-
Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
-
-
18 Kisha, Nebukadneza akamtawaza Sedekia, mwana mwingine wa Yosia, awe mfalme wa Yuda. Ndiye aliyekuwa mfalme wa mwisho wa Yuda. Utawala wake ulikoma mwaka wa 607 K.W.K., Yerusalemu na hekalu lake lilipoharibiwa. (2 Fal. 24:17) Hata hivyo, kwa miaka 11 ambayo Sedekia alitawala, kulikuwa na misukosuko mingi ya kijamii na kisiasa katika taifa la Yuda.
-
-
Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
-
-
SIKU ZA MWISHO ZA UTAWALA WA KINASABA
20. Kwa nini wakati wa utawala wa Sedekia ulikuwa kipindi kigumu katika mgawo wa Yeremia? (Ona sanduku katika ukurasa wa 29.)
20 Huenda kipindi kigumu zaidi katika mgawo wa Yeremia kilikuwa wakati wa utawala wa Sedekia. Kama wengi waliomtangulia, Sedekia ‘aliendelea kufanya yaliyokuwa mabaya machoni pa Yehova.’ (Yer. 52:1, 2) Alikuwa mfalme kibaraka wa Wababiloni, naye Nebukadneza alimwapisha kwa jina la Yehova kwamba atajitiisha kwa mfalme wa Babiloni. Licha ya kufanya hivyo, mwishowe Sedekia aliasi. Nao adui za Yeremia walikuwa wakimshinikiza ajiunge na waasi.—2 Nya. 36:13; Eze. 17:12, 13.
21-23. (a) Taifa la Yuda lilikuwa limegawanyika katika pande gani mbili wakati wa utawala wa Sedekia? (b) Yeremia alitendewa jinsi gani kwa sababu ya msimamo wake, nasi tunaweza kufaidika jinsi gani kwa kutafakari juu ya hali yake?
21 Inaonekana kwamba, mapema katika utawala wa Sedekia, wafalme wa Edomu, Moabu, Amoni, Tiro, na Sidoni, walituma wajumbe Yerusalemu. Labda lengo lao lilikuwa kumshawishi Sedekia ajiunge nao dhidi ya Nebukadneza. Hata hivyo, Yeremia alimsihi Sedekia ajitiishe kwa Babiloni. Yeremia aliwapa wajumbe hao nira ili kuonyesha kwamba mataifa yao pia yanapaswa kuwatumikia Wababiloni. (Yer. 27:1-3, 14)c Ujumbe huo wa Yeremia haukuwafurahisha, naye Hanania alifanya mambo yawe magumu hata zaidi. Hanania alikuwa nabii wa uwongo ambaye alidai katika jina la Mungu kwamba nira ya Wababiloni itavunjwa. Hata hivyo, Yehova alitangaza kupitia Yeremia kwamba mlaghai huyo, Hanania, atakufa kabla ya mwaka kwisha. Hivyo ndivyo ilivyokuwa.—Yer. 28:1-3, 16, 17.
22 Taifa la Yuda lilikuwa limegawanyika katika pande mbili, wale waliokuwa tayari kujitiisha kwa Babiloni na wale waliokuwa wakichochea uasi. Mwaka wa 609 K.W.K., Sedekia aliasi kwa kutafuta usaidizi wa jeshi la Misri. Yeremia alilazimika kukabiliana na mchafuko uliosababishwa na watu waliokuwa wakiunga mkono maasi. (Yer. 52:3; Eze. 17:15) Nebukadneza pamoja na jeshi lake walirudi Yuda ili kuzima ghasia hizo, akayapiga na kuyashinda majiji yote ya Yuda na kuuzingira tena mji wa Yerusalemu. Wakati huo, Yeremia alitangaza kwamba Yerusalemu litaanguka mikononi mwa Wababiloni. Wowote ambao watabaki jijini watauawa. Nao wale ambao watakaoenda kwa Wakaldayo wataokoka.—Soma Yeremia 21:8-10; 52:4.
23 Wakuu wa Yuda walidai kwamba Yeremia anaunga mkono Babiloni. Aliposema ukweli wa mambo, wakuu wa Yuda walimpiga na kumtia kizuizini. (Yer. 37:13-15) Hata hivyo, Yeremia hakupunguza uzito wa ujumbe wa Yehova. Kwa hiyo, wakuu wakamchochea Sedekia amuue Yeremia. Wakamtupa Yeremia ndani ya tangi ambalo halikuwa na maji ambamo angeweza kuangamia kwenye matope. Hata hivyo, aliokolewa na Ebed-meleki, Mwethiopia aliyekuwa mtumishi katika nyumba ya mfalme. (Yer. 38:4-13) Leo pia, watumishi wa Yehova hujikuta hatarini kwa sababu ya kukataa kuunga mkono mizozo ya kisiasa. Bila shaka, kutafakari mambo yaliyompata Yeremia kunaweza kukupa nguvu za kukabili majaribu na kuyashinda.
24. Mwaka wa 607 K.W.K. kulikuwa na matukio gani?
24 Hatimaye, mwaka wa 607 K.W.K., Wababiloni walibomoa kuta za Yerusalemu na kuliangusha jiji hilo. Jeshi la Nebukadneza likateketeza hekalu la Yehova, likabomoa kuta za jiji, na kuwaua watu wenye vyeo wa Yuda. Sedekia alijaribu kukimbia, lakini akakamatwa na kutiwa mikononi mwa Wababiloni. Wana wake wakauawa mbele ya macho yake, kisha Nebukadneza akaagiza apofushwe, afungwe kwa pingu, na kupelekwa Babiloni. (Yer. 39:1-7)
-