-
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”‘Njoo Uwe Mfuasi Wangu’
-
-
Sura ya 3
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”
“Tazama! mfalme wako anakuja kwako”
1-3. Yesu anaingia Yerusalemu jinsi gani, na kwa nini huenda watazamaji fulani wanashangaa?
KUNA makelele mengi jijini Yerusalemu. Mtu mkuu anakuja! Nje ya jiji, watu wamekusanyika kandokando ya barabara. Wana hamu kubwa ya kumpokea mtu huyo kwa sababu watu fulani kati yao wanasema kwamba ni mrithi wa Mfalme Daudi na ana haki ya kuwa Mtawala wa Israeli. Wengine wao wana matawi ya mitende ya kumpungia; hali wengine wanatandaza mavazi yao na matawi ya miti barabarani ili kuilainisha njia atakayopitia. (Mathayo 21:7, 8; Yohana 12:12, 13) Inaonekana wengi wao wanataka kuona jinsi atakavyoingia jijini.
2 Labda wengine wanatazamia aingie kwa fahari nyingi. Bila shaka, wanawajua watu fulani mashuhuri waliokuwa na misafara ya kifahari. Kwa mfano, Absalomu mwana wa Daudi alipojitangaza kuwa mfalme, alituma wanaume 50 wakimbie mbele ya gari lake. (2 Samweli 15:1, 10) Mtawala Mroma, Kaisari Yulio alidai mengi hata zaidi; pindi moja aliongoza msafara wa ushindi mpaka bunge la Roma, akiwa amezingirwa na tembo 40 waliokuwa wamebeba taa! Hata hivyo, sasa, watu wa Yerusalemu wanamngojea mtu mkuu hata zaidi. Iwe umati huo unajua au haujui, huyo ndiye Masihi, mwanadamu mkuu zaidi aliyepata kuishi. Lakini, mtu huyo atakayekuwa Mfalme wa wakati ujao anapoingia jijini, labda wengine wanashangaa.
3 Hawaoni magari, wakimbiaji, farasi, wala tembo wowote. Yesu amepanda punda, mnyama wa kubeba mizigo.a Mpandaji huyo na punda wake hawana mapambo yoyote. Badala ya matandiko ya gharama kubwa, wafuasi fulani wa karibu wa Yesu wametumia mavazi kutandika mgongo wa punda huyo. Kwa nini Yesu ameamua kuingia Yerusalemu bila kujionyesha, hali watu wengine wasio mashuhuri kama yeye wamesisitiza kuingia kwa sherehe kubwakubwa?
4. Biblia ilitabiri nini kuhusu jinsi ambavyo Mfalme wa Kimasihi angeingia Yerusalemu?
4 Yesu anatimiza unabii huu: “Shangilia sana . . . Piga kelele za ushindi, Ee binti Yerusalemu. Tazama! mfalme wako anakuja kwako. Yeye ni mwadilifu, ndiyo, ameokolewa; ni mnyenyekevu, naye amepanda juu ya punda.” (Zekaria 9:9) Unabii huo unaonyesha kwamba siku moja Mtiwa-Mafuta wa Mungu, Masihi, angewatokea watu wa Yerusalemu akiwa Mfalme aliyewekwa na Mungu. Isitoshe, jinsi ambavyo angetokea, kutia ndani mnyama ambaye angechagua kumpanda, kungeonyesha sifa yenye kupendeza aliyo nayo moyoni, sifa ya unyenyekevu.
-
-
“Mimi Ni . . . Mnyenyekevu Moyoni”‘Njoo Uwe Mfuasi Wangu’
-
-
a Kikizungumzia tukio hilo, kichapo kimoja kinasema wanyama hao ni “viumbe wa hali ya chini.” Kisha kinaongezea: “Wanajikokota-kokota, ni wakaidi, wanatumiwa na maskini kufanya kazi, na sura yao si ya kuvutia.”
-