-
Mapacha Waliokuwa TofautiKitabu Changu cha Hadithi za Biblia
-
-
HADITHI YA 17
Mapacha Waliokuwa Tofauti
WAVULANA wawili hapa ni tofauti sana, sivyo? Unajua majina yao? Yule mwindaji ni Esau, na yule anayechunga kondoo ni Yakobo.
Esau na Yakobo walikuwa mapacha wa Isaka na Rebeka. Isaka baba yao, alimpenda sana Esau, kwa sababu alikuwa mwindaji mzuri naye aliiletea jamaa chakula. Lakini Rebeka alimpenda sana Yakobo, kwa sababu alikuwa mtulivu, mwenye amani.
Ibrahimu babu yao alikuwa bado hai. Tunaweza kuwaza namna Yakobo alivyopenda kumsikiliza akisema habari za Yehova. Mwishowe Ibrahimu akafa akiwa mwenye miaka 175, mapacha hao walipokuwa wenye miaka 15.
Esau alipokuwa mwenye miaka 40 alioa wanawake wawili kutoka nchi ya Kanaani. Hilo lilihuzunisha sana Isaka na Rebeka kwa sababu wanawake hao hawakumwabudu Yehova.
Ikawa siku moja Esau akamkasirikia sana Yakobo ndugu yake. Ulifika wakati Isaka alipotaka kumbariki mwanawe mkubwa. Kwa kuwa alikuwa mkubwa kuliko Yakobo, Esau alitazamia kupokea baraka hiyo. Lakini Esau alikuwa amekwisha kumwuzia Yakobo haki hiyo ya kupokea baraka. Pia, wavulana hao wawili walipozaliwa Mungu alikuwa amesema kwamba Yakobo angepokea baraka hiyo. Na ndivyo ilivyokuwa. Isaka alimpa Yakobo mwanawe baraka hiyo.
Baadaye, Esau alipojua hivyo akamkasirikia sana Yakobo. Alikasirika sana hata akasema angemwua Yakobo. Rebeka aliposikia hayo, alisumbuka sana. Basi akamwambia Isaka mume wake hivi: ‘ltakuwa vibaya sana ikiwa Yakobo pia anaoa mwanamke Mkanaani.’
Kisha Isaka akamwita Yakobo mwanawe akamwambia hivi: ‘Usioe mwanamke wa kutoka Kanaani. Nenda kwenye nyumba ya babu yako Betueli katika Harani. Oa mmoja wa binti za Labani mwanawe.’
Yakobo akamsikiliza baba yake, na mara hiyo akaanza safari yake ndefu kwenda kwa watu wake wa ukoo huko Harani.
-
-
Yakobo Anakwenda HaraniKitabu Changu cha Hadithi za Biblia
-
-
HADITHI YA 18
Yakobo Anakwenda Harani
UNAWAJUA wanaume hawa ambao Yakobo anazungumza nao? Akiisha kusafiri siku nyingi, Yakobo alikutana nao penye kisima. Walikuwa wakichunga kondoo zao. Yakobo akauliza: ‘Mnatoka wapi?’
‘Harani,’ wakasema.
‘Mnamjua Labani?’ Yakobo akauliza.
‘Ndiyo,’ wakajibu. ‘Tazama anakuja Raheli binti yake akiwa na kondoo zake.’ Unamwona Raheli (Rakeli) yule anakuja kutoka mbali?
Yakobo alipomwona Raheli akiwa na kondoo za mjomba wake, alikwenda kuondoa jiwe katika kisima ili kondoo wanywe maji. Kisha Yakobo akambusu Raheli na kujijulisha kwake. Raheli alifurahi sana, akaenda nyumbani kumwambia Labani baba yake.
Labani alifurahi sana Yakobo akae naye. Yakobo alipoomba kumwoa Raheli, Labani alifurahi. Lakini, alimwomba Yakobo afanye kazi katika shamba lake miaka 7 ili apewe Raheli. Yakobo alifanya hivyo kwa sababu alimpenda sana Raheli. Lakini ulipofika wakati wa arusi, unajua ilivyokuwa?
Labani alimpa Yakobo Lea binti yake mkubwa badala ya Raheli. Yakobo alipokubali kumfanyia Labani kazi muda wa miaka mingine saba, Labani alimpa Raheli pia awe mke wake. Siku hizo Mungu aliruhusu wanaume wawe na wake wengi. Lakini sasa, kama Biblia inavyoonyesha, imempasa mwanamume awe na mke mmoja tu.
-
-
Yakobo Ana Jamaa KubwaKitabu Changu cha Hadithi za Biblia
-
-
HADITHI YA 19
Yakobo Ana Jamaa Kubwa
EBU tazama jamaa hii kubwa. Hawa ni wana 12 wa Yakobo. Ana binti pia. Unajua majina ya watoto hao? Na tujifunze majina yao.
Lea alizaa Reubeni, Simeoni, Levi na Yuda. Raheli alipoona kwamba hakuzaa watoto, alihuzunika. Basi akampa Yakobo Bilha, mtumishi wake naye Bilha akazaa wana wawili walioitwa Dani na Naftali. Kisha Lea pia akampa Yakobo Zilpa mtumishi wake, naye Zilpa akazaa Gadi na Asheri. Mwishowe Lea akazaa wana wengine wawili, Isakari na Zebuloni.
Halafu Raheli alizaa mtoto. Akamwita jina Yusufu. Baadaye tutajifunza mengi juu ya Yusufu, kwa sababu akawa mtu mkubwa sana. Hao ndio wana 11 wa Yakobo alipokuwa anakaa na Labani baba ya Raheli.
Yakobo pia alikuwa na mabinti fulani, lakini Biblia inataja jina la mmoja tu, Dina.
Ukafika wakati ambapo Yakobo aliamua kumwacha Labani arudi Kanaani. Akakusanya jamaa yake kubwa na kondoo wake wengi na ng’ombe, akaanza safari ndefu.
Muda kidogo Yakobo na jamaa yake waliporudi Kanaani, Raheli alizaa mwana mwingine. Alizaa walipokuwa katika safari. Raheli alipata taabu kisha akafa alipokuwa akizaa. Lakini mtoto huyo mchanga alipona. Yakobo akamwita Benyamini.
Tunataka tuyakumbuke majina ya wana 12 wa Yakobo kwa sababu taifa zima la Israeli lilitokana nao. Makabila 12 ya Israeli yanaitwa kwa majina ya wana 10 wa Yakobo na wana wawili wa Yusufu. Isaka alikaa miaka mingi baada ya kuzaliwa watoto hao wa kiume, na bila shaka alifurahi sana kuwa na wajukuu wengi sana. Lakini na tuone yaliyompata Dina, mjukuu wake.
-