-
Wataalamu wa Tiba wa Enzi za KatiAmkeni!—2012 | Septemba
-
-
ALBUCASIS ni mtu mwingine anayejulikana sana katika historia ya tiba. Mvumbuzi huyo wa karne ya kumi, aliyeishi Andalusia, ambayo leo ni sehemu ya Hispania, aliandika muhtasari wenye mabuku 30, kutia ndani tasnifu yenye kurasa 300 kuhusu upasuaji. Katika tasnifu hiyo, alifafanua kuhusu mbinu za hali ya juu kama vile kumshona mtu aliyefanyiwa upasuaji kwa kutumia uzi ulitengenezwa kwa utumbo wa kondoo, kuondoa mawe kwenye kibofu kwa kutumia kifaa kinachopitishwa kwenye njia ya mkojo, upasuaji wa dundumio, na namna ya kuondoa mtoto wa jicho.
Albucasis alitumia mbinu ambazo zinafafanuliwa kuwa “za kisasa zaidi” ili kurahisisha matatizo yanayotokea wakati wa kujifungua na kurekebisha mabega yaliyoteguka. Alianza kutumia pamba ili kusafisha vidonda na akatumia plasta ili kuunga mifupa iliyovunjika. Pia alifafanua mbinu ya kurudisha meno yaliyotoka mahali pake, kutengeneza meno bandia, na kurekebisha meno yaliyoota vibaya, na kuondoa ukoga wa meno.
Kwa mara ya kwanza, michoro ya vifaa vya upasuaji ilipatikana katika tasnifu hiyo ya Albucasis. Ilikuwa na michoro 200 hivi ya vifaa vya upasuaji na miongozo ya jinsi ya kuvitumia na wakati wa kuvitumia. Ingawa miaka 1,000 imepita tangu wakati huo, baadhi ya vifaa hivyo havijabadilika sana.
-