-
Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu YanaongezekaAmkeni!—2003 | Mei 22
-
-
Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu Yanaongezeka
NI WAKATI wa kulala huko Amerika Kusini. Mama mmoja anamlaza mtoto wake kitandani, anamfunika vizuri, na kumtakia usiku mwema. Lakini usiku huo mdudu mweusi mwenye urefu wa sentimeta tatu hivi ambaye huuma karibu na mdomo anatoka kwenye maficho yake katika dari la nyumba. Bila kujulikana, anamwangukia mtoto huyo usoni na kuuma ngozi yake nyororo kwa mdomo wake mrefu. Mdudu huyo ananyonya damu ya mtoto na kuacha kinyesi chake chenye vimelea. Akiwa angali usingizini, mtoto huyo anajikuna usoni na kueneza kinyesi hicho kwenye kidonda chote.
Kupitia kidonda hicho, mtoto huyo anaambukizwa maradhi ya Chagas. Baada ya juma moja hivi, anaugua homa na mwili wake unafura. Asipokufa, vimelea hivyo vinaweza kukaa mwilini mwake vikishambulia moyo, neva, na chembe zake. Huenda miaka 10 hadi 20 ikapita bila dalili zozote kuonekana. Hata hivyo, baadaye anaweza kupata vidonda katika mfumo wake wa kusaga chakula, kuathiriwa sehemu fulani ya ubongo, na hatimaye kufa kwa sababu ya moyo kushindwa kufanya kazi.
Hadithi hiyo ya kuwaziwa inaonyesha jinsi maradhi ya Chagas huambukizwa. Huko Amerika Kusini, mamilioni ya watu wamo katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo ambayo huua.
Wadudu Wanaoishi na Wanadamu
Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema hivi: “Magonjwa mengi ya kuambukizwa husababishwa na viini ambavyo huenezwa na wadudu.” Neno “wadudu” hutumiwa kurejelea wale wenye miguu sita kama nzi, viroboto, mbu, chawa, na mbawakavu, na pia walio na miguu minane kama vile kupe na utitiri.
Wadudu wengi hawadhuru watu, na wengine ni muhimu sana. Bila wadudu fulani, mimea na miti mingi ambayo wanadamu na wanyama hutegemea kwa chakula haiwezi kuchavushwa na hivyo haiwezi kuzaa matunda. Wadudu wengine hugeuza takataka kuwa bidhaa zenye faida. Wadudu wengi hula mimea tu, na wengine hula wadudu wengine.
Ni kweli kwamba baadhi ya wadudu huudhi kwa sababu ya kuwauma watu na wanyama, au hawapendezi kwa kuwa wametapakaa kila mahali. Wengine huharibu mimea. Hata hivyo, wadudu fulani hueneza magonjwa na wengine husababisha kifo. Duane Gubler wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa alisema kwamba magonjwa yanayoenezwa na wadudu “yaliathiri na kuua watu wengi zaidi katika karne ya 17 hadi mwanzoni mwa karne ya 20 kuliko sababu nyingine zote zikijumlishwa pamoja.”
Leo, karibu mtu 1 kati ya watu 6 anaugua ugonjwa ambao umeenezwa na wadudu. Licha ya kusababisha mateso, inagharimu pesa nyingi kutibu magonjwa yanayoenezwa na wadudu hasa katika nchi zinazoendelea ambazo hazina uwezo mkubwa wa kifedha. Hata mlipuko mmoja wa ugonjwa unaweza kugharimu pesa nyingi sana. Kisa kimoja kama hicho kilichotokea magharibi mwa India mnamo mwaka wa 1994 kiligharimu nchi hiyo na nchi nyingine mamilioni ya pesa. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, uchumi wa nchi maskini zaidi duniani hauwezi kusitawi mpaka magonjwa hayo yadhibitiwe.
Jinsi Wadudu Wanavyoambukiza Magonjwa
Wadudu huambukiza magonjwa kwa njia kuu mbili. Kwanza, wao hubeba viini hivyo nje ya miili yao. Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema kwamba kama vile tu uchafu ulio chini ya viatu unavyoingizwa nyumbani, “ndivyo nzi wanavyoweza kubeba mamilioni ya viini miguuni mwao na kusababisha magonjwa.” Kwa mfano, nzi wanaweza kubeba uchafu kutoka chooni na kuutia kwenye chakula au kinywaji. Kupitia njia hiyo, wanadamu wanaweza kuambukizwa magonjwa hatari kama vile homa ya matumbo, kuhara damu, na kipindupindu. Nzi wanaweza pia kueneza mtoto wa jicho, ugonjwa unaowafanya watu wengi zaidi duniani wawe vipofu. Ugonjwa huo hupofusha kwa kuharibu sehemu inayofanana na kioo mbele ya jicho. Watu 500,000,000 duniani kote huugua ugonjwa huo.
Mende hukaa kwenye maeneo machafu, na inasemekana kwamba wao hubeba viini vya magonjwa juu ya miili yao. Isitoshe, wataalamu wanasema kwamba ongezeko la watu wanaougua pumu, hasa watoto, linasababishwa na mizio ya mende. Kwa mfano, siku nyingi Ashley, msichana mwenye umri wa miaka 15, hakuweza kupumua kwa sababu ya ugonjwa huo. Daktari alipokuwa akipima mapafu yake, mende alianguka kutoka kwenye shati lake na kutembea juu ya meza ya daktari.
Wadudu Ambao Hubeba Viini Mwilini
Wadudu wanaweza pia kubeba virusi, bakteria, au vimelea mwilini mwao, na kuvipitisha kwa wanadamu wanapouma au kwa njia nyinginezo. Ni wadudu wachache tu ambao hueneza magonjwa kwa wanadamu kwa njia hiyo. Kwa mfano, ingawa kuna maelfu ya aina za mbu, aina moja tu ya mbu anayeitwa Anopheles ndiye anayeeneza viini vya malaria. Ugonjwa huo huua watu wengi zaidi kati ya magonjwa yote ya kuambukizwa duniani (baada ya kifua kikuu).
Hata hivyo, aina nyingine za mbu hueneza magonjwa mengine mengi. Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti hivi: “Kati ya wadudu wanaoeneza magonjwa, mbu ndio hatari zaidi kwa sababu wao hueneza malaria, kidingapopo, na homa ya manjano, magonjwa ambayo huua watu milioni kadhaa na kuwapata mamia ya mamilioni ya watu kila mwaka.” Angalau asilimia 40 ya watu duniani wamo katika hatari ya kuambukizwa malaria, na asilimia 40 hivi wamo katika hatari ya kupata ugonjwa wa kidingapopo. Katika sehemu nyingi, watu huambukizwa yote mawili.
Mbali na mbu, kuna wadudu wengine pia ambao hueneza magonjwa kupitia viini vilivyo ndani ya miili yao. Mbung’o hueneza viini vya protozoa ambavyo husababisha malale. Ugonjwa huo huwapata mamia ya maelfu ya watu na kufanya jamii nzima-nzima zihame na kuacha mashamba yao yenye rutuba. Wadudu wanaoitwa black flies hueneza upofu wa mtoni, na wamefanya watu wapatao 400,000 barani Afrika wawe vipofu. Wadudu wanaoitwa usubi hueneza protozoa ambao husababisha magonjwa fulani yanayolemaza, yanayoumbua sura, na mara nyingi kuua, na ambayo sasa yamewapata watu wengi wenye umri mbalimbali duniani kote. Kiroboto anayepatikana mahali pengi anaweza kueneza minyoo, uvimbe wa ubongo, ugonjwa wa tularemia, na hata tauni. Katika Zama za Kati (500 W.K. hadi 1500 W.K.), tauni ilisababisha vifo vya thuluthi moja ya watu au zaidi huko Ulaya katika kipindi cha miaka sita tu.
Chawa, utitiri, na kupe wanaweza kueneza magonjwa mbalimbali ya typhus na mengineyo. Kupe katika maeneo yenye joto la wastani wanaweza kueneza ugonjwa hatari wa Lyme unaopatikana sana huko Marekani na Ulaya. Uchunguzi uliofanywa nchini Sweden ulionyesha kwamba ndege wahamaji wanaweza kubeba kupe umbali wa maelfu ya kilometa, na huenda wakahama na magonjwa hadi maeneo mengine. Kitabu Britannica kinasema kwamba “kupe husafirisha viini vingi vya magonjwa kuliko wadudu wengine wote (isipokuwa mbu).” Kwa kweli, kupe wanaweza kusafirisha viini aina tatu vya magonjwa na kupitisha vyote wanapomuuma mtu mara moja tu!
Magonjwa Yalitoweka kwa Muda
Wanasayansi waligundua kwamba wadudu hueneza magonjwa katika mwaka wa 1877. Tangu wakati huo, kampeni kabambe zimefanywa ili kuzuia na kuua wadudu hao. Mnamo mwaka wa 1939, dawa ya kuua wadudu ya DDT iligunduliwa, na kufikia miaka ya 1960, magonjwa ambayo huenezwa na wadudu hayakuwa tena tisho kubwa kwa afya ya umma nje ya Afrika. Sasa badala ya kuzuia wadudu, jitihada ilifanywa kutibu magonjwa hayo haraka kwa kutumia dawa. Watu hawakuona haja ya kufanya utafiti kuhusu wadudu na makao yao. Dawa mpya ziligunduliwa, na ilidhaniwa kwamba wanasayansi wangegundua dawa ambayo ingeweza kutibu magonjwa yote bila madhara yoyote. Magonjwa ya kuambukizwa yalikuwa yametoweka. Lakini baada ya muda yalirudi. Makala ifuatayo itaonyesha kwa nini yalirudi.
[Blabu katika ukurasa wa 3]
Leo, mtu 1 kati ya watu 6 anaugua ugonjwa unaoenezwa na wadudu
[Picha katika ukurasa wa 3]
Mdudu ambaye huuma mdomoni
[Picha katika ukurasa wa 4]
Nzi hubeba viini vya magonjwa miguuni
[Picha katika ukurasa wa 5]
Wadudu wengi hubeba viini vya magonjwa ndani ya miili yao
Nzi anayeeneza upofu wa mtoni
Mbu hueneza malaria, kidingapopo, na homa ya manjano
Chawa wanaweza kueneza magonjwa ya “typhus”
Viroboto hueneza uvimbe wa ubongo na magonjwa mengineyo
Mbung’o hueneza malale
[Hisani]
WHO/TDR/LSTM
CDC/James D. Gathany
CDC/Dr. Dennis D. Juranek
CDC/Janice Carr
WHO/TDR/Fisher
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
Clemson University - USDA Cooperative Extension Slide Series, www.insectimages.org
-
-
Kwa Nini Yamerudi?Amkeni!—2003 | Mei 22
-
-
Kwa Nini Yamerudi?
MIAKA 40 hivi iliyopita, ilidhaniwa kwamba magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile malaria, homa ya manjano, na kidingapopo yalikuwa yamekomeshwa katika sehemu nyingi za ulimwengu. Lakini pasipo kutarajiwa, magonjwa hayo yakaanza kurudi tena.
Kwa nini? Sababu moja ni kwamba wadudu fulani na viini vilivyo mwilini mwao vimekuwa sugu hivi kwamba haviwezi kufa kwa dawa. Jambo hilo limetokea kwa sababu watu wanatumia dawa za kuua wadudu kupita kiasi na wanatumia vibaya dawa za matibabu. Kitabu Mosquito kinasema: “Katika familia nyingi maskini, watu hununua dawa halafu wanazitumia kidogo tu kutuliza maumivu yao, kisha wanahifadhi dawa zilizobaki ili wazitumie watakapougua tena.” Kwa kuwa hawaponi kabisa, viini vyenye nguvu vinaweza kuendelea kuishi miilini mwao na kutokeza viini vingine sugu.
Kubadilika kwa Hali ya Hewa
Jambo moja kuu ambalo limesababisha magonjwa yanayoenezwa na wadudu kurudi tena ni mabadiliko ya kimazingira na ya kijamii. Kwa mfano, hali ya hewa ulimwenguni pote inabadilika. Wanasayansi fulani wanatarajia kwamba wadudu wanaoeneza magonjwa watahamia katika maeneo ya baridi kwa kuwa joto linaongezeka ulimwenguni pote. Kuna uthibitisho kwamba huenda jambo hilo linatukia. Dakt. Paul R. Epstein wa Kituo cha Afya na Mazingira ya Ulimwenguni Pote cha Chuo cha Kitiba cha Harvard anasema hivi: “Inasemekana kwamba wadudu na magonjwa yanayoenezwa na wadudu (kutia ndani malaria na kidingapopo) yanarudi katika maeneo ya milimani huko Afrika, Asia, na Amerika Kusini.” Huko Costa Rica, kufikia hivi majuzi ugonjwa wa kidingapopo ulikuwa unapatikana tu katika Pwani ya Pasifiki ya nchi hiyo, lakini sasa umeenea katika maeneo ya milimani na katika nchi yote.
Lakini joto linaweza pia kusababisha hali nyinginezo. Katika maeneo fulani yenye joto, mito hukauka na kuwa vidimbwi, na katika maeneo mengine joto husababisha mvua na mafuriko ambayo hutokeza vidimbwi vyenye maji yaliyotuama. Mbu huzaana katika maji hayo. Joto hufanya mbu wazaane haraka, na kuwafanya wadumu kwa muda mrefu. Mbu huwa watendaji sana kunapokuwa na joto. Joto hilo huingia katika utumbo wao na kufanya viini vilivyomo vizaane haraka. Hivyo, mbu akimuuma mtu mara moja wakati wa joto, kuna uwezekano mkubwa kwamba mtu huyo ataambukizwa ugonjwa. Lakini, kuna mambo mengine ambayo yamesababisha magonjwa yazuke tena.
Mfano Unaoonyesha Jinsi Wadudu Wanavyoeneza Magonjwa
Mabadiliko ya kijamii yanaweza kusababisha magonjwa yanayoenezwa na wadudu. Ili kuelewa jambo hilo, tunahitaji kuchunguza jinsi wadudu wanavyohusika. Unapochunguza magonjwa mengi, utaona kwamba si wadudu tu ambao huchangia kuyaeneza. Mnyama au ndege anaweza kubeba viini vya ugonjwa nje ya mwili wake au ndani ya mwili wake. Mnyama huyo au ndege huyo anaweza kuendelea kuishi na viini hivyo bila kuathiriwa.
Mfano mmoja ni ugonjwa wa Lyme, ambao uligunduliwa mwaka wa 1975. Ugonjwa huo ulionekana kwanza huko Lyme, Connecticut, Marekani, na ndiyo sababu ulipewa jina hilo. Huenda bakteria inayosababisha ugonjwa huo iliingia Amerika Kaskazini miaka mia moja iliyopita kupitia kwa panya au mifugo waliokuwa ndani ya meli zilizotoka Ulaya. Kupe mdogo anayeitwa Ixodes anaponyonya damu ya mnyama mwenye ugonjwa huo, bakteria hudumu katika utumbo wa kupe huyo hadi anapokufa. Kupe huyo anaweza kueneza bakteria hizo anapomuuma mnyama mwingine au mwanadamu.
Kwa muda mrefu, ugonjwa wa Lyme umekuwa ukiwakumba hasa watu wanaoishi katika eneo lililo kaskazini-mashariki mwa Marekani. Katika eneo hilo, panya wenye miguu myeupe ndio huwa hasa na bakteria za ugonjwa wa Lyme. Panya hao pia hubeba kupe, hasa wale kupe wanaoendelea kukomaa. Kupe hao wakiisha kukomaa, wao huhamia kwenye miili ya mbawala. Kisha wao hujamiiana na kuwanyonya mbawala. Kupe wa kike akiisha kushiba damu, yeye huanguka chini ili kutaga mayai, kisha kupe wanaongezeka.
Hali Zinapobadilika
Wanyama na wadudu wamebeba viini kwa miaka mingi bila kuwaathiri wanadamu. Lakini hali zinapobadilika, ugonjwa ambao haukuwa ukienea unaweza kuenea kwa watu wengi wanaoishi katika eneo moja. Ni hali zipi zilizosababisha ugonjwa wa Lyme uenee?
Hapo zamani, mbawala hawakuwa wengi kwani wanyama fulani waliwawinda. Hivyo, wanadamu hawakuwa wakivamiwa sana na wale kupe wanaoishi kwenye miili ya mbawala. Wakati walowezi Wazungu walipokata misitu ili walime, mbawala na wanyama waliowawinda walihamia katika maeneo mengine. Lakini katikati ya miaka ya 1800, wakulima walihamia katika maeneo ya magharibi mwa Marekani. Basi, mashamba yakaachwa ukiwa, na msitu ukatokea tena. Mbawala wakarudi, lakini wale wanyama waliokuwa wanawawinda hawakurudi. Kwa hiyo, mbawala wakaongezeka sana, na kupe pia.
Muda fulani baadaye, bakteria ya ugonjwa wa Lyme ikaibuka, na ikadumu mwilini mwa wanyama kwa makumi ya miaka kabla ya wanadamu kuambukizwa. Hata hivyo, watu walianza kujenga nyumba karibu na msitu huo, na watoto na watu wazima wengi wakahamia katika eneo hilo lenye kupe. Kupe wakaanza kuwanyonya wanadamu, na wanadamu wakapata ugonjwa wa Lyme.
Magonjwa Katika Ulimwengu Wenye Msukosuko
Matukio hayo yanaonyesha njia moja tu ambayo magonjwa hutokea na kuenea na ni mfano mmoja tu unaoonyesha jinsi shughuli za wanadamu zinavyochangia kuzuka kwa magonjwa. Mwanamazingira Eugene Linden anasema hivi katika kitabu chake The Future in Plain Sight: “Magonjwa mengi sugu yamezuka tena kwa sababu ya shughuli za wanadamu.” Kuna mambo mengine pia yanayoonyesha jinsi wanadamu wanavyochangia kuenea kwa magonjwa. Kwa mfano, kwa kuwa watu wengi siku hizi wanaweza kusafiri haraka, viini vya magonjwa vinaweza kuenezwa ulimwenguni pote. Uharibifu wa makao ya viumbe wakubwa na wadogo unaangamiza jamii mbalimbali za mimea na wanyama. Linden anasema hivi: “Uchafuzi unaharibu hewa na maji na kudhoofisha mifumo ya kinga ya wanyama na wanadamu.” Kisha anaongezea kauli ya Dakt. Epstein kwa kusema hivi: “Kwa kuwa wanadamu wameharibu mazingira, wamedhoofisha uwezo wa kiasili wa kukinza magonjwa na kutokeza hali zinazofanya viini viongezeke.”
Msukosuko wa kisiasa husababisha vita ambavyo huharibu mazingira na njia za usafiri zinazowasaidia watu kupata matibabu na chakula. Zaidi ya hilo, kituo cha Internet cha jumba fulani la makumbusho huko Marekani kinachoitwa Biobulletin kinasema hivi: “Kwa kawaida wakimbizi, walio dhaifu na wanaoteseka kwa sababu ya utapiamlo, huwekwa katika kambi zenye watu wengi mno na zenye uchafu mwingi, hivyo wao hukabili hatari ya kuambukizwa magonjwa.”
Matatizo ya kiuchumi huwalazimu watu kuhamia sehemu nyingine za nchi au nchi nyingine, na mara nyingi wao huhamia miji yenye watu wengi kupita kiasi. Kituo cha Biobulletin kinasema hivi: “Viini husitawi katika maeneo yenye watu wengi.” Idadi ya watu inapoongezeka sana, “mara nyingi miradi ya utunzaji wa afya hukwama, kama vile kuwaelimisha watu, kuwapa chakula bora, na kuwadunga sindano za chanjo.” Watu wanaposongamana sana, inakuwa vigumu kudumisha usafi kwa sababu ya kukosa maji na mifumo ya kuondoa maji machafu. Katika hali hizo, wadudu huongezeka na viini huenea. Hata hivyo, kama makala inayofuata inavyoonyesha, kungali na matumaini.
[Blabu katika ukurasa wa 11]
“Magonjwa mengi sugu yamezuka tena kwa sababu ya shughuli za wanadamu”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Virusi vya West Nile Vyashambulia Marekani
Virusi vya West Nile, ambavyo huwapata wanadamu hasa wanapoumwa na mbu, viligunduliwa kwa mara ya kwanza huko Uganda mnamo mwaka wa 1937 na baadaye vikagunduliwa katika Mashariki ya Kati, Asia, Oceania, na Ulaya. Virusi hivyo viligunduliwa katika mabara ya Amerika mwaka wa 1999. Hata hivyo, tangu wakati huo imeripotiwa kwamba zaidi ya watu 3,000 wameambukizwa nchini Marekani na zaidi ya watu 200 wamekufa.
Ijapokuwa watu fulani huenda wakawa na dalili za ugonjwa huo, wengi hawajui kwamba wameambukizwa. Lakini wachache kati yao hupata magonjwa hatari kama vile ugonjwa wa kuvimba ubongo na homa ya uti wa mgongo. Kwa sasa hakuna chanjo wala tiba ya ugonjwa wa West Nile. Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vinaonya kwamba watu wanaweza pia kuambukizwa virusi vya West Nile wanapopandikizwa viungo au wanapotiwa damu ya mtu aliye navyo. Shirika la habari la Reuters lilisema hivi katika mwaka wa 2002: “Kwa sasa hakuna njia ya kupima damu yenye virusi vya West Nile.”
[Hisani]
CDC/James D. Gathany
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Jinsi Unavyoweza Kujikinga Madokezo Kadhaa
Waandishi wa Amkeni! walizungumza na wakazi wa maeneo yenye wadudu wengi na maeneo yanayokumbwa na magonjwa yanayoenezwa na wadudu ili kupata madokezo juu ya jinsi ya kudumisha afya bora. Huenda ukafaidika na mashauri yao.
Usafi Ndiyo Njia Bora ya Kujikinga
◼ Dumisha usafi nyumbani
“Funika vyombo vyenye vyakula. Funika vyakula vilivyopikwa hadi vinapopakuliwa. Safisha sehemu zilizomwagikiwa na vyakula bila kukawia. Usiache vyombo vilale vikiwa vichafu wala usiweke takataka nje usiku ukikusudia kuzitupa asubuhi. Funika au ufukie takataka kwani wadudu na panya hutafuta chakula usiku. Pia, hata ikiwa nyumba ina sakafu ya udongo, ni vizuri kuilainisha kwa saruji kwani hilo litasaidia kuzuia wadudu wasiingie nyumbani na pia kudumisha usafi.”—Afrika.
“Hifadhi matunda au vitu vyovyote vinavyowavutia wadudu nje ya nyumba. Weka mifugo yako kama vile mbuzi, nguruwe, na kuku nje ya nyumba. Funika vyoo vilivyo nje ya nyumba. Funika mbolea ya samadi udongoni bila kukawia au uifunike kwa chokaa ili kuzuia nzi. Hata ikiwa majirani hawafanyi mambo hayo, unaweza kuwawekea mfano mzuri kwa kupunguza idadi ya wadudu.”—Amerika Kusini.
[Picha]
Mtu asipofunika vyakula au takataka ni kana kwamba anawaalika wadudu wale naye
◼ Usafi wa mwili
“Sabuni si bei ghali, kwa hiyo nawa mikono mara nyingi na ufue nguo mara nyingi, hasa baada ya kuwasalimu watu au kuwagusa wanyama. Usiguse mizoga ya wanyama. Epuka kushika-shika mdomo, pua, na macho. Nguo zinapasa kufuliwa kwa ukawaida hata ikiwa zinaonekana kuwa safi. Marashi fulani huwavutia wadudu, kwa hiyo epuka sabuni zenye marashi.”—Afrika.
Njia za Kujikinga
◼ Haribu maeneo ambapo mbu huzaana
Funika tangi za maji na beseni za kufulia nguo. Haribu vyombo vyote vya kutekea maji ambavyo havina vifuniko. Usiache maji katika vyombo vya kuwekea maua. Mbu wanaweza kutaga mayai katika maji ya kidimbwi ambayo hayajasonga kwa muda wa siku nne.—Kusini-Mashariki mwa Asia.
◼ Jikinge na wadudu
Epuka kuwa nje wakati wadudu wengi wanapoanza kutokea na uepuke pia sehemu zote zenye wadudu. Jua hutua mapema katika maeneo ya kitropiki, kwa hiyo shughuli nyingi hufanywa usiku wakati wadudu wanapokuwa watendaji zaidi. Wakati magonjwa yanapozuka, ni rahisi kuambukizwa ikiwa utaketi na kulala nje.—Afrika.
[Picha]
Mtu anapolala nje katika maeneo yenye mbu wengi ni kana kwamba anawaalika wamtafune
Vaa mavazi yanayofunika mwili vizuri, hasa unapotembea msituni. Jipake dawa ya kufukuza wadudu ngozini na kwenye mavazi yako na ufuate maagizo yaliyoonyeshwa. Baada ya kutembea nje, angalia ikiwa wewe au watoto wako mna kupe. Wasafishe wanyama wako ili wasiwe na wadudu na uwatunze ifaavyo.—Amerika Kaskazini.
Epuka kuwa karibu na mifugo mara nyingi kwani unaweza kuambukizwa ugonjwa ukiumwa na wadudu waliowauma mifugo hao.—Asia ya Kati.
Washiriki wote wa familia wanapaswa kutumia vyandarua, hasa vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuwafukuza wadudu. Weka nyavu dirishani, na uzitengeneze zinapoharibika. Ziba nyufa zilizo pembeni mwa paa la nyumba ambapo wadudu wanaweza kuingia. Njia hizo za kujikinga zinagharimu kiasi fulani cha pesa, lakini unaweza kupoteza pesa nyingi sana ikiwa utalazimika kumpeleka mtoto hospitalini au mtu anayetegemewa katika familia anapougua.—Afrika.
[Picha]
Vyandarua vilivyotiwa dawa za kuwafukuza wadudu havigharimu pesa nyingi kama matibabu
Wazuie wadudu wasijifiche mahali popote nyumbani mwako. Piga lipu ukutani na kwenye dari, na uzibe nyufa na mashimo. Ikiwa nyumba imeezekwa kwa nyasi, funika dari hilo kwa kitambaa cha kuwazuia wadudu. Ondoa vitu vilivyorundamana kama vile marundo ya karatasi, marundo ya nguo, au picha nyingi zilizowekwa ukutani, kwani huko ndiko wadudu hujificha.—Amerika Kusini.
Watu wengine hudhani kwamba wadudu na panya ni wageni waheshimiwa. La hasha, wao si wageni! Usiwakaribishe kamwe. Tumia dawa za kuwafukuza na za kuwaua wadudu, lakini usisahau kufuata maagizo yaliyoonyeshwa. Tumia mitego ya nzi na vifaa vya kuwaua nzi. Uwe mbunifu: Mwanamke mmoja alitumia kitambaa kutengeneza mfuko, kisha akajaza mchanga katika mfuko huo na akauweka chini ya mlango ili kuwazuia wadudu wasiingie ndani ya nyumba.—Afrika.
[Picha]
Wadudu si wageni waheshimiwa. Wafukuze!
◼ Njia za kuzuia magonjwa
Imarisha mfumo wako wa kinga kwa kula vizuri, kupumzika vya kutosha, na kufanya mazoezi. Jitahidi kupunguza mfadhaiko.—Afrika.
Wasafiri: Jitahidini kupata habari za karibuni kuhusu visababishi vya magonjwa yanayoenezwa na wadudu. Habari hizo zinaweza kupatikana kwenye idara za afya na vituo vya Internet vya serikali. Kabla ya kusafiri, tumia dawa za kuzuia magonjwa ambayo hupatikana mahali unaposafiri.
Ukihisi U Mgonjwa
◼ Mwone daktari haraka
Magonjwa mengi yanaweza kutibiwa iwapo yanagunduliwa mapema.
◼ Hakikisha ugonjwa wako umetambuliwa kwa usahihi
Waone madaktari wanaotibu magonjwa yanayoambukizwa na wadudu na ikiwa umetembelea maeneo ya kitropiki mwone daktari anayetibu magonjwa yanayopatikana huko. Mweleze daktari dalili zako zote na maeneo yote ambayo umesafiri, hata sehemu ulizozitembelea zamani. Tumia dawa ikiwa lazima, na umalize vidonge vyote.
[Picha]
Magonjwa yanayoenezwa na wadudu yanaweza kufanana na magonjwa mengine. Mweleze daktari sehemu zote ulizozitembelea
[Hisani]
Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
Je, Wadudu Hueneza Virusi vya UKIMWI?
Baada ya kufanya utafiti kwa zaidi ya miaka kumi, wataalamu wa wadudu na wanasayansi wa kitiba hawajapata uthibitisho wowote unaoonyesha kwamba mbu au wadudu wengine hueneza virusi vya HIV vinavyosababisha UKIMWI.
Kwa mfano, mdomo wa mbu si kama sindano, kwani hauna njia moja tu ya kupitisha damu. Badala yake, mbu hufyonza damu kupitia njia moja na huondoa mate kupitia njia nyingine. Kisha, kulingana na Thomas Damasso, mtaalamu wa virusi vya UKIMWI anayefanya kazi katika Kikosi cha Utunzaji wa Afya cha Wilaya katika mji wa Mongu, Zambia, mfumo wa mbu wa kumeng’enya chakula huvunja-vunja damu na kuharibu virusi hivyo. Virusi vya UKIMWI havipatikani katika kinyesi cha wadudu. Tofauti na vimelea vya malaria, virusi vya UKIMWI haviingii katika tezi za mate za mbu.
Mtu huambukizwa virusi vya UKIMWI anapopata damu nyingi yenye virusi hivyo. Mbu hawezi kumwambukiza mtu virusi hivyo kwani damu inayobaki mdomoni mwake ni kidogo sana, hata ikiwa amemuuma baada tu ya kumuuma mtu mwingine mwenye UKIMWI. Wataalamu wanasema kwamba hata ukimgonga mbu aliye na damu nyingi yenye virusi vya UKIMWI juu ya kidonda, hutaambukizwa virusi hivyo.
[Hisani]
CDC/James D. Gathany
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kupe wanaoishi kwenye miili ya mbawala (picha kubwa kulia) wanawaambukiza wanadamu ugonjwa wa Lyme
Kushoto hadi kulia: kupe wa kike aliyekomaa, wa kiume aliyekomaa, na mtoto wa kupe, wote wana ukubwa wa kawaida
[Hisani]
All ticks: CDC
[Picha katika ukurasa wa 10, 11]
Mafuriko, uchafu, na uhamaji huchangia kuenea kwa magonjwa yanayosambazwa na wadudu
[Hisani]
FOTO UNACIONES (from U.S. Army)
-
-
Je, Kuna Matumaini Yoyote?Amkeni!—2003 | Mei 22
-
-
Je, Kuna Matumaini Yoyote?
SHIRIKA la Afya Ulimwenguni na mashirika mengine yanafanya utafiti na kujaribu kuzuia magonjwa leo. Mashirika kadhaa yanasambaza habari na kufanya utafiti kuhusu dawa mpya na njia mpya za kuzuia magonjwa. Jitihada hizo zinafanywa ili kukabiliana na tatizo hilo linalozidi kuwa sugu. Watu mmoja-mmoja na jamii zinaweza kujifunza kuhusu magonjwa hayo na kujikinga. Lakini, kuna tofauti kati ya kuwalinda watu mmoja-mmoja na kuyakomesha ulimwenguni kote.
Wataalamu wengi wanaamini kwamba watu wote wanapaswa kushirikiana na kutumainiana ili jitihada za kuzuia magonjwa ziweze kufaulu. Laurie Garrett, mwandishi wa habari na mshindi wa Tuzo ya Pulitzer, aliandika hivi katika kitabu chake The Coming Plague—Newly Emerging Diseases in a World out of Balance: “Utandawazi unawataka wanadamu kila mahali duniani waone kwamba wana mazingira mengine zaidi ya ujirani wao, mikoa yao, nchi zao, au maeneo yao. Viini na wadudu wanaovieneza hawatambui mipaka iliyowekwa na wanadamu.” Mlipuko wa ugonjwa huhangaisha watu duniani pote, bali si watu wa nchi moja tu.
Serikali na jamii fulani hushuku msaada wa aina yoyote ile unaotoka nje, hata kama unasaidia kuzuia magonjwa. Isitoshe, mara nyingi pupa ya kibiashara na kutopangia vizuri kwa ajili ya wakati ujao huharibu jitihada za kimataifa. Je, mwanadamu atashindwa kuzuia viini vya magonjwa? Mwandishi Eugene Linden, anayefikiri kuwa mwanadamu atashindwa, anasema hivi: “Tuna muda mfupi tu wa kubadili hali hiyo.”
Sababu ya Kuwa na Tumaini
Sayansi na tekinolojia hazijaweza kukomesha magonjwa yanayoenezwa na wadudu. Na, bila shaka, kuna magonjwa mengine mengi yanayohatarisha afya. Hata hivyo, kuna sababu ya kuwa na tumaini. Ingawa wanasayansi wameanza kuelewa ushirikiano tata ulioko kati ya viumbe hivi majuzi tu, wanatambua uwezo wa dunia wa kujifanya upya. Sayari yetu inaweza kujifanya upya na kurudia hali yake ya kawaida. Kwa mfano, misitu hukua tena inapokatwa na ushirikiano kati ya viini, wadudu, na wanyama huanza baada ya muda fulani.
La muhimu zaidi, ubuni tata wa viumbe huonyesha kuna Muumba, Mungu aliyeanzisha mifumo ya dunia. Wanasayansi wengi wanakubali kwamba kuna mtu fulani mwenye akili aliyeiumba dunia. Naam, watu wenye kufikiri hawawezi kukataa kwamba Mungu yuko. Biblia inasema kwamba Muumba, Yehova Mungu, ni Mweza-Yote na mwenye upendo. Anataka sana tuwe na furaha.
Biblia pia inasema kwamba mwanadamu wa kwanza alifanya dhambi kwa kukusudia, hivyo wanadamu wamerithi kutokamilika, ugonjwa, na kifo. Je, hiyo inamaanisha kwamba tutaendelea kuteseka daima? La! Kusudi la Mungu ni kufanya dunia hii iwe paradiso, ambapo wanadamu wataishi kwa amani na viumbe wengine wakubwa kwa wadogo. Biblia inatabiri kuhusu ulimwengu ambao hautakuwa na kiumbe yeyote atakayemdhuru mwanadamu, awe mnyama mkubwa au mdudu mdogo sana.—Isaya 11:6-9.
Hapana shaka kwamba wanadamu watakuwa na wajibu fulani katika kuleta mabadiliko hayo ya kijamii na ya kimazingira. Mungu alimpa mwanadamu wajibu wa “kuitunza” dunia. (Mwanzo 2:15) Katika paradiso ijayo, wanadamu watatekeleza wajibu huo kwa ukamili wakifuata maagizo kutoka kwa Muumba mwenyewe. Hivyo, tunaweza kutazamia wakati ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
-