-
Waovu Wataendelea Hata Lini?Mnara wa Mlinzi—2000 | Februari 1
-
-
Yehova Atenda “Tendo” Lisiloaminika
8, 9. Yehova anatenda “tendo” gani lisiloaminika?
8 Katika ono, Habakuki aona watu wa dini isiyo ya kweli, wanaomdharau Mungu. Sikiliza awaambiacho Yehova: “Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni.” Yaelekea Habakuki hajui ni kwa nini Mungu awaambia watu hao wabaya hivyo. Kisha amsikia Yehova akiwaambia: “Kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa.” (Habakuki 1:5) Kwa hakika, Yehova mwenyewe ndiye anayetenda tendo hilo wasiloweza kuamini. Lakini ni tendo gani hilo?
9 Habakuki asikiliza kwa makini maneno ya Mungu yanayofuata, yaliyorekodiwa kwenye Habakuki 1:6-11. Huu ni ujumbe wa Yehova—wala hakuna mungu asiye wa kweli wala sanamu isiyo na uhai iwezayo kuuzuia usitimizwe: “Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao. Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe. Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale. Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga. Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa. Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.”
10. Yehova awaondokesha akina nani?
10 Ni onyo la kiunabii lililoje kutoka kwa Aliye Juu Zaidi! Yehova awaondokesha Wakaldayo, taifa kali la Babiloni. Lipitapo “katikati ya dunia,” litayashinda makao mengi sana. Ni jambo lenye kuogofya kama nini! Jeshi la Wakaldayo ni lenye ‘kutisha sana na lenye kuogofya sana.’ Hilo hujitungia sheria zisizobadilika. ‘Hukumu yao hutoka katika nafsi zao wenyewe.’
11. Ungefafanuaje kuja kwa majeshi ya Babiloni dhidi ya Yuda?
11 Farasi za Babiloni ni wepesi kuliko chui wenye kasi. Jeshi lake la wapanda-farasi ni kali kuliko mbwa-mwitu wenye njaa wawindao usiku. Likiwa na hamu kubwa ya kwenda, ‘huitapa ardhi’ kwa kukosa subira. Tokea Babiloni lililo mbali waelekea Yuda. Hivi karibuni Wakaldayo watayavamia mawindo yao, wakiruka kama tai afanyaye haraka akale mlo mtamu. Je, huo ni uvamizi tu, uporaji ufanywao na askari wachache tu? La! “Waja wote ili kufanya udhalimu,” kama vile jeshi kubwa mno likusanyikavyo ili kuharibu. Nyuso zao zikiwa zimeelekezwa kwa bidii, wapanda-farasi waelekea Yuda na Yerusalemu, wakisonga kasi kama upepo wa mashariki. Majeshi ya Babiloni yateka wafungwa wengi hivi kwamba ni kana kwamba ‘wanakusanya mateka kama mchanga.’
12. Wababiloni wana mtazamo gani, na adui huyo mwenye nguvu sana ‘anakuwa na hatia’ ya nini?
12 Jeshi la Wakaldayo lawacheka wafalme na kuwadhihaki maofisa wakuu, ambao wote hawana nguvu za kukomesha mashambulizi yake makali. “Huidharau kila ngome,” kwa kuwa ngome yoyote ile huanguka Wababiloni ‘wafanyapo chungu ya mavumbi’ na kuishambulia toka hapo. Wakati uliowekwa rasmi wa Yehova ufikapo, adui huyo mwenye kutisha ‘atapita kwa kasi kama upepo.’ Katika kushambulia Yuda na Yerusalemu, ‘atakuwa na hatia’ ya kuwadhuru watu wa Mungu. Baada ya ushindi wa kasi, kamanda Mkaldayo atajivuna hivi: ‘Nguvu zetu ni mungu wetu.’ Lakini amekosea kama nini!
-
-
Waovu Wataendelea Hata Lini?Mnara wa Mlinzi—2000 | Februari 1
-
-
[Picha katika ukurasa wa 10]
Habakuki alitabiri msiba uliopata nchi ya Yuda mikononi mwa Wababiloni
-