-
Mambo Tunayojua Sasa Kuhusu HomaAmkeni!—2005 | Desemba 22
-
-
Je, Vitarudi Tena?
Kulingana na wataalamu wengi, swali, si ikiwa virusi hivyo vya homa yenye kuua vitarudi bali ni vitarudi lini na jinsi gani? Kwa kweli, wataalamu fulani wanatarajia kulipuka kwa aina mpya kabisa ya virusi vya homa kila baada ya miaka 11 hivi na homa mbaya sana baada ya kila miaka 30. Kulingana na utabiri huo, huenda tauni nyingine ikatokea hivi karibuni.
Jarida la kitiba Vaccine liliripoti hivi katika mwaka wa 2003: “Miaka 35 imepita tangu kutokea kwa tauni ya homa ulimwenguni, na kipindi kirefu zaidi kuwahi kurekodiwa kati ya tauni moja hadi nyingine ni miaka 39.” Makala hiyo iliendelea kusema: “Virusi hivyo vinaweza kutokea China au katika nchi iliyo karibu nayo na vinaweza kutia ndani antijeni au maambukizo mabaya yanayotokana na virusi vya homa ya wanyama.”
Makala hiyo ya jarida Vaccine ilitabiri hivi kuhusu virusi hivyo: “Vitaenea haraka ulimwenguni pote. Kutakuwa na milipuko kadhaa ya maambukizo. Virusi hivyo vitaenea haraka na kotekote, na watu wa kila umri wataambukizwa, navyo vitavuruga utendaji wa kijamii na kiuchumi katika nchi zote. Watu wengi sana wa karibu kila umri watakufa. Inaelekea kwamba vituo vya afya hata katika nchi zilizoendelea kiuchumi havitaweza kukabiliana ifaavyo na mahitaji ya afya.”
Hali hiyo ni mbaya kadiri gani? John M. Barry, mwandishi wa kitabu The Great Influenza, anatoa maoni haya: “Gaidi mwenye silaha ya nyuklia ni tisho kwa kila mwanasiasa. Tauni mpya ya homa inapaswa kuonwa kuwa tisho kama hilo.”
-
-
Mambo Tunayojua Sasa Kuhusu HomaAmkeni!—2005 | Desemba 22
-
-
Kwa hiyo, swali linalofadhaisha ni: Je, tauni ya mwaka wa 1918-1919 inaweza kutokea tena? Ona maoni yaliyochapishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kitiba ya London: “Katika njia fulani, hali za leo zinafanana na hali zilizokuwapo mwaka wa 1918: watu wengi sana wanasafiri kutoka nchi moja hadi nyingine kwa sababu ya kuboreshwa kwa njia za usafiri, kuna maeneo mengi yenye vita na matatizo ya utapiamlo na ukosefu wa usafi, idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka kufikia bilioni sita na nusu na idadi kubwa ya watu hao wanaishi mijini nayo miji mingi haina mifumo mizuri ya kuondoa maji machafu na takataka.”
Mtaalamu mashuhuri kutoka Marekani anakata kauli hivi: “Kwa ufupi, kila mwaka tunakaribia zaidi tauni nyingine.”
-