Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 6/15 kur. 9-11
  • Arusi ya Pekee Sana

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Arusi ya Pekee Sana
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Kujitayarisha kwa Ajili ya Tukio Hilo
  • Tukio Lenye Shangwe
  • Ugumu wa Safari
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 6/15 kur. 9-11

Arusi ya Pekee Sana

HUKO kaskazini mwa Msumbiji kuna bonde la kijani-kibichi linalozingirwa na milima mizuri—baadhi ya hiyo ikiwa yenye miamba, na mingine ikiwa imefunikwa kwa mimea yenye kusitawi sana. Hapo ndipo kipatikanapo kijiji cha Fíngoè. Nyakati za usiku wa majira yenye baridi kali, mbingu humetameta kwa mwangaza wa nyota, na mwezi huwa mwangavu sana hivi kwamba, humulika nyumba za wanakijiji zenye kuezekwa kwa nyasi. Ilikuwa katika mazingira hayo maridadi kwamba, arusi ya pekee ilifanyika.

Mamia ya watu walitembea kwa muda wa saa nyingi, hata kwa siku nyingi, ili kuhudhuria tukio hilo la pekee. Baadhi yao walivuka maeneo yasiyokalika na yaliyo hatari, ambayo hukaliwa na fisi, simba, na ndovu. Mbali na mizigo ya safari, wageni wengi walileta kuku, mbuzi, na mboga. Baada ya kufika kijijini, walienda katika eneo lililo wazi, ambalo kwa kawaida hutumiwa kufanyia mikusanyiko ya Kikristo. Ingawa walikuwa wamechoshwa na safari, walikuwa wenye furaha, na nyuso zao zenye tabasamu zilidhihirisha taraja lenye hamu ya yale yaliyokuwa yafuate.

Ni nani waliokuwa wakioana? Walikuwa watu wengi! Naam, wenzi wengi sana. Wenzi hao hawakuwa wakishiriki katika arusi ya watu wengi ya kusisimua tu. Kinyume cha hilo, hao walikuwa wenzi wenye mioyo myeupe na wenye nia nzuri ambao hapo awali, hawakuweza kusajili ndoa zao kwa sababu waliishi katika maeneo yaliyo mbali sana na ofisi za usajili. Wenzi hao wote walipata kujua viwango vya Mungu kuhusiana na ndoa walipojifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Walijifunza kwamba walihitaji kuoana kulingana na sheria za nchi ili kumpendeza Muumba wao, aliye Mwanzilishi wa ndoa, kama vile Yosefu na Maria walivyokubali matakwa ya usajili karibu na wakati wa kuzaliwa kwa Yesu.—Luka 2:1-5.

Kujitayarisha kwa Ajili ya Tukio Hilo

Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Msumbiji iliamua kusaidia. Kwanza, ofisi ya tawi iliwasiliana na Wizara za Haki na Mambo ya Ndani zilizo katika jiji kuu, Maputo, ili kuhakikisha ni utaratibu gani uliohitajiwa na sheria. Kisha, wamishonari katika jiji kuu la jimbo la Tete wakawasiliana na wenye mamlaka wa mahali hapo ili waratibu hiyo mipango zaidi. Tarehe iliwekwa ili wamishonari na maofisa kutoka Idara ya Uthibitishaji Rasmi wa Hati za Sheria na Utambulisho wa Raia, wasafiri hadi kijiji cha Fíngoè. Wakati uleule, ofisi ya tawi ilipeleka barua ya kueleza mambo, ikitoa maagizo kwa makutaniko yote yaliyohusika. Mashahidi na pia maofisa wa mahali hapo walitazamia tukio hilo la pekee kwa hamu sana.

Jumapili, Mei 18, 1997, wamishonari watatu pamoja na maofisa wa serikali waliwasili Fíngoè. Wenye mamlaka wa mahali hapo walikuwa wametayarisha mahali pa kulala penye starehe karibu na jengo la usimamizi, kwa ajili ya hao maofisa. Hata hivyo, hao maofisa wenye kuzuru walivutiwa sana na ukaribishaji-wageni wa Mashahidi wa Yehova hivi kwamba, walipendelea zaidi kulala pamoja na wamishonari katika vibanda vilivyojengwa papo hapo. Walishangaa kupata habari kwamba, mmoja wa wapishi alikuwa mzee katika kutaniko la mahali hapo na kwamba, mwangalizi asafiriye alikuwa miongoni mwa wajitoleaji waliofanya kazi za kuchosha za hali ya chini katika matayarisho ya hiyo arusi. Hali kadhalika waliona nia nzuri ya hao wamishonari, ambao, bila kulalamika, walilala katika kibanda sahili na kuoga kwa kutumia mkebe mdogo. Hawakuwa wameona kamwe kifungo chenye nguvu kama hicho kati ya watu wa malezi mbalimbali kama hayo. Hata hivyo, walivutiwa zaidi na imani iliyoonyeshwa katika kujidhabihu sana ili kuishi kupatana na sheria ya nchi na mpango wa Mungu.

Tukio Lenye Shangwe

Hao wenzi walipowasili, walijitayarisha mara moja kwa ajili ya hatua ya kwanza ya hiyo ndoa: kupata cheti cha kuzaliwa. Wote walingoja kwa subira wakiwa wamepiga foleni mbele ya kikundi cha Uandikishaji wa Raia ili kutoa habari zao za kibinafsi. Kisha walijiunga na foleni nyingine ili wapigwe picha, ambapo baada ya hilo walienda kwa kikundi kilichotoka katika Idara ya Utambulisho wa Raia ili kupata vitambulisho vyao. Halafu walirudi kwa kikundi cha Uandikishaji wa Raia kwa ajili ya kutayarishwa kwa cheti cha ndoa walichotamani sana. Baada ya hilo, walisimama kwa subira wakingoja majina yao yatajwe kwa kutumia kikuza sauti. Kutolewa kwa hivyo vyeti vya ndoa kulitokeza hali iliyoamsha hisia-moyo. Kulikuwa na shangwe kubwa huku kila wenzi wakishikilia juu vyeti vyao vya ndoa kama kikombe cha ushindi chenye thamani.

Hayo yote yalifanyika chini ya jua kali sana. Hata hivyo, joto na vumbi hazikuvuruga shangwe ya tukio hilo.

Wanaume walikuwa wamevalia vizuri, wengi wakiwa wamevalia makoti na tai. Wanawake walikuwa wamevalia katika njia ya kitamaduni, iliyotia ndani nguo ndefu yenye rangi nyingi iitwayo capulana ambayo huvaliwa viunoni. Baadhi yao walibeba watoto wakiwa wamefungwa kwa nguo sawa na hiyo.

Mambo yaliendelea vizuri, lakini kulikuwa na wenzi wengi sana hivi kwamba, vyeti havingeweza kutolewa kwa wote katika siku moja. Usiku ulipoingia, maofisa wa serikali waliamua kwa fadhili kuendelea kuwatumikia wenzi hao. Walisema kwamba hawangeweza kuwaacha “ndugu zetu” wakingoja baada yao kujidhabihu sana ili kuwa hapo. Roho hiyo ya ushirikiano na ya kujidhabihu itakumbukwa sikuzote.

Usiku ulikuwa wenye baridi kali. Ingawa wachache walikuwa na malazi katika vibanda, wenzi walio wengi walikuwa nje, wamekusanyika pamoja kando-kando ya mioto. Hilo halikupunguza kwa vyovyote furaha ya tukio hilo. Mvumo wa kicheko na nyimbo zenye sauti nne zenye upatanifu, ulikuwa wa juu kuliko mchakariko wa mioto. Wengi walisimulia juu ya safari yao, wakishikilia hati zao walizokuwa wametoka tu kupata.

Kwenye mapambazuko baadhi yao waliingia katikati mwa kijiji kuuza kuku, mbuzi, na mboga ili wachangie gharama ya kusajiliwa kwa ndoa zao. Wengi kwa kweli “walidhabihu” hao wanyama, wakiwauza kwa bei ya chini sana kuliko thamani yao halisi. Mbuzi ni kitu chenye thamani na chenye bei kubwa kwa maskini; hata hivyo walikuwa tayari kutoa dhabihu hiyo ili waoane na kumpendeza Muumba wao.

Ugumu wa Safari

Baadhi ya hao wenzi walikuwa wamesafiri umbali mrefu ili kuwa hapo. Ilikuwa hivyo kwa Chamboko na mke wake, Nhakulira. Walisimulia kisa chao usiku wa pili wa tukio hilo huku wakipasha miguu yao moto. Ingawa Chamboko ana umri wa miaka 77, mwenye jicho moja lisiloweza kuona kabisa na jingine lisiloweza kuona vizuri, alitembea bila viatu kwa siku tatu, akiandamana na wengineo wote katika kutaniko lake, kwa kuwa alikuwa ameazimia kuhalalisha muungano wake wa miaka 52.

Anselmo Kembo, mwenye umri wa miaka 72, alikuwa tayari ameishi pamoja na Neri kwa miaka ipatayo 50. Siku chache kabla ya kufunga hiyo safari, alidungwa na mwiba mkubwa mguuni alipokuwa akilima shamba lake. Alikimbizwa kwenye hospitali iliyo karibu ili apate matibabu. Hata hivyo, aliamua kusafiri kwa miguu, akichechemea kwa maumivu hadi Fíngoè. Ilimchukua siku tatu. Huku akishika mkononi cheti chake cha ndoa, Anselmo hangeweza kuzuia furaha yake.

Mwingine aliyetoka tu kuoa ambaye astahili kukumbukwa alikuwa Evans Sinóia, aliyekuwa na wake wengi hapo zamani. Alipojifunza kweli ya Neno la Mungu, aliamua kuhalalisha muungano wake pamoja na mke wake wa kwanza, lakini huyo mke alikataa na kumwacha kwenda kuolewa na mwanamume mwingine. Mke wake wa pili, ambaye pia alikuwa akijifunza Biblia alikubali kuolewa naye. Wote wawili walitembea kupitia eneo hatari ambalo lilikuwa makao ya simba na wanyama wengine wa mwituni. Baada ya safari ya siku tatu, wao pia walifaulu kuoana kihalali.

Ijumaa, siku tano baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza kwa hao wamishonari na maofisa, kazi ilikamilishwa. Matokeo yalikuwa kwamba vitambulisho 468 na vyeti vya kuzaliwa 374 vilitolewa. Hesabu ya vyeti vya ndoa vilivyotolewa ilikuwa 233! Hali ilikuwa yenye furaha. Licha ya uchovu, wote walikubali kwamba kwa kweli tukio hilo lilistahili. Bila shaka, tukio hilo litabaki bila kufutika katika akili na mioyo ya wale waliohusika. Kwa kweli ilikuwa arusi ya pekee sana!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki