Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Watamani Sana Ulimwengu Wenye Haki?
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Novemba 15
    • Je, Watamani Sana Ulimwengu Wenye Haki?

      MERIKEBU ya mbao inayosafiri yenye milingoti mitatu na sitaha mbili yakaribia kingo za rasi ambayo sasa ni Cape Cod, Massachusetts, Marekani. Wafanyakazi na abiria 101 walio merikebuni wamechoka kuwa baharini kwa siku 66. Wakijitahidi kutoroka mnyanyaso wa kidini na shida ya kiuchumi, wamefanya safari ngumu kuvuka Bahari ya Atlantiki.

      Abiria wa chombo hicho, Mayflower, waonapo nchi kavu Novemba 11, 1620, macho yao yang’aa wakiwa na tumaini la mwanzo mpya. Wakitamani kuweka msingi wa ulimwengu bora zaidi, wengi wa wanaume wa kikundi hicho walio watu wazima watia sahihi Mapatano ya Mayflower. Katika mapatano hayo wakubaliana kuanzisha “sheria za haki na usawa” kwa “manufaa ya ujumla ya koloni.” Je, ndoto yao ya kuwa na ulimwengu mnyoofu kiadili na wenye kufaa kila mtu—ulimwengu wenye haki—imepata kuwa uhalisi?

      Ingawa Mapatano yaliyotiwa sahihi ndani ya Mayflower yafikiriwa kuwa mojawapo ya mawe ya pembeni ya mfumo wa serikali ya Marekani, ukosefu wa haki ni tukio la kawaida Marekani, kama vile ulivyo ulimwenguni pote. Kwa kielelezo, fikiria mwanamume aliyepigwa risasi na polisi alipokuwa akijaribu kutoroka baada ya kumpokonya na kumpiga risasi mwenye duka fulani. Aliwashtaki polisi na jiji la New York, akalipwa mamilioni ya dola.

      Fikiria kielelezo kingine. Wanafunzi wa shule ya sheria walipokuwa wakifanya mtihani wa uwakili huko Pasadena, California, mmoja wao alipatwa na ugonjwa wa ghafula na kupoteza fahamu. Wanafunzi wawili waliokuwa karibu walimfanyia uhuishaji wa moyo na mapafu mpaka madaktari-wasaidizi walipowasili. Walitumia dakika 40 wakimsaidia huyo mwanamume. Lakini walipoomba muda wa ziada wa dakika 40 ili kumaliza mtihani, ofisa wa uwakili alikataa.

      Pia kuna lile suala la kuadhibiwa kwa sababu ya utendaji wa uhalifu. Mchanganuzi wa kiuchumi Ed Rubenstein asema hivi: “Uhalifu ulio mwingi zaidi hautokezi kamwe kukamatwa. Wengi wakamatwao hawashtakiwi. Wenye hatia wengi hufungwa kifungo cha nje. Kwa maoni ya mhalifu, adhabu itazamiwayo, ni welekeo si uhakika.” Akitumia data ya uvunjaji wa nyumba usiku, Rubenstein amalizia kwa kusema kwamba mtu awezaye kuwa mvunja-nyumba usiku “ataponyoka kifungo kwa zaidi ya asimilia 98 ya pindi zote afanyapo hivyo.” Ile hatari ya kuadhibiwa yenye kiwango cha chini huongoza kwenye uhalifu zaidi na kwenye wahasiriwa zaidi wa uhalifu.—Mhubiri 8:11.

      Katika nchi nyingi wachache walio matajiri hufuliza kuwa matajiri zaidi huku matungamano ya maskini yakikabili ukosefu wa haki kiuchumi. Ukosefu huo wa haki huenea wakati ambapo watu wana fursa ndogo ya kuboresha hali yao au hata ya kujitegemeza kwa sababu ya rangi ya ngozi yao, au malezi ya kikabila, lugha, jinsia, au dini. Kwa kielelezo, kulingana na gazeti la The New York Times, “karibu robo ya wanadamu bilioni moja huko Asia Kusini iliyo na Wahindu wengi—wengi wao wakiwa India na Nepal—huzaliwa na kufa wakiwa jamii ya Wahindi wa tabaka la chini kabisa.” Tokeo ni kwamba mamilioni hukumbwa na umaskini, njaa, na maradhi. Ukosefu wa haki huwapata tangu wazaliwe hadi kufa.

      Namna gani ule uonekanao kuwa ukosefu mbalimbali wa haki ambao umepita udhibiti wa kibinadamu? Fikiria watoto wachanga ambao huzaliwa wakiwa na kasoro—wakiwa vipofu, wamevia, au wenye kasoro za umbo. Je, mwanamke hangekuwa na hisi ya ukosefu wa haki ikiwa mtoto wake mchanga angezaliwa akiwa kiwete au akiwa mfu huku wanawake walio karibu wakikumbatia vitoto vichanga vyenye afya?

      Kwa kusikitisha, ukosefu wa haki wazidi, na ndivyo na matokeo yake—kuteseka sana na ukosefu wa amani, shangwe, na uradhi. Kwa kukasirishwa na ukosefu wa haki ambao wao hushuhudia au kupatwa nao, watu wengi wameishia kufanya ujeuri, wakizidisha tu kuteseka kwa kibinadamu. Vita vingi vimepiganwa kwa sababu ya ukosefu wa haki wenye kuhisiwa.

      Kwa nini mwanadamu ameshindwa kuleta ulimwengu wenye haki? Je, ulimwengu wa namna hiyo ni ndoto tu?

  • Ulimwengu Wenye Haki Si Ndoto!
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Novemba 15
    • Kwa Nini Mwanadamu Ameshindwa?

      Sababu ya msingi ya kushindwa kupata ulimwengu wenye haki ni lile waa ambalo tumerithi kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa. Biblia hueleza hivi: “Kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi.” (Waroma 5:12) Hilo waa ni dhambi. Ingawa waliumbwa wakiwa wakamilifu, Adamu na Hawa waliamua kuasi dhidi ya Mungu na hivyo wakajifanya watenda-dhambi. (Mwanzo 2:16, 17; 3:1-6) Kwa sababu hiyo, waliwaachia watoto wao mielekeo yenye dhambi na yenye kosa.

      Je, vitabia vya utu kama vile pupa na ubaguzi si matokeo ya mielekeo yenye dhambi? Na je, vitabia hivyo havichangii ukosefu wa haki ulimwenguni? Naam, pupa ndio mzizi wa kutumia mazingira vibaya kimakusudi na wa kuonea kiuchumi! Bila shaka ubaguzi ndio usababishao zogo la kikabila na ukosefu wa haki wa kijamii. Vitabia kama hivyo pia hushawishi watu wapokonye, wadanganye, na kutenda katika njia ambayo huwadhuru wengine.

      Mara nyingi hata jitihada zenye nia nzuri za kutumia haki na kufanya mema hushindwa kwa sababu ya mielekeo yetu yenye dhambi. Mtume Paulo mwenyewe aliungama hivi: “Lile jema nitakalo silifanyi, bali lile baya nisilotaka ndilo nazoea kulifanya.” Aendelea kueleza hilo shindano, kwa kusema hivi: “Napendezwa na sheria ya Mungu kulingana na mtu niliye kwa ndani, lakini mimi naona katika viungo vyangu sheria nyingine ikifanya vita dhidi ya sheria ya akili yangu na kunichukua mateka kwa sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.” (Waroma 7:19-23) Yaelekea, sisi leo tuna pambano hilohilo. Hiyo ndiyo sababu ukosefu wa haki hutokea mara nyingi sana.

      Njia ya kibinadamu ya kutawala pia imechangia ukosefu wa haki ulimwenguni. Katika kila nchi, kuna sheria na vilevile wale ambao huzitekeleza. Na bila shaka, kuna mahakimu na mahakama mbalimbali. Hakika, watu fulani wenye kanuni wamejaribu kutegemeza haki za kibinadamu na kuhakikisha kwamba kuna haki iliyo sawa kwa wote. Na bado, jitihada zao zilizo nyingi zimeshindwa. Kwa nini? Akitoa muhtasari wa mambo mbalimbali yenye kuhusika katika kushindwa kwao, Yeremia 10:23 hutaja hivi: “Ee BWANA, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” Akiwa amefarakana na Mungu, mwanadamu hawezi kuanzisha ulimwengu wenye uadilifu na wenye haki waziwazi.—Mithali 14:12; Mhubiri 8:9.

      Kizuizi kikubwa kwa jitihada za mwanadamu za kujenga ulimwengu wenye haki ni Shetani Ibilisi. Biblia hutaarifu waziwazi kwamba yule malaika mwasi Shetani ndiye “muua-binadamu” na “mwongo” wa awali na kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu ya mwovu.” (Yohana 8:44; 1 Yohana 5:19) Mtume Paulo humtambulisha kuwa “mungu wa huu mfumo wa mambo.” (2 Wakorintho 4:3, 4) Akiwa mchukiaji wa uadilifu, Shetani hufanya lolote awezalo ili kuendeleza uovu. Maadamu yeye huongoza ulimwengu, ukosefu wa haki wa namna zote na ole zitokanazo na huo zitawafanya wanadamu kuwa watumwa.

      Je, hayo yote humaanisha kwamba ukosefu wa haki ni jambo lisiloepukika katika jamii ya kibinadamu? Je, ulimwengu wenye haki ni ndoto isiyoweza kuwa kweli?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki