-
Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
-
-
Miaka miwili tu baadaye, Amoni aliuawa, na mwaka wa 659 K.W.K., mwana wake Yosia, mwenye umri wa miaka minane akaanza kutawala.
6 Katika wa miaka 31 ya utawala wa Yosia, ukuu wa Babiloni ulianza kupita ule wa Ashuru. Yosia aliuona huo kuwa wakati unaofaa kukomboa Yuda kutoka mikononi mwa utawala wa kigeni. Tofauti na baba na babu yake, Yosia alimtumikia Yehova kwa uaminifu na kuanzisha mabadiliko makubwa ya kidini. (2 Fal. 21:19–22:2) Katika mwaka wa 12 wa utawala wake, Yosia aliondolea mbali mahali pa juu, miti mitakatifu, na sanamu za dini ya uwongo kotekote katika eneo lote la ufalme wake na kuagiza hekalu la Yehova lifanyiwe marekebisho. (Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:1-8.) Katika mwaka wa 13 wa utawala wa Yosia (647 K.W.K.), ndipo Yeremia alipopewa mgawo wa kuwa nabii wa Mungu.
Ungeuona namna gani mgawo wa kuwa nabii katika siku za Yeremia?
7, 8. (a) Ni kwa njia gani utawala wa Mfalme Yosia ulikuwa tofauti na utawala wa Manase na Amoni? (b) Yosia alikuwa mtu wa aina gani? (Ona sanduku katika ukurasa wa 20.)
7 Hekalu lilipokuwa likirekebishwa, katika mwaka wa 18 wa utawala wa mfalme Yosia, kuhani mkuu alikipata “kile kitabu chenyewe cha sheria.” Mwandishi akamsomea mfalme kitabu hicho. Yosia akatambua makosa ya watu wake, akatafuta mwongozo wa Yehova kupitia nabii Hulda, na kuwasihi watu washike amri za Mungu. Hulda alimfahamisha Yosia kwamba Yehova ataleta “msiba” juu ya Yudea kwa sababu ya kukosa uaminifu. Hata hivyo, kwa sababu Yosia alikuwa na maoni mazuri kuhusu ibada safi, msiba haungekuja wakati wake.—2 Fal. 22:8, 14-20.
8 Mfalme Yosia alianzisha tena jitihada zake za kuondolea mbali ibada yoyote ya sanamu iliyokuwa imebaki. Akiwa na bidii hiyo alienda mpaka eneo lililokuwa la ufalme wa kaskazini wa Israeli, ili kuharibu mahali pa juu na madhabahu ya Betheli. Pia, alifanya mipango kwa ajili ya sherehe kubwa ya Pasaka. (2 Fal. 23:4-25) Haikosi hatua hiyo ilimfurahisha sana Yeremia! Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa watu kubadili njia zao. Manase na Amoni walikuwa wameanzisha ibada ya sanamu yenye kuchukiza, kwa hiyo, hali ya kiroho ya watu ilikuwa imezorota sana. Licha ya mabadiliko ambayo Yosia alikuwa amefanya, Mungu alisema kupitia Yeremia kwamba bado kuna miungu mingi Yudea. Watu walioishi siku za Yeremia walikuwa kama mke mwasherati, walikuwa wamemwacha Yehova na kufanya ukahaba na miungu ya kigeni. Yeremia aliwaambia: “Mmeweka madhabahu nyingi kama barabara za Yerusalemu kwa ajili ya kile kitu cha aibu, madhabahu za kumfukizia Baali moshi wa dhabihu.”—Soma Yeremia 11:1-3, 13.
9. Ni mambo gani yaliyohusisha mataifa mengine yaliyotokea katika miaka ya mwishomwisho ya utawala wa Yosia?
9 Ujumbe wa Yeremia haukuwabadili Wayahudi wala mataifa yaliyokuwa yaking’ang’ania kuwa na mamlaka katika eneo hilo. Mwaka wa 632 K.W.K., majeshi ya Wababiloni na Wamedi yaliteka Ninawi, mji mkuu wa Ashuru. Miaka mitatu baadaye, Farao Neko wa Misri aliongoza majeshi yake upande wa kaskazini kwenda kuwasaidia Waashuru waliokuwa taabani. Kwa sababu zisizojulikana, Yosia alijaribu kuyazuia majeshi ya Misri yalipokuwa Megido, hata hivyo, aliumizwa vibaya sana, naye akafa. (2 Nya. 35:20-24) Tukio hilo lenye kuhuzunisha lingeleta mabadiliko gani ya kisiasa na kidini katika taifa la Yuda? Ni hali gani ngumu ambazo Yeremia angekabili?
MABADILIKO YA KIDINI
10. (a) Hali zilizokuwapo baada ya kifo cha Yosia zinalingana jinsi gani na siku zetu? (b) Tunaweza kufaidika jinsi gani kwa kuchunguza maisha ya Yeremia?
10 Wazia jinsi Yeremia alivyohisi aliposikia kwamba Yosia amekufa! Akiwa na huzuni nyingi, aliimba nyimbo za maombolezo. (2 Nya. 35:25) Tayari hali ilikuwa ngumu katika taifa la Yuda. Isitoshe, kulikuwa na mizozo kati ya mataifa mbalimbali. Misri, Ashuru, na Babiloni yalikuwa yaking’ang’ania eneo hilo. Mazingira ya ibada katika Yuda yalikuwa yamebadilika baada ya kifo cha Yosia. Huo ndio uliokuwa mwisho wa utawala uliomfaa Yeremia na kazi yake ya kutoa unabii, na mwanzo wa utawala mkatili.
-