-
Imani Yangu Ilivyonisaidia Kukabiliana na MisibaMnara wa Mlinzi—2008 | Oktoba 1
-
-
Kukabiliana na Lukemia
Miezi minane baada ya baba yangu kufa, daktari wetu aliniambia nimpeleke Saúl hospitalini kwani alikuwa akichoka sana. Baada ya uchunguzi, madaktari waliniambia kwamba Saúl alikuwa na lukemia.a
Kwa miaka miwili na nusu iliyofuata, Saúl alilazwa hospitalini mara nyingi alipokuwa akikabiliana na ugonjwa huo na matibabu ambayo madaktari walitumia wakijaribu kumtibu kwa kemikali. Miezi sita ya kwanza ya matibabu hayo, yalimfanya apate nafuu kwa miezi 18 hivi. Lakini kansa ilirudi tena na Saúl akatibiwa tena kwa kemikali kwa muda mfupi. Matibabu hayo yalimdhoofisha sana. Saúl alipata nafuu kwa muda mfupi tu na hangeweza kustahimili matibabu mengine ya kemikali. Saúl alijiweka wakfu kwa Mungu na alitaka kubatizwa na kuwa Shahidi wa Yehova, lakini alikufa baada ya kufikia umri wa miaka 17.
Mara nyingi, madaktari walipendekeza atiwe damu mishipani ili kupunguza madhara ya matibabu ya kemikali. Bila shaka, kutiwa damu mishipani hakungetibu ugonjwa. Madaktari walipogundua ana lukemia, mimi na Saúl tulihitaji kuwaambia waziwazi kwamba hatungeweza kukubali matibabu hayo, kwani tulitaka kutii sheria ya Yehova ya ‘kujiepusha na damu.’ (Matendo 15:19, 20) Mara kadhaa, Saúl alihitaji kuwasadikisha madaktari wakati sikuwepo kwamba huo ulikuwa uamuzi wake mwenyewe. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 31.)
Mwishowe, madaktari walikata kauli kwamba Saúl alikuwa mtoto mkomavu ambaye alielewa vizuri ugonjwa wake. Walikubali kuheshimu msimamo wetu na wakapendekeza matibabu yasiyohusisha damu, ingawa tulishinikizwa mara nyingi tubadili uamuzi wetu. Nilifurahi sana kumsikia Saúl akieleza msimamo wake mbele ya madaktari. Kwa wazi, alikuwa amesitawisha uhusiano wa karibu pamoja na Yehova.
Tulipogundua kwamba Saúl alikuwa na ugonjwa huo, kitabu Mkaribie Yehova kilitolewa katika kusanyiko la wilaya huko Barcelona. Kitabu hicho chenye thamani kilithibitika kuwa kama nanga iliyotuimarisha tulipokabili wakati ujao usio hakika na wenye kuogopesha. Tulipokuwa hospitalini, tulitumia wakati huo kusoma sehemu za kitabu hicho pamoja. Katika pindi nyingi ngumu ambazo tulivumilia baadaye, mara nyingi tulikumbuka habari zake. Wakati huo andiko la Isaya 41:13, lililonukuliwa mwanzoni mwa kitabu hicho, lilikuwa na maana ya pekee kwetu. Linasema: “Mimi, Yehova Mungu wako, ninaushika mkono wako wa kuume, Mwenye kukuambia, ‘Usiogope. Mimi mwenyewe nitakusaidia.’”
Imani ya Saúl Inagusa Mioyo ya Wengine
Ukomavu na mtazamo mzuri wa Saúl uliwapendeza sana madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Vall d’Hebrón. Wote waliomtunza walimpenda sana. Tangu wakati huo, mtaalamu mkuu wa damu anayeshughulika na kansa amewatibu watoto wengine Mashahidi wanaougua lukemia, na amewaheshimu sana. Anakumbuka uamuzi imara wa Saúl wa kushikilia imani yake, ujasiri wake alipokabili kifo, na mtazamo wake wenye furaha maishani. Wauguzi waliomshughulikia walimwambia Saúl kwamba alikuwa mgonjwa bora zaidi waliowahi kupata katika wodi hiyo. Walisema hakuwahi kulalamika na hakuacha ucheshi wake, hata alipokuwa karibu kufa.
Mwanasaikolojia mmoja aliniambia kwamba watoto wengi wanaopata ugonjwa usioweza kupona wakiwa na umri huo wanaasi madaktari na wazazi kwa sababu ya maumivu na kukata tamaa. Aliona kwamba Saúl hakuwa hivyo. Alishangaa kuona kwamba Saúl alikuwa mtulivu na mwenye mtazamo mzuri. Hilo lilitupatia nafasi ya kumhubiria kuhusu imani yetu.
Pia ninakumbuka jinsi Saúl alivyomsaidia Shahidi mmoja katika kutaniko letu katika njia isiyo ya moja kwa moja. Alikuwa ameshuka moyo kwa miaka sita hivi na dawa hazikuwa zimemsaidia. Alikaa hospitalini mara kadhaa usiku mzima akimtunza Saúl. Aliniambia kwamba alipendezwa sana na mtazamo wa Saúl ingawa alikuwa na lukemia. Aliona kwamba hata kama alikuwa amechoka, Saúl alijaribu kumtia moyo kila mtu aliyemtembelea. “Mfano wa Saúl ulinipa ujasiri wa kukabiliana na mshuko wa moyo,” akasema Shahidi huyo.
-
-
Imani Yangu Ilivyonisaidia Kukabiliana na MisibaMnara wa Mlinzi—2008 | Oktoba 1
-
-
a Saúl alikuwa na kansa hatari sana ya damu ambayo inaharibu chembe nyeupe za damu.
-