-
Mkono wa Yehova WainuliwaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
1. Kwa nini Isaya amthamini Yehova?
ISAYA ampenda sana Yehova naye afurahia kumsifu. Yeye apaaza sauti: “Ee BWANA, wewe u Mungu wangu; nitakutukuza na kulihimidi jina lako.” Ni nini kinachomsaidia nabii huyo kumthamini Muumba wake kwa njia bora hivyo? Jambo muhimu ni ujuzi alio nao juu ya Yehova na matendo yake. Maneno yafuatayo ya Isaya yaufunua ujuzi huo: “Kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu, mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.” (Isaya 25:1) Kama vile Yoshua aliyeishi kabla yake, Isaya ajua kuwa Yehova ni mwaminifu na mwenye kutumainika, na kwamba “mashauri” yake yote—mambo anayokusudia—hutimia.—Yoshua 23:14.
2. Isaya sasa atangaza shauri gani la Yehova, na huenda shauri lake laelekezwa wapi?
2 Mashauri ya Yehova yahusisha matangazo yake ya hukumu dhidi ya adui za Israeli. Isaya sasa atangaza mojawapo ya hukumu hizo: “Umefanya mji kuwa ni chungu; mji wenye boma kuwa ni magofu; jumba la wageni kuwa si mji; hautajengwa tena milele.” (Isaya 25:2) Ni mji gani huo usio na jina? Huenda Isaya akawa anarejezea Ari wa Moabu—Moabu imekuwa adui ya watu wa Mungu kwa muda mrefu.a Au huenda analirejezea jiji jingine, lenye nguvu zaidi—Babiloni.—Isaya 15:1; Sefania 2:8, 9.
3. Adui za Yehova wamtukuzaje?
3 Adui za Yehova watatendaje wakati wa kutekelezwa kwa shauri lake dhidi ya jiji lao lenye nguvu? “Watu walio hodari watakutukuza, mji wa mataifa watishao utakuogopa.” (Isaya 25:3) Yaeleweka kwamba adui za Mungu Mweza Yote watamwogopa. Lakini wao wamtukuzaje? Je, wataiacha miungu yao isiyo ya kweli na kuikubali ibada safi? Hata kidogo! Badala yake, kama vile Farao na Nebukadreza, wamtukuza Yehova walazimikapo kutambua ukuu wake mkubwa.—Kutoka 10:16, 17; 12:30-33; Danieli 4:37.
4. “Mji wa mataifa watishao” uliopo leo ni upi, nao walazimikaje kumtukuza Yehova?
4 Leo, “mji wa mataifa watishao” ni “jiji kubwa lililo na ufalme juu ya wafalme wa dunia,” yaani, “Babiloni Mkubwa,” milki ya ulimwengu ya dini isiyo ya kweli. (Ufunuo 17:5, 18) Sehemu kuu ya milki hiyo ni Jumuiya ya Wakristo. Viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo humtukuzaje Yehova? Kwa kukiri kwa uchungu mambo mazuri ambayo amewatimizia Mashahidi wake. Hasa mwaka wa 1919 Yehova alipowarudisha watumishi wake kwenye utendaji wenye bidii baada ya kuachiliwa kutoka utekwani wa kiroho katika Babiloni Mkubwa, viongozi hao “wakawa wenye kuogopa na kumpa utukufu Mungu wa mbinguni.”—Ufunuo 11:13.b
5. Yehova huwalindaje wale wanaomtumaini kabisa?
5 Ingawa Yehova ni mwenye kutisha machoni pa adui zake, yeye ni kimbilio kwa wasikivu na wanyenyekevu wanaotaka kumtumikia. Huenda watu watishao wa kidini na kisiasa wakajaribu kwa njia zote kuivunja imani ya waabudu wa kweli, lakini wao hushindwa kwa sababu waabudu hawa humtumaini Yehova kwa ukamili. Hatimaye, yeye huwanyamazisha wapinzani wake kwa urahisi, naye hufanya hivyo kana kwamba anafunika jua kali la jangwani kwa wingu au anaizuia dhoruba kwa ukuta.—Soma Isaya 25:4, 5.
‘Karamu kwa Mataifa Yote’
6, 7. (a) Yehova aandaa karamu ya aina gani, naye awaandalia nani? (b) Karamu aliyoitabiri Isaya yawakilisha nini?
6 Kama vile baba mwenye upendo, Yehova huwalinda na pia kuwalisha watoto wake, hasa kiroho. Baada ya kuwakomboa watu wake mwaka wa 1919, aliwaandalia karamu ya ushindi, yaani, chakula kingi cha kiroho: “Katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.”—Isaya 25:6.
7 Karamu hiyo yafanyiwa katika “mlima” wa Yehova. Mlima huo ni nini? Huo ni “mlima wa nyumba ya BWANA [“Yehova,” NW]” ambao mataifa yote yanauendea “katika siku za mwisho.” Huo ni ‘mlima mtakatifu’ wa Yehova, ambako waabudu wake waaminifu hawadhuru wala hawaharibu. (Isaya 2:2; 11:9) Katika mahali hapo pa ibada palipoinuliwa, Yehova aandaa karamu ya vitu vitamu kwa ajili ya watu waaminifu. Na vitu vizuri vya kiroho vinavyoandaliwa kwa wingi sasa vyaonyesha kimbele vitu vitamu vya kimwili vitakavyoandaliwa Ufalme wa Mungu utakapokuwa serikali pekee ya wanadamu. Wakati huo njaa haitakuwepo tena. ‘Kutakuwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.’—Zaburi 72:8, 16.
8, 9. (a) Ni adui gani wawili wakuu wa wanadamu watakaoondolewa? Eleza. (b) Mungu atafanya nini ili kuiondoa aibu ya watu wake?
8 Wale wanaokula sasa karamu ya kiroho ambayo Mungu ameandaa wana matazamio matukufu. Yasikilize maneno yafuatayo ya Isaya. Azilinganishapo dhambi na kifo na ‘utaji uliotandwa’ ambao husonga pumzi, au “sitara,” asema: “Katika mlima huu [Yehova] atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote.”—Isaya 25:7, 8a.
9 Naam, dhambi na kifo hazitakuwapo tena! (Ufunuo 21:3, 4) Zaidi ya hayo, aibu inayotokana na uwongo ambayo watumishi wa Yehova wamevumilia kwa maelfu ya miaka itaondolewa pia. “Aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo.” (Isaya 25:8b) Hayo yatatukiaje? Yehova atakiondoa chanzo cha aibu hiyo, yaani, Shetani na mbegu yake. (Ufunuo 20:1-3) Haishangazi kwamba watu wa Mungu watashurutika kupaaza sauti wakisema: “Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, ndiye tuliyemngoja atusaidie; huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.”—Isaya 25:9.
Wenye Kiburi Washushwa
10, 11. Yehova ataitendaje Moabu kwa ukali?
10 Yehova huwaokoa watu wake waonyeshao unyenyekevu. Hata hivyo, Moabu, jirani ya Israeli ina kiburi, na Yehova huchukia kiburi. (Mithali 16:18) Basi Moabu imekusudiwa kuaibishwa. “Mkono wa BWANA utatulia katika mlima huu, na Moabu atakanyagwa chini huko aliko, kama vile majani makavu yakanyagwavyo katika maji ya jaa [“katika mahali pa mbolea,” “NW”]. Naye atanyosha mikono yake katikati yake, kama vile aogeleaye anyoshavyo mikono yake ili aogelee, naye atashusha kiburi chake, pamoja na hila za mikono yake. Na boma la ngome ya kuta zako ameliinamisha, na kulilaza chini, na kulitupa chini hata mavumbini.”—Isaya 25:10-12.
11 Mkono wa Yehova “utatulia” katika mlima wa Moabu. Ni nini kitakachotokea? Moabu yenye kiburi itapigwa kofi na kukanyagiwa chini mfano wa ‘mahali pa mbolea.’ Wakati wa Isaya, majani makavu hukanyagwa-kanyagwa katika samadi ili kutengeneza mbolea, kwa hiyo Isaya atabiri aibu kwa Moabu, licha ya kuwa na kuta ndefu zinazoonekana kuwa salama.
12. Kwa nini Moabu yateuliwa kwa ajili ya matangazo ya hukumu ya Yehova?
12 Kwa nini Yehova aiteua Moabu ili aishauri kwa ukali hivyo? Wamoabi ni wazao wa Loti, mpwa wa Abrahamu aliye pia mwabudu wa Yehova. Basi, wao ni jirani za taifa la agano la Mungu na vilevile watu wa jamaa yao. Licha ya hayo, wamefuata miungu isiyo ya kweli na kuonyesha uadui mkubwa kwa Israeli. Matokeo hayo makali yawastahili. Kwa habari hiyo, Moabu ni kama adui za watumishi wa Yehova leo. Yeye hasa ni kama Jumuiya ya Wakristo, inayodai kwamba chanzo chake ni kutaniko la Kikristo la karne ya kwanza, lakini kama tulivyoona mapema, hiyo ni sehemu kuu ya Babiloni Mkubwa.
-
-
Mkono wa Yehova WainuliwaUnabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
-
-
[Picha katika ukurasa wa 275]
“Karamu ya vitu vinono”
-