Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Huenda Akabadalika”
    Amkeni!—2001 | Novemba 8
    • “Huenda Akabadalika”

      ROXANAa ni mwanamke mchangamfu, mama mwenye kuvutia wa watoto wanne na mke wa daktari-mpasuaji anayeheshimiwa sana huko Amerika Kusini. Yeye asema, “mume wangu huwavutia sana wanawake na hupendwa sana na wanaume.” Hata hivyo mume huyu hutenda mambo yenye kuchukiza ambayo hata marafiki wake wa karibu hawajui. “Yeye ni mtu katili nyumbani. Ana wivu mbaya sana.”

      Roxana anaonekana mwenye woga anapoendelea kusimulia yanayompata. “Matatizo yalianza majuma machache tu baada ya kuolewa. Ndugu zangu na mama yangu walipotutembelea, nilifurahi sana kuzungumza na kucheka pamoja nao. Lakini walipoondoka, mume wangu alinibwaga kwenye sofa akiwa amepandwa na hasira kali. Sikuweza kamwe kuamini yaliyokuwa yakitendeka.”

      Huo ulikuwa mwanzo tu wa mateso ya Roxana, kwani kwa miaka mingi amepigwa sana na mume wake. Yaelekea mashambulizi hayo hufuata utaratibu fulani. Kwanza yeye humpiga, kisha anaomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena. Yeye huacha kumshambulia angalau kwa muda fulani. Halafu anaanza tena kumshambulia kwa ukatili. “Mimi hufikiri tena na tena kwamba huenda akabadilika wakati huu,” asema Roxana. “Hata nikitoroka mimi bado humrudia.”

      Roxana anahofu kwamba ukatili wa mume wake huenda ukaongezeka. Yeye asema, “alitisha kuniua, kuua watoto na kisha kujiua. Siku moja aliniwekea makasi kooni. Wakati mwingine alielekeza bunduki kwenye sikio langu na kuifyatua! Jambo zuri ni kwamba haikuwa na risasi, lakini nilishtuka, karibu nife.”

      Wameamua Kunyamaza

      Kama Roxana, mamilioni ya wanawake ulimwenguni pote wameteswa na wanaume wenye jeuri.b Wengi wao hunyamaza wakisababu kwamba hata wakiripoti mambo hayo huenda wasisaidiwe. Kwani wanaume wengi wakatili hukataa madai hayo kwa kusema “Mke wangu hubabaika-babaika tu” au “Yeye hufanya mambo madogo yaonekane kuwa makubwa mno.”

      Inasikitisha kwamba wanawake wengi wanaishi wakiwa na hofu ya kushambuliwa nyumbani, mahali ambapo wanapaswa kuhisi wakiwa salama zaidi. Tena, mara nyingi mkosaji huhurumiwa badala ya aliyekosewa. Inakuwa vigumu kwa wengi kuamini kwamba mwanamume anayeonekana kuwa raia mwenye kuheshimika anaweza kumpiga mwenzi wake. Fikiria kisa cha Anita, mwanamke aliyezungumza waziwazi kuhusu jinsi alivyotendewa kikatili na mume wake aliyeheshimiwa sana. “Mtu tunayefahamiana aliniambia hivi: ‘Unawezaje kumlaumu mwanamume huyu mwenye kuheshimiwa sana?’ Mwingine alisema kwamba haikosi mimi ndiye ninayemchokoza! Hata baada ya ukatili wa mume wangu kujulikana wazi, baadhi ya marafiki wangu walianza kuniepuka. Walihisi kwamba nilipaswa kuvumilia ‘eti kwa sababu hivyo ndivyo wanaume walivyo.’”

      Kama simulizi la Anita linavyoonyesha, wengi hawaelewi jinsi mtu anavyoweza kumtendea mwenzi wake wa ndoa kwa ukatili. Ni nini humfanya mwanamume anayedai kumpenda mke wake kuwa katili sana? Je wale wanaotendewa kwa jeuri wanaweza kusaidiwa?

  • Kwa Nini Wanaume Huwapiga Wanawake?
    Amkeni!—2001 | Novemba 8
    • Kwa Nini Wanaume Huwapiga Wanawake?

      WATAALAMU fulani wanasema kwamba wanawake wengi wanakabili hatari ya kuuawa na wenzi wao wa kiume kuliko na wahalifu wote wakijumlishwa. Uchunguzi mwingi umefanywa katika jitihada za kukomesha jeuri kati ya wenzi wa ndoa. Ni mwanamume wa aina gani humpiga mke wake? Maisha yake ya utotoni yalikuwaje? Je, alikuwa mwenye jeuri wakati wa uchumba? Mwanamume huyo amefanya maendeleo gani baada ya kutibiwa?

      Kulingana na uchunguzi wa wataalamu fulani, wanaume wanaowapiga wanawake hutofautiana. Kuna yule aliye mjeuri mara moja moja. Hatumii silaha wala hana zoea la kumpiga mwenzi wake. Kwake kutenda jeuri si jambo la kawaida na yaelekea huchochewa na watu au mambo yanayomzunguka. Kwa upande mwingine, kuna yule aliye na zoea la kumpiga mwenzi wake. Kwa mtu huyo, jeuri ni jambo la kawaida na hajuti wala kuonyesha dalili za kuacha zoea hilo.

      Hata hivyo, uhakika wa kwamba watu wanaopiga wanawake hutofautiana haimaanishi kwamba njia fulani za kuwapiga wanawake si hatari. Kwa hakika, kumtendea mtu vibaya kwa njia yoyote kunaweza kutokeza majeraha—hata kifo. Hivyo, uhakika wa kwamba mtu fulani hatendi jeuri kila wakati au si katili sana haimaanishi kwamba anakubalika. Bila shaka hakuna kupiga “kunakokubalika.” Hata hivyo, ni mambo gani humfanya mwanamume amjeruhi mwanamke ambaye aliahidi kumtunza kwa muda wote wa maisha yake?

      Athari ya Familia

      Si ajabu kwamba wanaume wengi wanaowapiga wake zao walikulia katika familia zenye jeuri. “Wengi wao walilelewa katika nyumba zilizofanana na maeneo ya vita,” aandika Michael Groetsch, ambaye kwa miaka 20 amefanya utafiti kuhusiana na jeuri kati ya wenzi wa ndoa. “Wakiwa watoto, walikulia katika mazingira hatari ambapo kutendewa vibaya kihisia-moyo na kimwili yalikuwa mambo ya ‘kawaida.’” Kulingana na mtaalamu mmoja, mwanamume aliyekulia mazingira kama hayo “anaweza kuiga chuki ya baba yake kuelekea wanawake akiwa angali mchanga sana. Mvulana huyo anajifunza kwamba ni lazima mwanamume awadhibiti wanawake kwa kuwatisha, kuwaumiza, na kuwadharau. Na wakati huohuo anajifunza kwamba, ili apate kibali cha baba yake ni lazima amwige.”

      Biblia inaonyesha wazi kwamba mwenendo wa mzazi unaweza kumwathiri mtoto kwa njia ifaayo au isiyofaa. (Mithali 22:6; Wakolosai 3:21) Bila shaka mazingira ya familia hayampi mtu sababu ya kumpiga mwenzi wake, lakini yanaweza kuonyesha chanzo cha mwenendo huo wenye jeuri.

      Athari ya Kitamaduni

      Katika nchi fulani kumpiga mwanamke ni jambo linalokubaliwa na hata la kawaida. “Jamii nyingi zinaamini sana kwamba mume ana haki ya kumpiga au kumuumiza mkewe,” yaeleza ripoti moja ya Umoja wa Mataifa.

      Hata katika nchi ambazo ukatili wa aina hii haukubaliwi, watu mmoja-mmoja hutenda kwa jeuri. Inashangaza kwamba wanaume fulani wana maoni hayo yasiyo na msingi kuelekea jambo hilo. Kulingana na gazeti la Weekly Mail and Guardian la Afrika Kusini, uchunguzi uliofanywa huko Cape Peninsula, uligundua kwamba wanaume wengi waliodai kutowatendea wake zao kwa ukatili walihisi kwamba kumpiga mwanamke kunakubaliwa na si ujeuri.

      Ni wazi kwamba maoni hayo yaliyopotoka yanaanza utotoni. Kwa mfano, kulingana na uchunguzi mmoja huko Uingereza, asilimia 75 ya wavulana wenye umri wa miaka 11 na 12 wanahisi kwamba mwanamume anaweza kumpiga mwanamke anapomkasirisha.

      Hakuna Sababu ya Kumpiga Mwenzi wa Ndoa

      Mambo yaliyotangulia kutajwa huenda yakasaidia kufafanua visababishi vya ukatili kuelekea mwenzi wa ndoa, lakini hayaonyeshi kuwa ukatili huo unakubaliwa. Kwa ufupi, kumpiga mwenzi wa ndoa ni dhambi nzito machoni pa Mungu. Katika Neno lake Biblia, twasoma: “Waume wapaswa kuwa wakiwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Yeye apendaye mke wake ajipenda mwenyewe, kwa maana hakuna mtu aliyepata wakati wowote kuuchukia mwili wake mwenyewe; bali huulisha na kuutunza sana kama vile Kristo pia alifanyiavyo kutaniko.”—Waefeso 5:28, 29.

      Biblia ilitabiri kwamba katika “siku za mwisho” za huu mfumo wa mambo, watu wengi watakuwa “wakatili,” “wasio na shauku ya asili,” na “wakali.” (2 Timotheo 3:1-3; The New English Bible) Kuongezeka kwa ukatili katika ndoa ni mmojawapo wa uthibitisho wa kwamba tunaishi katika kipindi kinachozungumziwa na unabii huo. Lakini wanaotendewa ukatili wanaweza kusaidiwaje? Je, kuna tumaini lolote kwamba wanaowatendea wengine ukatili watabadili mwenendo wao?

      [Blabu katika ukurasa wa 5]

      “Mtu anayempiga mkewe hatofautiani na mhalifu anayempiga mtu fulani.”—When Men Batter Women

      [Sanduki katika ukurasa wa 6]

      Jeuri Nyumbani Ni Tatizo Lililoenea Ulimwenguni Pote

      Ripoti ifuatayo inaonyesha kwamba “wanaume wenye kiburi, walio na mwelekeo wa ukatili kuelekea wanawake wameongezeka ulimwenguni pote.”

      Misri: Uchunguzi wa miezi mitatu uliofanywa huko Aleksandria, ulionyesha kwamba wanawake wengi sana wanajeruhiwa hasa kupitia jeuri nyumbani. Jeuri hiyo inasababisha pia asilimia 27.9 ya wanawake kwenda kutibiwa kwenye vituo vya matibabu ya dharura.—Muhtasari wa 5 wa Mkutano wa Nne Unaohusu Wanawake Ulimwenguni.

      Thailand: Asilimia 50 ya wanawake walioolewa hupigwa mara kwa mara katika kitongoji kikubwa zaidi cha Bangkok.—Shirika la Pasifiki la Kutetea Afya ya Wanawake.

      Hong Kong: “Idadi ya wanawake wanaoripoti kupigwa na wenzi wao iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 mwaka uliopita.”—Gazeti South China Morning Post la Julai 21, 2000.

      Japani: Idadi ya wanawake wanaotafuta makao iliongezeka kutoka 4,843 mwaka wa 1995 kufikia 6,340 mwaka wa 1998. “Karibu theluthi moja walisema kwamba walitafuta makao kwa sababu ya ujeuri wa waume zao.”—Gazeti The Japan Times la Septemba 10, 2000.

      Uingereza: “Kila sekunde sita, mwanamke hubakwa, hupigwa, au hushambuliwa kwa kisu katika nyumba fulani kotekote Uingereza.” Kulingana na ripoti moja ya Idara ya Uingereza ya Upelelezi wa Jinai, “kila siku polisi hupokea simu 1,300 kutoka kwa wale wanaotendewa jeuri nyumbani, yaani wanapokea zaidi ya simu 570,000 kwa mwaka. Asilimia 81 ni wanawake walioshambuliwa na wanaume.”—Gazeti The Times, la Oktoba 25, 2000.

      Peru: Asilimia 70 ya visa vyote vya uhalifu vinavyoripotiwa kwa polisi vinahusu wanawake waliopigwa na waume zao. —Shirika la Pasifiki la Kutetea Afya ya Wanawake.

      Urusi: “Katika mwaka mmoja, wanawake Warusi 14,500 waliuawa na waume zao, na wengine 56,400 walilemazwa au kujeruhiwa vibaya katika mashambulizi ya nyumbani.”—The Guardian.

      China: “Ni tatizo jipya linaloongezeka upesi hasa katika miji mikubwa,” asema Profesa Chen Yiyun, Mkurugenzi wa Kituo cha Familia cha Jinglun. “Hata uvutano wa majirani hauzuii jeuri nyumbani.”—The Guardian.

      Nikaragua: “Jeuri dhidi ya wanawake inazidi kuongezeka. Uchunguzi mmoja ulidai kwamba mwaka uliopita pekee, asilimia 52 ya wanawake wa Nikaragua waliteseka kutokana na jeuri iliyosababishwa na waume zao.”—Shirika la Habari la Uingereza.

      [Sanduku katika ukurasa wa 7]

      Visababishi vya Jeuri Nyumbani

      Kulingana na uchunguzi uliosimamiwa na Richard J. Gelles katika Chuo Kikuu cha Rhode Island, Marekani, vifuatavyo ni visababishi vya kutendewa vibaya kimwili na kihisia-moyo nyumbani.

      1. Mwanamume huyo alihusika katika jeuri nyumbani hapo awali.

      2. Hana kazi ya kuajiriwa.

      3. Anatumia dawa haramu za kulevya angalau mara moja kwa mwaka.

      4. Alipoishi na wazazi wake, aliona baba akimpiga mama yake.

      5. Wenzi hawa hawajafunga ndoa; wanaishi pamoja tu.

      6. Iwapo ameajiriwa, ana mapato ya chini.

      7. Hakupata elimu ya kutosha.

      8. Ana umri wa kati ya miaka 18 na 30.

      9. Huenda mmoja wao au wote wawili huwatendea watoto wao kwa jeuri.

      10. Ni maskini hohehahe.

      11. Mwanamume na mwanamke huyo wanatoka katika tamaduni mbalimbali.

  • Msaada kwa Wanawake Wanaopigwa
    Amkeni!—2001 | Novemba 8
    • Msaada kwa Wanawake Wanaopigwa

      WANAWAKE wanaotendwa jeuri wanaweza kusaidiwaje? Kwanza, ni lazima mtu aelewe magumu wanayokabili. Mara nyingi wale wanaowapiga wenzi wao huwaumiza kimwili na katika njia nyinginezo pia, kutia ndani kuwatisha na kuwafadhaisha kwa maneno ili kuwafanya wajihisi hoi na wasiofaa kitu.

      Mfikirie Roxana aliyezungumziwa katika makala iliyotangulia. Wakati mwingine mume wake humzomea kwa ukali. “Yeye huniita majina yenye kuaibisha,” asema Roxana. “Yeye huniambia: ‘Hata hukumaliza shule. Ungewezaje kuwatunza watoto bila msaada wangu? Wewe ni mama mvivu asiyefaa kitu. Unafikiri serikali itakuruhusu uendelee kukaa na watoto ukiniacha?’”

      Mume wa Roxana hupiga ubwana kwa kumnyima pesa. Hamruhusu kutumia gari, naye hupiga simu nyumbani kila wakati ili kujua anachofanya. Akijaribu kutoa maoni yake, mume wake humfokea kwa hasira. Roxana ameamua kunyamaza.

      Kama tuonavyo, kumtendea mwenzi wa ndoa kikatili ni suala gumu mno. Ili kuandaa msaada na kitia-moyo, sikiliza kwa fadhili. Kumbuka kwamba kwa kawaida mhasiriwa hushindwa kabisa kuzungumzia mambo yanayompata. Lengo liwe kumwimarisha mhasiriwa anapopambana na hali hiyo ngumu kadiri awezavyo.

      Baadhi ya wanawake wanaopigwa huenda wakahitaji kutafuta msaada kutoka kwa wenye mamlaka. Wakati mwingine, upeo wa mgogoro—kama vile kuwahusisha polisi—unaweza kumfanya mwanamume anayemtendea mwenzi wake kikatili kufikiria kwa uzito matendo yake. Hata hivyo, nia yao ya kutaka kubadilika hudidimia hali inapokuwa shwari.

      Je, mke anayepigwa amwache mume wake? Biblia haipendekezi kutengana kwa watu waliofunga ndoa. Na wakati huohuo haimshurutishi mwanamke kuishi na mwanamume anayehatarisha afya na hata uhai wake. Paulo, mtume Mkristo aliandika hivi: “Lakini kwa kweli akiondoka, acha akae bila kuolewa au sivyo apatane tena na mume wake.” (1 Wakorintho 7:10-16) Biblia huruhusu wenzi wa ndoa kutengana hali zinapokuwa mbaya sana, lakini ni juu ya mwanamke huyo kufanya uamuzi wake binafsi kuhusiana na jambo hilo. (Wagalatia 6:5) Hakuna anayepaswa kumshurutisha mke kumwacha mume wake, wala kumlazimisha mwanamke anayepigwa kuendelea kuishi na mwanamume katili iwapo afya yake, uhai wake na hali yake ya kiroho imo hatarini.

      Je, Wale Wanaowapiga Wenzi Wao Wanaweza Kubadilika?

      Kumtendea mwenzi wa ndoa kwa ukatili ni kukiuka kanuni za Biblia kimakusudi na moja kwa moja. Kwenye Waefeso 4:29, 31, twasoma hivi: “Msiache usemi uliooza utoke kinywani mwenu . . . . Acheni uchungu wote wenye nia ya kudhuru na hasira na hasira ya kisasi na kupiga kelele na usemi wenye kuudhi viondolewe mbali kutoka kwenu pamoja na ubaya wote.”

      Mume yeyote anayedai kuwa mfuasi wa Kristo hawezi kusema kwamba anampenda mke wake ikiwa anamtendea kikatili. Matendo yake yote mazuri yangekosa maana iwapo angemtendea vibaya mke wake. “Mpiga-watu” hastahili mapendeleo yoyote ya pekee katika kutaniko la Kikristo. (1 Timotheo 3:3; 1 Wakorintho 13:1-3) Bila shaka yeyote anayedai kuwa Mkristo ambaye mara kwa mara na bila kuomba msamaha anapandwa na hasira za ghafula anaweza kutengwa na ushirika wa kutaniko la Kikristo.—Wagalatia 5:19-21; 2 Yohana 9, 10.

      Je, wanaume waliozoea jeuri wanaweza kubadili mazoea yao? Wengine wamebadilika. Hata hivyo anayempiga mwenzi hatabadilika isipokuwa (1) akubali kwamba mwenendo wake haufai, (2) anataka kubadili mwenendo wake, na (3) atafute msaada. Mashahidi wa Yehova wanajua kwamba Biblia ina nguvu inayoweza kumbadili mtu. Wengi wanaojifunza nao Biblia, wamesitawisha tamaa ya kutaka kumpendeza Mungu. Wanafunzi hao wapya wa Biblia wanajifunza kwamba Yehova Mungu ‘humchukia yeyote anayependa jeuri.’ (Zaburi 11:5, NW) Ili yule anayempiga mwenzi wake abadili mwenendo wake anahitaji kufanya mengi mbali na kuacha kumpiga. Kunahusisha pia kuwa na mtazamo tofauti kabisa kuelekea mke wake.

      Wakati mwanamume anapopata ujuzi wa Mungu, anajifunza kumwona mke wake kama “msaidizi” wala si mtumwa wala mtu wa cheo cha chini bali kama anayestahili ‘kuheshimiwa.’ (Mwanzo 2:18; 1 Petro 3:7) Anajifunza pia kuwa mwenye huruma na kuona uhitaji wa kusikiliza maoni ya mke wake. (Mwanzo 21:12; Mhubiri 4:1) Programu ya funzo la Biblia inayoandaliwa na Mashahidi wa Yehova imesaidia wenzi wengi wa ndoa. Mtu katili, mkandamizaji au mwonevu hana sehemu katika familia ya Kikristo.—Waefeso 5:25, 28, 29.

      “Neno la Mungu liko hai na hukazia nguvu.” (Waebrania 4:12) Hivyo, hekima ya Biblia inaweza kuwasaidia wenzi wa ndoa kuchanganua na kupata kitia-moyo ili kushughulikia matatizo wanayokabili. Zaidi ya hayo, Biblia inatupatia tumaini hakika na lenye kufariji la kwamba hakutakuwa tena na jeuri ulimwenguni wakati Mfalme wa kimbingu wa Yehova atakapotawala wanadamu wote watiifu. Biblia husema: ‘Atamkomboa fukara anayemwomba, na maskini asiye na wa kumsaidia. Atawatoa katika udhalimu na ukatili.’—Zaburi 72:12, 14, Biblia Habari Njema.

      [Blabu katika ukurasa wa 12]

      Mtu katili, mkandamizaji, au mwonevu hana sehemu katika familia ya Kikristo

      [Sanduku katika ukurasa wa 8]

      Kurekebisha Maoni Yasiyofaa

      • Wake wanaopigwa hulaumiwa kwa matendo ya waume zao.

      Wanaume wengi wanaowapiga wake zao hukataa kulaumiwa kwa matendo yao wakidai eti wake zao huwakasirisha. Huenda hata baadhi ya marafiki wa familia wakakubali kwamba mke huyo ni mwenye matata na ndio sababu mume wake hukosa kujidhibiti mara kwa mara. Lakini hiyo ni sawa na kumlaumu anayepigwa na kumtetea mshambuliaji. Hata hivyo, wake wanaopigwa hujitahidi sana kuwatuliza waume zao. Zaidi ya hilo, si halali chini ya hali zozote zile mtu kumpiga mwenzi wake. Kitabu The Batterer—A Psychological Profile chasema: “Wanaume wanaopelekwa kupata matibabu kwa sababu ya kuwapiga wake zao wana zoea la jeuri. Wao hutumia jeuri kama kitulizo cha hasira na mshuko wa moyo, njia ya kujidhibiti, kutatua mzozano, na kupunguza mikazo. . . . Mara nyingi hawakubali kwamba wana tatizo, wala hawalifikirii kwa uzito.”

      • Pombe humfanya mtu ampige mke wake.

      Ni kweli kwamba wanaume wengine hutenda kwa jeuri baada ya kunywa pombe. Lakini je, ni jambo la busara kuilaumu pombe? “Badala ya kujilaumu mwenyewe kwa mwenendo wake, mlevi hupata kitu cha kusingizia,” aandika K. J. Wilson katika kitabu chake When Violence Begins at Home. Yeye aendelea kusema: “Yaelekea jamii yetu inapuuza jeuri inayotokea nyumbani iwapo inasababishwa na mlevi.” Mwanamke anayetendewa kikatili huenda akapuuza kuwa mwenzi wake ni katili, na kumwona kama mtu anayekunywa kupita kiasi tu au mlevi sugu.” Mawazo hayo, aeleza Wilson, yanamfanya mwanamke awe na tumaini bandia kwamba “iwapo mwanamume huyo ataacha tu kunywa pombe, jeuri itakoma.”

      Sasa, watafiti wengi wanaona kwamba kulewa na kumpiga mke ni matatizo mawili yanayotofautiana kabisa. Hata hivyo, wanaume wengi wanaotumia vibaya vileo hawawapigi wenzi wao. Waandishi wa kitabu When Men Batter Women wanakiri hivi: “Kwa kumpiga mwanamke, mwanamume hufaulu kumtawala, kumtumikisha na kumtisha mwanamke huyo na hilo humchochea kuendeleza zoea hilo. . . . Pombe na dawa za kulevya ni vitu vya kawaida katika maisha ya mwanamume huyo. Lakini ni kosa kufikiri kwamba matumizi ya pombe husababisha jeuri.”

      • Ni wajeuri kwa kila mtu.

      Mara nyingi mtu anayempiga mke wake anaweza kuwa rafiki mzuri kwa wengine. Yeye huwa na utu tofauti kabisa. Ndiyo sababu marafiki wao huenda wasiamini wanapoambiwa kwamba yeye ni mjeuri. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, anayempiga mke huchagua kutumia ukatili kama njia ya kumtawala mke wake.

      • Wanawake hawakatai kutendewa vibaya.

      Huenda wazo hilo likatokana na kutoelewa hali yenye kusikitisha ya mwanamke asiye na mahali pa kutorokea. Huenda marafiki wakakaa naye kwa juma moja au mawili, lakini atafanya nini baada ya hapo? Si rahisi kupata kazi na kulipa kodi ya nyumba huku akiwatunza watoto wake. Na huenda sheria isimruhusu kutoroka na watoto. Wengine wamejaribu kutoroka lakini wamefuatwa na kurudishwa, ama kwa lazima au kwa kubembelezwa. Marafiki wasioelewa huenda wakaamini kimakosa kwamba wanawake hao hawakatai kutendewa vibaya.

  • “Wakati Mwingine Mimi Hufikiri Ninaota Ndoto!”
    Amkeni!—2001 | Novemba 8
    • “Wakati Mwingine Mimi Hufikiri Ninaota Ndoto!”

      Lourdes atazama mji akiwa kwenye dirisha la chumba chake, aufumba mdomo wake unaotetemeka. Yeye ni mwanamke wa Amerika-Kusini aliyeteswa kwa jeuri na mume wake Alfredo, kwa zaidi ya miaka 20. Alfredo alikuwa na nia ya kubadilika. Hata hivyo, Lourdes bado anashindwa kuzungumzia maumivu ya kimwili na ya kihisia-moyo aliyovumilia.

      “Ilianza majuma mawili tu baada ya harusi,” asema Lourdes kwa sauti ya chini. “Wakati mmoja alinigonga hata akaning’oa meno mawili. Wakati mwingine nilikwepa, akalipiga ngumi kabati la nguo. Lakini matusi yaliniumiza hata zaidi. Aliniita ‘takataka isiyofaa kitu’ na kunitendea kama mtu asiye na akili. Nilitaka kutoroka, lakini ningewezaje nikiwa na watoto watatu?”

      Alfredo amshika Lourdes begani kwa wororo. “Mimi ni mtaalamu wa cheo cha juu,” yeye asema. “Niliaibika sana nilipoitwa kortini na kuamriwa nisikutendee jeuri. Nilijaribu kubadili mazoea yangu, lakini upesi nilirudia mazoea yaleyale.”

      Mambo yalibadilikaje? Lourdes aeleza hivi kwa utulivu zaidi, “mwanamke mmoja aliye na duka pembeni mwa barabara ni Shahidi wa Yehova. Alijitolea kunifunza Biblia. Nilijifunza kwamba Yehova Mungu anathamini wanawake. Nikaanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova, ijapokuwa mwanzoni Alfredo alikasirika sana. Lilikuwa jambo geni kwangu kuwa na marafiki katika Jumba la Ufalme. Nilistaajabu kwamba ningeweza kuwa na imani, uhuru wa kusema, na hata kuwafundisha wengine imani yangu. Nilitambua kwamba Mungu ananithamini, na hilo lilinitia moyo.

      “Kulikuwa na kipindi cha badiliko kubwa nisiloweza kusahau. Bado Alfredo alikuwa akihudhuria Misa ya Katoliki kila Jumapili, na alinikataza kujifunza na Mashahidi wa Yehova. Nilimtazama kwa macho nikamwambia kwa upole lakini kwa ujasiri: ‘Alfredo, maoni yako si sawa na yangu.’ Na hakunipiga! Baadaye nilibatizwa, na kwa miaka mitano sasa hajawahi kunipiga.”

      Lakini bado kulikuwa na mabadiliko makubwa zaidi. Alfredo aeleza: “Miaka mitatu hivi baada ya Lourdes kubatizwa, mfanyakazi mwenzangu aliye mmoja wa Mashahidi wa Yehova alinialika nyumbani kwake, naye akanieleza mambo yenye kuvutia kutoka kwa Biblia. Bila kumjulisha mke wangu, nilianza kujifunza Biblia na mwanamume huyo. Hatimaye niliambatana na Lourdes mikutanoni. Hotuba nyingi nilizozisikia zilihusu maisha ya familia, na mara nyingi zilinifanya niaibike sana.”

      Alfredo alivutiwa kuona washiriki wa kutaniko, kutia ndani wanaume wakifagia baada ya mikutano. Alipowatembelea nyumbani, aliona waume wakiwasaidia wake zao kuosha vyombo. Mambo hayo yalimthibitishia Alfredo jinsi upendo wa kweli unavyoonyeshwa kwa vitendo.

      Muda mfupi baadaye, Alfredo alibatizwa, na sasa yeye na mke wake wanatumikia wakiwa wahudumu wa wakati wote. “Mara nyingi yeye hunisaidia kuondoa vyombo mezani baada ya milo na kutandika vitanda,” asema Lourdes. “Yeye hunisifu kwa upishi wangu, na huniruhusu kuchagua muziki nipendao kusikiliza au bidhaa tutakazonunua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Hayo ni mambo ambayo Alfredo hangefanya kamwe hapo awali! Hivi majuzi kwa mara ya kwanza, alininunulia shada la maua. Wakati mwingine mimi hufikiri ninaota ndoto!”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      “Nilitambua kwamba Mungu ananithamini, na hilo lilinitia moyo”

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Alfredo alivutiwa kuona washiriki wa kutaniko, kutia ndani wanaume wakifagia baada ya mikutano

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      Aliona waume wakiwasaidia wake zao kuosha vyombo

      [Picha katika ukurasa wa 10]

      “Hivi majuzi, kwa mara ya kwanza, alininunulia shada la maua”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki