-
Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
Ubongo Hauna Kifani kwa Stadi za Kuwasiliana
Sehemu nyinginezo za ubongo pia huchangia kuwa kwetu viumbe vya kipekee. Nyuma ya utando wa sehemu ya mbele ya bongo kubwa kuna ukanda unaovuka juu ya ubongo—ule utando unaoongoza miendo ya misuli. Huo una mabilioni ya chembe za neva ambazo zimeunganishwa kwa misuli yetu. Pia una sehemu mbalimbali zinazofanya tuwe tofauti kabisa na nyani au wanyama wengine. Utando mkuu wa kuongoza miendo ya misuli hutupatia “(1) uwezo bora sana wa kutumia mikono, vidole, na kidole gumba ili kutimiza mambo yanayohitaji ustadi sana, na (2) matumizi ya kinywa, midomo, ulimi, na misuli ya uso ili kuweza kuzungumza.”—Textbook of Medical Physiology cha Guyton.
Ebu fikiria kifupi jinsi utando huo wa kudhibiti miendo ya misuli unavyohusiana na uwezo wako wa kuzungumza. Zaidi ya nusu ya sehemu hiyo hudhibiti viungo vya mawasiliano pekee. Jambo hili lasaidia kuelewa sababu inayofanya wanadamu wawe na stadi zisizo na kifani za kuwasiliana. Ingawa mikono yetu inatimiza fungu kubwa katika kuwasiliana (katika maandishi, ishara za kawaida, au lugha ya ishara), mara nyingi mdomo huchangia sehemu kubwa sana. Usemi wa mwanadamu—tokea neno la kwanza la mtoto mchanga hadi sauti ya mtu aliye mzee kwa umri—ni ajabu sana isiyotilika shaka. Misuli ipatayo 100 iliyo katika ulimi, midomo, utaya, koo, na kifua hushirikiana ili kutokeza sauti mbalimbali. Ebu tazama tofauti hii: Chembe moja ya ubongo inaweza kuongoza nyuzi 2,000 zilizo katika msuli mmoja wa shavu la mguu la mwanariadha lakini chembe za ubongo zenye kuongoza zoloto zaweza kuongoza nyuzi 2 tu au 3 za msuli. Je, hilo halidokezi kwamba ubongo wetu umeandaliwa kwa njia ya kipekee kwa ajili ya mawasiliano?
Kila fungu la maneno mafupi ambayo wewe hutamka huhitaji mwendo fulani hususa wa misuli. Maana ya neno moja yaweza kubadilika kwa kutegemea kadiri ya mwendo na kuingiliana barabara kabisa kwa misuli mingine mingi. “Kwa kawaida,” aeleza mtaalamu wa usemi Dakt. William H. Perkins, “sisi hutamka karibu sauti 14 kwa sekunde moja. Hiyo inashinda kwa mara mbili uwezo wetu wa kudhibiti ulimi, midomo, utaya au sehemu yoyote ya usemi tunapozisogeza zikiwa tofauti-tofauti. Lakini ukitumia sehemu hizo zote pamoja ili zitokeze usemi, hizo hutenda kama vidole vya mstadi wa kuchapa taipu na jinsi ambavyo vidole vya wacheza-piano hucheza. Miendo yao hutokeza mchanganyiko uliopimwa barabara.”
Ile habari hasa inayohitajika ili kuuliza tu swali rahisi, “Hujambo leo?” imehifadhiwa katika eneo fulani la sehemu ya mbele ya bongo kubwa liitwalo eneo la Broca, ambalo wengine huliona kuwa kitovu cha usemi. Mshindi wa tuzo la Nobeli aliye mwanasayansi wa ubongo, Sir John Eccles aliandika: “Hakuna eneo lolote linalolingana . . . na eneo la usemi la Broca ambalo limetambuliwa katika nyani.” Hata kama sehemu nyinginezo zinazofanana na hizo zinapatikana katika wanyama, ukweli ni kwamba wanasayansi hawawezi kuwafundisha nyani watokeze usemi ila tu sauti chache tu rahisi. Lakini, wewe unaweza kutokeza lugha yenye mambo mengi sana. Ili kufanya hivyo, unapanga maneno yako kulingana na sarufi ya lugha yako. Eneo la Broca hukusaidia kufanya hivyo, katika usemi na katika maandishi.
Bila shaka, huwezi kudhihirisha muujiza huu wa usemi ila tu uwe unafahamu angalau lugha moja na kuelewa maana ya maneno yake. Hilo lahusisha sehemu nyingine ya pekee ya ubongo wako, ambayo huitwa eneo la Wernicke. Hapa, mabilioni ya chembe za neva hutambua maana na maneno yanayozungumzwa au kuandikwa. Eneo la Wernicke hukusaidia kuelewa maneno na kufahamu yale unayoyasikia au kusoma; likikusaidia kuweza kujifunza habari na kutenda ifaavyo.
Kuna mambo mengi hata zaidi yanayohusu usemi wenye ufasaha. Kwa mfano: Kusema “Hujambo” kwaweza kutokeza maana tofauti-tofauti. Sauti yako yaonyesha ikiwa umefurahi, umesisimuka, umechoshwa, una shughuli nyingi, umekasirika, una huzuni, au unaogopa, na pia inaweza kufunua kiwango cha kihisia-moyo cha hisia hizo. Eneo jingine la ubongo wako huandaa habari za hali yako ya kihisia-moyo katika usemi wako. Kwa hiyo sehemu mbalimbali za ubongo wako huhusika unapowasiliana.
Sokwe wengine wamefunzwa kutoa ishara chache, lakini ishara hizo ni za kuomba chakula au mambo mengine ya msingi pekee. Baada ya kufundisha sokwe mawasiliano rahisi ya ishara, Dakt. David Premack alikata kauli hivi: “Lugha ya wanadamu inafedhehesha sana nadharia ya mageuzi kwa sababu hiyo [lugha] ina uwezo sana kuliko inavyoweza kufafanuliwa.”
Huenda tukajiuliza: ‘Kwa nini wanadamu wana ustadi huu wa ajabu wa kuwasilisha mawazo na hisia, wa kuulizia na kuitikia?’ Kitabu The Encyclopedia of Language and Linguistics chasema kwamba “usemi wa [wanadamu] ni wa kipekee” nacho chakiri kwamba “utafutaji wa usemi wa awali katika mawasiliano ya wanyama hausaidii kuziba lile pengo kubwa lililopo kati ya lugha [ya wanadamu] na sauti za wanyama.” Profesa Ludwig Koehler alitaja kifupi tofauti iliyopo: “Usemi wa binadamu ni siri; ni zawadi ya Mungu, na muujiza.”
Kuna tofauti kubwa kama nini kati ya jinsi nyani atumiavyo ishara na uwezo mkubwa wa lugha ya watoto! Sir John Eccles alirejezea kile ambacho wengi wetu tumeona, uwezo “udhihirishwao na hata watoto wenye umri wa miaka 3 waulizapo maswali mengi wakitaka kuelewa mambo mengi wanayoyaona.” Yeye aliongezea: “Kwa kutofautisha, nyani hawaulizi maswali.” Ndiyo, ni wanadamu pekee waulizao maswali, kutia ndani maswali kuhusu maana ya maisha.
-
-
Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 59]
Lugha na Akili
Kwa nini akili ya binadamu inashinda sana akili ya wanyama, kama vile nyani? Jambo kubwa ni uwezo wetu wa kuunganisha sauti kufanyiza maneno na kutumia maneno kufanyiza sentensi. Mtaalamu wa utendaji wa ubongo Dakt. William H. Calvin aeleza:
“Sokwe wasiofugwa hutoa karibu dazani tatu za sauti tofauti-tofauti ili kuwasilisha karibu dazani tatu za maana tofauti-tofauti. Wao waweza kurudia sauti ili kukazia maana, lakini wao hawaunganishi sauti tatu tofauti-tofauti ili kufanyiza neno jipya katika msamiati wao.
“Sisi wanadamu pia hutumia karibu dazani tatu za sauti, ambazo huitwa fonimi. Lakini ni miunganisho ya hizo ndiyo hutokeza maana: sisi huunganisha sauti zisizo na maana ili kuunda maneno yenye maana.” Dakt. Calvin alitaja kwamba “hakuna mtu ambaye ameeleza sababu ya kuwako kwa” tofauti kubwa sana kati ya “sauti moja/maana moja” ya wanyama na uwezo mkubwa wa ajabu wa mwanadamu wa kuunda maneno.
-
-
Jinsi Ulivyo Kiumbe cha Kipekee!Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 60]
Unaweza Kufanya Mengi Kuliko Kuchora Tu Vitu Visivyo na Maana
“Je, ni mwanadamu tu ambaye ana uwezo wa kuwasiliana kwa lugha? Kwa wazi ni lazima jibu litegemee kile kinachomaanishwa na ‘lugha’—kwa kuwa wanyama huwasiliana kwa njia nyingi tofauti-tofauti kama vile ishara, harufu, miito, milio na nyimbo, na hata kucheza dansi kama vile nyuki. Lakini inaonekana kwamba mbali na mwanadamu, wanyama hawana lugha yenye kufuata sarufi. Na jambo muhimu zaidi ni kwamba wanyama hawachori picha za kuwakilisha mambo wanayotaka kuwasilisha. Hawawezi kufanya chochote zaidi ya kuchora tu vitu visivyo na maana.”—Profesa R. S. na D. H. Fouts.
-