Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Mei 15
    • Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani

      “NILIKUWA nimesisimuka sana usiku nilipoingia katika chumba changu cha kulala baada ya kusherehekea pamoja na wenzangu uvumbuzi wetu usiotarajiwa,” asema André Parrot, mchunguzi wa vitu vya kale kutoka Ufaransa. Mnamo Januari 1934, katika eneo la Tell Hariri, karibu na mji mdogo wa Abu Kemal, kwenye Mto Efrati huko Siria, Parrot na wenzake walivumbua sanamu yenye maandishi haya: “Lamgi-Mari, mfalme wa Mari, kuhani mkuu wa Enlil.” Walifurahia sana uvumbuzi huo.

      Hatimaye, jiji la Mari lilikuwa limepatikana!

  • Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Mei 15
    • Yalipoliharibu jiji la Mari, majeshi ya Hammurabi yaliwasaidia, bila kujua, wanahistoria na wachunguzi wa vitu vya kale wa siku hizi. Majeshi hayo yalipobomoa kuta za matofali yasiyochomwa, vifusi vilifunika majengo fulani ambayo katika sehemu nyingine yako meta tano chini ya vifusi hivyo. Hivyo, majengo hayo yakahifadhiwa. Wachunguzi hao wamevumbua mabomoko ya mahekalu, majumba ya wafalme, vitu mbalimbali vya kale, na maandishi mengi yanayoeleza kuhusu eneo hilo la kale lenye ustaarabu.

  • Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Mei 15
    • Mabomoko Hayo Yanafunua Nini?

      Watu wa Mari, sawa na watu wa sehemu nyingine za Mesopotamia, walipenda dini sana. Waliona kwamba watu wana wajibu wa kuitumikia miungu. Walitafuta kujua maoni ya miungu kabla ya kufanya maamuzi yoyote muhimu. Wachunguzi wa vitu vya kale wamepata magofu ya mahekalu sita. Mahekalu hayo yanatia ndani Hekalu la Simba (ambalo wengine hufikiri ni la Dagan, yaani, Dagoni, mungu anayetajwa katika Biblia), Ishtar, mungu wa kike wa uzazi, na pia Shamash, mungu wa jua. Mwanzoni, mahekalu hayo yalikuwa na sanamu ya mungu ambaye waabudu walimtolea sala na matoleo. Waabudu hao walitengeneza sanamu zenye kutabasamu zilizofanana nao ambazo zilionyesha jinsi walivyokaa walipotoa sala, kisha wakaziweka juu ya viti kwenye madhabahu. Waliamini kwamba sanamu hizo ziliwawakilisha na kurefusha ibada yao. Parrot anasema: “Sanamu [hizo], sawa na mshumaa unaotumiwa sana katika ibada ya Wakatoliki leo, zilimwakilisha muumini.”

      Uvumbuzi wa pekee uliofanywa kwenye mabomoko ya Tell Hariri ni kugunduliwa kwa mabaki ya jumba la mfalme, ambalo limepewa jina la Mfalme Zimri-Lim, aliyekuwa mfalme wa mwisho kuishi humo. Louis-Hugues Vincent, mchunguzi wa vitu vya kale kutoka Ufaransa, alisema jumba hilo “ndilo jengo la kale la Mashariki lililojengwa kwa ustadi mkubwa sana.” Jumba hilo lililojengwa kwenye eneo la ekari sita, lilikuwa na vyumba 300 na nyua. Hata zamani, jumba hilo lilionwa kuwa mojawapo ya maajabu ya ulimwengu. Katika kitabu chake Ancient Iraq, Georges Roux anasema: “Jumba hilo lilikuwa maarufu sana hivi kwamba Mfalme wa Ugarit, aliyeishi kwenye pwani ya Siria, alikuwa tayari kumtuma mwanawe umbali wa kilometa 600 ndani ya nchi, kusudi tu aitembelee ‘nyumba ya Zimri-Lim.’”

      Kabla ya kufika kwenye ua mkubwa, wageni waliingia katika jumba hilo la mfalme lenye ngome kupitia lango moja lenye minara. Zimri-Lim, mfalme wa mwisho wa Mari, aliketi kwenye kiti cha enzi kilichokuwa juu ya jukwaa aliposhughulikia mambo ya kijeshi, kibiashara, na kibalozi, na pia alipotoa hukumu na kupokea wageni na mabalozi. Kulikuwa na vyumba vya wageni, ambao walikaribishwa na mfalme kula na kunywa katika karamu zake kubwa. Walikula nyama ya ng’ombe iliyochomwa au kuchemshwa, nyama ya kondoo, swala, samaki, na kuku, ambazo ziliandaliwa pamoja na mchuzi uliotengenezwa kwa kitunguu saumu. Walikula pia mboga za aina mbalimbali na jibini. Baada ya mlo mkuu, wageni walikula matunda yaliyotoka tu kuchumwa, matunda yaliyokaushwa au kugandishwa kwa sukari, na keki zilizookwa katika miundo mbalimbali. Ili kukata kiu, wageni waliandaliwa pombe au divai.

      Kulikuwa na mfumo wa kudumisha usafi katika jumba la mfalme. Bafu zilizovumbuliwa zina vyoo na beseni za kuogea zilizotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa. Sakafu na sehemu za chini za kuta za bafu hizo zilipakwa lami ili kuzuia maji yasipenye. Maji machafu yaliondolewa kupitia mifereji iliyotengenezwa kwa matofali, nayo mabomba ya udongo yaliyopakwa lami ili maji yasipenye bado yanatumika sasa, miaka 3,500 hivi baadaye. Wakati wake watatu wa mfalme waliposhikwa na ugonjwa unaoweza kusababisha kifo, maagizo makali yalitolewa. Mwanamke mwenye ugonjwa huo alipaswa kutengwa kabisa na wengine. “Hakuna mtu anayepaswa kutumia kikombe chake, kula pamoja naye, au kuketi kwenye kiti chake.”

      Tunayoweza Kujifunza Kutokana na Mabamba ya Kale

      Parrot na wenzake walivumbua mabamba ya kikabari 20,000 hivi yaliyoandikwa katika lugha ya Akkad. Mabamba hayo yalitumiwa kuandika barua na mambo ya uchumi na utawala. Ni theluthi moja tu ya habari zinazopatikana kwenye mabamba hayo ambazo zimechapishwa, nazo zimechapishwa katika mabuku 28! Mabuku hayo yana umuhimu gani? Jean-Claude Margueron, msimamizi wa Tume ya Kuchunguza Vitu vya Kale vya Mari, alisema: “Kabla ya mabamba ya Mari kuvumbuliwa, tulijua mambo machache sana kuhusu historia, utamaduni, na jinsi watu walivyoishi huko Mesopotamia na Siria muda mfupi baada ya mwaka wa 2000 K.W.K. Mabamba hayo yametusaidia kuandika habari nyingi zaidi na sahihi kuhusu kipindi hicho.” Kama Parrot alivyosema, kuna “ufanani wenye kushangaza kati ya watu wanaotajwa katika mabamba hayo na yale ambayo Agano la Kale linasema kuhusu kipindi cha Wazee wa Ukoo.”

      Mabamba hayo yaliyovumbuliwa Mari pia hufafanua habari fulani katika Biblia. Kwa mfano, yanaonyesha kwamba “wakati huo lilikuwa jambo la kawaida kwa mfalme” kuchukua wake au masuria wa adui yake. Hivyo, shauri la msaliti Ahithofeli kwa Absalomu, mwana wa Mfalme Daudi kwamba alale na masuria wa babake, halikuwa jambo jipya.—2 Samweli 16:21, 22.

      Eneo la Tell Hariri limechimbuliwa mara 41 tangu mwaka wa 1933. Hata hivyo, kwa sasa ni ekari 20 tu kati ya ekari 270 za jiji la Mari ambazo zimechimbuliwa. Yaelekea vitu vingi vyenye kuvutia vitavumbuliwa huko Mari, jiji maarufu la kale la jangwani.

  • Mari—Jiji Maarufu la Kale la Jangwani
    Mnara wa Mlinzi—2005 | Mei 15
    • [Picha katika ukurasa wa 11]

      Katika maandishi haya, Mfalme Iahdun-Lim wa Mari anajigamba kuhusu kazi yake ya ujenzi

      [Picha katika ukurasa wa 11]

      Kuvumbuliwa kwa sanamu hii ya Lamgi-Mari kulisaidia kutambua mahali jiji la Mari lilipokuwa

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Ebih-Il, ofisa wa Mari, akisali

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Jukwaa katika jumba la mfalme ambapo huenda sanamu fulani ya mungu wa kike ilisimama

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Mabomoko ya Mari yanayoonyesha jengo la matofali yasiyochomwa

      [Picha katika ukurasa wa 12]

      Bafu katika jumba la mfalme

      [Picha katika ukurasa wa 13]

      Bamba linaloonyesha ushindi wa Naram-Sin dhidi ya Mari

      [Picha katika ukurasa wa 13]

      Mabamba ya kikabari 20,000 hivi yalipatikana katika mabomoko ya jumba la mfalme

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki