Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Jinsi Kijiji cha Wavuvi Kilivyokuja Kuwa Jiji Kubwa
    Amkeni!—2008 | Januari
    • Jinsi Kijiji cha Wavuvi Kilivyokuja Kuwa Jiji Kubwa

      MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI

      SIKU moja mnamo Agosti (Mwezi wa 8) 1590, Ieyasu Tokugawa (kulia), aliyekuja kuwa kamanda wa kwanza wa jeshi la Tokugawa,a alifika katika kijiji cha wavuvi cha Edo mashariki mwa Japani. Wakati huo, “Kijiji cha Edo kilikuwa na nyumba chache mbovu za wakulima na wavuvi,” kinasema kitabu The Shogun’s City—A History of Tokyo. Katika ujirani huo kulikuwa na ngome iliyoachwa ukiwa ambayo ilijengwa zaidi ya karne moja mapema.

      Kijiji hicho ambacho hakikujulikana kwa karne nyingi, kingekuja kuwa Tokyo, mji mkuu wa Japani na jiji kubwa sana ambalo leo lina wakaaji zaidi ya milioni 12. Tokyo lingekuja kuwa kati ya majiji yanayoongoza katika teknolojia, mawasiliano, usafiri, na biashara, likiwa makao makuu ya mashirika makubwa ya kibiashara. Mabadiliko hayo makubwa yalitokeaje?

      Kijiji Kinakuwa Jiji la Makamanda

      Karne moja baada ya 1467, mababe wa kivita waligawa Japani katika sehemu mbalimbali. Mwishowe, Hideyoshi Toyotomi, mbabe aliyekuwa na malezi ya hali ya chini, aliunganisha taifa hilo kwa kiasi fulani na akawa mtawala mnamo 1585. Mwanzoni, Ieyasu alipigana dhidi ya Hideyoshi mwenye nguvu, lakini baadaye wakaungana. Wakiwa pamoja walizingira na kuteka kasri la Odawara, ngome ya ukoo wa Hōjō wenye nguvu, na hivyo kushinda eneo la Kanto mashariki mwa Japani.

      Hideyoshi alimpa Ieyasu eneo kubwa la Kanto lenye majimbo manane, ambalo zamani lilikuwa la ukoo wa Hōjō, na hivyo kumfanya Ieyasu asonge mashariki mbali na eneo alilotawala awali. Hiyo ilikuwa mbinu ya kumfanya Ieyasu awe mbali na Kyoto, ambako maliki, mtawala mkuu wa Japani, aliishi. Licha ya hayo, Ieyasu alikubali, na akafika Edo kama tulivyosimulia mwanzoni. Aliamua kubadili kijiji hicho cha wavuvi kuwa kitovu cha utawala wake.

      Baada ya kifo cha Hideyoshi, Ieyasu aliongoza jeshi la muungano, hasa kutoka mashariki mwa Japani, dhidi ya majeshi kutoka magharibi mwa Japani, na mnamo 1600, katika siku moja tu, alishinda eneo hilo. Mnamo 1603, Ieyasu alitawazwa kuwa kamanda wa jeshi, na hivyo kuwa mtawala halisi wa taifa lote. Sasa Edo kikawa kituo kipya cha usimamizi wa Japani.

      Ieyasu aliamuru mababe wa vita wampe wanaume na vifaa vya kumaliza ujenzi wa kasri kubwa. Wakati mmoja, meli 3,000 hivi zilitumiwa kubeba mawe makubwa ya matale ambayo yalikuwa yamechimbuliwa kwenye miamba ya Rasi ya Izu, kilomita 100 hivi upande wa kusini. Mawe hayo yalipopakuliwa bandarini, wanaume mia moja au zaidi waliyabeba hadi kwenye eneo la ujenzi.

      Ujenzi wa kasri hilo ambalo ndilo kubwa zaidi nchini Japani, ulikamilishwa miaka 50 baadaye, wakati wa utawala wa kamanda wa tatu, nalo lilikuwa ishara kubwa ya utawala wenye nguvu wa Tokugawa. Samurai, au mashujaa wa vita, ambao walimtumikia kamanda waliishi kando ya kasri hilo. Kamanda huyo aliwataka mababe hao wa vita wawe na nyumba nyingine kubwa huko Edo mbali na makasri waliyokuwa nayo katika meneo yao.

      Ili kutosheleza mahitaji ya samurai, vikundi vya wafanyabiashara na wasanii walihamia huko kutoka sehemu mbalimbali nchini. Kufikia 1695, karne moja hivi baada ya Ieyasu kuingia Edo, idadi ya wakaaji wa Edo ilikuwa imeongezeka kufikia milioni moja! Jiji hilo likaja kuwa jiji kubwa zaidi ulimwenguni wakati huo.

      Wafanyabiashara Wachukua Mahali pa Mashujaa wa Vita

      Serikali ya makamanda hao ilifanikiwa sana kudumisha amani hivi kwamba mashujaa wa vita hawakuwa na kazi nyingi ya kufanya. Bila shaka, bado samurai walijivunia kazi yao, lakini mahali pao palianza kuchukuliwa na wafanyabiashara waliotumia abakusi (kifaa cha kufanyia hesabu) kilichotumiwa sana katika nchi za Mashariki. Kwa miaka zaidi ya 250 kulikuwa na amani. Raia kwa ujumla, hasa wafanyabiashara, walifanikiwa kiuchumi na walikuwa na uhuru mwingi zaidi. Hivyo, utamaduni wa pekee ulianzishwa.

      Watu walijihusisha katika michezo ya Kabuki (michezo ya kuigiza ya kihistoria), Bunraku (maonyesho ya vikaragosi), na rakugo (hadithi zinazochekesha). Nyakati za jioni katika majira ya kiangazi, watu walikusanyika kwenye fuo za Mto Sumida wenye upepo mwanana huko Edo. Pia walienda huko wakati wa majira ya kiangazi ili kutazama fataki zikilipuliwa, desturi ambayo inaendelea mpaka leo.

      Hata hivyo, jiji la Edo halikujulikana na watu wengi ulimwenguni. Kwa zaidi ya miaka 200, watu wa nchi hiyo hawakuruhusiwa kuwa na uhusiano na watu wa nchi nyingine isipokuwa uhusiano mdogo na Waholanzi, Wachina, na Wakorea. Kisha siku moja, tukio lisilotazamiwa likabadili jiji hilo na taifa nzima.

      Edo Yaitwa Tokyo

      Karibu na pwani ya Edo, meli zisizo za kawaida zilizotoa moshi mweusi zilionekana. Wavuvi walioshtuka walifikiri kwamba ni volkano zinazoelea! Uvumi kuhusu jambo hilo ulienea huko Edo, na hivyo kuwafanya watu wengi wahame.

      Meli hizo nne zilizokuwa chini ya Kamanda Matthew C. Perry wa Jeshi la Majini la Marekani, zilitia nanga kwenye Bandari ya Edo Julai 8, 1853 (8/7/1853) (kushoto). Perry aliomba serikali ya Japani iwaruhusu wafanye biashara nao. Ziara ya Perry iliwafanya Wajapani wagundue kwamba nchi yao ilikuwa imebaki nyuma sana katika maendeleo ya kijeshi na kiteknolojia.

      Jambo hilo lilianzisha matukio yaliyokomesha utawala wa Tokugawa na kurudisha tena utawala wa maliki. Mnamo 1868, Edo ilibadilishwa jina na kuitwa Tokyo, jina linalomaanisha “Mji Mkuu wa Mashariki,” kwa sababu ya mahali lilipoonekana kutoka Kyoto. Maliki alihamisha makao yake kutoka jumba la kifalme la Kyoto hadi kasri la Edo, na baadaye likabadilishwa na kuwa Jumba jipya la Maliki.

  • Jinsi Kijiji cha Wavuvi Kilivyokuja Kuwa Jiji Kubwa
    Amkeni!—2008 | Januari
    • a Katika jeshi la Japani, cheo cha kamanda kilipitishwa kupitia urithi na kamanda alikuwa na mamlaka kubwa chini ya uongozi wa maliki.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki