Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ukristo Waenea Miongoni mwa Wayahudi wa Karne Ya Kwanza
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Oktoba 15
    • Ulimwengu wa Wayahudi Katika Karne ya Kwanza

      Ni Wayahudi wangapi walioishi nje ya Palestina katika karne ya kwanza? Yaelekea wasomi wengi wanakubaliana na kichapo Atlas of the Jewish World kinachosema hivi: “Ni vigumu kujua hesabu kamili, lakini imekadiriwa kwamba muda mfupi kabla ya mwaka wa 70 kulikuwa na Wayahudi milioni mbili na nusu huko Yudea na zaidi ya milioni nne katika sehemu ile nyingine iliyotawaliwa na Roma. . . . Yaelekea kwamba Wayahudi walifanyiza asilimia 10 hivi ya watu walioishi chini ya milki ya Roma, na katika maeneo yenye Wayahudi wengi, katika majiji ya mikoa ya mashariki, huenda walifanyiza asilimia 25 au zaidi ya idadi ya wakaaji.”

      Vituo vikuu vya Wayahudi vilikuwa Siria, Asia Ndogo, Babiloni, na Misri, katika Mashariki, na jamii ndogo za Wayahudi zilikuwa huko Ulaya. Baadhi ya Wakristo Wayahudi wa mapema waliojulikana sana waliishi nje ya Israeli, kama vile Barnaba kutoka Kipro, Priska na Akila kutoka Ponto na Roma, Apolo kutoka Aleksandria, na Paulo kutoka Tarso.—Matendo 4:36; 18:2, 24; 22:3.

      Wayahudi walioishi nje ya Palestina waliunganishwa na nchi yao kwa njia nyingi. Njia moja ilikuwa kodi ya kila mwaka iliyotumwa kwenye hekalu huko Yerusalemu ambayo iliwawezesha Wayahudi hao kushiriki katika ibada na shughuli za hekalu. Kuhusiana na hilo, msomi John Barclay anasema hivi: “Kuna uthibitisho wa kutosha kwamba jamii za Wayahudi zilizoishi nje ya Palestina zilikusanya kwa bidii pesa hizo na vilevile michango ya ziada iliyotolewa na matajiri.”

      Pia, makumi ya maelfu ya watu walienda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya sherehe mbalimbali. Masimulizi kwenye Matendo 2:9-11 kuhusu Pentekoste ya mwaka wa 33 W.K., yanaonyesha hivyo. Wasafiri wa Kiyahudi waliokuwapo walitoka Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Kapadokia, Ponto, Asia, Frigia, Pamfilia, Misri, Libya, Roma, Krete, na Arabia.

      Wasimamizi wa hekalu huko Yerusalemu waliwasiliana na Wayahudi walioishi nje ya Palestina kwa kuandikiana nao. Inajulikana kwamba Gamalieli, mwalimu wa sheria anayetajwa kwenye Matendo 5:34, alituma barua Babiloni na sehemu nyingine za ulimwengu. Mtume Paulo alipofika huko Roma akiwa mfungwa yapata mwaka wa 59 W.K., “wakuu wa Wayahudi” walimwambia hivi: “Wala sisi hatujapokea barua zinazokuhusu wewe kutoka Yudea, wala hakuna yeyote wa akina ndugu ambaye amefika aliyetujulisha au kusema jambo lolote baya juu yako.” Hilo linaonyesha kwamba barua na ripoti zilitumwa kwa ukawaida kutoka Israeli hadi Roma.—Matendo 28:17, 21.

      Biblia iliyotumiwa na Wayahudi walioishi nje ya Palestina, ilikuwa tafsiri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania iliyoitwa Septuajinti. Kichapo kimoja kinasema hivi: “Ni jambo linalopatana na akili kukata kauli kwamba tafsiri ya LXX [Septuajinti] ilisomwa kotekote katika jumuiya ya Wayahudi walioishi nje ya Palestina na kukubaliwa kuwa Biblia ya Kiyahudi au ‘maandiko matakatifu.’” Tafsiri hiyohiyo ilitumiwa sana na Wakristo wa mapema katika mafundisho yao.

  • Ukristo Waenea Miongoni mwa Wayahudi wa Karne Ya Kwanza
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Oktoba 15
    • Jumuiya za Wayahudi Zilizokuwa Mashariki

      Katika karne ya kwanza W.K., Misri ilikuwa na Wayahudi wengi zaidi, hasa katika mji wake mkuu, Aleksandria. Kituo hicho cha biashara na utamaduni kilikuwa na mamia ya maelfu ya Wayahudi, pamoja na masinagogi yaliyotawanyika katika jiji lote. Philo, Myahudi wa Aleksandria, alidai kwamba katika nchi yote ya Misri kulikuwa na Wayahudi milioni moja hivi wakati huo. Pia, Wayahudi wengi waliishi karibu na Libya, katika jiji la Kirene na maeneo jirani.

      Baadhi ya Wayahudi waliokuwa Wakristo walitoka katika maeneo hayo. Tunasoma kuhusu watu fulani waliolitegemeza kutaniko huko Antiokia ya Siria, kama vile “Apolo, mzaliwa wa Aleksandria,” “wanaume fulani wa Kipro na Kirene,” na “Lukio wa Kirene.” (Matendo 2:10; 11:19, 20; 13:1; 18:24) Hata hivyo, Biblia haisemi kuhusu kazi ya Wakristo wa karne ya kwanza katika nchi ya Misri na ujirani wake, isipokuwa jinsi mhubiri Mkristo Filipo alivyomhubiria towashi Mwethiopia.—Matendo 8:26-39.

      Eneo la Babiloni, lililotia ndani Parthia, Umedi, na Elamu, lilikuwa kituo kingine kikuu cha Wayahudi. Mwanahistoria mmoja anasema kwamba “kila eneo katika bonde la Tigri na Efrati, toka Armenia hadi ghuba ya Uajemi, na pia toka upande wa kaskazini-mashariki hadi Bahari ya Kaspiani, na toka upande wa mashariki hadi Umedi, lilikuwa na Wayahudi.” Kichapo Encyclopaedia Judaica kinakadiria hesabu yao kuwa 800,000 au zaidi. Yosefo, mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza, anatueleza kwamba Wayahudi wengi wa Babiloni walisafiri kwenda Yerusalemu kwa ajili ya sherehe za kila mwaka.

      Miongoni mwa wale waliobatizwa kwenye Pentekoste mwaka wa 33 W.K., je, kulikuwamo watu fulani waliosafiri kutoka Babiloni hadi Yerusalemu? Hatujui. Hata hivyo, kati ya wale waliomsikiliza mtume Petro siku hiyo walikuwamo watu kutoka Mesopotamia. (Matendo 2:9) Tunajua kwamba mtume Petro alikuwa Babiloni yapata mwaka wa 62-64 W.K. Alipokuwa huko, aliandika barua yake ya kwanza na inawezekana pia barua yake ya pili. (1 Petro 5:13) Ni wazi kwamba Babiloni ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya Wayahudi lilionwa kuwa sehemu ya eneo ambalo Petro, Yohana, na Yakobo waligawiwa wakati wa mkutano unaozungumziwa katika barua kwa Wagalatia.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki