Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Krismasi Katika Mashariki
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Desemba 15
    • Krismasi Katika Mashariki

      • MIAKA IPATAYO MIA MBILI ILIYOPITA, msomi maarufu kutoka Korea alizuru Peking, China. Akikazia macho mchoro uliokuwa kwenye dari la kanisa moja, aliona Maria akiwa amemshika mtoto Yesu mikononi mwake. Yeye alisema hivi kuhusu mchoro huo wenye kushtua:

      “Mwanamke fulani alikuwa amemshika mapajani mtoto mwenye umri wa miaka mitano au sita hivi, aliyeonekana mgonjwa. Inaonekana mwanamke huyo hakuwa na nguvu za kuinua kichwa, kana kwamba alimsikitikia mwanaye asiweze kumtazama. Na kule-e-e nyuma yao, kulikuweko mizuka mingi na watoto wenye mabawa walioruka kuwazunguka. Nilipowakazia macho wakiwa juu yangu, walionekana kana kwamba wangeniangukia wakati wowote. Kwa kushtuka, nikanyosha mkono wangu niwashike.”

      JAMBO hilo lilitukia muda mrefu baada ya kuanza kwa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini huko Ulaya, muda mrefu baada ya kipindi cha giza cha Enzi za Kati. Lakini watu wengi wa nchi za Mashariki waliuona Ukristo kuwa jambo geni kama vile mchoro wenyewe. Hali hiyo imebadilika jinsi gani! Mandhari ya mtoto Yesu huonyeshwa kila msimu wa Krismasi. Nchi za Mashariki zimezoea mandhari hiyo, na sasa barabara nyingi huko hupambwa kama zile za Ulaya.

      Jioni ya Novemba 25, 1998, mwezi mmoja kabla ya Krismasi, barabara ya Champs Élysées jijini Paris huangazwa kwa taa zaidi ya 100,000 kwenye miti 300 kandokando ya barabara hiyo maarufu. Hali kadhalika, kwenye barabara iliyoko eneo la biashara la jiji la Seoul, Korea, mti mkubwa mno wa Krismasi unaonyeshwa kwenye duka moja kubwa na unaanza kuangaza usiku katika jiji hilo kuu. Upesi barabara zake zinapambwa kwa mapambo ya Krismasi.

      Televisheni, redio, na magazeti yanatangaza habari zinazohusiana na Krismasi siku baada ya siku. Kwa kuchochewa na shamrashamra hizo za Krismasi, nchi nzima inaanza kukaribisha mwisho wa mwaka. Makanisa huko Seoul, ambayo idadi yake yawashangaza wageni wengi, yanapambwa haraka-haraka. Hivyo, Korea na nchi nyinginezo katika Mashariki zinaanza shamrashamra za Krismasi yapata wakati ule ambapo Marekani husherehekea Sikukuu ya Kushukuru mwishoni mwa mwezi wa Novemba.

      Nchi nyingi za Mashariki hazionwi kuwa sehemu ya Jumuiya ya Wakristo. Kwa mfano, asilimia 26.3 tu ya watu katika Korea ndio hudai kuwa Wakristo. Asilimia 7.9 katika Hong Kong, asilimia 7.4 katika Taiwan, na asilimia 1.2 pekee katika Japani. Ni wazi kwamba watu wengi wa nchi za Mashariki si Wakristo, lakini hawapingi kusherehekea Krismasi. Kwa kweli, mara nyingi wao huonekana kuifurahia zaidi kuliko wenzao wa nchi za Magharibi. Kwa mfano, Hong Kong yajulikana sana kwa sherehe za Krismasi zenye madoido, hata ingawa wengi wa wakazi wake ni Wabuddha au wafuasi wa dini ya Tao. Hata katika China, ambako asilimia 0.1 ya watu ndio hudai kuwa Wakristo, wanaosherehekea Krismasi wanazidi kuongezeka haraka sana.

      Kwa nini Krismasi husherehekewa sana hivyo katika Mashariki? Kwa nini watu wasiomkubali Yesu kuwa Mesiya wanasherehekea Krismasi, ambayo wengi wanaojidai kuwa Wakristo huiona kuwa siku ya Yesu ya kuzaliwa? Je, Wakristo wa kweli waige maoni ya watu hao kuhusu Krismasi? Tutapata majibu tunapochunguza namna Krismasi ilivyopata kupendwa sana katika Korea, nchi ya kale ya Mashariki.

  • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Desemba 15
    • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?

      KUNA imani ya zamani katika Mashariki inayotukumbusha Baba Krismasi. Hiyo ni imani ya Wakorea katika mungu aitwaye Chowangshin, na baadhi ya Wachina na Wajapani wana imani kama hiyo.

      Chowangshin alionwa kuwa mungu aliyesimamia mambo ya jikoni, mungu wa moto aliyehusiana na ibada ya kale ya moto ya Wakorea. (Zamani za kale, Wakorea walibeba kwa uangalifu makaa yenye kuwaka, wakihakikisha kwamba hayakuzimika.) Iliaminika kwamba mungu huyo alichunguza mwenendo wa washiriki wa familia kwa mwaka mmoja, kisha akapaa mbinguni kupitia meko na dohani ya jikoni.

      Inadhaniwa kwamba Chowangshin alipiga ripoti kwa mfalme wa mbinguni tarehe 23 mwezi-luna wa Desemba. Alitarajiwa kurudi mwishoni mwa mwaka kupitia dohani na meko, akileta zawadi na adhabu kulingana na mwenendo wa kila mmoja. Siku aliporudi, washiriki wa familia walipaswa kuwasha mishumaa jikoni na penginepo katika nyumba. Picha za mungu huyo wa jikoni zinafanana na Baba Krismasi kwa njia nyingine—alionyeshwa akiwa na nguo nyekundu! Ilikuwa ni desturi kwa binti-mkwe kushona soksi nyekundu kulingana na utamaduni wa Wakorea, na kumpa mama-mkwe wake mwanzoni mwa majira ya baridi kali. Alifanya hivyo ili kuonyesha kwamba alitaka mama-mkwe aishi muda mrefu, kwa kuwa siku zinakuwa ndefu zaidi baada ya tarehe hiyo.

      Je, huoni ufanani fulani kati ya mambo ambayo tayari yametajwa na Krismasi? Kuna hadithi na desturi zinazofanana: dohani, mishumaa, kupeana zawadi, soksi, mzee mwenye nguo nyekundu, na tarehe. Hata hivyo, si mambo hayo yenye kufanana pekee ambayo yamefanya Krismasi ikubaliwe kwa urahisi nchini Korea. Imani katika Chowangshin ilikuwa karibu kutoweka kabisa wakati Krismasi ilipoanza kusherehekewa nchini Korea. Kwa kweli, leo Wakorea wengi hawajui kwamba imani kama hiyo ilikuwako.

      Hata hivyo, jambo hilo laonyesha jinsi desturi zinazohusiana na mwanzo wa baridi kali na mwisho wa mwaka zilivyoenea kwa njia mbalimbali ulimwenguni kote. Katika karne ya nne W.K., kanisa mashuhuri katika Milki ya Roma lilibadili jina la Saturnalia, msherehekeo wa kipagani wa Roma wa kuzaliwa kwa mungu-jua, na kuufanya sehemu ya Krismasi. Sherehe ya Krismasi ilifufua tu desturi za Korea zikiwa na jina tofauti. Jambo hilo liliwezekanaje?

      Fungu la Kupeana Zawadi

      Desturi ya kutoa zawadi haikutoweka kamwe. Kwa muda mrefu, Wakorea wamefurahia kupeana zawadi. Hiyo ikawa sababu moja iliyofanya sherehe ya Krismasi ipendwe sana Korea.

      Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, wanajeshi wa Marekani nchini Korea, ambao walitaka kuimarisha uhusiano wao na watu, walikutana makanisani ili kuwapa zawadi na misaada. Walifanya hivyo hasa Siku ya Krismasi. Watoto wengi walienda makanisani kwa sababu ya udadisi tu, na huko wakapewa zawadi za chokoleti kwa mara ya kwanza. Kama uwezavyo kuona, wengi wao walikuwa wakitazamia kwa hamu Krismasi iliyofuata.

      Kwa watoto kama hao, Baba Krismasi alikuwa mwanajeshi Mmarekani aliyevaa kofia nyekundu. Andiko la Mithali 19:6 lasema: “Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.” Naam, kupeana zawadi kukawa na matokeo mazuri. Lakini kama uwezavyo kuona kutokana na mstari huo, zawadi kama hizo si uhakikisho wa urafiki wenye kudumu. Hata nchini Korea, watu wengi walienda kanisa walipokuwa wadogo ili kula chokoleti tu. Lakini hawakusahau Krismasi. Pamoja na ukuzi wa haraka wa uchumi wa Korea, biashara pia ilikua, na kupeana zawadi wakati wa Krismasi kukawa njia rahisi ya kuongeza uuzaji wa bidhaa. Biashara zilitumia Krismasi vibaya ili kuongeza faida.

      Mambo hayo yanakupa ufahamu wa kindani kuhusu Krismasi katika nchi za Mashariki leo. Bidhaa nyingi hutengenezwa zikikusudiwa kuuzwa wakati wa zile shamrashamra za Krismasi. Mipango ya matangazo ya bidhaa huanza katikati ya msimu wa kiangazi. Uuzaji hufikia upeo mwishoni mwa mwaka, kutokana na ununuzi wa zawadi za Krismasi, kadi, na rekodi za muziki. Kwani matangazo ya bidhaa yanaweza kufanya kijana wa kawaida ahuzunike ikiwa yeye anakaa nyumbani asipokee zawadi zozote katika Mkesha wa Krismasi!

      Siku ya Krismasi ikaribiapo, watu hujazana madukani jijini Seoul wakinunua zawadi, na hivyo ndivyo inavyokuwa katika majiji mengine ya Mashariki. Kuna msongamano wa magari. Wateja humiminika kwenye hoteli, maeneo ya biashara, mikahawa, na klabu za usiku. Sherehe zenye kelele za ulevi—kuimba kwa sauti kubwa—huweza kusikika. Katika Mkesha wa Krismasi, hata wanaume na wanawake walevi huonekana wakitembea kwenye barabara zilizojaa takataka.

      Hivyo ndivyo Krismasi inavyokuwa. Krismasi katika nchi za Mashariki haisherehekewi tu na wale wanaodai kuwa Wakristo peke yao. Ni wazi kwamba nchini Korea kama kwingineko, biashara ndizo hunufaika zaidi kutokana na sikukuu hiyo ya Jumuiya ya Wakristo. Je, ni biashara pekee inayofanya Krismasi kuwa tofauti kabisa na roho ya Kristo? Wakristo wa kweli wapaswa kuchunguza zaidi suala hili zito linalohusika.

  • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Desemba 15
    • Duka moja katika eneo la biashara la Seoul, ambalo huuza chupi pekee, lilizungumziwa kwenye habari za televisheni kwa kuonyesha kwenye madirisha yake mti wa Krismasi ukiwa umepambwa kwa chupi pekee. Shamrashamra za Krismasi zilikuwa dhahiri, lakini hakukuwepo ishara yoyote ya kumkaribisha Kristo.

  • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?
    Mnara wa Mlinzi—1999 | Desemba 15
    • Picha katika ukurasa wa 7]

      Mkesha wa Krismasi katika eneo la biashara la Seoul, Korea

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki