-
Huu Ndio Wakati Muhimu Zaidi wa Kukaa Macho!Mnara wa Mlinzi—2003 | Januari 1
-
-
Mwisho wa Mfumo wa Mambo wa Kiyahudi
3. Uharibifu wa Yerusalemu unafananaje na wa majiji ya Pompeii na Herculaneum?
3 Uharibifu wenye kuogopesha wa jiji la Pompeii na Herculaneum haukuwa mkubwa kama ule wa Yerusalemu uliotukia miaka tisa mapema, na ambao ulisababishwa na watu. Uharibifu huo unaotajwa kuwa “mazingiwa mabaya zaidi katika historia,” ulisababisha vifo vya Wayahudi zaidi ya milioni moja. Hata hivyo, msiba uliopata jiji la Pompeii na Herculaneum ulitanguliwa na onyo na ndivyo na uharibifu uliopata jiji la Yerusalemu.
4. Yesu alitoa ishara gani ya unabii ili kuonya wafuasi wake kwamba mwisho wa mfumo wa mambo ulikuwa umekaribia, na ishara hiyo ilitimizwaje mara ya kwanza katika karne ya kwanza?
4 Yesu Kristo alikuwa ametabiri kwamba jiji hilo lingeharibiwa na kutaja matukio ambayo yangetangulia uharibifu huo—mambo ya kuogopesha kama vita, upungufu wa chakula, matetemeko ya ardhi, na uvunjaji wa sheria. Kungekuwa na manabii wasio wa kweli, lakini habari njema ya Ufalme wa Mungu ingehubiriwa ulimwenguni pote. (Mathayo 24:4-7, 11-14) Ingawa maneno ya Yesu yanatimizwa kwa kiwango kikubwa leo, yalitimizwa kwa kiwango kidogo wakati huo. Historia inaonyesha kwamba kulikuwa na njaa kali huko Yudea. (Matendo 11:28) Mwanahistoria Myahudi Josephus anaripoti kwamba kulikuwa na tetemeko la ardhi huko Yerusalemu kabla tu ya jiji hilo kuharibiwa. Uharibifu wa Yerusalemu ulipokaribia, mara nyingi kulikuwa na maasi yasiyokoma, vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikundi vya kisiasa vya Wayahudi, na mauaji katika majiji kadhaa ambayo wakazi wake walikuwa Wayahudi na watu wasio Wayahudi. Licha ya hayo, habari njema ya Ufalme ilikuwa ikihubiriwa “katika viumbe vyote chini ya mbingu.”—Wakolosai 1:23.
5, 6. (a) Ni unabii gani wa Yesu uliotimizwa mwaka wa 66 W.K.? (b) Kwa nini watu wengi sana walikufa Yerusalemu lilipoharibiwa mwaka wa 70 W.K.?
5 Hatimaye, mnamo mwaka wa 66 W.K., Wayahudi waliasi dhidi ya Roma. Wakati Cestius Gallus alipoongoza majeshi yake yazingire Yerusalemu, wafuasi wa Yesu walikumbuka maneno haya ya Yesu: “Wakati mwonapo Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwalo kumekaribia. Ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbia hadi kwenye milima, na waacheni wale walio katikati yalo waondoke, na waacheni wale walio katika sehemu za mashambani wasiingie ndani yalo.” (Luka 21:20, 21) Wakati wa kuondoka Yerusalemu ulikuwa umefika. Lakini wangeondokaje? Gallus na majeshi yake yaliondoka kwa ghafula, hivyo Wakristo huko Yerusalemu na Yudea wakapata fursa ya kutii maneno ya Yesu na kukimbilia milimani.—Mathayo 24:15, 16.
6 Miaka minne baadaye, yapata wakati wa Sikukuu ya Kupitwa, jeshi la Roma lilirudi likiongozwa na Jenerali Titus, aliyekuwa ameazimia kukomesha kabisa uasi wa Wayahudi. Majeshi yake yalizingira Yerusalemu na kujenga “boma lenye miti iliyochongoka,” na hivyo kuzuia mtu yeyote asiweze kutoroka. (Luka 19:43, 44) Licha ya tisho la vita, Wayahudi kutoka Milki yote ya Roma walikuwa wamekuja Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa. Sasa wakawa wamenaswa. Kulingana na Josephus, idadi kubwa ya waliokufa wakati Roma lilipozingirwa ni wageni hao wa kusikitikiwa.a Wakati Yerusalemu lilipoharibiwa, karibu Myahudi mmoja kati ya kila Wayahudi saba alikufa katika Milki ya Roma. Kuharibiwa kwa Yerusalemu na hekalu lake kulimaanisha kukomeshwa kwa taifa la Kiyahudi na mfumo wake wa kidini uliotegemea Sheria ya Musa.b—Marko 13:1, 2.
7. Kwa nini Wakristo waaminifu waliokoka uharibifu wa Yerusalemu?
7 Mnamo mwaka wa 70 W.K., Wakristo Wayahudi wangaliuawa au kupelekwa utumwani pamoja na watu wote waliokuwa Yerusalemu. Hata hivyo, historia inathibitisha kwamba walitii onyo la Yesu lililokuwa limetolewa miaka 37 mapema. Walikuwa wameondoka jijini na hawakuwa wamerudi.
-
-
Huu Ndio Wakati Muhimu Zaidi wa Kukaa Macho!Mnara wa Mlinzi—2003 | Januari 1
-
-
a Haielekei kwamba Yerusalemu lilikuwa na wakazi zaidi ya 120,000 katika karne ya kwanza. Eusebius anakadiria kwamba wakazi 300,000 kutoka mkoa wa Yudea walisafiri hadi Yerusalemu kusherehekea Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka wa 70 W.K. Bila shaka, wengine waliokufa walitoka sehemu nyingine za milki hiyo.
-