Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mfalme Apata Thawabu kwa Sababu ya Imani Yake
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • Imani Yajaribiwa

      4, 5. (a) Hezekia ameonyeshaje uhuru wake kutoka kwa Ashuru? (b) Senakeribu amechukua hatua gani ya kijeshi dhidi ya Yuda, na Hezekia achukua hatua gani ili kuepuka shambulio la upesi dhidi ya Yerusalemu? (c) Hezekia afanya matayarisho gani ya kulinda Yerusalemu dhidi ya Waashuri?

      4 Majaribu mazito yalikuwa mbele ya Yerusalemu. Hezekia amevunja mwungano ambao Ahazi, baba yake asiye na imani, alifanya pamoja na Waashuri. Hata amewatiisha Wafilisti, ambao ni washirika wa Ashuru. (2 Wafalme 18:7, 8) Hayo yamemkasirisha mfalme wa Ashuru. Basi twasoma: “Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.” (Isaya 36:1) Hezekia, labda akitumaini kulinda jiji la Yerusalemu lisishambuliwe upesi na jeshi lenye ukatili la Ashuru, akubali kumpa Senakeribu ushuru mkubwa wa talanta 300 za fedha na 30 za dhahabu.a—2 Wafalme 18:14.

      5 Kwa kuwa hazina ya mfalme haina dhahabu na fedha ya kutosha kulipa ushuru huo, Hezekia atwaa vito vyovyote awezavyo kupata hekaluni. Yeye pia aing’oa milango ya hekalu, ambayo imetandwa kwa dhahabu, na kuipeleka kwa Senakeribu. Hilo lamridhisha Mwashuri, lakini kwa muda mfupi tu. (2 Wafalme 18:15, 16) Labda Hezekia atambua kuwa Waashuri hawataachana na Yerusalemu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, sharti matayarisho yafanywe. Watu waziba chemchemi za maji ambapo Waashuri wanaovamia waweza kupata maji. Hezekia pia aimarisha ngome za Yerusalemu na kukusanya zana za vita, zikiwemo “silaha na ngao tele.”—2 Mambo ya Nyakati 32:4, 5.

      6. Hezekia amtumaini nani?

      6 Hata hivyo, Hezekia hatumaini mbinu za vita zenye ujanja wala katika ngome, bali amtumaini Yehova wa majeshi. Awahimiza wakuu wake wa kijeshi: “Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye; kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA [“Yehova,” NW], Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu.” Kwa kuitikia, watu waanza ‘kuyategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.’ (2 Mambo ya Nyakati 32:7, 8) Hebu piga picha ya matukio yenye kusisimua yanayofuata tuchunguzapo sura ya 36 hadi 39 ya unabii wa Isaya.

      Rabshake Atoa Hoja Yake

      7. Rabshake ni nani, na kwa nini atumwa Yerusalemu?

      7 Senakeribu amtuma Rabshake (ni jina la cheo cha kijeshi, wala si jina la mtu binafsi) pamoja na wakuu wengine wawili kwenda Yerusalemu ili kulilazimisha jiji kusalimu amri. (2 Wafalme 18:17) Eliakimu msimamizi wa nyumba ya Hezekia, Shebna mwandishi, na Yoa mwana wa Asafu mwenye kuandika tarehe, ambao ni wawakilishi watatu wa Hezekia wawalaki watu hao nje ya ukuta wa jiji.—Isaya 36:2, 3, kielezi-chini.

      8. Rabshake ajaribu kuuvunjaje upinzani wa Yerusalemu?

      8 Lengo la Rabshake ni moja tu, yaani, kushawishi Yerusalemu kusalimu amri pasipo pigano. Huku akiongea katika Kiebrania, kwanza apaaza sauti: “Ni tumaini gani hili unalolitumainia? . . . Unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?” (Isaya 36:4, 5) Kisha Rabshake awadhihaki Wayahudi waliojaa woga, akiwakumbusha kuwa wameachwa peke yao kabisa. Waweza kumwendea nani awasaidie? Je, wauendee ‘mwanzi uliopondeka,’ yaani, Misri? (Isaya 36:6) Wakati huu, Misri yafanana na mwanzi uliopondeka; kwa kweli, Ethiopia imeishinda kwa muda serikali hiyo ya ulimwengu ya awali, na Farao wa sasa wa Misri, Mfalme Tirhaka, si Mmisri bali ni Mwethiopia. Na Ashuru yakaribia kumshinda. (2 Wafalme 19:8, 9) Kwa kuwa Misri haiwezi kujiokoa, haitafaa kitu kwa Yuda.

      9. Yaelekea ni nini kinachomfanya Rabshake aamue kwamba Yehova atawaacha watu Wake, lakini ukweli wa mambo ni nini?

      9 Rabshake sasa abisha kwamba Yehova hatawapigania watu Wake kwa sababu wamemchukiza Yeye. Rabshake asema: “Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA [“Yehova,” “NW”], Mungu wetu, je! si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake?” (Isaya 36:7) Ni wazi kwamba Wayahudi wamemrudia, wala siyo kumkataa, Yehova hasa kwa kuondoa mahali pa juu na madhabahu nchini.

      10. Kwa nini si kitu iwapo walinzi wa Yuda ni wengi au ni wachache?

      10 Kisha Rabshake awakumbusha Wayahudi kwamba wao ni hoi kabisa kijeshi. Atoa mwito huu wenye dhihaka: “Nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.” (Isaya 36:8) Hata hivyo je, kweli ni kitu iwapo askari wapanda-farasi waliozoezwa wa Yuda ni wengi au ni wachache? La, kwa sababu wokovu wa Yuda hautegemei nguvu kubwa za kijeshi. Andiko la Mithali 21:31 laeleza mambo hivi: “Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; lakini BWANA [“Yehova,” NW] ndiye aletaye wokovu.” Kisha Rabshake asema Yehova awabariki Waashuri, wala si Wayahudi. Kama sivyo, yeye adai, Waashuri wasingaliweza kamwe kupenya kadiri hiyo katika eneo la Yuda.—Isaya 36:9, 10.

      11, 12. (a) Kwa nini Rabshake asisitiza kusema katika “lugha ya Kiyahudi,” naye ajaribuje kuwashawishi Wayahudi wanaosikiliza? (b) Huenda maneno ya Rabshake yakawaathirije Wayahudi?

      11 Wawakilishi wa Hezekia wahangaikia athari za hoja za Rabshake juu ya watu wanaomsikia wakiwa juu ya ukuta wa jiji. Maofisa hao Wayahudi waomba hivi: “Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani.” (Isaya 36:11) Lakini Rabshake hanuii kusema katika lugha ya Kiashuri. Ataka kutia shaka na hofu katika Wayahudi ili wasalimu amri na jiji la Yerusalemu lishindwe pasipo pigano! (Isaya 36:12) Kwa hiyo, Mwashuri asema tena katika “lugha ya Kiyahudi.” Awaonya wakazi wa Yerusalemu: “Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa.” Baada ya kusema hayo, ajaribu kuwashawishi wale wanaomsikiliza kwa kufafanua jinsi ambavyo maisha yangekuwa kwa Wayahudi chini ya utawala wa Ashuru: “Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu.”—Isaya 36:13-17.

      12 Wayahudi hawatavuna mwaka huu—uvamizi wa Ashuru umewazuia wasipande mimea. Hapana budi kwamba tazamio la kula zabibu tamu na kunywa maji safi lawavutia sana watu wanaosikiliza ukutani. Lakini Rabshake bado aendelea kujaribu kuwadhoofisha Wayahudi.

      13, 14. Licha ya hoja za Rabshake, kwa nini mambo yaliyolikumba Samaria hayafai kwa hali ya Yuda?

      13 Rabshake atoa silaha nyingine ya maneno kutoka katika ghala ya hoja zake. Awaonya Wayahudi wasimwamini Hezekia iwapo asema: “BWANA [“Yehova mwenyewe,” “NW”] atatuokoa.” Rabshake awakumbusha Wayahudi kuwa miungu ya Samaria haikuweza kuwazuia Waashuri wasiyashinde yale makabila kumi. Na je, vipi kuhusu miungu ya mataifa mengine ambayo Ashuru imeshinda? “Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi?” yeye adai. “Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! wameiokoa Samaria na mkono wangu?”—Isaya 36:18-20.

      14 Ni wazi kwamba Rabshake, mwabudu wa miungu isiyo ya kweli haelewi kwamba kuna tofauti kubwa kati ya Samaria lenye kuasi na Yerusalemu linalotawaliwa na Hezekia. Miungu isiyo ya kweli ya Samaria haikuwa na nguvu zozote za kuuokoa ufalme huo wa makabila kumi. (2 Wafalme 17:7, 17, 18) Kwa upande mwingine, Yerusalemu linalotawaliwa na Hezekia limeikataa miungu isiyo ya kweli nalo limerudia kumtumikia Yehova. Hata hivyo, wale wawakilishi watatu Wayudea hawajaribu kumweleza Rabshake jambo hilo. “Wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno.” (Isaya 36:21) Eliakimu, Shebna, na Yoa wamrudia Hezekia na kutoa ripoti rasmi ya maneno ya Rabshake.—Isaya 36:22.

  • Mfalme Apata Thawabu kwa Sababu ya Imani Yake
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • [Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 384]

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki