Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Wanadamu Sisi Ni Nani?
    Amkeni!—1998 | Juni 22
    • Wanadamu Sisi Ni Nani?

      YAONEKANA kwamba wanadamu hawajijui wao ni nani. Mwanamageuzi Richard Leakey aonelea hivi: “Kwa karne kadhaa wanafalsafa wameshughulika na hali za ubinadamu. Lakini, kwa kushangaza hakuna fasili inayokubaliwa kuwa ubinadamu.”

      Hata hivyo, Bustani ya Wanyama ya Copenhagen ilitoa maoni yake kwa ujasiri kupitia maonyesho yaliyowekwa katika jumba la kuonyeshea wanyama wa hali ya juu. Kitabu 1997 Britannica Book of the Year chaeleza hivi: “Wenzi fulani kutoka Uholanzi walihamia makao ya muda katika bustani hiyo ya wanyama wakiwa na kusudi la kuwakumbusha wageni juu ya ukoo wao wa karibu pamoja na nyani.”

      Vitabu vya marejezo huunga mkono madai hayo ya kuwa kuna ukoo wa karibu kati ya wanyama fulani na wanadamu. Kwa kielelezo, The World Book Encyclopedia, chasema hivi: ‘Binadamu pamoja na nyani, komba, tumbili, ni jumuiya ya mamalia wa hali ya juu.’

      Lakini, kwa hakika wanadamu wana tabia nyingi za kipekee ambazo hazifanani na za wanyama. Baadhi ya hizo ni upendo, dhamiri, adili, hali ya kiroho, haki, rehema, ucheshi, ubunifu, ufahamu wa wakati, kujifahamu, uthamini wa umaridadi, hangaiko kuhusu wakati ujao, uwezo wa kuongeza ujuzi katika vizazi vyote, na tumaini la kwamba kifo si mwisho wa kuwapo kwetu.

      Katika kujaribu kupatanisha tabia hizi na za wanyama, wengine hutaja saikolojia ya mageuzi, ambayo ni mchanganyiko wa mageuzi, saikolojia, na sayansi ya jamii. Je, saikolojia ya mageuzi imetuelimisha juu ya fumbo la utu wa binadamu?

      Ni Nini Kusudi la Uhai?

      “Kauli ya saikolojia ya mageuzi ni sahili,” asema mwanamageuzi Robert Wright. “Akili ya binadamu, kama kiungo chochote kile, ilibuniwa kwa kusudi la kupitisha jeni hadi kizazi kifuatacho; hisia na mawazo ambayo akili hufanyiza zaweza kueleweka kwa kutegemea kauli hii.” Yaani, kusudi letu lote maishani, linaloongozwa na jeni zetu na kuonyeshwa katika utendaji wa akili zetu, ni kuzaana.

      Kwa kweli, “mwingi wa utu wa kibinadamu,” kulingana na saikolojia ya mageuzi, “kwa ufupi ni ubinafsi unaochangiwa na jeni.” Kitabu The Moral Animal chasema hivi: “Uteuzi asilia ‘wawataka’ wanaume wafanye ngono na wanawake wengi kupindukia.” Kulingana na dhana hii ya mageuzi, chini ya hali fulani ukosefu wa adili kwa upande wa wanawake huonekana pia kuwa jambo la asili. Hata upendo wa wazazi huonekana kuwa mbinu iletwayo na jeni ili kuhakikisha kwamba uzao utasalimika. Hivyo, maoni fulani husisitiza umaana wa urithi wa kijeni katika kuhakikisha kwamba familia ya kibinadamu imeendelezwa.

      Vitabu fulani vya mwongozo sasa vimeandikwa kwa kutegemea mawazo mapya ya saikolojia ya mageuzi. Kimojawapo cha vitabu hivyo hufafanua utu wa binadamu kuwa “usio tofauti sana na utu wa sokwe au utu wa nyani.” Pia kinataarifu hivi: “Kuhusu mageuzi, . . . kuzaana ndilo jambo la maana.”

      Kwa upande mwingine, Biblia hufundisha kwamba Mungu aliwaumba wanadamu si kwa kusudi la kuzaana tu. Tuliumbwa kwa “mfano” wa Mungu, tukiwa na uwezo wa kudhihirisha sifa zake, hasa upendo, haki, hekima, na nguvu. Ukiongezea zile sifa za kipekee za wanadamu zilizotangulia kutajwa, inakuwa wazi ni kwa nini Biblia hukuza wanadamu juu ya wanyama. Kwa kweli, Biblia hufunua kwamba Mungu aliwaumba wanadamu si wakiwa na tamaa ya kuishi milele tu bali pia wakiwa na uwezo wa kufurahia kutimizwa kwa tamaa hiyo katika ulimwengu mpya wenye uadilifu utakaoletwa na Mungu.—Mwanzo 1:27, 28; Zaburi 37:9-11, 29; Mhubiri 3:11; Yohana 3:16; Ufunuo 21:3, 4.

      Tunaloamini Huathiri Maisha Zetu

      Kujua sisi ni nani hasa si jambo la kinadharia hata kidogo, kwa kuwa tunaloamini kuhusu asili zetu laweza kuathiri jinsi tunavyoishi. Mwanahistoria H. G. Wells aliandika mikataa ambayo wengi walifikia baada ya kuchapishwa kwa kitabu cha Charles Darwin Origin of Species katika mwaka wa 1859.

      “Maadili yakapotoka kabisa. . . . Imani ikazorota kabisa baada ya mwaka wa 1859. . . . Watu wenye uwezo kufikia mwishoni mwa karne ya kumi na tisa waliamini kwamba walipata uwezo kupitia ule Mng’ang’ano wa Kuishi, yaani wenye nguvu na wajanja huwakandamiza walio dhaifu na wenye kuaminika. . . . Waliamua kwamba mwanadamu ni mnyama wa kijumuiya kama mbwa-mwitu wa India wakali. . . . Ilionekana sawa kwao kwamba wenye nguvu kati ya binadamu walipaswa kukandamiza na kutiisha walio dhaifu.”

      Kwa wazi, ni muhimu kwamba tupate maoni sahihi kuhusu sisi ni nani hasa. Kwa maana, kama alivyouliza mwanamageuzi mmoja, “ikiwa Nadharia ya Darwin iliyo sahili na ya kikale . . . ilidhoofisha maadili ya ustaarabu wa Magharibi, ni nini litakalotukia wakati [saikolojia mpya ya mageuzi] itakapopata umashuhuri?”

      Kwa kuwa jambo tunaloamini kuhusu asili zetu huathiri maoni yetu ya msingi juu ya uhai na kuhusu mema na mabaya, ni muhimu kwamba tuchunguze swali hili kwa makini.

  • Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?
    Amkeni!—1998 | Juni 22
    • Je, Ni kwa Mfano wa Mungu Au wa Mnyama?

      MWANADAMU wa kwanza, Adamu, aliitwa “mwana wa Mungu.” (Luka 3:38) Hakuna mnyama yeyote ambaye amewahi kuitwa hivyo kamwe. Na Biblia huonyesha kwamba wanadamu wana mambo mengi yanayofanana na ya wanyama. Kwa kielelezo, wote wanadamu na wanyama ni nafsi. Mungu alipomwumba Adamu, “mtu akawa nafsi hai,” yasema Mwanzo 2:7. (Italiki ni zetu.) Wakorintho wa Kwanza 15:45 lakubaliana na jambo hili hivi: “Mtu wa kwanza Adamu akawa nafsi hai.” Wanadamu ni nafsi, kwa hiyo nafsi si kitu fulani kisichoonekana ambacho huendelea kuishi baada ya mwili kufa.

      Kuhusu wanyama, Mwanzo 1:24 husema hivi: “Nchi na izae kiumbe hai [“nafsi zilizo hai,” “NW”] kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake.” Kwa hiyo ingawa Biblia yawapa adhama wanadamu kwa kufunua kwamba tuliumbwa kwa mfano wa Mungu, hiyo hutukumbusha pia juu ya hali yetu ya chini, pamoja na wanyama. Na bado, kuna kitu fulani ambacho hupatikana kwa wanadamu na wanyama.

      Biblia hueleza hivi: “Kwa maana linalowatukia wanadamu linawatukia wanyama; jambo moja lawatukia; anavyokufa huyu ndivyo anavyokufa huyu . . . mwanadamu hana kitu cha kumpita mnyama . . . Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena.” Ndiyo, katika kifo mwanadamu na wanyama hufanana pia. Wote hurudi kwenye “ardhi,” “mavumbini,” mahali walipotoka.—Mhubiri 3:19, 20; Mwanzo 3:19.

      Lakini kwa nini wanadamu huhuzunishwa sana na kifo? Kwa nini sisi hutamani kuishi milele? Na kwa nini twapaswa kuwa na kusudi maishani? Kwa hakika, twatofautiana sana na wanyama!

      Mambo Ambayo Hututofautisha na Wanyama

      Je, ungefurahi kuishi maisha ambayo hayana kusudi isipokuwa kula, kulala, na kuzaana? Wazo hili hata huwasumbua wanamageuzi wenye bidii. “Mwanadamu wa kisasa mwenye elimu na ambaye ni mwagnosti na mwenye kushuku,” aandika mwanamageuzi T. Dobzhansky, “hawezi kujiepusha angalau kisiri kujiuliza yale maswali ya zamani: Je, maisha yangu yana kusudi fulani kwa kuongezea kuendelea kuishi na kuzaana? Je, ulimwengu ninaoishi una kusudi fulani?”

      Kwa kweli, kukana kuwepo kwa Muumba hakumalizi kiu ya mwanadamu ya kutaka kujua maana ya maisha. Akimnukuu mwanahistoria Arnold Toynbee, Richard Leakey aandika hivi: “Kipaji hiki cha kiroho cha [mwanadamu] humfanya ang’ang’ane daima kujipatanisha na ulimwengu ambamo amezaliwa.”

      Na bado, maswali ya msingi yadumu kuhusu utu wa binadamu, asili zetu, na hali yetu ya kiroho. Bila shaka kuna pengo kubwa kati ya mwanadamu na wanyama. Pengo hilo ni kubwa kadiri gani?

      Je, Ni Pengo Kubwa Sana Lisiloweza Kuzibwa?

      Tatizo la msingi linalokabili nadharia ya mageuzi ni lile pengo kubwa ambalo huwatenganisha wanadamu na wanyama. Kwa kweli, ni kubwa kadiri gani? Fikiria baadhi ya mambo ambayo wanamageuzi wenyewe wamesema kuhusu pengo hilo.

      Mtetezi mashuhuri wa nadharia ya mageuzi katika karne ya 19, Thomas H. Huxley, aliandika hivi: “Hakuna mtu yeyote aliye na usadikisho mwingi kunishinda juu ya ukubwa wa pengo lililoko kati ya . . . mwanadamu na mnyama . . . , kwa kuwa yeye pekee ana kipawa cha kustaajabisha cha akili na usemi wenye kueleweka [na] . . . kwa hiyo kuwa juu kana kwamba juu ya kilele cha mlima, juu ya kiwango cha wanyama wa hali ya chini.”

      Mwanamageuzi Michael C. Corballis aonelea kwamba “kuna pengo kubwa kati ya binadamu na nyani . . . ‘Ubongo wetu ni mkubwa mara tatu zaidi kuliko ule ambao tungetarajia kwa nyani atoshanaye na sisi.’” Na mtaalamu wa ubongo Richard M. Restak aeleza hivi: “Ubongo wa [binadamu] ndicho kiungo pekee kijulikanacho ulimwenguni ambacho hujaribu kujielewa chenyewe.”

      Leakey akiri hivi: “Utambuzi hutokeza utatanishi kwa wanasayansi, ambao wengine huamini kuwa hauwezi kutatuliwa. Hali ya kujitambua ambayo kila mmoja wetu anayo ni dhahiri sana hivi kwamba hiyo huonekana katika kila kitu tufikiricho na kufanya.” Pia asema hivi: “Kwa kweli lugha hutokeza pengo kati ya [wanadamu] na viumbe vingine vya ulimwengu.”

      Akitaja ajabu nyingine ya akili ya binadamu, Peter Russell aandika hivi: “Bila shaka kumbukumbu ndiyo mojawapo ya uwezo wa binadamu ulio wa maana sana. Hatungeweza kujifunza bila hiyo . . . , hakungekuwako utendaji wenye akili, hakungekuwako ukuzi wa lugha, wala sifa zozote . . . ambazo kwa kawaida hushirikishwa na wanadamu.”

      Zaidi ya hayo, hakuna mnyama yeyote ambaye huabudu. Hivyo, Edward O. Wilson aonelea hivi: “Mwelekeo wa kuwa na itikadi ya kidini ndilo jambo lenye nguvu zaidi na lililo tata zaidi katika akili ya kibinadamu na ni utu usioondoleka wa binadamu.”

      “Tabia ya binadamu hutokeza mafumbo mengine mengi ya Nadharia ya Darwin,” akiri mwanamageuzi Robert Wright. “Ucheshi na kicheko zina kusudi gani? Kwa nini watu hufanya maungamo wanapokufa? . . . Maombolezo yana kusudi gani hasa? . . . Ikiwa tayari mtu amekufa, kuomboleza kunafaaje jeni?”

      Mwanamageuzi Elaine Morgan akiri hivi: “Manne kati ya mambo yenye kujitokeza sana na yasiyoeleweka juu ya binadamu ni kama yafuatavyo: (1) kwa nini wao hutembea kwa miguu miwili? (2) kwa nini wamepoteza manyoya yao? (3) kwa nini wamekuza ubongo mkubwa? (4) kwa nini walijifunza kusema?”

      Maswali haya hujibiwaje na wanamageuzi? Morgan aeleza hivi: “Majibu ya kawaida kwa maswali haya ni kama yafuatavyo: (1) ‘Bado hatujui’; (2) ‘Bado hatujui’; (3) ‘Bado hatujui’, na (4) ‘Bado hatujui.’”

      Nadharia Isiyotegemeka

      Mwandishi wa kitabu The Lopsided Ape alisema kwamba lengo lake “lilikuwa kuandaa picha ya ujumla ya kufafanua mageuzi ya binadamu yaliyofanyika polepole. Mikataa mingi imekuwa makisio tu, ikitegemezwa hasa kwa meno, mifupa, na mawe machache ya kale.” Kwa kweli, hata nadharia ya awali ya Darwin haikubaliwi na wengi. Asema Richard Leakey: “Fasili ya Darwin juu ya namna tulivyogeuka ilitawala sayansi ya elimu ya binadamu mpaka miaka michache iliyopita, na kumbe ikawa yenye makosa.”

      Wanamageuzi wengi, kulingana na Elaine Morgan, “wamepoteza uhakika katika majibu ambayo walifikiri walijua miaka thelathini iliyopita.” Hivyo, haishangazi kwamba baadhi ya nadharia zilizoaminiwa na wanamageuzi zimeanguka.

      Matokeo ya Kuhuzunisha

      Uchunguzi fulani umepata kwamba idadi ya wanyama wa kike ambao mnyama wa kiume hujamiiana nao huhusiana na tofauti iliyoko katika ukubwa wa mwili kati ya mnyama wa kiume na wa kike. Basi, wengine wamefikia mkataa kwamba mazoea ya wanadamu ya kufanya ngono yapaswa kufanana na ya sokwe, kwa kuwa sokwe wa kiume, kama wenzao binadamu, ni wakubwa kidogo tu kuliko sokwe wa kike. Kwa hiyo wengi husababu kwamba kama sokwe, wanadamu wanapaswa kuruhusiwa wawe na zaidi ya mwenzi mmoja wa kufanya naye ngono. Na kwa kweli wengi wanao.

      Lakini jambo lionekanalo kufaulu kwa sokwe kwa kawaida limekuwa msiba kwa wanadamu. Mambo ya hakika huonyesha kuwa ngono za ovyoovyo huongoza kwenye familia zilizovunjika, utoaji-mimba, maradhi, vurugu la akili na la kihisia-moyo, wivu, ujeuri katika familia, na watoto walioachwa wanaokua bila mwongozo, ambao nao huendelea kupatwa na mambo haya yenye madhara. Ikiwa ni kweli kwamba wanadamu wana utu ulio sawa na wa wanyama, kwa nini mambo haya husababisha uchungu wa kihisia-moyo kwa wanadamu?

      Kufikiri kimageuzi hutokeza shaka juu ya utakatifu wa uhai wa kibinadamu. Ni chini ya msingi gani uhai wa kibinadamu ulivyo mtakatifu ikiwa twasema hakuna Mungu na kujiona kuwa sisi ni wanyama tu wa hali ya juu? Je, labda ni akili yetu? Ikiwa ndivyo, basi swali lililozushwa katika kitabu The Human Difference lingefaa sana: “Je, ni haki kuwaona wanadamu kuwa bora kuliko mbwa na paka eti kwa sababu tu tulifanikiwa na [mageuzi]?”

      Kadiri fasili mpya ya dhana ya kimageuzi ieneapo, “bila kuepukika itaathiri sana mawazo ya kiadili,” chasema kitabu The Moral Animal. Lakini ni adili mbaya sana ambayo hutegemea kauli ya kwamba tulifanyizwa kwa “uteuzi asilia,” ambao kuupitia, kama aelezavyo H. G. Wells “wenye nguvu na wajanja huwakandamiza walio dhaifu na wenye kuaminika.”

      La maana zaidi, nadharia nyingi za wanamageuzi ambazo zimenyofoa maadili kwa miaka iliyopita zimeshindwa na kikundi kipya cha wenye kufikiri. Lakini jambo la kuhuzunisha ni kwamba madhara ambayo nadharia hizo zimesababisha yangali yako.

      Je, Uabudu Uumbaji au Muumba?

      Mageuzi huelekeza mtu atazame chini kwa uumbaji ili kupata majibu, si juu kwa Muumba. Kwa upande mwingine, Biblia, hutuelekeza juu kwa Mungu wa kweli kwa ajili ya kanuni zetu za kiadili na kusudi letu maishani. Pia hueleza kwa nini twahitaji kung’ang’ana ili kujiepusha na ukosaji na kwa nini ni wanadamu peke yao ambao wametaabishwa sana na kifo. Zaidi ya hayo, ufafanuzi wa Biblia kuhusu kwa nini sisi huelekea kutenda lililo baya huonekana kuwa kweli katika akili na moyo wa binadamu. Twakualika uchunguze ufafanuzi huo wenye kuridhisha.

  • Kutazama Juu, Si Chini, kwa Majibu
    Amkeni!—1998 | Juni 22
    • Kutazama Juu, Si Chini, kwa Majibu

      MAGEUZI hufundisha kwamba mfululizo wa mabadiliko ulitubadilisha polepole kuwa wanyama wa hali ya juu. Kwa upande mwingine, Biblia husema kwamba tuliumbwa tukiwa wakamilifu, kwa mfano wa Mungu, lakini kwamba muda mfupi baadaye, tuliingizwa kwenye kutokamilika na mwanadamu akaanza kudhoofika.

      Wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, walianzisha hali hii mbaya walipojitafutia uhuru wa adili na kuharibu dhamiri zao kwa kutomtii Mungu kimakusudi. Ilikuwa kana kwamba waliendesha gari na wakavunja kimakusudi kingo za sheria ya Mungu na kutumbukia mahali tulipo sasa, tukiteseka kwa ugonjwa, uzee, na kifo, kwa kuongezea ubaguzi wa rangi, chuki za kidini, na vita vyenye kuogofya.—Mwanzo 2:17; 3:6, 7.

      Je, Ni Jeni za Wanyama au Ni Jeni Zenye Dosari?

      Bila shaka, Biblia haifafanui kwa njia ya kisayansi kilichopata miili mikamilifu ya Adamu na Hawa walipofanya dhambi. Biblia si kitabu cha sayansi, kama vile kijitabu cha maagizo cha mwenye kumiliki gari kisivyo kitabu cha mafundisho juu ya injini ya gari. Lakini kama vile kijitabu cha maagizo cha mwenye kuimiliki, Biblia ni sahihi; si ngano.

      Adamu na Hawa walipovunja kingo za sheria ya Mungu, viungo vyao viliharibiwa. Baada ya hapo, walianza kudhoofika polepole wakielekea kifo. Kupitia sheria za urithi, watoto wao, familia ya binadamu, walirithi kutokamilika. Hivyo, wao pia hufa.—Ayubu 14:4; Zaburi 51:5; Waroma 5:12.

      Kwa kusikitisha, urithi wetu watia ndani mwelekeo wa kufanya dhambi, ambao hujitokeza kwa njia ya ubinafsi na ukosefu wa adili. Bila shaka ngono inafaa inapowekwa mahali pake. Mungu aliwaamuru hivi wenzi wa kwanza wa kibinadamu: “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi.” (Mwanzo 1:28) Na akiwa Muumba mwenye upendo, alifanya kutimiza sheria hii kuwe jambo liletalo raha kwa mume na mke. (Mithali 5:18) Lakini kutokamilika kwa binadamu kumeongoza kwenye matumizi mabaya ya ngono. Kwa kweli, kutokamilika huathiri kila upande wa maisha zetu, kutia ndani utendaji wa akili na mwili wetu, kama tujuavyo sote.

      Lakini kutokamilika hakujaondoa hisi yetu ya adili. Kwa kweli tukitaka, twaweza kuelekeza mwendo wetu na kuepuka mitego ya maisha kwa kupinga mwelekeo wa kukengeuka ndani ya dhambi. Bila shaka, hakuna binadamu asiyekamilika awezaye kupigana na dhambi kwa mafanikio kamili, na kwa rehema Mungu hujua jambo hili.”—Zaburi 103:14; Waroma 7:21-23.

      Sababu ya Kutotaka Kufa

      Biblia pia hueleza juu ya fumbo jingine ambalo mageuzi hayaelezi kwa njia yenye kuridhisha: ile kawaida ya binadamu ya kutokubali kifo, hata ingawa kifo chaweza kuonekana kuwa kitu cha kawaida kisichoepukika.

      Kama ifunuavyo Biblia, kifo kilisababishwa na dhambi, kwa kutomtii Mungu. Kama wazazi wetu wa kwanza wangebaki watiifu, wangeishi milele, pamoja na watoto wao. Kwa kweli, Mungu alibuni akili ya kibinadamu ikiwa na tamaa ya kuishi milele. “Pia ameweka umilele ndani ya mioyo ya wanadamu,” yasema Mhubiri 3:11, kulingana na New International Version. Kwa hiyo, kuhukumiwa kwao kifo kulizusha pambano la kindani katika wanadamu, pambano la daima.

      Ili kupatanisha pambano hili la kindani na kutuliza tamaa ya asili ya kutaka kuendelea kuishi, wanadamu wamebuni itikadi za namna zote, kuanzia lile fundisho la kutokufa kwa nafsi hadi itikadi ya kuzaliwa upya katika umbo jingine. Wanasayansi wanachunguza fumbo la kuzeeka kwa kuwa wao pia wanataka kuepa kifo au angalau kukiahirisha. Wanamageuzi waatheisti hupuuza tamaa ya uhai udumuo milele kuwa udanganyifu wa mageuzi, kwa kuwa huo hupingana na maoni yao ya kwamba wanadamu ni wanyama tu wa hali ya juu. Kwa upande mwingine, taarifa ya Biblia kwamba kifo ni adui hupatana na tamaa yetu ya asili ya kutaka kuishi.—1 Wakorintho 15:26.

      Basi, je, miili yetu huonyesha kwa njia yoyote kwamba tulikusudiwa tuishi milele? Jibu ni ndiyo! Ubongo wa binadamu pekee una uthibitisho wa kushangaza wa kwamba tuliumbwa tuishi kwa muda mrefu zaidi ya tuishivyo.

      Tuliumbwa Tuishi Milele

      Ubongo una uzito wa kilogramu 1.4, na una nyuroni kati ya bilioni 10 hadi bilioni 100, na yasemekana kwamba hakuna nyuroni ambazo hufanana kabisa. Kila nyuroni yaweza kuwasiliana na nyuroni nyingine 200,000, zikifanya njia katika ubongo ziwe nyingi sana. Zaidi ya hayo, “kila nyuroni ni kompyuta ya hali ya juu sana,” lasema gazeti Scientific American.

      Ubongo hutumia kemikali nyingi ambazo huathiri namna nyuroni zinavyotenda. Na ubongo ni tata zaidi hata kuliko kompyuta yenye nguvu nyingi zaidi. “Ndani ya kila kichwa,” waandika Tony Buzan na Terence Dixon, “kuna kiungo chenye nguvu nyingi za kutisha, chenye kushikamana ambacho uwezo wake huonekana kana kwamba hauna kikomo kadiri tujifunzavyo mengi zaidi juu yake.” Wakimnukuu Profesa Pyotr Anokhin, waongezea hivi: “Bado hakuna mtu aliye hai awezaye kutumia uwezo wote wa akili yake. Ndiyo sababu hatukubali makadirio yoyote yasiyofaa juu ya mipaka ya ubongo wa binadamu. Hauna mipaka.”

      Mambo haya ya kushangaza hupingana moja kwa moja na nadharia ya mageuzi. Kwa nini mageuzi ‘yangewabunia’ watu wa hali ya chini wenye kukaa mapangoni, au hata kuwabunia watu wa kisasa walioelimika sana, kiungo kilicho na uwezo wa kutumika kwa muda wa maisha uzidio milioni mara kadhaa au hata mabilioni kadhaa? Kwa kweli, ni uhai udumuo milele tu ulio na maana! Lakini namna gani mwili wetu?

      Kitabu Repair and Renewal—Journey Through the Mind and Body chataarifu hivi: “Namna ambavyo mifupa iliyovunjika, tishu, na viungo hujiponesha kwa kweli ni muujiza. Kama tungechukua muda kufikiri juu ya jambo hili, tungetambua kwamba ile hali ya ngozi na nywele na makucha kujifanyiza upya—na vilevile sehemu nyingine za mwili—kuwa yenye kushangaza sana: Hiyo huendelea saa 24 kwa siku, mfululizo, ikitufanyiza upya kihalisi, mara nyingi katika muda wote wa maisha zetu.”

      Katika wakati wa Mungu uliowekwa, halitakuwa tatizo kwake kuendeleza kwa wakati usio dhahiri utaratibu huu wa kimuujiza wa kujifanyiza upya. Ndipo, hatimaye, “kifo kitafanywa kuwa si kitu.” (1 Wakorintho 15:26) Lakini ili tuwe wenye furaha kikweli, twahitaji zaidi ya uhai udumuo milele. Twahitaji amani—amani pamoja na Mungu na wanadamu wenzetu. Amani hiyo yaweza kupatikana tu ikiwa watu wanapendana kwa kweli.

      Ulimwengu Mpya Unaotegemea Upendo

      “Mungu ni upendo,” lasema 1 Yohana 4:8. Upendo ni wenye nguvu sana—hasa upendo wa Yehova Mungu—hivi kwamba ndiyo sababu ya msingi ambayo huweza kutufanya tutumaini kuishi milele. “Mungu aliupenda ulimwengu sana,” lasema Yohana 3:16, “hivi kwamba akatoa Mwana mzaliwa-pekee wake, ili kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele.”

      Uhai udumuo milele! Ni tazamio la kustaajabisha kama nini! Lakini kwa kuwa tumerithi dhambi, hatuna haki ya kupata uhai. “Mshahara ambao dhambi hulipa ni kifo,” Biblia husema. (Waroma 6:23) Ingawa hivyo, kwa kupendeza, upendo ulimsukuma Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, afe kwa niaba yetu. Mtume Yohana aliandika hivi kuhusu Yesu: “Huyo alitoa nafsi yake kwa ajili yetu.” (1 Yohana 3:16) Ndiyo, alitoa uhai wake mkamilifu wa kibinadamu kuwa “fidia katika kubadilishana kwa ajili ya wengi” ili kwamba sisi ambao hudhihirisha imani katika yeye tufutiwe dhambi na kufurahia uhai udumuo milele. (Mathayo 20:28) Biblia hueleza hivi: “Mungu alituma Mwana wake mzaliwa-pekee kuingia katika ulimwengu ili tuweze kupata uhai kupitia kwake.”—1 Yohana 4:9.

      Ni jinsi gani, basi, tupaswavyo kuitikia upendo ambao Mungu na Mwana wake wametuonyesha? Biblia yaendelea kusema hivi: “Wapendwa, ikiwa hivi ndivyo Mungu alivyotupenda, basi sisi wenyewe tuko chini ya wajibu kupendana.” (1 Yohana 4:11) Lazima tujifunze kupendana, kwa kuwa sifa hiyo itakuwa msingi wa ulimwengu mpya wa Mungu. Leo wengi wamethamini umuhimu wa upendo, kama vile unavyosisitizwa na Yehova Mungu katika Neno lake, Biblia.

      Kitabu Love and Its Place in Nature kilisema kwamba bila upendo “watoto huelekea kufa.” Na bado, uhitaji huo wa upendo hauishi watu wazeekapo. Mtaalamu mmoja mashuhuri wa elimu ya binadamu hata alisema kwamba upendo “huwa jambo kuu zaidi katika mahitaji yote ya kibinadamu kama vile jua lilivyo la maana zaidi katika mfumo wetu wa jua . . . Mtoto ambaye ameonyeshwa upendo huwa tofauti sana na mtoto ambaye hakuonyeshwa upendo kimwili, kifiziolojia, na kisaikolojia. Watoto wasioonyeshwa upendo hata hukua kwa njia tofauti na wale walioonyeshwa upendo.”

      Je, waweza kuwazia jinsi maisha yatakavyokuwa wakati watu wote duniani watakapopendana kikweli? Kwani, hakutakuwa na mtu yeyote kamwe atakayekuwa na ubaguzi eti kwa sababu mtu ni wa taifa tofauti, ni wa jamii tofauti, au ana rangi ya ngozi iliyo tofauti na yake! Chini ya usimamizi wa Mfalme wa Mungu aliyewekwa rasmi, Yesu Kristo, dunia itajawa na amani na upendo, katika utimizo wa Biblia wa zaburi hii iliyopuliziwa:

      “Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako . . . Atawahukumu walioonewa wa watu, atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea. . . . Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka Mto hata miisho ya dunia. Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa.”—Zaburi 72:1, 4, 7, 8, 12, 13.

      Waovu hawataruhusiwa kuishi katika ulimwengu mpya wa Mungu, kama vile inavyoahidiwa na zaburi nyingine ya Biblia: “Watenda mabaya wataharibiwa, bali wamngojao BWANA ndio watakaoirithi nchi. Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:9-11.

      Ndipo, akili na miili ya wanadamu wote watiifu, kutia ndani wale watakaoinuliwa kutoka makaburini kupitia ufufuo wa wafu, itakuwa imeponywa. Hatimaye, kila mtu atakayekuwa hai atadhihirisha kikamili mfano wa Mungu. Hatimaye lile shindano kubwa la kufanya lililo sawa litakuwa limeisha. Lile pigano kati ya kutamani kuishi na hali mbaya zilizo halisi za kisasa za kifo zitakuwa zimeisha pia! Ndiyo, hii ndiyo ahadi hakika ya Mungu wetu mwenye upendo: “Kifo hakitakuwapo tena.”—Ufunuo 21:4; Matendo 24:15.

      Kwa hiyo, usizimie kamwe katika pigano la kufanya lililo sawa. Sikiza onyo hili la upole la kimungu: “Pigana pigano bora la imani, pata mshiko imara juu ya uhai udumuo milele.” Uhai huo katika ulimwengu mpya wa Mungu ndio Biblia huuita “uhai ulio halisi.”—1 Timotheo 6:12, 19.

      Na uthamini ukweli huu unaoelezwa katika Biblia: “BWANA ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba.” Kuthamini ukweli huo ni hatua muhimu kuelekea kustahili uhai katika ulimwengu mpya wa Yehova wenye upendo na uadilifu.—Zaburi 100:3; 2 Petro 3:13.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki