisheni, habari chafu zilichujwa. Lakini jambo hilo halikudumu. William Bennett, ambaye awali alikuwa waziri wa elimu wa Marekani, alieleza hivi: “Hata hivyo, kufikia miaka ya 1960, ustaarabu ulianza kuporomoka kwa kasi nchini Marekani.” Jambo hilo lilionekana pia katika nchi nyingine nyingi. Kwa nini maadili yaliporomoka kwa kasi sana katika miaka ya 1960?

      Kana kwamba mambo hayo yalitendeka kwa mfululizo, harakati ya kuwakomboa wanawake na kubadilika kwa mitazamo kuhusu ngono pamoja na yale yaliyoitwa maadili mapya, yalianza mwongo huohuo. Pia, dawa za kupanga uzazi zilibuniwa. Kwa kuwa sasa watu wangeweza kufurahia ngono bila hofu ya kupata mimba, walianza kufanya ngono ovyoovyo bila kuwajibika.

      Wakati huohuo, vyombo vya habari, sinema, na televisheni vililegeza viwango vyake vya maadili. Baadaye, Zbigniew Brzezinski, ambaye hapo awali alikuwa mkuu wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani alisema hivi kuhusu maadili yanayoonyeshwa katika televisheni: “Wanatukuza kujitosheleza, wao huonyesha jeuri na ukatili kuwa mambo ya kawaida, [na] wanaunga mkono kufanya ngono na watu wengi.”

      Kufikia miaka ya 1970, mashine za kuchezea kanda za video zilikuwa zimeanza kutumiwa sana. Sasa watu wangeweza kuona picha chafu sana wakiwa faraghani, habari ambazo hawangeweza kutazama katika majumba ya sinema ya umma. Katika nyakati za karibuni, mtu yeyote aliye na kompyuta, popote alipo ulimwenguni anaweza kupata ponografia chafu zaidi kwenye Intaneti.

      Matokeo yake yanatisha. Hivi majuzi, msimamizi mmoja wa gereza huko Marekani alisema: “Miaka kumi iliyopita vijana walipoletwa hapa, ningeweza kuwapa mashauri kuhusu lililo sawa na lililo kosa. Lakini vijana wanaoletwa siku hizi hawaelewi ninasema nini.”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki