Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mtumaini Yehova Ukabilipo Janga
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • Matabiri Sahihi

      23. (a) Isaya sasa aamuriwa afanye nini? (b) Ishara kwenye ubao yathibitishwaje?

      23 Sasa Isaya airudia hali iliyopo. Yerusalemu likiwa lingali limezingirwa na muungano wa Siria na Israeli, Isaya aripoti: “BWANA akaniambia, Ujipatie ubao mkubwa ukaandike juu yake kwa kalamu ya binadamu, Kwa Maher-shalal-hash-bazi; nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia.” (Isaya 8:1, 2) Jina Maher-shalal-hash-bazi lamaanisha “Fanya Hima, Ewe Nyara! Amekuja Upesi Kwenye Nyara.” Isaya awaomba wanaume wawili wanaoheshimiwa katika jumuiya washuhudie aandikapo jina lake kwenye ubao mkubwa, ili kwamba baadaye waweze kuthibitisha uasilia wa hati hiyo. Hata hivyo, ishara hiyo itathibitishwa na ishara ya pili.

      24. Ishara ya Maher-shalal-hash-bazi yapasa kuwaathirije watu wa Yuda?

      24 Isaya asema: “Nami nikamwendea huyo nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume. Kisha BWANA akaniambia, Mwite jina lake Maher-shalal-hash-bazi. Kwa maana kabla mtoto huyo hajapata kujua kusema, Baba yangu, na Mama yangu, hazina za Dameski na mateka ya Samaria yatachukuliwa mbele ya mfalme wa Ashuru.” (Isaya 8:3, 4) Ubao huo mkubwa na mvulana aliyezaliwa hivi punde zitakuwa ishara kwamba karibuni Ashuru itawapora wakandamizaji wa Yuda, yaani, Siria na Israeli. Karibuni kadiri gani? Kabla mvulana huyo hajaweza kutamka maneno ambayo vitoto vingi hujifunza kwanza—“Baba” na “Mama.” Utabiri barabara kama huo wapasa kuimarisha imani ya watu katika Yehova. Au labda utawafanya wengine wamdhihaki Isaya na wanawe. Hata iweje, maneno ya unabii wa Isaya yatimia.—2 Wafalme 17:1-6.

      25. Siku za Isaya zafananaje na wakati wetu?

      25 Maonyo yaliyorudiwa-rudiwa ya Isaya yaweza kuwafundisha Wakristo. Mtume Paulo alitufunulia kwamba katika tukio hilo la kihistoria, Isaya alifananisha Yesu Kristo na wana wa Isaya wakafananisha wanafunzi watiwa-mafuta wa Yesu. (Waebrania 2:10-13) Yesu, kupitia wafuasi wake watiwa-mafuta duniani, amekuwa akiwakumbusha Wakristo wa kweli uhitaji wa ‘kufuliza kuwa macho’ katika nyakati hizi zenye hatari. (Luka 21:34-36) Na wakati huohuo, wapinzani wasiotubu wanaonywa juu ya kuharibiwa kwao kunakokuja, ijapo mara nyingi maonyo hayo hudhihakiwa. (2 Petro 3:3, 4) Utimizo wa unabii mbalimbali uhusuo wakati katika siku ya Isaya wahakikisha kuwa ratiba ya wakati ya Mungu kwa siku yetu pia “haina budi kuja, haitakawia.”—Habakuki 2:3.

      “Maji” Yenye Kuangamiza Kabisa

      26, 27. (a) Isaya atabiri matukio gani? (b) Maneno ya Isaya yaonyesha nini kwa watumishi wa Yehova leo?

      26 Isaya aendelea na maonyo yake: “Kwa sababu watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na huyo mwana wa Remalia, basi sasa angalia; Bwana aleta juu yao maji ya huo Mto, yenye nguvu, mengi sana, nayo ni mfalme wa Ashuru na utukufu wake wote; naye atakuja, na kupita juu ya mifereji yake yote, atafurika juu ya kingo zake zote; naye atapita, atapita kwa kasi na kuingia Yuda; atafurika na kupita katikati, atafika hata shingoni; na kule kuyanyosha mabawa yake kutaujaza upana wa nchi yako, Ee Imanueli.”—Isaya 8:5-8.

      27 “Watu hawa,” ufalme wa kaskazini wa Israeli, wakataa agano la Yehova na Daudi. (2 Wafalme 17:16-18) Kwa maoni yao, agano hilo ni hafifu kama maji yanayotiririka ya Shiloa, mfereji unaoleta maji Yerusalemu. Wanafurahia vita yao dhidi ya Yuda. Lakini dharau hilo halitakosa kuadhibiwa. Yehova atawaruhusu Waashuri ‘wafurike,’ au wapindue, Siria na Israeli, kama vile Yehova atakavyoiruhusu sehemu ya kisiasa ya ulimwengu ifurike milki ya dini isiyo ya kweli. (Ufunuo 17:16; linganisha Danieli 9:26.) Kisha, Isaya asema, “maji” yanayofurika “[y]atapita kwa kasi na kuingia Yuda,” na kufika “hata shingoni,” hadi Yerusalemu, ambako kichwa (mfalme) cha Yuda chatawala.b Katika wakati wetu, vivyo hivyo wafishaji wa kisiasa wa dini isiyo ya kweli watavamia watumishi wa Yehova na kuwazingira “hata shingoni.” (Ezekieli 38:2, 10-16) Tokeo litakuwa nini? Basi, ni nini kinachotukia wakati wa Isaya? Je, Waashuri wafurika kupitia kuta za jiji na kuwafagilia mbali watu wa Mungu? La. Mungu yuko pamoja nao.

      Msiogope—“Mungu Yu Pamoja Nasi”!

      28. Licha ya juhudi nyingi za adui zao, Yehova ahakikishia Yuda nini?

      28 Isaya aonya: “Fanyeni ghasia, enyi kabila za watu [wapingao watu wa agano wa Mungu], nanyi mtavunjwa vipande vipande; tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande. Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; semeni neno, lakini halitasimama; kwa maana Mungu yu pamoja nasi.” (Isaya 8:9, 10) Maneno hayo yatimia miaka kadhaa baadaye, wakati wa utawala wa Hezekia, mwana mwaminifu wa Ahazi. Waashuri watishapo Yerusalemu, malaika wa Yehova aangamiza 185,000 kati yao. Kwa wazi, Mungu yu pamoja na watu wake na pamoja na nasaba ya Daudi. (Isaya 37:33-37) Katika pigano linalokuja la Har–Magedoni, vivyo hivyo Yehova atamtuma Imanueli Mkuu kuwavunja vipande vipande adui Zake na kuwaokoa wote wanaomtumaini Yeye.—Zaburi 2:2, 9, 12.

      29. (a) Wayahudi wa siku ya Ahazi watofautianaje na wale wa siku za Hezekia? (b) Kwa nini watumishi wa Yehova leo huepuka kujiingiza katika miungano ya kidini na ya kisiasa?

      29 Tofauti na Wayahudi katika siku ya Hezekia, watu wa wakati wa Ahazi wakosa kuwa na imani katika ulinzi wa Yehova. Wao wapendelea muungano, au “njama,” (BHN), pamoja na Waashuri wakiwa ngome dhidi ya muungano wa Siria na Israeli. Hata hivyo, “mkono” wa Yehova wamchochea Isaya kuilaani “njia ya watu hawa,” au mtazamo unaopendwa. Aonya hivi: “Msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA [“Yehova,” “NW”] wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.” (Isaya 8:11-13) Wakizingatia hayo, watumishi wa Yehova leo hujilinda dhidi ya kupanga njama na, au kuyatumaini, mabaraza ya kidini na mashirikisho ya kisiasa. Watumishi wa Yehova wana hakika kamili katika uwezo wa Mungu wa kuwalinda. Kwani, ikiwa ‘Yehova yuko upande wetu, mwanadamu atatutenda nini?’—Zaburi 118:6, NW.

      30. Watu wasiomtumaini Yehova watapatwa na nini hatimaye?

      30 Isaya arudia kusema tena kwamba Yehova atathibitika kuwa “mahali patakatifu,” ulinzi, kwa wanaomtumaini. Kinyume cha hilo, wanaomkataa “watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa”—vitenzi vitano vyenye nguvu vinavyoondoa shaka yoyote kuhusu yatakayowapata wale wasiomtumaini Yehova. (Isaya 8:14, 15) Katika karne ya kwanza, vivyo hivyo wale waliomkataa Yesu walijikwaa na kuanguka. (Luka 20:17, 18) Mwisho kama huo unawangojea watu wa leo wanaokataa kumwunga mkono Mfalme wa mbinguni aliyetawazwa, Yesu.—Zaburi 2:5-9.

      31. Wakristo wa kweli leo waweza kufuataje kielelezo cha Isaya na cha wale wanaosikiliza mafundisho yake?

      31 Katika siku ya Isaya, si wote wanaojikwaa. Isaya asema: “Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. Nami nitamngojea BWANA, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia.” (Isaya 8:16, 17) Isaya pamoja na wale wanaotii mafundisho yake hawataiacha Sheria ya Mungu. Wao waendelea kumtumaini Yehova, hata ingawa wenzao wahalifu wakataa na hivyo kumfanya Yehova awafiche uso wake. Na tufuate kielelezo cha wale wanaomtumaini Yehova na tuazimie vivyo hivyo kushikamana na ibada safi!—Danieli 12:4, 9; Mathayo 24:45; linganisha Waebrania 6:11, 12.

      “Ishara” na “Ajabu”

      32. (a) Ni nani walio “ishara na ajabu” leo? (b) Kwa nini Wakristo wapaswa kuonekana tofauti na ulimwengu?

      32 Sasa Isaya atangaza: “Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na BWANA tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa BWANA wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni.” (Isaya 8:18) Naam, Isaya, Shear-yashubu, na Maher-shalal-hash-bazi ni ishara za makusudi ya Yehova kwa Yuda. Leo pia, Yesu na ndugu zake watiwa-mafuta ni ishara. (Waebrania 2:11-13) Na “umati mkubwa” wa “kondoo wengine” wamejiunga nao katika hiyo kazi yao. (Ufunuo 7:9, 14; Yohana 10:16) Bila shaka, ishara ni muhimu ikiwa tu yaonekana waziwazi katika mazingira yake. Hali kadhalika, Wakristo hutimiza utume wao wakiwa ishara iwapo tu waonekana waziwazi kwamba wao ni tofauti na ulimwengu huu, wakimtumaini Yehova kikamili na kutangaza kwa ujasiri makusudi yake.

      33. (a) Wakristo wa kweli wameazimia kufanya nini? (b) Sababu gani Wakristo wa kweli watasimama imara?

      33 Basi, wote na washike viwango vya Mungu, wala si vile vya ulimwengu huu. Endelea kuonekana waziwazi kwa ujasiri—kama ishara—ukitekeleza utume aliopewa Isaya Mkuu, Yesu Kristo: ‘Tangaza mwaka . . . uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu.’ (Isaya 61:1, 2; Luka 4:17-21) Naam, mafuriko ya Ashuru yatapakaapo duniani kote—hata yakifikia shingo zetu—Wakristo wa kweli hawatafagiliwa mbali. Tutasimama imara kwa sababu “Mungu yu pamoja nasi.”

  • Mtumaini Yehova Ukabilipo Janga
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • b Ashuru pia yafananishwa na ndege ambaye mabawa yake yaliyonyoshwa “[ya]ujaza upana wa nchi yako.” Kwa hiyo, jeshi la Ashuru litajaza pembe zote za nchi.

  • Mtumaini Yehova Ukabilipo Janga
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • [Picha katika ukurasa wa 111]

      Sababu gani Isaya aliandika “Maher-shalal-hash-bazi” kwenye ubao mkubwa?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki