-
Imani Katika Unabii wa Biblia Inaokoa UhaiMnara wa Mlinzi—2007 | Aprili 1
-
-
Mwishowe, katika mwaka wa 66 W.K., Florus, Gavana Mroma aliye mpotovu anachukua talanta 17 za “deni la kodi” kutoka katika hazina takatifu ya hekalu. Wayahudi wanakasirika na kuanza kuasi serikali. Wayahudi waasi wanamiminika Yerusalemu na kuwachinja askari-jeshi Waroma jijini humo. Kisha, wanatangaza kwa ujasiri kwamba Yudea haiko tena chini ya Roma. Sasa vita vinazuka kati ya Roma na Yudea!
Katika muda wa miezi mitatu, gavana Mroma wa Siria, Sesho Galo, anashuka kusini akiwa na askari-jeshi 30,000 ili kuzima uasi wa Wayahudi. Jeshi lake linafika Yerusalemu wakati wa Sherehe ya Vibanda na kuingia moja kwa moja vijijini. Wayahudi waasi ambao ni wachache wanakimbilia katika ngome ya hekalu. Muda si muda, askari-jeshi Waroma wanaanza kuuharibu ukuta wa hekalu. Wayahudi wanaudhika, kwa sababu, askari-jeshi wapagani sasa wanatia unajisi mahali patakatifu zaidi pa dini ya Kiyahudi! Hata hivyo, Wakristo walio jijini wanakumbuka maneno haya ya Yesu: ‘Mtakapoona lile chukizo, likiwa limesimama katika mahali patakatifu, wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani.’ (Mathayo 24:15, 16) Je, wangeonyesha imani katika maneno ya Yesu ya kinabii na hivyo kuchukua hatua inayofaa? Kama ilivyotukia, uhai wao ulitegemea kufanya hivyo. Lakini wangekimbia jinsi gani?
Kwa ghafula na bila sababu yoyote nzuri, Sesho Galo anawaondoa askari-jeshi wake na kuelekea pwani huku wakikimbizwa mbio na Wayahudi waasi. Kwa kushangaza, dhiki juu ya jiji hilo ilikuwa imefupishwa! Wakristo wanaonyesha imani yao katika onyo la kinabii la Yesu na kutoka Yerusalemu na kukimbilia Pela, jiji lisilomilikiwa na yeyote lililo milimani ng’ambo ya Mto Yordani. Wanakimbia kwa wakati unaofaa kabisa. Punde si punde, Wayahudi hao waasi wanarudi Yerusalemu na kuwalazimisha watu waliobaki jijini kuunga mkono uasi wao.a
-
-
Imani Katika Unabii wa Biblia Inaokoa UhaiMnara wa Mlinzi—2007 | Aprili 1
-
-
Hali Inazorota
Baada ya miezi michache, jeshi lingine la Roma linaelekea Yerusalemu. Mnamo mwaka wa 67 W.K., Jenerali Vespasian na mwana wake Tito wanakusanya pamoja jeshi kubwa sana lenye askari 60,000. Kwa miaka miwili inayofuata, jeshi hilo lenye kuharibu linaelekea Yerusalemu, likiponda wapinzani wote njiani. Wakati huo, ndani ya Yerusalemu, vikundi vinavyopingana vya Wayahudi vinapambana vikali. Majengo ya kuhifadhi mbegu jijini yanaharibiwa, eneo linalozunguka hekalu linaharibiwa kabisa, na Wayahudi zaidi ya 20,000 wanauawa. Vespasian anasita kushambulia Yerusalemu, huku akisema: ‘Mungu anatenda kama jenerali Mroma kwa njia bora kuliko mimi; maadui wetu wanaangamizana wenyewe.’
Wakati Maliki Nero wa Roma anapokufa, Vespasian anaenda Roma kuchukua kiti cha ufalme, anamwacha Tito amalize kampeni ya kushambulia Yudea. Tito anashambulia Yerusalemu karibu Pasaka ya mwaka wa 70 W.K., akiwanasa jijini humo wakaaji na wasafiri waliotoka maeneo mengine. Majeshi yake yanakata miti katika maeneo ya mashambani ya Yudea ili kujenga ukuta wenye miti iliyochongoka. Wanajenga ukuta huo umbali wa kilomita 7 kuzunguka jiji hilo. Ni kama tu Yesu alivyotabiri: ‘Adui zako watajenga kukuzunguka ngome yenye miti iliyochongoka nao watakuzunguka na kukutaabisha kutoka kila upande.’—Luka 19:43.
Punde si punde, kunakuwa na njaa kali jijini. Vikundi vyenye silaha vinapora nyumba za watu waliouawa na za wale wanaokufa. Angalau mwanamke mmoja mwenye njaa kali anamuua na kumla mtoto wake mchanga, na hivyo anatimiza unabii uliosema: “Utalazimika kula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako na binti zako . . . kwa sababu ya mbano na mkazo ambao adui yako atakusonga nao.”—Kumbukumbu la Torati 28:53-57.
Mwishowe, baada ya kuzingirwa kwa miezi mitano, Yerusalemu linaanguka. Jiji hilo na hekalu lake kubwa linaporwa na kuteketezwa kisha, linabomolewa jiwe kwa jiwe. (Danieli 9:26) Jumla ya watu 1,100,000 hivi wanakufa; na wengine 97,000 wanauzwa utumwani.b (Kumbukumbu la Torati 28:68) Yudea linabaki karibu ukiwa bila Wayahudi. Kwa kweli, huo ni msiba wa kitaifa ambao hauna kifani. Maisha ya kisiasa, kidini, na ya kitamaduni ya Wayahudi yanabadilika kabisa.c
-