Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Isaya Atabiri ‘Tendo la Ajabu’ la Yehova
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • 1, 2. Kwa nini Israeli na Yuda zahisi ziko salama?

      ISRAELI na Yuda zahisi kwa kitambo kidogo kwamba ziko salama. Viongozi wao wameanzisha miungano ya kisiasa na mataifa makubwa zaidi na yenye nguvu, katika jitihada ya kupata usalama katika ulimwengu hatari. Samaria, jiji kuu la Israeli, limegeukia Siria iliyo karibu, ilhali Yerusalemu, jiji kuu la Yuda, limetumainia Ashuru yenye ukatili.

      2 Mbali na kuwatumainia washirika wao wapya wa kisiasa, baadhi ya watu katika ufalme wa kaskazini huenda wakamtazamia Yehova awalinde—licha ya kwamba wanaendelea kuabudu ndama za dhahabu. Vivyo hivyo, Yuda inasadiki kwamba Yehova atailinda. Kwani, hekalu la Yehova haliko Yerusalemu, jiji lao kuu? Ijapokuwa hivyo, kuna matukio yasiyotarajiwa yatakayoyapata mataifa hayo mawili. Yehova ampulizia Isaya kutabiri matukio yatakayoonekana kuwa ya ajabu kwelikweli kwa watu wake waliopotoka. Maneno yake pia yana mafundisho muhimu kwa kila mtu leo.

      “Walevi wa Efraimu”

      3, 4. Ufalme wa kaskazini wa Israeli wajivunia nini?

      3 Isaya aanza unabii wake kwa maneno yenye kushangaza: “Ole wa taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu, na ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, la hao walioshindwa na divai! Tazama, BWANA ana mmoja aliye hodari, mwenye nguvu; kama dhoruba ya mvua ya mawe, . . . ndivyo atakavyotupa chini kwa mkono. Taji ya kiburi ya walevi wa Efraimu itakanyagwa kwa miguu.”—Isaya 28:1-3.

      4 Kabila la Efraimu, ambalo ndilo mashuhuri zaidi kati ya makabila kumi ya kaskazini, lawakilisha ufalme wote wa Israeli. Samaria, jiji lake kuu, liko “kichwani mwa bonde linalositawi,” mahali pazuri penye umashuhuri. Viongozi wa Efraimu wanajivunia ‘taji yao ya kiburi’ ya kuwa huru kutokana na wafalme wa nasaba ya Daudi huko Yerusalemu. Lakini wao ni “walevi,” ulevi wa kiroho kwa sababu ya ushirikiano wao na Siria dhidi ya Yuda. Kila kitu wakipendacho chakaribia kukanyagwa chini ya miguu ya wavamizi.—Linganisha Isaya 29:9.

      5. Israeli imo katika hatari gani, lakini Isaya atoa tumaini gani?

      5 Efraimu haitambui kuwa imo hatarini. Isaya aendelea: “Ua la uzuri wa fahari yake linalonyauka, lililo kichwani mwa bonde linalositawi, litakuwa kama tini iliyotangulia kuiva kabla ya wakati wa hari, ambayo, aionapo yeye aiangaliaye, huila mara anapoishika mkononi mwake.” (Isaya 28:4) Efraimu itaanguka mkononi mwa Ashuru, kama tonge tamu linaloliwa mara moja. Basi, je, hilo lamaanisha kwamba hakuna tumaini lolote? Kama ilivyo mara nyingi, unabii mbalimbali wa hukumu wa Isaya hutia ndani tumaini. Taifa hilo lijapoanguka, watu mmoja-mmoja walio waaminifu wataokoka kwa msaada wa Yehova. “BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi atakuwa ni taji ya fahari, na kilemba cha uzuri, kwa mabaki ya watu wake. Naye atakuwa roho ya hukumu kwake yeye aketiye ili ahukumu; naye atakuwa nguvu kwao wageuzao nyuma vita langoni.”—Isaya 28:5, 6.

      “Wamekosa”

      6. Israeli yaangamizwa lini, lakini kwa nini haipasi Yuda ifurahi?

      6 Siku ya kulipiza kisasi juu ya Samaria yafika mwaka wa 740 K.W.K., Waashuri waiharibupo nchi na ufalme wa kaskazini ukomeshwapo ukiwa taifa huru. Na Yuda je? Nchi yake itavamiwa na Ashuru, na baadaye Babiloni itaharibu jiji lake kuu. Lakini katika wakati wa maisha ya Isaya, hekalu na ukuhani wa Yuda zitaendelea kutenda na manabii wake wataendelea kutoa unabii. Je, Yuda ifurahie maangamizi yanayokuja juu ya jirani yake wa kaskazini? La hasha! Yuda na viongozi wake watawajibika mbele za Yehova kwa sababu ya kutotii kwao na kukosa imani.

      7. Viongozi wa Yuda wamelewaje, na matokeo ni nini?

      7 Akielekeza ujumbe wake kwa Yuda, Isaya aendelea: “Lakini hawa nao wamekosa kwa divai, wamepotea kwa kileo; kuhani na nabii wamekosa kwa kileo, wamemezwa kwa divai, wamepotea kwa kileo; hukosa katika maono, hujikwaa katika hukumu. Maana meza zote zimejaa matapiko na uchafu, hapana mahali palipo safi.” (Isaya 28:7, 8) Yachukiza kama nini! Ulevi halisi nyumbani mwa Mungu ni mbaya sana. Lakini makuhani na manabii hao wamelewa kiroho—akili zao zimepumbazwa kwa kuitumaini mno miungano ya kibinadamu. Wamejidanganya kwa kufikiri kwamba mwendo wao ndio mwendo pekee unaofaa, labda wakiamini kwamba sasa wana mpango mwingine iwapo ulinzi wa Yehova wakosa kutosha. Katika hali yao ya ulevi wa kiroho, viongozi hao wa kidini waropoka usemi wenye kuchukiza na mchafu, unaoonyesha ukosefu mbaya wa imani ya kweli katika ahadi za Mungu.

      8. Ujumbe wa Isaya wapokewaje?

      8 Viongozi wa Yuda waitikiaje onyo la Yehova? Wamdhihaki Isaya, wakimshutumu kwamba anasema nao kama watoto: “Atamfundisha nani maarifa? atamfahamisha nani habari hii? Je! ni wale walioachishwa maziwa, walioondolewa matitini? Kwa maana ni amri juu ya amri, amri juu ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku kidogo.” (Isaya 28:9, 10) Kwa maoni yao, Isaya arudia-rudia mambo kiajabu! Ayarudia-rudia maneno yake mwenyewe, akisema: ‘Yehova ameamuru hivi! Yehova ameamuru hivi! Hii ndiyo kanuni ya Yehova! Hii ndiyo kanuni ya Yehova!’a Lakini karibuni Yehova “atasema” na wakazi wa Yuda kupitia tendo fulani. Atatuma majeshi ya Babiloni dhidi yao—wageni ambao kwa kweli wanasema lugha nyingine. Pasipo shaka, majeshi hayo yatatekeleza “amri juu ya amri,” za Yehova, na Yuda itaanguka.—Soma Isaya 28:11-13.

      Walevi wa Kiroho Leo

      9, 10. Maneno ya Isaya yamepata kuwa na maana kwa vizazi vya baadaye lini, na jinsi gani?

      9 Je, unabii mbalimbali wa Isaya ulitimizwa juu ya Israeli na Yuda za kale pekee? Hata kidogo! Yesu na Paulo waliyanukuu maneno yake na kuyahusianisha na taifa la wakati wao. (Isaya 29:10, 13; Mathayo 15:8, 9; Waroma 11:8) Hali kadhalika, leo hali fulani inayofanana na ile ya siku ya Isaya imezuka.

      10 Wakati huu, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo ndio wanaotumaini siasa. Wao huyumba-yumba huku na huku, kama walevi wa Israeli na Yuda, wakijiingiza katika masuala ya kisiasa, wakifurahia kuombwa mashauri na wale waitwao eti wakuu katika ulimwengu huu. Badala ya kusema kweli safi ya Biblia, wao husema uchafu. Mwono wao wa kiroho umefifia, nao sio viongozi salama wa wanadamu.—Mathayo 15:14.

      11. Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo huitikiaje habari njema ya Ufalme wa Mungu?

      11 Viongozi wa Jumuiya ya Wakristo hutendaje Mashahidi wa Yehova wanapowaonyesha tumaini pekee la kweli, yaani, Ufalme wa Mungu? Hawaelewi. Wanaona kwamba Mashahidi wanaropoka kwa kurudia-rudia, kama watoto. Viongozi wa kidini huwadharau wajumbe hao na kuwadhihaki. Sawa na Wayahudi wa siku ya Yesu, hawautaki Ufalme wa Mungu wala hawataki wafuasi wao waelezwe kuuhusu. (Mathayo 23:13) Kwa hiyo, wanaonywa kuwa Yehova hatasema nao daima kupitia wajumbe wake wapole. Wakati utafika ambapo wale wasiotaka kujitiisha kwa Ufalme wa Mungu ‘watavunjwa, na kunaswa, na kuchukuliwa,’ naam, waangamizwe kabisa.

      “Agano na Mauti”

      12. Ni nini kinachodaiwa kuwa “agano na mauti” la Yuda?

      12 Isaya aendelea na tangazo lake: “Mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo ya kweli.” (Isaya 28:14, 15) Viongozi wa Yuda wajigamba wakisema kuwa miungano yao ya kisiasa inawalinda wasishindwe. Wanaona kwamba wamefanya “agano na mauti” ili isiwaguse. Lakini kimbilio lao la uwongo halitawalinda. Miungano yao ni uwongo, si ya kweli. Vivyo hivyo leo, uhusiano wa karibu wa Jumuiya ya Wakristo na viongozi wa ulimwengu hautailinda wakati ufikapo Yehova aihukumu. Kwa kweli, uhusiano huo ndio utakaosababisha maangamizi yake.—Ufunuo 17:16, 17.

      13. Ni nani aliye “jiwe lililojaribiwa,” na Jumuiya ya Wakristo imemkataaje?

      13 Basi, viongozi hao wa kidini wapaswa kuwa wakitazama wapi? Isaya sasa arekodi ahadi ya Yehova: “Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka. Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.” (Isaya 28:16, 17) Muda mfupi baada ya Isaya kuyasema maneno hayo, Mfalme Hezekia mwaminifu atawazwa huko Sayuni, na ufalme wake waokolewa, si kupitia kwa washirika jirani, bali kupitia kwa Yehova kuingilia kati. Hata hivyo, Hezekia siye anayeyatimiza maneno hayo yaliyopuliziwa. Mtume Petro, akinukuu maneno ya Isaya, alionyesha kuwa Yesu Kristo, mzao wa baadaye sana wa Hezekia, ndiye “jiwe lililojaribiwa” na yeyote anayedhihirisha imani katika Yeye hapaswi kuogopa kamwe. (1 Petro 2:6) Yachukiza sana kwa sababu viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, wajapojiita Wakristo, wamefanya mambo ambayo Yesu alikataa kufanya! Wametafuta umashuhuri na mamlaka katika ulimwengu huu badala ya kumngojea Yehova alete Ufalme wake chini ya Yesu Kristo aliye Mfalme.—Mathayo 4:8-10.

      14. “Agano na mauti” la Yuda litabatilishwa lini?

      14 “Pigo lifurikalo” la majeshi ya Babiloni lipitapo nchini humo, Yehova atalifunua kimbilio la kisiasa la Yuda kuwa ni uwongo. “Agano lenu mliloagana na mauti litabatilika,” asema Yehova. “Pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo. Kila wakati litakapopita . . . kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu.” (Isaya 28:18, 19) Naam, kuna fundisho kubwa tuwezalo kupata kutokana na mambo yanayowakumba watu wanaodai kumtumikia Yehova lakini badala yake wanaweka matumaini yao katika miungano na mataifa.

      15. Isaya atoaje kielezi cha kutofaa kwa ulinzi wa Yuda?

      15 Fikiria hali wanamojikuta sasa viongozi hao wa Yuda. “Kitanda kile ni kifupi asiweze mtu kujinyosha juu yake, na nguo ile ya kujifunika ni nyembamba asipate mtu kujizingisha.” (Isaya 28:20) Ni kana kwamba walala chini wapate pumziko, ila hilo ni bure tu. Miguu yao yabaki nje kwenye baridi, au waikunja miguu yao na nguo ya kujifunika ni nyembamba mno isiweze kuwafunika wapate joto. Hali ilikuwa isiyostarehesha jinsi hiyo katika siku ya Isaya. Na hali iko hivyo leo kwa mtu yeyote anayeweka tumaini lake katika kimbilio la uwongo la Jumuiya ya Wakristo. Yachukiza kama nini kwamba kwa sababu ya kujiingiza katika siasa, viongozi fulani wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wamehusika katika ukatili kama vile mauaji ya kikabila na mauaji ya jumla!

      ‘Tendo la Ajabu’ la Yehova

      16. ‘Tendo la ajabu’ la Yehova ni nini, na kwa nini kazi hiyo ni ya ajabu?

      16 Hali ya mwisho ya mambo itakuwa kinyume kabisa cha matumaini ya viongozi wa kidini wa Yuda. Yehova atawafanyia walevi wa kiroho wa Yuda jambo la ajabu. “BWANA ataondoka kama vile katika mlima Perasimu, ataghadhibika kama vile katika bonde la Gibeoni; apate kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu; na kulitimiza tendo lake, tendo lake la ajabu.” (Isaya 28:21) Katika siku za Mfalme Daudi, Yehova aliwapa watu wake ushindi mkubwa juu ya Wafilisti katika Mlima Perasimu na katika bonde la Gibeoni. (1 Mambo ya Nyakati 14:10-16) Katika siku za Yoshua, hata alifanya jua lisimame tuli juu ya Gibeoni ili ushindi wa Israeli juu ya Waamori ukamilike. (Yoshua 10:8-14) Hiyo ilikuwa ajabu! Sasa Yehova atapigana tena, lakini mara hii dhidi ya wale wanaodai kuwa watu wake. Je, kwaweza kuwapo ajabu nyingine kuliko hiyo? Haiwezekani, uzingatiapo uhakika wa kwamba Yerusalemu ndicho kituo cha ibada ya Yehova na jiji la mfalme wa Yehova aliyetiwa mafuta. Kufikia sasa, nyumba ya kifalme ya Daudi huko Yerusalemu haijawahi kupinduliwa kamwe. Ijapokuwa hivyo, pasipo shaka Yehova atatekeleza “tendo lake la ajabu.”—Linganisha Habakuki 1:5-7.

      17. Kuonyesha dharau kutakuwa na matokeo gani kwa utimizo wa unabii wa Isaya?

      17 Basi, Isaya atahadharisha: “Msiwe watu wenye kudharau, vifungo vyenu msije vikakazwa; maana nimesikia kwa Bwana, BWANA wa majeshi, habari ya hukumu itakayotimizwa, nayo imekusudiwa, itakayoipata dunia yote pia.” (Isaya 28:22) Ingawa viongozi hao waonyesha dharau, ujumbe wa Isaya ni wa kweli. Ameusikia kutoka kwa Yehova, ambaye viongozi hao wana uhusiano wa agano pamoja naye. Hali kadhalika leo, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo huonyesha dharau wasikiapo ‘tendo la ajabu’ la Yehova. Wao hata hujigamba na kusema kwa hasira. Lakini ujumbe ambao Mashahidi wa Yehova hutangaza ni wa kweli. Umo katika Biblia, kitabu ambacho viongozi hao hudai kukiwakilisha.

      18. Isaya atoaje kielezi cha usawaziko wa Yehova atoapo nidhamu?

      18 Lakini Yehova atawarekebisha upya na kuwarudishia upendeleo wake watu wanyofu wasiofuata viongozi hao. (Soma Isaya 28:23-29.) Sawa na mkulima atumiaye mbinu za uangalifu ili kupura nafaka iliyo laini zaidi, kama vile kunde, vivyo hivyo Yehova huibadili nidhamu yake kulingana na mtu mmoja-mmoja na hali zake. Yeye hapiti kiasi au kuonea kamwe bali hutenda akiwa na kusudi la kuwarekebisha wakosaji. Naam, iwapo watu mmoja-mmoja wakubali sihi za Yehova, basi kuna tumaini. Vivyo hivyo leo, ingawa kwa jumla hatima ya Jumuiya ya Wakristo imetiwa muhuri, mtu yeyote anayejitiisha kwa Ufalme wa Yehova aweza kuepuka hukumu kali inayokuja.

  • Isaya Atabiri ‘Tendo la Ajabu’ la Yehova
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • [Picha katika ukurasa wa 289]

      Jumuiya ya Wakristo imetegemea miungano na watawala wa kibinadamu badala ya kumtegemea Mungu

      [Picha katika ukurasa wa 290]

      Yehova atekeleza “tendo lake la ajabu” anaporuhusu Babiloni iharibu Yerusalemu

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki