Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuishi na Kasoro ya Kujifunza
    Amkeni!—1997 | Februari 22
    • Kuishi na Kasoro ya Kujifunza

      Sehemu ya siku aipendayo sana David mwenye umri wa miaka sita ni wakati wa hadithi. Yeye hupenda kusomewa na mama yake, naye hana tatizo kukumbuka anachosikia. Lakini David ana tatizo. Hawezi kujisomea mwenyewe. Kwa hakika, kazi yoyote inayohitaji uwezo wa kuona humfadhaisha.

      Sarah yuko katika mwaka wake wa tatu shuleni, hata hivyo mwandiko wake ni wa kizembe sana isivyo kawaida. Herufi zake hufanyizwa isivyofaa, nyinginezo huandikwa kuelekea nyuma. Jambo linaloongeza hangaiko la wazazi wake ni uhakika wa kwamba Sarah hutatizika hata kuandika jina lake mwenyewe.

      Josh, tineja mchanga, hufanya vizuri katika kila somo shuleni isipokuwa hisabati. Wazo la thamani za tarakimu humfadhaisha kabisa. Kutazama tarakimu tu humfanya Josh akasirike, na anapoketi kufanya mgawo wake wa masomo ya nyumbani wa hisabati, hali yake ya moyoni huzorota kwa haraka.

      NI KASORO gani waliyo nayo David, Sarah, na Josh? Je, wao ni wavivu tu, wenye shingo ngumu, labda wenye akili ifanyayo kazi polepole? Sivyo hata kidogo. Kila mmoja wa watoto hawa ana akili ya kawaida ya kiwango kilichopita wastani. Hata hivyo, kila mmoja wao huzuiwa na kasoro fulani ya kujifunza. David ana dyslexia, neno litumiwalo kwa idadi kadhaa za matatizo ya kusoma. Tatizo la Sarah baya sana la kushindwa kuandika huitwa dysgraphia. Na kutoweza kwa Josh kufahamu mawazo ya hisabati huitwa dyscalculia. Hizi ni kasoro tatu tu za kujifunza. Kuna nyinginezo nyingi, na wataalamu fulani hukadiria kwamba zote huathiri angalau asilimia 10 ya watoto huko Marekani.

      Kufafanua Kasoro za Kujifunza

      Ni kweli, nyakati fulani vijana wengi huona kujifunza kuwa jambo gumu. Ingawa hivyo, kwa kawaida, hilo haliashirii kasoro ya kujifunza. Badala ya hivyo, huonyesha tu kwamba watoto wote wana uwezo na udhaifu tofauti-tofauti wa kujifunza. Wengine wana uwezo wenye nguvu wa kusikia; wanaweza kufahamu habari vizuri sana kwa kusikiliza. Wengine hukazia fikira sana upande wa kuona; wanajifunza vyema zaidi kwa kusoma. Hata hivyo, shuleni wanafunzi huwekwa pamoja darasani na wote wanatarajiwa kujifunza haidhuru ni njia gani ya kufundisha yatumiwa. Kwa sababu hiyo, ni jambo lisiloepukika kwamba wengine watakuwa na matatizo ya kujifunza.

      Hata hivyo, kulingana na wataalamu fulani, kuna tofauti kati ya matatizo ya kujifunza yaliyo sahili na kasoro za kujifunza. Inaelezwa kwamba matatizo ya kujifunza yaweza kutatuliwa kwa subira na jitihada. Kinyume na hilo, kasoro za kujifunza husemekana kuwa zenye kina zaidi. “Ubongo wa mtoto aliye na kasoro ya kujifunza huelekea kutambua, kuchakata, au kukumbuka aina fulani za kazi ya kiakili katika namna iliyo na kasoro,” waandika Madakt. Paul na Esther Wender.a

      Hata hivyo, kasoro ya kujifunza si lazima imaanishe kwamba mtoto ni mlemavu kiakili. Ili kueleza hili, akina Wender hufanya ulinganifu na viziwi wa namna za sauti, watu ambao hawawezi kutofautisha namna za sauti ya muziki. “Viziwi wa namna za sauti hawajaharibika ubongo na hawana kasoro yoyote na kusikia kwao,” waandika akina Wender. “Hakuna mtu awezaye kudokeza kwamba uziwi wa namna za sauti unasababishwa na uvivu, ufundishaji wa hali ya chini, au kichocheo cha hali ya chini.” Na ndivyo ilivyo na wale walio na kasoro za kujifunza, wao wasema. Mara nyingi tatizo, hukazia sehemu moja ya kujifunza.

      Hili hueleza kwa nini watoto wengi walio na kasoro za kujifunza huwa na akili ipitayo kiwango cha wastani; kwa hakika wengine wana akili sana. Ni hali hii iliyo kinyume ambayo huwatahadharisha madaktari juu ya uwezekano wa kuwapo kwa kasoro ya kujifunza. Kitabu Why Is My Child Having Trouble at School? hueleza: “Mtoto mwenye kasoro ya kujifunza hufanya kazi miaka miwili au zaidi chini ya kiwango kitarajiwacho kwa umri wake na uwezo wake wa akili uliopimwa.” Yaani, tatizo si tu kwamba mtoto huyo ana tatizo kuwa katika kiwango sawa na marika wake. Badala ya hivyo, matokeo yake hayatoshani na uwezo wake mwenyewe unaotarajiwa.

      Kuandaa Msaada Uhitajiwao

      Athari za kihisia-moyo za kasoro ya kujifunza mara nyingi huongezea tatizo hilo. Watoto wenye kasoro za kujifunza wasipofanya vyema shuleni, wao huonwa na walimu na marika, labda hata familia zao kuwa walioshindwa. Kwa kuhuzunisha, watoto wengi kama hao husitawisha kujiona vibaya ambako kwaweza kuendelea kadiri wanavyokua. Hilo ni hangaiko halali, kwa kuwa kasoro za kujifunza kwa kawaida hazitoweki.b “Kasoro za kujifunza ni kasoro za muda wote wa maisha,” aandika Dakt. Larry B. Silver. “Kasoro zilezile ambazo huzuia kusoma, kuandika, na kufanya hisabati pia zitazuia michezo na utendaji mwingineo, maisha ya familia, na kupatana na marafiki.”

      Kwa hiyo, ni muhimu kwamba watoto walio na kasoro za kujifunza wapate utegemezo wa kimzazi. “Watoto wajuao kwamba wazazi wao huwaunga mkono kwa nguvu wana msingi wa kusitawisha hisi ya kufaa na kujiheshimu,” chasema kitabu Parenting a Child With a Learning Disability.

      Lakini ili kuwa waungaji-mkono, ni lazima wazazi kwanza wachunguze hisia zao wenyewe. Wazazi fulani huhisi kuwa wana hatia, kana kwamba wanapaswa kulaumiwa kwa kadiri fulani kwa sababu ya hali ya mtoto wao. Wengine hupatwa na wasiwasi, wakihisi kushindwa na magumu yaliyo mbele yao. Maitikio yote hayo hayasaidii. Hufanya wazazi washindwe kuchukua hatua yoyote na kumzuia mtoto kupata msaada ahitajio.

      Kwa hiyo ikiwa mtaalamu mwenye ustadi aamua kwamba mtoto wako ana kasoro ya kujifunza, usikate tumaini. Kumbuka kwamba watoto walio na kasoro za kujifunza wanahitaji tu utegemezo wa ziada katika ustadi hususa wa kujifunza. Chukua wakati wa kufahamu programu yoyote ambayo huenda yapatikana katika eneo lenu kwa watoto walio na kasoro za kujifunza. Shule nyingi zina vifaa vizuri vya kushughulikia hali kama hizo kuliko zilivyokuwa miaka mingi iliyopita.

      Wataalamu hukazia kwamba wapaswa kumsifu mtoto wako kwa chochote anachotimiza, hata kiwe kidogo kadiri gani. Uwe mkarimu wa kutoa pongezi. Kwa wakati huohuo, usipuuze nidhamu. Watoto wahitaji muundo, na ndivyo ilivyo hasa na wale walio na kasoro ya kujifunza. Acha mtoto wako ajue unachotarajia, na ushikamane na viwango ulivyoweka.

      Hatimaye, jifunze kuona hali yako kwa njia halisi. Kitabu Parenting a Child With a Learning Disability hutolea hali hiyo kielezi hivi: “Wazia unakwenda kwenye mkahawa wako uupendao sana na kuitisha kipande cha nyama ya ndama. Mhudumiaji anapoweka sahani mbele yako, wagundua kwamba ni sehemu ya mbavu za kondoo. Vyote ni vyakula vitamu, lakini ulikuwa ukitarajia nyama ya ndama. Wazazi wengi wahitaji kubadili kufikiri kwao. Huenda hukuwa ukitarajia nyama ya kondoo, lakini wagundua kwamba ina ladha nzuri sana. Ndivyo ilivyo unapolea watoto walio na mahitaji ya kipekee.”

      [Maelezo ya Chini]

      a Uchunguzi fulani hudokeza kwamba kasoro za kujifunza huenda zikawa na sehemu ya tabia ya urithi au kwamba visababishi vya kimazingira, kama vile kusumishwa na madini ya risasi au dawa au alkoholi wakati wa ujauzito, huenda vikachangia. Hata hivyo, kisababishi au visababishi hususa havijulikani.

      b Katika visa fulani, watoto hudhihirisha kasoro ya kujifunza ya muda kwa sababu ukuzi wao katika sehemu fulani unachelewa. Baada ya muda, watoto hao hukua na dalili hizo hutoweka.

  • “Kaa Tuli na Ukaze Fikira!”
    Amkeni!—1997 | Februari 22
    • “Kaa Tuli na Ukaze Fikira!”

      Kuishi na Tatizo la Upungufu wa Makini Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi

      “Kwa muda wote, Jim alikuwa amesema kwamba Cal alikuwa tu mtoto aliyedekezwa na kwamba ikiwa tungemtolea—yaani ikiwa mimi ningemtolea—nidhamu ifaayo, angerekebika. Sasa daktari alikuwa akituambia kwamba halikuwa kosa langu, halikuwa kosa letu, halikuwa kosa la walimu wa Cal: kulikuwa na tatizo kweli na mwana wetu mdogo.”

      CAL ana Tatizo la Upungufu wa Makini Kutokana na Utendaji wa Kupita Kiasi (ADHD), hali ambayo hutambulishwa na ukosefu wa kuwa makini, mwenendo wa kutenda kutokana na msukumo wa ghafula, na utendaji wa kupita kiasi. Tatizo hilo hukadiriwa kuathiri kuanzia asilimia 3 hadi 5 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shuleni. “Akili zao ni kama viteua-stesheni vyenye kasoro vya televisheni,” asema mtaalamu wa kujifunza Priscilla L. Vail. “Wazo moja huongoza kwa jingine, bila muundo wala utaratibu.”

      Acheni tuzungumzie kifupi dalili tatu kuu za ADHD.

      Ukosefu wa makini: Mtoto aliye na ADHD hawezi kupuuza mambo yasiyo na maana na kukazia fikira jambo moja. Hivyo, anakengeushwa fikira kwa urahisi na mambo anayoona, sauti, na harufu zilizopo. Yeye anakaza fikira, lakini hakuna jambo fulani hususa katika mazingira yake ambalo linashika uangalifu wake. Hawezi kupambanua ni jambo gani analostahili kulikazia fikira hasa.

      Mwenendo wa msukumo wa ghafula: Mtoto aliye na ADHD hutenda kabla ya kufikiri, bila kufikiria matokeo. Yeye hudhihirisha upangaji na uamuzi wa hali ya chini, na nyakati fulani matendo yake ni hatari. “Yeye hukimbia barabarani, kupanda ushi, kisha kupanda mtini,” aandika Dakt. Paul Wender. “Likiwa tokeo yeye hupata mikato, majeraha, mikwaruzo, na ziara nyingi za kwenda kwa daktari isivyo lazima.”

      Utendaji wa kupita kiasi: Watoto wenye utendaji wa kupita kiasi huhangaika daima. Hawawezi kukaa tuli. “Hata wakiwa na umri mkubwa zaidi,” aandika Dakt. Gordon Serfontein katika kitabu chake The Hidden Handicap, “mtu akichunguza kwa makini atagundua kwamba kuna namna ya msogeo wenye kuendelea unaohusisha miguu, wayo, mikono, midomo au ulimi.”

      Hata hivyo, watoto fulani wanaokosa makini na wenye kutenda kwa msukumo wa ghafula si watendaji kupita kiasi. Tatizo lao nyakati fulani hurejezewa kuwa tu Kasoro ya Upungufu wa Makini, au ADD. Dakt. Ronald Goldberg aeleza kwamba ADD “yaweza kutokea bila utendaji wowote wa kupita kiasi. Au yaweza kutokea kwa kiwango chochote cha utendaji wa kupita kiasi—kuanzia usioonekana sana, kufikia wenye kuchukiza, hadi wenye kulemaza kabisa.”

      Ni Nini Kisababishacho ADHD?

      Kwa miaka ambayo imepita, matatizo ya kuwa makini yamelaumiwa kwa kila kitu toka ulezi mbaya hadi nuru memetevu. Sasa yafikiriwa kwamba ADHD inahusiana na vurugu katika kazi fulani za ubongo. Katika 1990 Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Kiakili ilichunguza watu wazima 25 wenye dalili za ADHD na kupata kwamba walimeng’enyusha glukosi polepole sana katika sehemu za ubongo ambazo ndizo huongoza misogeo na ukazaji fikira. Katika asilimia 40 ya visa vya ADHD, yaonekana mfanyizo wa mtu wa kijeni huchangia. Kulingana na The Hyperactive Child Book, mambo mengine yawezayo kuhusianishwa na ADHD ni utumizi wa alkoholi au dawa za kulevya na mama wakati wa ujauzito, kusumishwa kutokana na madini ya risasi, na katika visa fulani, ulaji.

      Wabalehe na Watu Wazima Walio na ADHD

      Katika miaka ya majuzi madaktari wamepata kwamba ADHD si hali ya utotoni tu. “Kwa kawaida,” asema Dakt. Larry Silver, “wazazi watamleta mtoto kutibiwa na kusema, ‘nilikuwa vivyo hivyo nilipokuwa mtoto.’ Kisha watakiri kwamba bado wana matatizo kungoja katika foleni, kukaa tuli wakati wa mikutano, kumaliza kazi.” Inaaminiwa sasa kwamba nusu hivi ya watoto wote wenye ADHD huingia katika ubalehe na utu mzima wakiwa na angalau baadhi ya dalili zao.

      Wakati wa ubalehe, wale walio na ADHD huenda wakaacha tabia ya hatari na kuwa wakosaji. “Nilikuwa nikipatwa na wasiwasi kwamba hataingia chuoni,” asema mama mmoja wa balehe aliye na ADHD. “Sasa nasali kwamba asiingie jela.” Kwamba hofu hizo zaweza kuwa halali yaonyeshwa na uchunguzi uliolinganisha vijana 103 wenye utendaji wa kupita kiasi na kikundi cha watoto 100 wasio na tatizo hilo. “Kufikia miaka yao ya mapema ya 20,” laripoti Newsweek, “watoto katika kikundi cha walio na utendaji kupita kiasi walielekea kuwa na rekodi za kufungwa maradufu, walielekea mara tano kushtakiwa kwa makosa makubwa na kufungwa gerezani mara tisa kuliko wale wengine.”

      Kwa mtu mzima, ADHD hutokeza matatizo ya kipekee. Dakt. Edna Copeland asema: “Mtoto mwenye utendaji kupita kiasi aweza kuwa mtu mzima ambaye hubadili kazi mara nyingi, kufutwa kazi mara nyingi sana, kutumia wakati katika utendaji usio na maana siku nzima na asiyeweza kutulia.” Visababishi visipofahamika, dalili hizi zaweza kuwekea ndoa mkazo. “Katika mazungumzo sahili,” asema mke wa mwanamume mmoja aliye na ADHD, “hata anaweza kukosa kusikia kila kitu nilichosema. Ni kana kwamba alikuwa mahali kwingine.”

      Bila shaka, vitabia hivi ni vya kawaida kwa watu wengi—angalau kwa kiwango fulani. “Ni lazima uulize ikiwa dalili hizo zimekuwapo sikuzote,” asema Dakt. George Dorry. Kwa kielelezo, yeye ataja kwamba ikiwa mwanamume amekuwa msahaulifu tangu apoteze kazi yake au tangu mke wake azae, hiyo si kasoro. Zaidi ya hayo, ikiwa mtu kwa kweli ana ADHD, dalili huenea—yaani, huathiri karibu kila sehemu ya maisha ya mtu. Ndivyo ilivyokuwa na Gary mwenye umri wa miaka 38, mwanamume mwenye akili sana, mwenye nishati nyingi ambaye alionekana kwamba hangeweza kumaliza kazi hata moja bila kukengeushwa. Tayari ameandikwa kazi zaidi ya mara 120. “Nilikuwa nimekubali tu kwamba singeweza kufaulu kabisa,” yeye akasema. Lakini Gary na wengine wengi—watoto, wabalehe, na watu wazima wengi—wamesaidiwa kukabiliana na ADHD. Jinsi gani?

  • Kulikabili Hilo Tatizo
    Amkeni!—1997 | Februari 22
    • Kulikabili Hilo Tatizo

      KWA miaka ambayo imepita matibabu kadhaa yametokezwa kwa ajili ya ADHD. Baadhi yayo yamekazia ulaji. Hata hivyo, uchunguzi fulani unadokeza kwamba viongezwaji vya chakula kwa kawaida havisababishi utendaji wa kupita kiasi na kwamba masuluhisho ya lishe mara nyingi hayana matokeo. Njia nyinginezo za kutibu ADHD ni dawa, kurekebisha mwenendo, na uzoezaji wa kufahamu tatizo hilo.a

      Dawa. Kwa kuwa ADHD kwa wazi huhusisha kasoro ya ubongo, dawa za kurudisha usawaziko ufaao wa kemikali zimethibitika kuwa za msaada kwa wengi.b Hata hivyo, dawa hazichukui mahali pa kujifunza. Hizo zasaidia tu mtoto akaze fikira, zikimpa msingi ambao juu yao aweza kujifunza stadi mpya.

      Watu wazima wengi wenye ADHD wamesaidiwa na dawa pia. Hata hivyo, tahadhari yafaa—kwa vijana na watu wazima—kwa kuwa dawa chochezi zitumiwazo kutibu ADHD zaweza kuraibisha.

      Kurekebisha mwenendo. ADHD ya mtoto haiondolei wazazi wajibu wa kutoa nidhamu. Ingawa huenda mtoto akawa na mahitaji ya kipekee kwa habari hii, Biblia huonya wazazi hivi: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.” (Mithali 22:6) Katika kitabu chake Your Hyperactive Child, Barbara Ingersoll ataja: “Mzazi ambaye hujiacha ashindwe na kumwacha mtoto wake mwenye utendaji wa kupita kiasi atende bila kuzuiwa hamsaidii mtoto wake. Kama tu vile mtoto yeyote, mtoto mwenye utendaji wa kupita kiasi ahitaji nidhamu yenye kuendelea yenye staha kwa mtoto akiwa mtu. Hilo lamaanisha mipaka iliyowekwa wazi na thawabu na adhabu zifaazo.”

      Kwa hiyo ni jambo la muhimu kwamba wazazi waandae kanuni thabiti. Zaidi ya hayo, kwapasa kuwa na kawaida yenye kufuatwa sana ya utendaji wa kila siku. Huenda wazazi wakataka kumpa mtoto uhuru wa kutengeneza ratiba hii, kutia ndani wakati wa mgawo wa masomo ya nyumbani, kujifunza, kuoga, na kadhalika. Kisha dumu katika kufuatia ratiba hiyo. Hakikisha kwamba kawaida ya kila siku inafuatwa. Phi Delta Kappan lataja hivi: “Madaktari, wanasaikolojia, maofisa wa shule, na walimu wana wajibu kwa mtoto na kwa wazazi wa mtoto kueleza kwamba kuainishwa ADD au ADHD hakumaanishi kwamba mtoto aweza kufanya chochote bila kutiwa nidhamu, bali badala ya hivyo kuainishwa huko ni elezo liwezalo kuongoza kwenye msaada ufaao kwa mtoto aliye na kasoro hiyo.”

      Uzoezaji wa kufahamu tatizo hilo. Hii yatia ndani kumsaidia mtoto kubadili maoni yake kujihusu na kuhusu tatizo lake. “Watu walio na kasoro ya upungufu wa makini huhisi kwamba ni ‘wasiovutia, wapumbavu, na wasiofaa kitu’ hata ingawa ni wenye kuvutia, wenye akili, na wenye moyo mzuri,” aonelea Dakt. Ronald Goldberg. Kwa hivyo, mtoto aliye na ADD au ADHD ahitaji kuwa na maoni yafaayo ya thamani yake, na ahitaji kujua kwamba matatizo yake ya kukosa makini yaweza kushughulikiwa. Hili ni muhimu hasa wakati wa ubalehe. Kufikia wakati mtoto mwenye ADHD yuko katika umri wa utineja, huenda tayari akawa amepatwa na kejeli nyingi kutoka kwa marika wake, walimu, ndugu zake, na labda hata kutoka kwa wazazi wake. Sasa yeye ahitaji kuweka miradi ya kihalisi na kujichanganua istahilivyo badala ya kujiona kuwa mbaya.

      Njia za matibabu zilizo juu zaweza pia kufuatiwa na watu wazima walio na ADHD. “Marekebisho ni ya muhimu yakitegemea umri,” aandika Dakt. Goldberg, “lakini misingi ya matibabu—dawa mahali pafaapo, kurekebisha mwenendo, na [mazoezi ya] kufahamu tatizo hilo—hubaki ikiwa njia zifaazo kwa muda wote wa maisha.”

      Kuandaa Utegemezo

      John, baba ya balehe aliye na ADHD, awaambia wazazi walio katika hali kama hiyo: “Jifunze yote uwezayo kuhusu tatizo hili. Fanya maamuzi yategemeayo ujuzi. Juu ya yote, mpende mtoto wako, msaidie akuze kujiheshimu. Kutojiheshimu kutaangamiza mtazamo wake.”

      Ili mtoto aliye na ADHD apate utegemezo wa kutosha, ni lazima wazazi wote wawili washirikiane. Dakt. Gordon Serfontein aandika kwamba mtoto aliye na ADHD ahitaji “kujua kwamba anapendwa nyumbani na kwamba upendo huo hutoka kwa upendo uliopo kati ya wazazi.” (Italiki ni zetu.) Kwa kuhuzunisha, upendo huo haudhihirishwi sikuzote. Dakt. Serfontein aendelea: “Imehakikishwa kwamba katika familia ambapo kuna [mtoto mwenye ADHD], kuna karibu asilimia 33 ya tukio la mgawanyiko na mvunjiko wa ndoa kuliko katika familia ya kawaida.” Ili kuzuia mgawanyiko huo, baba apaswa kuchangia sana katika kumlea mtoto aliye na ADHD. Daraka halipasi kuwekewa mama tu.—Waefeso 6:4; 1 Petro 3:7.

      Marafiki wa karibu, ingawa si sehemu ya familia, waweza kutoa utegemezo mkubwa sana. Jinsi gani? “Uwe mwenye fadhili,” asema John, aliyenukuliwa mapema. “Usitazame tu mambo ya nje-nje. Pata kumjua mtoto huyo. Zungumza pamoja na wazazi wake pia. Wanaendeleaje? Wanakabiliana na nini kila siku?”—Mithali 17:17.

      Washiriki wa kutaniko la Kikristo waweza kufanya mengi ili kutegemeza mtoto aliye na ADHD na vilevile wazazi. Jinsi gani? Kwa kuwa wenye mtazamo ufaao kwa matarajio yao. (Wafilipi 4:5) Nyakati fulani, mtoto aliye na ADHD huenda akawa mwenye kusumbua. Badala ya kusema bila kuwa na hisia, “Kwa nini huwezi kumdhibiti mtoto wako?” au “Kwa nini humtii nidhamu?” mwamini mwenzi mwenye kufikiri atatambua kwamba huenda tayari wazazi wamelemezwa na kazi ngumu ya kila siku ya kumlea mtoto aliye na ADHD. Bila shaka, wazazi wapaswa kufanya kila wawezalo ili kuwekea mipaka mwenendo wenye kusumbua wa mtoto huyo. Hata hivyo, badala ya kushambulia kwa maneno ya hasira, wale wenye uhusiano katika imani wapaswa kujaribu kuonyesha “hisia-mwenzi” na ‘kutoa baraka.’ (1 Petro 3:8, 9) Kwa hakika, mara nyingi Mungu “hufariji wale walioshushwa chini,” kupitia waamini wenzi.—2 Wakorintho 7:5-7.

      Wanafunzi wa Biblia wanatambua kwamba kutokamilika kote kwa kibinadamu, kutia ndani matatizo ya kutoweza kujifunza na ADHD, kumerithiwa kutoka kwa mwanadamu wa kwanza, Adamu. (Waroma 5:12) Wanajua pia kwamba Muumba, Yehova, atatimiza ahadi yake ya kuleta ulimwengu mpya wenye uadilifu ambapo magonjwa yenye kuhuzunisha hayatakuwapo tena. (Isaya 33:24; Ufunuo 21:1-4) Hakikisho hilo ni nanga ya utegemezo kwa wale wenye matatizo kama vile ADHD. “Umri, mazoezi, na yaliyoonwa yanamsaidia mtoto wetu kufahamu na kushughulikia tatizo lake,” asema John. “Lakini hatatibiwa kikamili kamwe katika mfumo huu wa mambo. Faraja yetu ya kila siku ni kwamba katika ulimwengu mpya, Yehova atarekebisha tatizo la mwana wetu na kumsaidia kufurahia maisha kikamili.”

      [Maelezo ya Chini]

      a Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Wakristo wapaswa kuwa waangalifu kwamba matibabu yoyote wanayotafuta hayapingani na kanuni za Biblia.

      b Wengine hupatwa na athari za kando kutokana na dawa, kutia ndani wasiwasi na matatizo mengineyo ya kihisia-moyo. Zaidi ya hayo, dawa chochezi zaweza kuchochea mivuto katika wagonjwa walio na matatizo ya mitetemo kama vile ugonjwa wa Tourette. Kwa hiyo dawa zapasa kutumiwa chini ya usimamizi wa daktari.

      [Sanduku katika ukurasa wa 8]

      Neno la Hadhari kwa Wazazi

      KARIBU watoto wote nyakati fulani hawakazi fikira, ni wenye kutenda kwa msukumo wa ghafula, na wenye kutenda kupita kiasi. Kuwapo kwa vitabia hivi hakuashirii sikuzote kwamba mtoto ana ADHD. Katika kitabu chake Before It’s Too Late, Dakt. Stanton E. Samenow asema: “Nimeona visa vingi mno ambapo mtoto ambaye hataki kufanya jambo fulani anaachwa kwa sababu anafikiriwa kwamba ana ulemavu fulani au hali fulani ambayo si kosa lake.”

      Dakt. Richard Bromfield pia aona uhitaji wa kuwa na hadhari. “Kwa hakika, watu fulani walio na ADHD wana tatizo katika mfumo wa neva na wanahitaji dawa,” yeye aandika. “Lakini tatizo hilo huonwa kimakosa kuwa kisababishi cha namna zote za kutenda vibaya, unafiki, upuuzaji na matatizo mengine ya jamii ambayo katika visa vingi hayahusiani hata kidogo na ADHD. Kwa hakika, ukosefu wa kanuni katika maisha ya kisasa—jeuri ya kila mahali, utumizi mbaya wa dawa za kulevya na, mambo ambayo hayatishi sana, kama vile nyumba ambamo hakuna nidhamu na zenye fujo—waweza kusitawisha ukosefu wa utulivu kama ule wa ADHD kuliko upungufu wowote ule wa kiakili.”

      Kwa hiyo ni kwa sababu nzuri kwamba Dakt. Ronald Goldberg aonya dhidi ya “kuona dalili tofauti-tofauti kuwa uthibitisho wa kuwapo kwa ADHD.” Yeye atoa shauri kwamba “kila udodosaji uwezekanao ufanywe ili kufikia mkataa sahihi.” Dalili zinazofanana na ADHD huenda zikaonyesha lolote la matatizo mengi ya kimwili au kihisia-moyo. Kwa hiyo usaidizi wa daktari mwenye uzoefu ni wa muhimu katika kufanya udodosaji sahihi.

      Hata ikiwa udodosaji unafanywa, wazazi wafanya vyema kupima mazuri na mabaya ya dawa zitakazotumiwa. Ritalin yaweza kuondosha dalili zisizotakwa, lakini yaweza pia kuwa na athari za kando zisizofurahisha, kama vile kukosa kupata usingizi, hangaiko lililoongezeka, na wasiwasi. Hivyo, Dakt. Richard Bromfield atahadharisha dhidi ya kumpa mtoto dawa haraka sana ili tu kumwondoshea dalili zake. “Watoto wengi sana, na watu wazima wengi zaidi, wanapewa Ritalin isivyofaa,” yeye asema. “Kutokana na uzoefu wangu, utumizi wa Ritalin hutegemea hasa uwezo wa wazazi na walimu wa kuvumilia mwenendo wa watoto. Najua kuhusu watoto ambao wamepewa ili kuwatuliza badala ya kushughulikia mahitaji yao.”

      Kwa hiyo wazazi hawapaswi kufanya haraka sana kuamua kwamba watoto wao wana ADHD au tatizo la kutoweza kujifunza. Badala ya hivyo, wanapaswa kupima uthibitisho kwa uangalifu, kwa msaada wa mtaalamu mwenye ustadi. Ikiwa yaamuliwa kwamba mtoto ana tatizo la kasoro ya kujifunza au ADHD, wazazi wapaswa kuchukua wakati kujua vyema tatizo hilo ili kwamba waweze kutenda kwa matokeo mema ya watoto wao.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki