Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ahadi ya Mkuu wa Amani
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • Kugeukia Roho Waovu

      4, 5. Mambo yakoje katika siku ya Isaya, na wengine wamgeukia nani?

      4 Kwa sababu ya kutotii kwao, watu wa siku ya Isaya wamo katika hali mbaya sana ya kiadili, shimo kubwa lenye giza la kiroho. Hata ufalme wa kusini wa Yuda, liliko hekalu la Mungu, hauna amani. Watu wa Yuda wametishwa na uvamizi wa Waashuri, na nyakati ngumu zawakabili, hayo yakiwa matokeo ya ukosefu wao wa uaminifu. Je, watafute msaada kwa nani? Kwa kusikitisha, wengi wamgeukia Shetani, wala si Yehova. Hasha! hawamwombi Shetani kwa jina. Badala yake, kama vile Mfalme Sauli wa zamani, wao wanawasiliana na roho, wakitafuta utatuzi wa matatizo yao kwa kujaribu kuwasiliana na wafu.—1 Samweli 28:1-20.

      5 Hata wengine wao wanachangia kusitawi kwa zoea hilo. Isaya ataja uasi huo asemapo: “Wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi [“wawasiliani-roho au kwa wale wenye roho ya kutabiri,” “NW”]; waliao kama ndege na kunong’ona; je! haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? je! waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?” (Isaya 8:19) Wawasiliani-roho waweza kuhadaa watu, “[wakilia] kama ndege na kunong’ona.” Sauti hizo zisemwazo eti ni za roho za wafu, zaweza kutolewa na mwasiliani-roho aliye hai afanyaye ionekane kana kwamba zatokana na wafu. Ingawa hivyo, nyakati nyingine huenda roho waovu wakahusika moja kwa moja na kujifanya kuwa wafu, kama ambavyo huenda ilitukia Sauli alipotafuta habari kwa mchawi wa Endori.—1 Samweli 28:8-19.

      6. Sababu gani Waisraeli ambao wamegeukia uwasiliani-roho ndio hasa wanaostahili kulaumiwa?

      6 Mambo hayo yote yanatendeka katika Yuda licha ya kwamba Yehova amekataza zoea la kuwasiliana na roho. Chini ya Sheria ya Kimusa, ni kosa linalostahili kifo. (Mambo ya Walawi 19:31; 20:6, 27; Kumbukumbu la Torati 18:9-12) Kwa nini watu wa pekee wa Yehova wakiuka sheria kwa njia mbaya hivyo? Kwa sababu wameikataa Sheria ya Yehova na shauri lake nao ‘wamefanywa kuwa wagumu kwa nguvu ya udanganyifu ya dhambi.’ (Waebrania 3:13) “Mioyo yao imenenepa kama shahamu,” nao wametengwa na Mungu wao.—Zaburi 119:70.a

      7. Wengi leo huigaje Waisraeli wa siku ya Isaya, na wakati ujao wa watu hao utakuwaje wasipotubu?

      7 Labda wao wafikiri hivi, ‘Kwani Sheria ya Yehova ina faida gani tukabilipo shambulio la Waashuri hivi karibuni?’ Wanataka utatuzi wa haraka na ulio rahisi kwa msiba wao nao hawana nia ya kumngojea Yehova afanye mapenzi yake. Katika siku yetu pia, wengi huipuuza sheria ya Yehova na kugeukia wawasiliani-roho, nyota, na namna nyingine za mafumbo ili watatue matatizo yao. Hata hivyo, ni upumbavu kwa walio hai leo kutafuta majibu kwa wafu, kama vile ilivyokuwa zamani. Wakati ujao wa yeyote anayezoea mambo hayo bila kutubu utakuwa na “wauaji-kimakusudi na waasherati na . . . waabudu-sanamu na waongo wote.” Hawana matazamio yoyote ya kuishi wakati ujao.—Ufunuo 21:8.

      “Sheria na Ushuhuda” wa Mungu

      8. Ni nini “sheria na ushuhuda” tunazopaswa kuziendea leo ili kupata mwelekezo?

      8 Sheria ya Yehova inayopiga marufuku uwasiliani-roho, pamoja na amri zake nyingine, haijafichika katika Yuda. Imehifadhiwa kwa maandishi. Leo Neno lake lililokamilika lapatikana kwa maandishi. Neno hilo ni Biblia, ambayo ina mkusanyo wa sheria na kanuni za Mungu na vilevile masimulizi ya jinsi Mungu alivyoshughulika na watu. Masimulizi hayo ya Biblia ya shughuli za Yehova huandaa ushuhuda, au uthibitisho, unaotufundisha utu na sifa za Yehova. Badala ya kuwaendea wafu, Waisraeli wapaswa kutafuta mwelekezo kutoka wapi? Isaya ajibu: “Kwa sheria na ushuhuda”! (Isaya 8:20a) Naam, wale wanaotaka ujuzi wa kweli wapaswa kuligeukia Neno la Mungu lililoandikwa.

      9. Je, watenda-dhambi wasiotubu watapata faida yoyote kwa kunukuu Biblia mara kwa mara?

      9 Huenda baadhi ya Waisraeli wanaopendezwa na uwasiliani-roho wakadai kuwa wanalistahi Neno la Mungu lililoandikwa. Lakini hayo ni madai tu nayo ni ya kinafiki. Isaya asema: “Ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” (Isaya 8:20b) Isaya arejezea neno gani hapa? Labda kwa neno: “Kwa sheria na ushuhuda.” Labda baadhi ya Waisraeli waasi-imani wanalirejezea Neno la Mungu, kama vile huenda waasi-imani na wengine leo wakanukuu Andiko. Lakini hayo ni maneno matupu tu. Kunukuu Andiko hakutatokeza “asubuhi [“nuru ya alfajiri,” NW],” au nuru ya Yehova, iwapo hakuandamani na kutenda mapenzi ya Yehova na kukataa mazoea yasiyo safi.b

      “Si Njaa ya Kukosa Chakula”

      10. Watu wa Yuda wanatesekaje kwa sababu ya kumkataa Yehova?

      10 Kutomtii Yehova husababisha giza la akili. (Waefeso 4:17, 18) Watu wa Yuda wamekuwa vipofu kiroho, hawana uelewevu. (1 Wakorintho 2:14) Isaya afafanua hali yao: “Watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa.” (Isaya 8:21a) Kwa sababu taifa hilo limekosa uaminifu—hasa wakati wa utawala wa Mfalme Ahazi—kuendelea kwa Yuda ikiwa ufalme ulio huru kumetishwa. Adui wamelizingira taifa hilo. Jeshi la Ashuru lashambulia majiji ya Yuda, moja baada ya jingine. Adui aharibu nchi yenye kuzaa, hali inayotokeza uhaba wa chakula. Wengi “wamedhikika sana na kuwa na njaa.” Lakini njaa ya aina nyingine yaikumba nchi. Makumi kadhaa ya miaka mapema, Amosi alitabiri: “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA.” (Amosi 8:11) Yuda sasa yadhikika kwa njaa ya kiroho kama hiyo!

      11. Je, Yuda itajifunza kutokana na nidhamu inayopokea?

      11 Je, Yuda itajifunza na kumrudia Yehova? Je, watu wake wataacha kuwasiliana na roho na kuabudu sanamu nao warudi “kwa sheria na ushuhuda”? Yehova aona kimbele itikio lao: “Na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa [“kumlaani,” “BHN”] kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu.” (Isaya 8:21b) Naam, wengi watamlaumu mfalme wao wa kibinadamu kwa kuwasababishia hali hiyo. Hata wengine, kwa upumbavu, watamlaumu Yehova kwa maafa yao! (Linganisha Yeremia 44:15-18.) Leo, wengi huitikia vivyo hivyo, wakimlaumu Mungu kwa misiba isababishwayo na uovu wa binadamu.

      12. (a) Kumwacha Mungu kumeleta nini kwa Yuda? (b) Ni maswali gani muhimu yanayozushwa?

      12 Je, kumlaani Mungu kutawaletea wakazi wa Yuda amani? La. Isaya atabiri: “Wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.” (Isaya 8:22) Baada ya kuinua macho yao mbinguni ili wamlaumu Mungu, warudi kuiangalia nchi, wayarudia matazamio yao yasiyo na matumaini. Kumwacha kwao Mungu kumeleta maafa. (Mithali 19:3) Hata hivyo, namna gani juu ya ahadi za Mungu kwa Abrahamu, Isaka, na Yakobo? (Mwanzo 22:15-18; 28:14, 15) Je, Yehova atazipuuza? Je, Waashuri au mamlaka nyingine ya kijeshi zitakomesha nasaba ya kifalme waliyoahidiwa Yuda na Daudi? (Mwanzo 49:8-10; 2 Samweli 7:11-16) Je, Waisraeli watahukumiwa adhabu ya kukaa gizani milele?

  • Ahadi ya Mkuu wa Amani
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • a Wengi huamini kuwa Zaburi 119 iliandikwa na Hezekia kabla hajawa mfalme. Ikiwa hivyo, labda iliandikwa Isaya akiwa bado anatoa unabii.

      b Usemi, “neno hili” katika Isaya 8:20 labda warejezea neno linalohusu wawasiliani-roho, lililonukuliwa katika Isaya 8:19. Ikiwa ndivyo ilivyo, Isaya amaanisha kwamba watu wanaochangia kusitawi kwa uwasiliani-roho katika Yuda wataendelea kuwasihi wengine waende kwa wawasiliani-roho na hivyo wasipate nuru ya Yehova.

  • Ahadi ya Mkuu wa Amani
    Unabii wa Isaya I—Nuru kwa Wanadamu Wote
    • [Picha katika ukurasa wa 121]

      Kutakuwa na njaa iliyo mbaya sana kuliko ile njaa ya kukosa chakula na kiu ya kukosa maji

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki